Mar 30, 2011

UVCCM vs Baba zao Hii ni 'Part 2' ya filamu ya Dowans?

 Kaimu Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM, Beno Malisa

 Waziri Mkuu mstaafu, Fredrick Sumaye

BISHOP J. HILUKA
Dar es Salaam

FILAMU (kwa Kiingereza huitwa Movie au Motion pictures). Ni mfululizo wa picha zinazoonesha mwendo wa watu au vitu na kuonekana mbele ya watazamaji kwenye skrini. Ni aina ya mawasiliano yanayotumiwa kutolea hadithi au kuwaelezea watu kuhusiana na kujifunza fikra au mitazamo mipya katika jamii.

Wafuatiliaji wa filamu sehemu mbalimbali duniani huangalia filamu ambazo zinaelezea hadithi fulani kama sehemu ya burudani, au njia mojawapo ya upenzi. Filamu nyingi zinatengenezwa zikitegemewa kuoneshwa katika kumbi za video au majumba ya sinema.

Mtu wa kwanza anayeiona filamu ni mwandishi wa muswaada andishi (scriptwriter) ambaye huiona filamu hiyo mawazoni mwake kisha huandika muswaada utakaotumika katika filamu (script), kabla waigizaji hawajapewa muswaada huo kwa ajili ya kuigiza. Kisha mtayarishaji hutafuta watu watakaoshiriki kuitengeneza filamu baada ya kuwa na pesa zitakazohitajika kuwalipa waigizaji na vyombo vya utenegezaji wa filamu.

Zipo njia nyingi ambazo mtayarishaji anaweza kuzitumia kupata pesa za kuandaa filamu yake zikiwemo zile za kupitia mikopo ya benki au kupitia wawekezaji. Watayarishaji katika tasnia ya filamu wamegawanyika katika aina kuu mbili; watayarishaji wanaofanya kazi katika studio kubwa za utengenezaji wa filamu (mainstream), na wengine wa kujitegemea (independent).

Kuna aina kadhaa za filamu ambazo hugawanyika katika makundi yafuatayo; Maigizo, Uzushi wa kisayansi, Vichekesho na Filamu za mapigano.

Pindi filamu inapokamilika, nakala nyingi za filamu hutengenezwa na kusambazwa kupitia diski (DVD na VCD) au mikanda maalum ya kuhifadhia filamu (VHS) na kusambazwa katika majumba ya sinema kwa ajili ya kuzinduliwa na kisha kuingizwa sokoni.

Tangu kumalizikika uchaguzi mkuu wa mwaka jana, 2010, nimekuwa nikishuhudia vituko kadha wa kadha ambavyo kwangu ni kama filamu ya vichekesho (comedy). Kwanza ilianzia kwenye filamu ya Dowans, ambayo hadi sasa simjui steringi wala muongozaji wake.

Hili la Dowans ni kisa kilichoandaliwa siku nyingi kidogo; tatizo lilianzia ndani ya CCM kufuatia makundi yaliyozaliwa mwaka 1995, na baadaye kufuatiwa na mgawanyiko mkubwa ulioanzisha kundi la wanaharakati maarufu kama “Mtandao” mwaka 2005.

Bahati mbaya mtandao haukudumu muda mrefu kutokana na wajumbe wake kuhitilafiana katika masuala kadhaa, na hivyo kuufanya usambaratike miezi michache tu baada ya uchaguzi wa 2005 na kutokea makundi matatu. Mgawanyiko huo ndiyo umepelekea makundi yake kufikia kiwango ambacho si rahisi sana kuyaunganisha au kuyamaliza, na wala hayawezi kuzikwa kama watu wengine wanavyojidanganya. Kuyaunganisha makundi haya ni kama kuwaunganisha wana wa Israel na Wapalestina. Na kulazimisha kuyazika makundi haya watajikuta wakiyazika pamoja na chama.

Katika filamu hii mpya “UVCCM vs Baba zao”, ambayo kwa mtazamo wangu ni muendelezo (part two) wa filamu ya kwanza (Dowans), imejengwa katika maudhui (concept) yaleyale japo kisa chake kinaonekana kuwa tofauti kidogo. Kabla ya yote ningependa kuwapongeza sana waongozaji wa filamu hizi kwa kuwa wanafanya kazi yao kwa umakini mkubwa sana. Kwani ni wao pekee wanaojua kwa nini filamu hizi zinapaswa kuandaliwa kipindi hiki cha sasa.

Katika filamu yoyote, mwandishi anayeandika mwongozo anapaswa kuzingatia sana kitu kimoja muhimu ambacho endapo kitakosekana sinema itakwenda shaghalabaghala; PLOT. Plot ni kisa halisi kinachoendelea kwenye hadithi, kisa hiki huwa na hatua muhimu tano ambazo kitaalam hujulikana kama; Introduction, Rising action, Climax, Falling action na Conclusion.

Katika filamu zinazoendelea sasa plot yake imebebwa na hoja za viongozi wa Umoja wa Vijana wa CCM tangu tamko lao zito kuhusu sakata la kampuni ya kufua umeme ya Dowans, wakipendekeza kuwa hoja kuhusu sakata hilo irudishwe bungeni ili Watanzania wajue nani kaifikisha serikali ilipo, na hatua zichukuliwe dhidi ya wahusika! Kwangu mimi hii ilikuwa ni hatua (stage) ya kwanza kabisa ya plot ya filamu hii, 'introduction'.

Kwa mtazamo wa juujuu unaweza kudhani tamko lililotolewa katika mkutano wa wajumbe wa Kamati ya Utekelezaji ya Baraza Kuu la Umoja huo na Jukwaa la Wahariri Tanzania, kwenye hoteli ya Peacock, mjini Dar es Salaam lilikuwa na nia njema ya kutaka kuokoa fedha za Watanzania zisichukuliwe na mafisadi, lakini ukitazama kwa undani utagundua kuwa lililenga kutaka kuwasaidia baadhi ya viongozi waliokumbwa na kashfa ili kuwasafishia njia ya ikulu 2015.

Hatua ya pili ya plot 'rising action', ilianzia kwenye kulaani kitendo cha mawaziri (si wote waliolengwa) kupingana hadharani na kutokuwa na uwajibikaji wa pamoja, na kuwataka kama wamechoka kuziongoza wizara waachie ngazi, wawapishe vijana wengine wenye nia njema ya kuongoza na kufuata maadili ya taifa.

Kauli ya Umoja huo kuapa kuwa utafanya kampeni za kuhakikisha viongozi fulani, uliodai kuwa wana malengo ya kupata Urais mwaka 2015, hawapati nafasi yoyote ya uongozi ni hatua ya tatu “climax” ya plot, na hapa ndo' filamu ilipoanza kunoga zaidi kwani iliwaibua baadhi ya wastaafu, wanaopaswa kuwa baba wa vijana hawa waliolazimika kujibu hoja hizo.

Kutishana huku hata kama wenyewe wanajaribu kukanusha kunaonekana wazi kuwa na agenda iliyojificha kuelekea uchaguzi wa 2015, kupitia uchaguzi ndani ya CCM unaotarajiwa kufanyika mwaka 2012. Kauli ya kwamba wanaokikosoa chama hadharani wasipewe nafasi za uongozi wa chama kwenye uchaguzi wa chama wa mwaka 2012 ni dalili za maandalizi ya mbio za kuelekea Ikulu 2015.

Eti wenyewe wanadai kuwa wanajivua gamba la zamani na kukivika chama gamba jipya! Nawashauri wajaribu kuwa na tahadhari kwani wasije wakadhani kwamba wanajivua gamba kama nyoka kumbe wanavua nguo na kubaki watupu!

Wadadisi wamekuwa wakijiuliza maswali yasiyopata majibu; inakuwaje kiongozi mwandamizi wa jumuiya ya chama tena nyeti ya vijana kuwachambua na hata kuwatusi baadhi ya viongozi wastaafu na hata waliopo serikalini kiasi hicho kama siyo 'picha' au hana baraka za wakubwa fulani?

Kwa upande mwingine, wananchi walio wengi sasa wanaamini kwamba chama kikongwe kimeanza kupauka na kama juhudi za makusudi hazitachukuliwa kurekebisha hali hii, basi kitakosa sifa za kuongoza nchi yetu kuelekea kwenye maendeleo. Wananchi wanaanza kukosa imani, wakidhani kuwa vijana wanatumiwa na kundi fulani ili waliaibishe kundi jingine kwa manufaa ya kundi wanalolitetea.

Bila kuweka wazi dira katika masuala haya nyeti kwa maslahi ya taifa, matokeo yataendelea kuwa ni malumbano endelevu, na kila kukicha mafisadi, ambao mimi nadhani ndiyo waandishi na waongozaji wa filamu hizi, watazidi kubuni mbinu mpya za kuendelea kulididimiza na hatimaye kuliteka na kulitawala taifa hili!

Kama ilivyo kwa filamu yoyote ile, lazima kuwe na muongozaji wa filamu na hadithi lazima iwe na mchezaji kinara 'steringi' anayeinogesha, hivi katika sakata hili kuna mtu anaweza kuniambia nani hasa kinara aliye nyuma ya sakata zima, ambalo linalitikisa taifa hili?

Kama haya yanafanyika kwa nia njema au kwa kutumiwa na watu fulani, bora kwanza wahusika wangejiuliza maswali kuhusu faida na hasara ya mchezo huu, isije ikawa ni mchezo wa paka na panya kwani siku zote majuto ni mjukuu!

Nawasihi wasomaji wangu wasiwe na haraka, hivi karibuni tutazishuhudia hatua mbili (falling action na conclusion) zilizobakia za plot yetu katika kukamilisha filamu hii.

Mungu ibariki Tanzania.

SHEIKH SHARIF AHMED: Akabiliana na Spika wa Bunge nchini Somalia aliyetangaza azma ya kuwa Rais

 Rais wa Somalia, Sheikh Sharif Sheikh Ahmed

MOGADISHU
Somalia

MWEZI Januari mwaka huu Spika wa Bunge la Somalia, Sharif Sheikh Hassan alionesha azma ya kuwa rais wa Somalia baada ya kufanya mkutano na koo za Digil na Mirifle jijini Nairobi, Kenya.

Hata hivyo, mkutano huo ulitibuka baada ya wabunge waliowakilisha pande zote mbili kuchukuwa mirengo tofauti juu ya azimio hilo la spika dhidi ya rais Sheikh Sharif Ahmed. Kwa siku za hivi karibuni, Sharif Sheikh Hassan amekuwa akijitahidi kuungwa mkono na Wasomali walio nchi za nje na kuwepo utata kati yake na Rais wa serikali hiyo ya mpito, Sheikh Sharif.

Na katika kuendeleza kampeni zake mapema mwezi wa tatu, Spika huyo wa Bunge alitangaza kuwa, bunge la serikali ya mpito ya Somalia limeongeza muda wake kwa miaka mitatu. Muda wa bunge hilo pamoja na wa serikali ya mpito ya Somalia ulitarajiwa kumalizika mwezi Agosti mwaka huu lakini wabunge wa Somalia wamepiga kura na kuongeza muda huo.

Alisema kuwa, bunge litafanya mabadiliko makubwa katika kuwahudumia wananchi wa Somalia na kusisitiza kwamba hatua hiyo waliyochukua, itazuia Somalia kubaki bila serikali. Spika wa Bunge la Somalia aidha ameongeza kuwa, bunge la nchi hiyo litamchagua rais na spika mpya wakati kipindi cha kwanza cha bunge hilo kitakapofikia ukingoni hapo mwezi Julai mwaka huu.

Mwaka jana Rais Sheikh Sharif Ahmed, alimteua Mmarekani mwenye asili ya Kisomali kuwa Waziri Mkuu wa Somalia. Uteuzi wa Mohammed Abdullahi, mwanadiplomasia wa zamani aliyesomea nchini Marekani, ilikuwa ni juhudi mpya ya kuimarisha mchakato wa kukabiliana na wanamgambo wanaolidhibiti eneo kubwa la Somalia.

Abdulahi anakabiliwa na kibarua kipevu cha kuiongoza serikali ya mpito inayoyumba, inayokabiliwa na mizozo ya ndani ya kisiasa, rushwa na iliyobanwa na wanamgambo katika sehemu ndogo ya mji mkuu Mogadishu.

Lakini kubwa linaloisumbua nchi hiyo ni ugomvi wa madaraka unaojitokeza baina ya Spika na Rais, ugomvi ambao pia uliikumba serikali ya zamani ya mpito nchini humo.

Sheikh Sharif ni na hasa:

Sheikh Sharif Sheikh Ahmed alizaliwa Julai 25, 1964. Ahmed Alizaliwa katika eneo la Shabeellaha Dhexe, Jimbo la Kusini mwa Somalia, na alisoma katika vyuo vikuu vya nchi za Libya na Sudan.

Sharif Ahmed alianza elimu yake katika Taasisi ya Sheikh Sufi, ambayo ilikuwa ikihusishwa na Chuo Kikuu cha Al-Azhar kilichopo nchini Misri. Baada ya hapo alikwenda Sudan katika Chuo Kikuu cha Kordufan mwishoni mwa mwaka 1992, alikopata shahada ya kwanza katika lugha ya Kiarabu na Jiografia katika mji wa Aldalanj.

Mwaka 1994, Chuo Kikuu kilibadilishwa jina na kuitwa Chuo Kikuu cha Dalanj, na Sheikh Sharif alielekea Tripoli, mji mkuu wa Libya, baada ya kumaliza miaka miwili tu kati ya minne iliyohitajika. Nchini Libya, alijiunga na Chuo Kikuu Huria ambako alipata shahada ya kwanza ya Sheria na Sharia za Kiislam, na kuhitimu mwaka 1998.

Ameshawaahi kufanya kazi kama mwalimu wa shule ya sekondari wa masomi ya Jiografia, Lugha ya Kiarabu na masomo ya dini. Ukiachia lugha yake ya asili inayotumika Somalia, Ahmed huzungumza kwa ufasaha lugha ya Kiarabu, Kitaliano na Kiingereza.

Muungano wa Mahakama za Kiislamu (ICU):

Baada ya kurudi kutoka nje ya nchi, Ahmed akaingia ICU na kuchaguliwa kwa kiongozi wa mahakama ndogo ndogo za ukoo katika eneo la Jowhar. Miaka michache baadaye, genge moja la kihalifu lenye makao yake mjini Mogadishu, mji mkuu wa Somalia, lilimteka nyara mwanafunzi na kudai fidia kutoka kwa familia yake kama malipo ya kurudishwa kwa kijana huyo.

Tukio hili ni moja ya matukio mengi ya utekaji nyara na mauaji yanayofanywa na makundi yenye silaha katika mji mkuu wa Somalia ambao umesababisha serikali kuu ya Somalia kushindwa kuudhibiti. Tukio hili liliripotiwa kuwa lilikuwa ni jaribio la kiuongozi katika maisha ya Sheikh Ahmed na kupelekea ushiriki wake zaidi ndani ya ICU.

Mwaka 2004, Sheikh Ahmed alikuwa mmoja wa viongozi katika Mahakama za Kiislamu mjini Mogadishu. Marafiki wake wa karibu na washirika wake ni pamoja na Sheikh Hassan Dahir Aweys, mmoja wa waanzilishi wa ICU, na Aden Hashi Farah “Eyrow”, mtu ambaye Washington inadai ana uhusiano na mtandao wa kigaidi wa Al-Qaida na aliwahi kupigana vita vya Afganistan mwaka 2001.

Septemba 9, 2006, chini ya mwamvuli wa Abdiqasim Saladi Hassan, Rais wa zamani wa Serikali ya Mpito ya Taifa nchini Somalia, Sheikh Ahmed na wenzake kadhaa walihudhuria sherehe za Umoja wa Afrika (AU) mjini Sirte, Libya, kuashiria kumbukumbu ya miaka saba ya mkutano wa kilele wa viongozi wa Afrika.

Katika mahojiano na mashirika ya habari ya Reuters na BBC, Sheikh Ahmed alipendekeza kuwa ujumbe wake utafute msaada kutoka Libya na mataifa mengine ya Afrika ili kupata suluhu kati ya Waislam na Serikali ya Mpito ya Taifa nchini Somalia.

Hata hivyo, aliripotiwa kuwasili Khartoum, Sudan saa 48 kabla ya kuanza kwa mkutano kati ya serikali ya Somalia na ICU. Sheikh Ahmed alisema Ethiopia ilikuwa adui wa Somalia kwa zaidi ya miaka 500, na alitoa mashtaka kutokana na vikosi vya Ethiopia kuingilia kati nchini Somalia. Ethiopia ilikana kwa askari wake kuhusika na mapigano nchini Somalia.

Disemba 28, 2006, baada ya miezi sita tu ya kuwa madarakani na kushindwa kwa jeshi la ICU, aliamua kupambana na vikosi vya Ethiopia nchini Somalia. Baada ya ICU kushindwa katika vita ya Jilib na kutelekezwa Kismayo, aliamua kukimbilia mpaka wa Kenya.

Kabla ya kukimbia, Sheikh Sharif aliishi na mke wake na watoto wawili, Ahmad, mwenye umri wa miaka 9 na Abdullah, ambaye alikuwa ameanza kutembea, katika nyumba ya kawaida mjini Mogadishu. Alikutana na Balozi wa Marekani nchini Kenya kwa ajili ya mazungumzo kuhusu ushirikiano na TFG. Wakati huo alikuwa akiishi chini ya ulinzi wa mamlaka ya Kenya akikaa katika hoteli jijini Nairobi.

Tarehe 1 Februari 2007 Ahmed Sharif aliondolewa kutoka mamlaka ya polisi wa Kenya. Februari 8, alielekea Yemen ambapo wanachama wengine wa ICU walikwenda pia.

Uchaguzi wa rais 2009:

Duru ya kwanza ya upigaji kura ilipoanza, wagombea kadhaa walijiondoa, na kuongeza uvumi kwamba ulikuwa ni uchaguzi kati ya Nur Hassan Hussein na Sharif Ahmed. Katika raundi ya kwanza, Sharif Ahmed alipata kura 215, Maslah Mohamed Siad alipata kura 60, na Hussein alipata kura 59.

Hata hivyo Hussein alijiondoa katika kugombea, hivyo kuongeza uwezekano wa Sharif Ahmed kuwa rais. Katika raundi ya mwisho ya uchaguzi wa rais, Sharif alishinda kwa kura 293. Baada ya kushinda uchaguzi mapema Januari 31, 2009, Ahmed aliapishwa baadaye mchana wa siku hiyo katika hoteli ya Kempinski iliyopo Djibout.

Mwezi Aprili na Mei 2010, kulijitokeza ufa mkubwa kati ya Waziri Mkuu wa Somalia, Omar Abdirashid Ali Sharmarke na aliyekuwa Spika wa Bunge, Adan Mohamed Nuur Madobe, ambao ulipelekea Spika ajiuzulu mbele ya bunge, baada ya bunge kupiga kura ya kumuondoa.

Licha ya Madobe kukubaliana na uamuzi wa kuondoka madarakani kama Spika, Rais Sharif alitangaza muda mfupi baadaye kufukuzwa kazi kwa Waziri Mkuu, Sharmarke na nia yake ya kuunda serikali mpya. Hatua hii haraka ilikaribishwa kwa mikono miwili na Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia, Ahmedou Ould-Abdallah, mshirika wa karibu na msaidizi wa Sharif.

Katika kujibu, Waziri Mkuu Sharmarke aliwaambia waandishi wa habari kwamba Sharif hakuwa na mamlaka ya kumfukuza, na alisema kuwa angeweza kubaki madarakani hadi bunge lipige kura ya kutokuwa na imani naye.

Mei 20, Rais Sharif aliacha uamuzi wake wa kumtimua Waziri Mkuu Sharmarke. Mabadiliko yalikuja baada ya kushauriana na wanasheria, waliomshauri kuwa kufukuzwa kwa waziri mkuu huyo kulikuwa ni kinyume cha katiba.

Mei 26, kufuatia kutokubaliana tena na Waziri Mkuu Sharmarke, Rais Sharif alitangaza tena mpango wake wa nchi moja kuteua Waziri mpya. Washirika wa Sharif pia waliripotiwa kujaribu kumshawishi Sharmarke kujiuzulu, lakini alikataa tena hatua hiyo na aliapa kukaa madarakani mpaka muda wake wa kikatiba uishe.

Na ilipofika mwezi Oktoba 14, 2010, ndipo Rais Sharif alipofanikiwa adhma yake na kumteua katibu maalum wa kwanza wa zamani wa ubalozi wa Somalia mjini Washington, Mohamed Abdullahi Mohamed, kuwa Waziri Mkuu mpya wa Somalia.

Makala haya yameandaliwa na Bishop J. Hiluka kwa msaada wa mashirika mbalimbali ya habari ya kimataifa.

Kulikoni tuzo za muziki za Kili?

 Mratibu wa Tuzo za Kili Music 2011, kutoka BASATA, Angelo Luhala

Msanii Abbas Kinzasa maaruf kama 20%


BISHOP J. HILUKA
Dar es Salaam

KOMBINENGA, Man Walter, Man Maji...” kibwagizo hiki kimetokea kuwa maarufu sana miongoni mwa wadau wa muziki wa kizazi kipya na sasa kinatamba kwenye vituo mbalimbali vya redio na televisheni kila unapopigwa wimbo wowote wa msanii Abbas Kinzasa, maaruf kwa jina la 20 percent.

Naomba nikiri kuwa mimi binafsi ni mpenzi mkubwa wa nyimbo za msanii huyu kutokana na ujumbe wake kuigusa jamii moja kwa moja na wala sikushangaa kuona akizoa tuzo tano na kuweka rekodi ya aina yake tangu tuzo zianze kufanyika miaka 12 iliyopita zilipoasisiwa. Sina shaka kuwa rekodi iliyowekwa na msanii huyu haitavunjwa na msanii yeyote katika miaka mingi ijayo. Ama kweli Wabongo sasa wanaelewa asili na vionjo vya muziki wa nyumbani.

Kama ambavyo wadau wengi wa muziki wamebainisha, kwa kweli usiku wa Jumamosi iliyopita ulikuwa ni ‘Usiku mwaka' wa msanii 20 percent (20%), katika tamasha liliooneshwa moja kwa moja na kituo cha televisheni cha ITV, kutokea ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam. Hongera sana 20 percent.

Umahiri wa 20 percent katika tungo zenye kuigusa jamii ulidhihirishwa na mashabiki wengi walioonekana kumshangilia kila jina au wimbo wake ulipokuwa ukitajwa, taswira iliyoonesha kwamba anakubalika vilivyo katika jamii kwa ujumla na alistahili kutwaa tuzo hizo.

Tuzo alizonyakua msanii huyo ni; Msanii Bora wa Kiume, Wimbo Bora wa mwaka, Mwimbaji Bora wa Kiume, Mtunzi Bora wa nyimbo na Wimbo Bora wa Afro Pop.

Katika tamasha la mwaka huu kulikuwa na tuzo 23 zilizotolewa. Binafsi sikuona sababu ya kuwa na tuzo nyingi kiasi chicho kulikopelekea baadhi ya tuzo kukanganya kwa kuonekana zinafanana sana. Sijui waratibu wa tuzo hizo, Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), na wadhamini wake, Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia Bia ya Kilimanjaro Premium Lager waliziweka kwa maslahi ya nani?

Mfano sikuona sababu ya kutenganisha tuzo ya Msanii bora wa kiume na Mwimbaji Bora wa Kiume. Halikadhalika Msanii Bora wa Kike na Mwimbaji Bora wa Kike.

Hata hivyo, kama kawaida, tuzo za mwaka huu hazikukosa kulalamikiwa na wadau kuwa kulikuwa na uchakachuaji wa makusudi ili kuwabeba baadhi ya wasanii wasiostahili ili kukidhi matakwa ya watu fulani wenye nguvu katika kamati inayoratibu tuzo hizo.

Kwa mfano, inawezekanaje msanii 20 percent ang'are katika sehemu tano halafu mtayarishaji wa nyimbo zake, Man Walter ambaye naye alikuwa akiwania nafasi ya Mtayarishaji Bora akose tuzo kwa kushindwa na Lamar? Kwa wadau walio makini huu ni ubababishaji wa wazi.

Halikadhalika chombo kimoja cha habari kilimnukuu mwimbaji gwiji wa mipasho, Hadija Kopa akipinga kukosa tuzo huku akisema kuwa baadhi ya washindi waliandaliwa na wahusika. Chazo hicho cha habari kilimnukuu Kopa kushangazwa kwake katika tuzo ya Mwimbaji Bora wa Kike kuchukuliwa na msanii chipukizi, Linah Sanga na kuwabwaga wakongwe akiwemo Kopa mwenyewe.

Malalamiko hayakuishia hapo, kuna mdau mmoja mfuatiliajia mkubwa wa masuala ya muziki aliniuliza inawezekana vipi Msanii Bora wa Hip hop asiwe na wimbo bora ya Hip hop? Aliniuliza akichukulia kuwa Joh Makini kapata tuzo ya Msanii Bora wa Hip hop lakini ameshindwa kwenye wimbo bora ya Hip hop na JCB, akienda mbali zaidi kwa kusema kuwa JCB ndiye aliyestahili kupewa tuzo ya Msanii bora wa mwaka.

Sikuwa nimelifikiria hilo kwa sababu binafsi nikiri kuwa sizifahamu nyimbo za wasanii hao wawili na wala mimi si mpenzi wa aina ya nyimbo wanazoziimba, hivyo nilijaribu kufanya utafiti mdogo na kuulizia uhusiano wa mambo hayo mawili. Wapo baadhi ya wadau walionieleza ya kwamba kuwa na wimbo bora ya Hip hop hakumaanishi kuwa Msanii Bora wa Hip hop, kwani Msanii Bora wa Hip hop ni mshindi wa moja kwa moja (overall winner) katika Hip hop.

Lakini kuna waliopinga kwa kusema utakuwaje overall winner wa kipengele ambacho hujashinda hata wimbo mmoja? Je, inawezekana kuwa hiki ni kituko cha mwaka? Au ndo kama tulivyojionea kituko kingine cha wimbo wa Mpoki 'Shangazi' kuushinda 'Adela' wa Mrisho Mpoto!

Kwa nini waandaaji wasitafute namna nzuri ya kuzishindanisha nyimbo ili kuondoa malalamiko yanayojitokeza kila mwaka? Mbona tuzo kama Grammy Music Awards zinaendeshwa kwa uwazi na vigezo vyake vinajionesha dhahiri kiasi cha kupelekea kutokuwepo manung'uniko, na hata kama kunatokea lawama basi huwa ni za kawaida sana.

Tuzo za Kili ni mfano wa tuzo maarufu za Grammy ambazo huratibiwa na National Academy of Recording Arts and Science ya Marekani na hutolewa ili kutambua mafanikio bora katika sekta ya muziki. Tofauti na tuzo za Kili, Grammy Awards huwa na Vipengele vichache, hasa wakikazia kwenye Albamu ya Mwaka, Rekodi ya Mwaka, Wimbo wa Mwaka, Msanii bora Anayechipukia na kadhalika.

Jambo jingine lisilopendeza machoni mwa wadau wa muziki ni kusahauliwa kwa muasisi wa tuzo hizo, marehemu James Dandu kana kwamba hakuwahi kuwepo wala kuzianzisha tuzo hizo! Jambo hili linakwenda sambamba na kutoa tuzo (trophy) zisizo na ubora wowote kabisa.

Inasikitisha kwa msanii aliyefanya kazi mwaka mzima akirekodi nyimbo zake kwa gharama kubwa anapokuja kuzawadiwa kipande cha mbao kilichopakwa rangi ya chuma na shilingi laki tano tu! Basata na TBL mnatupeleka wapi?

Washindi wa tuzo za muziki za Kili 201 ni kama ifuatavyo: Wimbo Bora wa Asili (Shangazi – Mpoki Ft. Kassim), Wimbo Bora wa Bendi (Shika Ushikapo – Mapacha Watatu Ft. Mzee Yusuph), Wimbo Bora wa Taarab (My Valentine – Jahazi), Wimbo Bora wa R&B (Nikikupata – Ben Paul), Wimbo Bora wa Hip-Hop (Ukisikia Pah! – JCB Ft. Fid Q, Jay Mo na Chidi Benz), Wimbo Bora wa Afro-Pop (Tamaa Mbaya – 20 percent), Wimbo Bora wa Zouk/Rhumba (Nabembelezwa – Barnaba) na Wimbo Bora wa Reggae (Ujio Mpya – Hard Mad Ft. Enika & BNV).

Tuzo zingine ni Wimbo Bora wa Ragga Dancehall (Action – Cpwaa Ft. Ms. Triniti, Dully Sykes na Ngwear), Wimbo Bora wa Kushirikiana (Ukisikia Pah! – JCB Ft. Fid Q, Jay Mo na Chidi Benz), Wimbo Bora wa Afrika Mashariki (Nitafanya – Kidum Ft. Lady Jay Dee), Video Bora ya Mwaka ya Muziki (Action – Cpwaa Ft. Ms. Triniti, Dully Sykes na Ngwear), Mtunzi Bora wa Nyimbo (20 percent), Mtayarishaji Bora wa Nyimbo (Lamar) na Rapa Bora wa Mwaka kwa Bendi (Khalid Chokoraa).

Nyingine ni pamoja na Msanii Bora wa Hip-Hop (Joh Makini), Msanii Bora Anayechipukia (Linah), Hall of Fame;
Taasisi – (TBC), Binafsi – Said Mabela. Mwimbaji Bora wa Kike (Linah), Mwimbaji Bora wa Kiume (20 percent), Wimbo Bora wa Mwaka (Tamaa Mbaya – 20 percent), Msanii Bora wa Muziki wa Kike (Lady Jay Dee) na Msanii Bora wa Muziki wa Kiume (20 percent).

Tuzo ya mwimbaji bora wa kike ilikwenda kwa Lina Sanga aliyekuwa akichuana na Judith Wambura ‘Lady Jay Dee’, Mwasiti Almasi, Khadija Kopa na Sara Kaisi ‘Shaa’.

Mar 23, 2011

Inahitajika elimu ya mahitaji maalum kwa Walemavu


 Watu wenye ulemavu wanapaswa kupewa fursa zilizo sawia kama watu wengine wasio na ulemavu.

BISHOP J. HILUKA
Dar es Salaam

HIVI karibuni nilisikitishwa sana na habari niliyoelezwa kwa njia ya ujumbe mfupi wa simu na mwananchi mmoja mwenye ulemavu aliyedai kunyanyaswa kutokana na ulemavu wake na wafanyakazi wa chombo kimoja cha usafiri.

Mwananchi huyo aliyewasiliana nami kwa namba ya simu 0754 440155 aliniandikia ujumbe huu: “Nilisafiri na Basi la (analitaja jina) toka Dar hadi Arusha, tulifika Arusha saa 2 usiku, watu wote walipoteremka nilibaki ndani ya gari huku kiti changu cha magurudumu (wheel chair) kinachoniwezeshwa kutembea kikiwa kwenye buti ya gari. Kila nilipowaomba wafanyakazi wa gari hiyo kunipatia kiti changu walikaa kimya hadi ilipotimu saa 5:00 usiku walipotaka kulaza gari ndipo walipoitoa wheel chair yangu. Nikapeleka shauri langu polisi, na sasa shauri lipo mahakamani. Kwa kweli nilifedheheka sana.”

Mwananchi huyo ambaye sintomtaja jina, naamini kuwa atakuwa ameumia sana moyoni kutokana na kitendo alichofanyiwa na wafanyakazi hao kutokana na ulemavu wake. Sipendi kuliongelea kwa kina suala lake kwa kuwa lipo mahakamani, lakini itoshe tu kusema jamii hii inahitaji kuelimishwa kuhusu walemavu.

Juzi asubuhi, wakati naangalia taarifa ya habari ya asubuhi kupitia televisheni nilimsikia mwananchi mmoja ambaye ni mlemavu wa macho, Amon Anastaz, kiongozi kutoka taasisi ya watu wenye ulemavu (Shivyata), akizungumza kuhusu uzinduzi wa mkakati wa watu wenye ulemavu 2010-2015 wenye lengo la kuhakikisha “kunakuwepo na taifa jumuishi” hasa ikizingatiwa kuwa asilimia 10 ya idadi ya watu nchini ni jamii ya watu wenye ulemavu.

Mkakati huo uliozinduliwa Jumatano ya Machi 23, 2011 katika hoteli ya Blue Pearl, Ubungo Plaza una nia ya kuielimisha jamii juu ya mtazamo wake na dhana kuwa watu wenye ulemavu ni watu wanaohitaji hisani badala ya kuwezeshwa.

Bahati mbaya wakati naandaa makala yangu sikuwa nimepata taarifa rasmi kuhusu kilichozungumzwa hapo Ubungo Plaza, lakini kwa kuwa tayari nilikuwa nimehuzunishwa na kitendo kilichofanywa huko Arusha, nilidhani ipo haja ya kuandika makala hii ili kuieleza serikali yetu pamoja na mambo mengine, umuhimu wa kuwepo elimu ya mahitaji maalum kwa walemavu.

Kama alivyodokeza kiongozi wa Shivyata kuwa watu wenye ulemavu hawahitaji hisani bali kuwezeshwa, hivyo pamoja na kusisitiza uwepo wa elimu ya mahitaji maalum pia watu wenye ulemavu katika jamii yetu wanatakiwa kutotengwa kwenye masuala mbalimbali ya kuliletea Taifa maendeleo, hususan kwenye suala la ajira ili kuwawezesha kuwaondoa katika hali ya utegemezi na hatimaye kujitegemea wenyewe.

Watu wenye ulemavu wanapaswa kupewa fursa zilizo sawia kama watu wengine wasio na ulemavu. Imekuwa ni kawaida kuona katika jamii zetu, taasisi ama katika mashirika walemavu wakinyimwa fursa hiyo hata kwa wale walemavu wenye elimu nzuri huku wakiwatolea visingizio vyenye lengo la kutowaajiri kutokana na ulemavu wao.

Kwa kweli hali hii inakatisha tamaa sana hasa kwa wale walemavu waliopata nafasi ya kujiendeleza kielimu kupitia tasnia tofauti hapa nchini lakini jamii ikawachukulia kama mzigo kwa taifa au kundi la watu wenye kungoja hisani.

Suala la mwananchi aliyenyanyaswa huko Arusha kwa sababu ya ulemavu wake linadhihirisha jinsi ambavyo jamii yetu bado haijastaarabika katika suala la walemavu, kitendo kinachopaswa kukemewa kwa nguvu zote za wanaharakati na wananchi wapenda usawa na maendeleo.

Na katika kutilia mkao suala hili, walezi na wazazi walio na watoto wenye ulemavu wanapaswa kuwatoa watoto hao bila kuwaficha au kuwaweka ndani pekee kwani kwa kufanya hivyo ni kuwanyima haki zinazostahili kwa watoto wote pasipo kubagua na hata misaada inayotolewa kwa watoto walio na ulemavu hususan katika elimu.

Kama nilivyoandika katika makala ya wiki iliyopita
“Ni lini walemavu watapewa fursa sawa kwenye jamii yetu?” nikashauri kuhusu kuangalia upya suala la miundombinu mbalimbali, jamii inatakiwa sasa kujenga mazingira rafiki yatakayoepusha malalamiko ya kuonekana kutengwa kwa walemavu, ikiwa ni pamoja na ofisi binafsi, mahoteli, nyumba za wageni, viwanda kwani yapo maeneo yanayowabana walemavu hasa wa miguu kushindwa kupita kwa urahisi kutokana na hali zao.

Naishukuru serikali japo imeanza kuona tatizo lililopo hasa katika muundo wetu wa elimu ya lazima ambao upo katika kipindi cha mabadiliko kwa kuanza kutoa fursa, ingawa bado hakuna juhudi za makusudi za kivitendo katika kumaliza tatizo hili linalopelekea watoto walemavu kuwa wengi kati ya wale wanaoacha shule.

Watoto walemavu wana fursa ndogo ya kupata elimu, hasa sehemu za mashambani. Shule chache za elimu maalum ziko kwa watoto wenye shida ya kusikia, watoto wasioona na wenye upungufu wa akili. Shule kama hizi zinapatikana katika maeneo machache kwa baadhi ya miji mikubwa tu.

Kwa kweli bado kuna shida nyingi zinazowakabili watoto walemavu. Watoto wengi wenye ulemavu ambao wanastahili kusoma mashuleni hawawezi kwenda kwa sababu ya uzito wa ulemavu kwenye maeneo ya vijijini. Ubaguzi wa jinsia katika elimu uko chini sana na kuna asilimia kubwa ya watoto walemavu katika shule za kawaida (badala ya shule maalum) kuliko nchi zingine.

Lakini, elimu waipatayo mara nyingi haileti faida, na ufikiaji mbaya kwa watoto walemavu. Mara nyingi utaratibu wa mafunzo hauwezi kubadilika sambamba kwa watoto walemavu, na walimu wengi hawana ufahamu mzuri wa mahitaji ya watoto walemavu, ama uwezo wao.

Walimu wengine bado wana hali ya ubaguzi kwa watoto wenye ulemavu, ambao mara nyingi hawatambulikani kwa sababu ya ukubwa wa madarasa. Watoto wengi wenye ulemavu mkubwa bado wako nyumbani.

Kufanikiwa katika kuendeleza miradi ya elimu ya mjumuisho kunahitaji uhusishaji na usaidizi wa wazazi wa watoto wenye ulemavu katika daraja zote. Tunahitaji kuwa na program ya usaidizi wa mradi wa kuokoa watoto, vikundi vya familia zenye watoto walemavu wanapaswa kuunda chama kitakachohusishwa kwa karibu sana programu hii katika kuanzisha shughuli za elimu ya mjumuisho kwao.

Tunaweza hata kujifunza kutoka Mongolia, moja ya nchi zenye matatizo ya sera kuhusu jamii ya watu wenye ulemavu ambao waliwahi kuwa na warsha ya kimataifa kuhusu sera za elimu mjumuisho kwa watoto walemavu, iliyofanyika Ulaanbaatar mnamo machi 2003, neno 'elimu mchanganyiko' lilibadilishwa kuwa 'elimu mjumuisho' kwa ajili ya mradi wa kuokoa watoto [SC UK].

Warsha hiyo ilisimamiwa na mradi wa watoto uliolenga: kuupa sura mpya uanzilishi wa elimu mjumuisho nchini Mongolia; kusaidia wahusika kusaidiana, na kujifundisha kutoka, nchi zingine kuhusu maendeleo na utekelezaji wa sera; kutambua mambo muhimu na mapendekezo ya kuendeleza na kutekeleza sera hizo nchini Mongolia. Mradi huo wa kuokoa watoto [SC UK] unaamini kwamba kuhimiza sera ndio njia ya kusuluhisha matatizo.

Mongolia pia wameanzisha ushirikiano thabiti na muungano wa wazazi wenye watoto walemavu [APDC], na, kupitia ushirikiano na programu maalum, utaratibu wa elimu mjumuisho kwa watoto walemavu ukabuniwa. Hii ilikubaliwa kwa pamoja na Waziri wa Elimu, Waziri wa Afya na Waziri wa Maswala ya Jamii na Uchumi mnamo Disemba 2003. Kwa sasa wizara hizi, mradi wa kuokoa watoto [SC UK], APDC na vyama vingine vyenye uhusiano vimeunda kamati tekelezi ya kuangalia utekelezaji wa mradi.

Kuwashirikisha wazazi ni njia bora ya kuwafanya kuamini kuwa kuhusika kwao na sauti yao ni kiungo muhimu katika kutekeleza elimu mjumuisho. Muungano wao una uwezo wa kusaidia katika uendelezaji wa huduma zaidi za elimu na kuinua hali ya kuishi ya watoto wao.

Kwa kweli kila mtoto hapa Tanzania ana haki ya kupata elimu. Kila mtoto angependa kwenda shule ya watoto wadogo na shule yenyewe, lakini kwa sasa sio kila mtoto ana fursa hii. Naamini elimu mjumuisho ndio njia mwafaka ya kufuata ili kutimiza haki ya kila mtoto ya kupata elimu. Hatua ya kwanza kwa elimu mjumuisho ianze kujengwa sasa hapa nchini, kwa usaidizi wa sehemu zote za jamii: watoto, wazazi, na hata mashirika ya serikali na yasiyokuwa ya kiserikali.

Bila kudhibiti Kifua Kikuu, Tz bila Ukimwi haiwezekani

 Nembo inayoonesha kuwa Kifua Kikuu na Ukimwi ni magonjwa pacha

 Muuguzi akitoa huduma kwa Mgonjwa mwenye VVU pamoja na TB

BISHOP J. HILUKA
Dar es Salaam


Alhamisi ya 24 Machi 2011, wiki hii ni maadhimisho ya siku ya Kifua Kikuu Duniani, kwa hapa Tanzania maadhimisho ya siku hii yanafanyika mjini Musoma mkoani Mara yakiwa na kaulimbiu ya “Shiriki kikamilifu katika kupambana na Kifua Kikuu”. Kitaifa, takwimu zinaonesha kuwa mkoa wa Mbeya ndiyo unaoongoza kwa kuwa na wagonjwa wengi wa Kifua Kikuu (TB) nchini.

Maadhimisho haya huwa yana lengo la kuamsha ari ya wadau mbalimbali duniani wakiwamo wagonjwa, watafiti, wataalam wa afya, viongozi wa serikali, wanasiasa na jamii kwa ujumla kutumia mbinu mpya katika udhibiti wake. Baadhi ya mbinu zinazotumiwa ni pamoja na kuongeza jitihada za utafiti wa kugundua tiba mpya, kuwasaidia wagonjwa kupata tiba sahihi na kuhamasisha jamii kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya Kifua Kikuu (TB).

Takwimu zilizopo, Mkoa wa Mbeya ndiyo unaoongoza kwa kuwa na wagonjwa wengi wa TB huku maambukizi yakiwa yamefikia kiwango cha asilimia 8, Iringa ni asilimia 7, Dar es Salaam asilimia 6, Kigoma ndio yenye maambukizi kidogo ya asilimia 3.

Taarifa za kitaalam zinasema kuwa siku hizi kumekuwa na ugonjwa wa kifua kikuu sugu, unaojulikana kama
Multi Drug Resistance Tuberculosis (MDR-TB), unaosababishwa na dawa kushindwa kufanya kazi vizuri au mgonjwa kutotumia dawa kwa mpangilio maalum na kufuata ushauri uliotolewa na wataalam wa matibabu.

Shida kama hii hutokea ikiwa mgonjwa ametumia dawa kwa njia isiyotakikana au alianza matibabu akakosa kumalizia ile miezi sita inayohitajika. Kawaida, inachukua miezi sita au zaidi kutibu kabisa ugonjwa wa Kifua Kikuu. Hata hivyo, mgonjwa akianza matibabu, baada ya muda kidogo hujihisi yuko sawa. Kama atakatiza matibabu, kuna hatari kwamba vimelea vilivyo mwilini mwake hujiunda upya na kujiongezea nguvu kiasi kwamba dawa aliyokuwa akiitumia haiwezi kumtibu tena.

Kifua Kikuu sugu wakati mwingi hakitibiki na mtu anayeugua aina hii ya Kifua Kikuu anaweza kuusambaza ugonjwa huu vilevile kama TB ya kawaida. Matibabu ya mgonjwa wa Kifua Kikuu sugu (MDR-TB) yanagharimu mara ishirini zaidi ya yule aliye na TB ya kawaida. Matibabu ya mgonjwa wa Kifua Kikuu sugu yanaweza kuchukua muda wa miezi kumi na nane.

Nchini Tanzania takwimu zinaonesha kuwepo wastani wa watu 63,000 wanaougua Kifua Kikuu kila mwaka, ambao ni sawa na wagonjwa 173 kila siku.

Kifua Kikuu ni ugonjwa wa kuambukiza ambao husababishwa na vimelea vidogo vidogo aina ya bakteria visivyoonekana kwa macho bali kwa kutumia darubini viitwavyo ‘tubercle bacilli’.

Wengi wetu tuna vimelea vya TB mapafuni mwetu lakini hii haimaanishi kwamba tunaugua ugonjwa huu. TB huwashambulia hasa wale wenye ukosefu wa kinga mwilini unaosababishwa na kutokula chakula kizuri, matumizi ya dawa za kulevya au wanaougua magonjwa mengine.

TB ya mapafu ndio imeenea zaidi. Hata hivyo, vimelea vya TB vinaweza kusafirishwa kutoka mapafuni kupitia damu hadi sehemu nyingine za mwili na kusababisha viungo viathiriwe na TB.

Njia kuu ya maambukizi ya Kifua Kikuu huambukizwa kwa njia ya hewa ambayo ina vimelea vya ugonjwa huo. Kifua Kikuu kinaambukizwa kwa njia ya hewa kutoka kwa mgonjwa mwenye Kifua Kikuu kwenda kwa watu wengine. Hali hii hutokea hasa katika sehemu zenye msongamano wa watu au nyumba ambazo hazipitishi hewa na mwanga wa kutosha.

Vimelea vya TB pia hupatikana kwenye mate ya mgonjwa. Wakati mgonjwa anakohoa, kupiga chafya au kutema mate kiholela, vimelea vya TB husambazwa kwa njia ya hewa.

Ingawa imekuwa ikisemwa kuwa Kifua Kikuu ni ugonjwa wa tatu baada ya Malaria na Ukimwi ambao unasumbua na kupoteza maisha ya Watanzania, lakini ugonjwa huu unapaswa kutiliwa mkazo zaidi kwani utafiti unaonesha kuwa asilimia 30 ya vifo vya watu walioathirika kwa Ukimwi vinatokana na Kifua Kikuu, hivyo ile kampeni ya Rais Kikwete ya 'Tanzania bila Ukimwi inawezekana' haiwezi kufanikiwa kama hatutakuwa makini na ugonjwa huu.

Inakadiriwa kuwa asilimia 10 ya waathirika wa Ukimwi wana maambukizo ya Kifua Kikuu na asilimia 50 ya wagonjwa wa Kifua Kikuu wana maambukizo ya Virusi vinavyoambukiza Ukimwi (VVU). Hali hii inafanya Kifua Kikuu kuwa miongoni mwa changamoto kubwa katika mapambano dhidi ya Ukimwi hapa nchini.

Takriban watu zaidi ya milioni mbili hufariki kwa ugonjwa wa Kifua Kikuu kila mwaka duniani, na asilimia kubwa ya vifo hivyo vinatokea barani Afrika, hususan Kusini mwa Jangwa la Sahara. Tanzania ni nchi ya 14 kati ya nchi 22 zenye idadi kubwa ya wagonjwa wa kifua kikuu duniani.

Wengi wa wagonjwa hawa wako katika umri wa miaka 15 na 45 ambao ndiyo umri wa wazalishaji mali na ustawi wa taifa kwa ujumla. Licha ya kupoteza maisha ya wananchi wengi, athari nyingine za kuendelea kuwepo kwa magonjwa haya hapa nchini ni kudumaza uchumi wa nchi, hali ambayo inafanya jamii ya Watanzania kuendelea kuwa katika lindi la umaskini.

Shirika la Afya Duniani, WHO mwaka jana 2010, lilizindua mpango wa kupambana na ugonjwa wa Kifua Kikuu katika kipindi cha miaka mitano ili kuokoa maisha ya wagonjwa milioni mbili wanaofariki dunia kila mwaka kutokana na ugonjwa huo. Mkakati huo unapania kuboresha majaribio, uchunguzi na tiba kwa ugonjwa wa Kifua Kikuu na mpango mzima unatarajiwa kugharimu kiasi cha Dola za Kimarekani bilioni 47.

Watalaam wa ugonjwa wa Kifua Kikuu wanasema kwamba, kama hakuna hatua madhubuti dhidi ya ugonjwa wa Kifua Kikuu, kiasi cha watu milioni kumi, watakuwa wamepoteza maisha ifikapo mwaka 2015, kutokana na magonjwa yanayoweza kutibika. Shirika la Afya Duniani limesema kwamba, Kifua Kikuu ni kati ya magonjwa ya kale, lakini, ukigundulika mapema, ukapata tiba muafaka ni ugonjwa unaotibika kabisa. Afrika na India ni kati ya sehemu zilizoathirika zaidi na ugonjwa wa Kifua Kikuu.

Shirika la Afya Duniani linapania kuboresha huduma ya tiba kwa wagonjwa wa Kifua Kikuu kwa asilimia tisini, ifikapo mwaka 2015 sanjari na kuhakikisha kwamba, wagonjwa wote wa Ukimwi wanapimwa pia ugonjwa wa Kifua kikuu. Takwimu zinabainisha kwamba, wagonjwa wengi wa Ukimwi wanaosumbuliwa pia na Kifua Kikuu, hufariki zaidi kwa ugonjwa huu.

Dalili za ugonjwa wa Kifua Kikuu:
-Kukohoa mfululizo kwa muda wa wiki mbili au zaidi
-Kutoa makohozi mazito/ yaliyochanganyika na damu au mate yaliyo na damu
-Uchovu na kuishiwa nguvu mwilini
-Kukonda au kupoteza uzito wa mwili
-Kupoteza hamu ya kula
-Kutokwa na jasho jingi usiku wakati mtu amelala hata wakati wa baridi
-Maumivu ndani ya kifua
-Kuishiwa na pumzi au kupumua kwa shida
-Homa za wakati wa jioni

Aina za Kifua Kikuu:
Kuna aina mbili za Kifua kikuu (TB); Kifua Kikuu cha mapafu (Pulmonary Tuberculosis) na Kifua Kikuu cha nje ya mapafu (Extrapulmonary Tuberculosis).
TB ya mapafu nayo imegawanyika sehemu mbili:
-TB inayoambukiza ambayo vimelea vinagunduliwa katika makohozi, ambao ndiyo ugonjwa hatari zaidi unaochukua asilimia 90 ya aina zote za ugonjwa wa Kifua Kikuu.
-TB isiyoambukizwa na vimelea katika makohozi.

Kifua Kikuu kinatibika na kupona kabisa kwa kupata dawa zinazopatikana katika hospitali, hivyo kwa yeyote anayeugua ugonjwa huu anatakiwa kuzingatia tiba kama atakavyoelekezwa na daktari, na wengine tunatakiwa tujenge mazoea ya kupima afya zetu kabla ugonjwa huu haujamaliza nguvu kazi ya taifa letu.

0755 666964
bjhiluka@yahoo.com

KALONZO MUSYOKA: Urais wa Kenya wamfanya ahahe kutaka Kenya ijitoe ICC

 Makamu wa Rais wa Kenya, Kalonzo Musyoka

 Kalonzo Musyoka (kulia) akifurahia jambo na swahiba wake, William Ruto

NAIROBI
Kenya

BAADA ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kukataa hoja ya serikali ya Kenya ya kutaka Mahakama ya Kimataifa ya ICC ihairishe kesi zinazowakabili watu wanaoshukiwa kuchochea ghasia za baada ya uchaguzi uliopita, Kenya imekuwa ikitafuta njia nyingine.

Njia pekee iliyobaki kwa Kenya ilikuwa kukata rufaa mbele ya mahakama hiyo. Lakini Kiongozi wa Mashataka, Louis Moreno Ocampo akiwa ziarani London alisema haoni uwezekano wa Kenya kufaulu katika hoja hiyo.

Kampeni za majuma kadhaa za serikali ya Kenya za kutaka kuungwa mkono na jamii ya kimataifa ili kesi hizo ziahirishwe zilifikia kikomo Ijumaa iliyopita, baada ya kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kisichokuwa rasmi, kukataa hoja hiyo ya Kenya.

Hatua hiyo ikapelekea kwa Kenya kuamua kutumia ibara ya 19 ya sheria iliyobuni mahakama ya ICC, inayoruhusu nchi kupinga uamuzi wa mahakama ya ICC. Hata hivyo Kiongozi wa mashtaka katika ICC, Luis Moreno Ocampo amesema ingawa serikali ya Kenya ina haki ya kukata rufaa, haoni uwezekano wa kesi kuahirishwa.

Ocampo aidha aliondolea mbali hofu ya kukamatwa kwa washukiwa hao sita watakapofika mbele ya mahakama ya ICC Mjini The Hague, tarehe 7 na 8 Aprili. Lakini alikumbusha kwamba yeyote anaweza kukamatwa akiwatishia mashahidi.

Ocampo alikuwa ameiandikia barua serikali ya Kenya akielezea wasiwasi wake kwamba washukiwa wawili: Naibu Waziri Mkuu, Uhuru Kenyatta na Mkuu wa Utumishi wa Umma, Francis Muthaura wanashikilia nafasi serikalini zinazowapa uwezo kuingilia ushahidi.

Washukiwa wanaotarajiwa kufika mahakamani The Hague tarehe saba mwezi ujao ni aliyekuwa Waziri wa Elimu ya Juu, William Ruto, Mbunge Henry Kosgey, Mtangazaji wa Radio, Joshua Arap Sang, Uhuru Kenyatta, Francis Mutahura na aliyekuwa Mkuu wa Polisi, Hussein Ali. Baada ya hatua hiyo, kwa mujibu wa Bwana Ocampo, watasubiri kipindi cha miezi sita kuipa mahakama muda wa kuthibitisha mashtaka.

Hata hivyo Chama cha Orange Democratic Movement (ODM), kimeonekana kupinga hatua ya serikali ya Kenya kutaaka kuwanusuru watuhumiwa kwa kuliandikia barua Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UN), kikilitaka kukataa ombi la kuahirisha kesi zinazowakabili watuhumiwa hao katika Mahakama ya Uhalifu ya Kimataifa (ICC).

Katika barua kali, ODM walilitaka Baraza la Usalama kutambua kuwa ombi la Kenya ni ushahidi kwamba Rais Mwai Kibaki pamoja na chama chake cha PNU ‘hawawezi na hawako tayari kuwaadhibu waliotenda uhalifu baada ya uchaguzi.
Chama hicho kilieleza sababu 16 kwa nini ombi hilo lipuuzwe, miongoni mwao zikisema kampeni za kutaka kuahirishwa kwa kesi hizo zinaendeshwa na vinara hao sita, ambao wametakiwa kufika ICC huko Hague, Aprili 7.

Hata hivyo, William Ruto aliyesimamishwa Uwaziri wa Elimu ya Juu ameiponda barua hiyo ya ODM kwenda Baraza la Usalama, akisema wanachama wa chama hicho hawakushirikishwa.

Kwa kadiri nijuavyo, huu ni uamuzi wa Profesa Nyong’o na Raila (Waziri Mkuu Raila Odinga) na washirika wao. Hawakutushirikisha kutaka maoni yetu au kutujulisha kuwapo kwa suala hilo,” alisema.

Mbunge huyo wa Eldoret Kaskazini alisema yeye na wafuasi wake ndani ya ODM wanatarajia kuandika barua nyingine kwa Baraza la Usalama la UN kuunga mkono kuahirishwa kwa kesi za ICC.

Hawaimiliki ODM. ODM ni mali yetu sote na tunatarajia kupinga uamuzi wao,” alisema.

Katika barua yake, ODM ilisema kwamba Kenya haina mahakama au wachunguzi wenye uwezo wa kushughulikia uhalifu uliotendeka wakati wa machafuko yaliyotokana na uchaguzi wenye utata.

Kampeni za kutaka kuahirishwa kwa mashtaka dhidi ya watuhumiwa hao sita katika Mahakama ya Uhalifu ya Kimataifa (ICC) zinaongozwa na Makamu wa Rais wa Kenya, Kalonzo Musokya.

Musyoka ambaye anahofia nguvu za Raila Odinga katika kuusaka urais wa Kenya aliamua kuunda ushirika na watu wawili katika ya watuhumiwa hao sita: Uhuru Kenyatta na Wiiliam Ruto katika umoja wao unaojulikana kama “K 3”.

Historia ya Kalonzo Musyoka:
Stephen Kalonzo Musyoka amezaliwa tarehe 24 Desemba 1953, ndiye Makamu wa Rais wa Kenya. Musyoka aliwahi kufanya kazi katika serikali ya Rais Daniel arap Moi akiwa Waziri wa Mambo ya Nje kati ya 1993 hadi 1998, na hatimaye, chini ya Rais Mwai KIbaki, akiwa Waziri wa Mambo ya Nje tena kati ya 2003 hadi 2004, na baadaye Waziri wa Mazingira 2004 hadi 2005. 
 
Alikuwa mmoja wa wagombea urais katika uchaguzi wa rais 2007 lakini hakufua dafu, ambapo baada ya uchaguzi aliteuliwa kuwa Makamu wa Rais na Kibaki mwezi Januari 2008. Pia amewahi kushika wadhiofa wa Kamishna Mkuu wa Chama cha Skauti cha Kenya (The Kenya Scouts Association).

Maisha ya awali:
Alizaliwa katika eneo la Tseikuru, sehemu ya Wilaya ya Mwingi (ambayo siku hizi ni sehemu ya Wilaya ya Kitui), mkoa wa Mashariki wa Kenya. Kati ya 1960 na 1967 alisoma katika Shule ya Msingi Tseikuru. Kisha akaenda Kitui High School iliyopo Kitui na hatimaye Meru High School, Meru ambapo alihitimu mwaka 1973. 
 
Kalonzo Musyoka alihitimu Shahada ya Sheria kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi mwaka 1977. Aliendelea na masomo zaidi katika Shule ya Sheria ya Kenya na Taasisi ya Usimamizi ya Mediterranean ya Cyprus.

Siasa:
Musyoka alijitosa kugombea ubunge katika Jimbo la Kitui Kaskazini mwaka 1983, lakini alishindwa. Wakati huo, Kenya ilikuwa nchi ya chama kimoja na wagombea wote walikuwa wa chama cha Kanu. Hata hivyo, miaka miwili tu baadaye, mwaka 1985, kiti cha ubunge cha Kitui Kaskazini kilibaki wazi na Musyoka alishinda katika uchaguzi huo mdogo, hivyo kuwa mbunge katika umri wa miaka 32. 
 
Mwaka 1986, aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Ujenzi. Alichaguliwa tena katika uchaguzi wa bunge wa mwaka 1988. Kuanzia 1988 hadi 1998 alikuwa Katibu wa oganaizeshi wa Taifa wa Kanu.

Uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi Kenya ulifanyika mwaka 1992. Musyoka alibaki katika chama cha Kanu, alifanikiwa kutetea kiti chake cha ubunge na kuteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa. Pia alishika nafasi nyingine katika wizara kadhaa katika serikali ya Kanu. Mwaka 1997 alichaguliwa tena kuwa mbunge, lakini sasa akiwa mbunge wa Jimbo la Mwingi Kaskazini, baada ya jimbo lake la zamani, Kitui Kaskazini kugawanywa katika majimbo mapya.

Katika mwezi wa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2002, chini ya uongozi wa aliyekuwa Katibu Mkuu wa Kanu, Raila Odinga, alijotoa Kanu na kujiunga na Liberal Democratic Party (LDP) chini ya mwamvuli wa muungano wa NARC (National Rainbow Coalition), ambao ulishinda uchaguzi mkuu.

Musyoka akawa Waziri wa Mambo ya Nje kwa mara ya pili chini ya Rais Mwai Kibaki, lakini baada ya kufanya mabadiliko ya baraza la mawaziri 30 Juni, 2004 alihamishiwa Wizara ya Mazingira. Mwishoni mwa Agosti 2004, aliondolewa kutoka nafasi yake kama mwenyekiti wa mazungumzo ya amani wa Sudan na Somalia na nafasi yake kuchukuliwa na John Koech.

Kalonzo Musyoka ilikuwa na matarajio ya kuwa urais katika uchaguzi wa Desemba 2007. Musyoka alifanya kampeni kupitia tiketi ya ODM-Kenya, huku akikabiliwa na wagombea wengine. Ufanisi wake kwa ajili ya uchaguzi wa Desemba 2007 ulishuka kwa kasi, na wachambuzi wa kisiasa walijiuliza kama angeweza kuwa na athari kubwa. Uhusiano wake na kiongozi mwenzake wa ODM-Kenya, Raila Odinga, ambaye pia aliutaka urais kupitia ODM-Kenya, ulisababisha kuwepo uvumi mwingi. 
 
Waangalizi wengi walihoji kama watarajiwa wa urais kupitia ODM-Kenya, hasa Raila na Musyoka, wangeweza kuunganisha nguvu na kumuunga mkono mgombea mmoja katika uchaguzi mkuu. 
 
Chama cha ODM-Kenya kiligawanyika katika makundi mawili, moja la Musyoka na jingine la Odinga, Agosti 2007. Musyoka alichaguliwa na chama chake kama mgombea urais, Agosti 31, 2007, akipata kura 2,835 dhidi ya Julia Ojiambo, aliyepata kura 791. Alizindua kampeni zake za urais katika Uwanja wa Uhuru Park mjini Nairobi, Oktoba 14, 2007.

Kwa mujibu wa matokeo ya uchaguzi, Musyoka alishika nafasi ya tatu nyuma ya Kibaki na Odinga kwa kupata asilimia 9 ya kura. Ulizuka mgogoro mkali kuhusu matokeo kati ya wafuasi wa Kibaki na Odinga, Kibaki alimteua Musyoka kuwa Makamu wa Rais na Waziri wa Mambo ya Ndani tarehe 8 Januari, 2008.

Maisha ya binafsi
Kalonzo Musyoka amemuoa Pauline. Wana watoto wanne.

Makala haya yameandaliwa na Bishop J. Hiluka kwa msaada wa vyombo mbalimbali vya habari.

Mar 16, 2011

Ni lini walemavu watapewa fursa sawa kwenye jamii yetu?

 Walemavu kama huyu wanahitaji kuwezeshwa

 Watoto wenye ulemavu wa ngozi wakifarijiwa

BISHOP J. HILUKA
Dar es Salaam

HIVI karibuni nilishuhudia kupitia moja ya vituo vya televisheni habari iliyonisikitisha sana kumhusu binti mwenye ulemavu wa ngozi, Mariam Juma, aliyefungwa minyororo miguuni na baba yake kwa zaidi ya miaka mitatu huko wilayani Muheza, Tanga.

Mariam ambaye ni mtoto wa kwanza katika familia ya Juma Salim Ngatu ambaye kwa sasa ni marehemu, amezaliwa mwaka 1982 katika familia ya watoto sita.

Kwa habari hiyo naamini kuwa kuna matatizo kwa pande zote; jamii na serikali. Bahati mbaya walemavu wengi walioko katika familia au jamii duni, na wengi wao wanafichwa na familia zao ndani ya nyumba na hawatoki nje kukubali ukweli wa mambo.

Nimepata bahati ya kuwa mmoja wa waandishi wa kwanza waliobahatika kupata mafunzo maalum ya Uandishi wa Habari za Walemavu yaliyoandaliwa na Baraza la Habari Tanzania (MCT), ambapo tulidokezwa kuwepo jinsi mbili za jamii inavyouangalia ulemavu:
Medical model; Mtizamo unaoangalia ulemavu kama ugonjwa, walemavu wanaangaliwa kama watu wanaohitaji matibabu ili waweze kupona pamoja na kusaidiwa. 
Bio-psychosocial model; Mtizamo unaoonesha ulemavu ni muunganiko wa mambo mengi na mitizamo ya kibinadamu, mila desturi na kadhalika.

Bahati mbaya walio wengi (nikiwemo mimi kabla sijapata mafunzo) wapo kwenye mtizamo wa kwanza, wakidhani kuwa walemavu wanahitaji kuhurumiwa badala ya kuwezeshwa. Suala la watu wenye ulemavu ni suala linalohitaji msukumo mkubwa wa kisiasa.

Kama Jamii tunapaswa kukazia umuhimu wa kulinda na kutunza utu na heshima ya mwanadamu, lengo likiwa kuhakikisha kuwa Jamii inafanikiwa, utu wa mwanadamu unapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika mikakati ya maendeleo endelevu.

Ili kulinda na kuheshimu zawadi ya maisha, changamoto inayokwenda sambamba na mapambano dhidi ya baa la umaskini, huduma bora za afya na fursa makini zitakazowawezesha watoto wote, hata walio na ulemavu kukuza karama na vipaji walivyokirimiwa na Mungu, katika mchakato wa makuzi ya mtu mzima.

Serikali pia inapaswa kuhakikisha kwamba, watu wanapata huduma bora za afya, bila kusahau kutoa msaada na huduma kwa walemavu ambao ni sehemu ya jamii, ili walau kila mtu aweze kuishi maisha yenye hadhi kama binadamu.

Ukirejea sera ya Taifa letu ya Ulemavu ya 2004 utaona tafsiri ifuatayo:Disability is the loss or limitation of opportunities to take part in the normal life of the community on an equal level with others due to temporary or permanent physical, mental or social barriers.

Watanzania tumekuwa tukiliangalia suala la walemavu kama fursa finyu ya kupata ajira pekee badala ya kuliangalia katika uwanja mzima wa maisha kwa ujumla kama ilivyo katika maana ya ulemavu.

Hivyo pamoja na suala la ajira pia tunapaswa kuangalia maeneo mengine ambayo mlemavu wa Tanzania hapewi haki sawa:
Mosi, elimu; hakuna mkazo wa kuongeza Shule za Sekondari na hata Vyuo Vikuu maalum kwa ajili ya walemavu wa aina fulani mfano viziwi, vipofu na kadhalika.
Pili, miundombinu; Ujenzi wa majengo na barabara zinazowajali walemavu.
Tatu, mawasiliano; Kuongeza Ukalimani katika vipindi vya televisheni kwa ajili ya viziwi, au majarida yenye maandishi maalum (braille) kwa ajili ya wasioona na kadhalika.
Nne, starehe na Michezo; Kubuniwa michezo na mashindano mbalimbali ambayo washiriki walemavu wasioona, wasiosikia, wasioongea na wale wenye ulemavu wa ngozi wangeshiriki na kupewa zawadi kama kujengewa nyumba na kupewa usafiri unaostahili.
Nawapongeza sana waandaaji wa michezo ya Olympic kwa kuliona hilo na kuanzisha mashindano maalum (
Paralympic) kwa ajili ya walemavu.

Naomba ieleweke kuwa sisi tunaodhani kuwa si walemavu twaweza kuwa si walemavu wa viungo, ubongo wala ngozi lakini tukawa Walemavu wa Kisiasa na Kifikra (
Politically and Mentally Disabled). Lakini pia tutambue kuwa kesho na keshokutwa tunaweza kujikuta tupo katika kundi hili.

Tusiwatenge au kuwanyanyasa walemavu kwa ulemavu wao. Badala yake tuwaoneshe upendo, tuwathamini na tuwatie moyo ili waweze kuendeleza vipaji vyao na hivyo kuboresha maisha yao. Tunapaswa tuondokane na ulemavu wetu wa kisiasa na kifikra ili kuwasaidia wenzetu wenye ulemavu wa viungo katika kujikwamua.

Pia kuna kosa kubwa sana ambalo tumekuwa tukilifanya bila kujua kwa kudhani aliye na ulemavu ni mtu asiyejiweza na anayestahili huruma (
charity), tukasahau kuwa wengi wa watu wenye ulemavu wakipewa fursa stahiki ni watu walio na uwezo mkubwa wa kuchangia maendeleo yao na maendeleo ya jamii kwa ujumla.

Walemavu wanaweza kuchangia kwa kiwango kikubwa kuliko hata watu wasio na ulemavu. Wenye ulemavu ni sehemu ya jamii yetu na wakiwezeshwa na kuthaminiwa wanaweza. Watu wenye ulemavu ni rasilimali watu ya taifa kama wale wasio na ulemavu.

Haya yote yanawezekana, pamoja na kumtambua mlemavu kuwa sehemu muhimu ya jumuiya tumruhusu atoe mchango wake inavyopaswa badala ya kudhani kuwa yeye ni mtu wa kuhurumiwa na kusaidiwa tu, huku tukifikiria kuwa haki yake ni kubeba kibakuli maeneo ya posta kuomba msaada au kusubiri Ijumaa. Kwa nini tunashindwa kuweka sheria zitakazompa haki sawa mlemavu kati yetu?

Katiba ya Tanzania inasema wazi kuwa ni wajibu wa serikali kuwahudumia watu wenye mahitaji maalumu kama walemavu na wazee. Huduma ni wajibu na siyo msaada. Walemavu mara nyingi hupata huduma toka mashirika ya dini na vyama vyao vya hiari vya kutetea haki zao. Hali hii inaonesha kuwa serikali na jamii kwa ujuma vimeyaachia mashirika ya dini jukumu hili muhimu.

Pengine sina taarifa sahihi, lakini naamini kuwa serikali inapaswa kuzidisha uboreshaji wa mifumo yetu ya elimu na mazingira yake ili kuwarahisishia watoto wenye ulemavu kupata fursa ya elimu. Pia serikali ina jukumu la kuwahamasisha wazazi wenye watoto wenye ulemavu kuwapeleka watoto wao shule.

Kutokana na baadhi ya imani potofu kuhusu wenye ulemavu, mara nyingi wamekuwa wanakumbana na vikwazo vingi kutoka katika ngazi za familia zao na jamii kwa ujumla katika kuendesha shughuli zao na kuendeleza maisha yao. Hata mauaji yaliyokuwa yakifanyika si walemavu wa ngozi tu waliokuwa wanauawa bali hata walemavu wengine. Baadhi ya jamii zilikuwa zikiwaua watoto wachanga waliozaliwa na ulemavu.

Ni wakati sasa tufikirie kuanzisha kitu kinachoitwa universal accessibility kwenye maeneo yetu ikiwemo vyoo kwa ajili ya walemavu na vyombo vya usafiri; mabasi yanayoshuka kumwezesha mlemavu apande bila bughudha. Kwenye majengo; milango mipana yenye kuruhusu walemavu kupita. Taa za barabarani (traffic light) pia ziboreshwe kwa kuziwekea sauti maalum itakayokuwa ikimruhusu mtu asiyeona kujua wakati gani anaweza kuvuka.

Nimekuwa nasita kuamini kuwa jamii yetu ina mapenzi kwa walemavu. Wengi katika jamii hii wanawaona walemavu kama mzigo na wasingependa kukumbushwa kuwepo kwao. Mtazamo huu vilevile upo katika tunavyowaona wenye kuishi na virusi vinavyosababisha ugonjwa wa Ukimwi (VVU). Ni aghalabu mtu kuutangazia umma kuwa ndugu yake ana VVU na anapofariki magonjwa mbadala yanatafutwa kuelezea kifo chake.

Kitu kingine tusichokijua ni kwamba watu wenye ulemavu hawahitaji “kuhurumiwa” kama tunavyowafanyia, wanachohitaji ni kutengenezewa sera bora na kuwezeshwa. Kunatakiwa kuwe na mfumo wa jamii utakaosimamia na kulinda haki zao, na kuwapa fursa zitakazowawezesha kuchangia katika maendeleo ya taifa.

Huruma haiwezi kujenga, sana sana itaendelea kuongeza watu wenye ulemavu wenye vibakuli wakiomba barabarani kama ilivyo pale Posta na Selander Bridge kwa jiji la Dar es Salaam na maeneo mengine mijini!

Kwa Tanzania Serikali huratibu huduma za walemavu kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii. Kabla ya hapo Walemavu walikuwa wanahudumiwa na Wizara ya Kazi, Vijana na Michezo. Kama mtakumbuka kutokana na mateso na shida, Walemavu walitaka kumpiga aliyekuwa Waziri wa wizara hiyo, Marehemu Sebastian Kinyondo, miaka ya 1990.

Kwa mtizamo wangu tunahitaji utashi wa kisiasa katika hili. Suala la walemavu linapaswa kushughulikiwa na ofisi ya juu: Ofisi ya Rais, Makamu wa Rais au Waziri Mkuu. Mojawapo kati ya ofisi hizi inapaswa iwe na shughuli ya kuratibu masuala yote ya walemavu toka sehemu mbalimbali.

Busara itumike kuanzisha Wizara itakayoshughulikia masuala ya watu wenye ulemavu na iwe chini ya Rais au Waziri Mkuu. Lakini kuiweka chini ya Wizara ya Afya ni kuendeleza ile dhana kwamba Walemavu ni watu wagonjwa wanaohitaji matibabu! Hii si kweli kwani walemavu wanahitaji fursa (opportunity) katika kutenda kazi zao.

Lakini pamoja na hayo, katika kila Wizara kuanzishwe dawati maalum la kushughulikia masuala ya walemavu (
Disability Desk). Kama imewezekana katika masuala ya jinsia (Gender) kwa nini isiwezekane kwa watu wenye ulemavu? Sidhani kama ni sahihi kuyaacha masuala ya walemavu kwa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kutaleta tija.

Nchi kama Afrika Kusini wamejitahidi katika hili kwa kuweka kurugenzi (
Directorate) ya watu wenye ulemavu chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais.
Nitwangie: 0755 666964
bjhiluka@yahoo.com