Jul 27, 2011

Hili la samaki wa sumu, wahusika wawajibike

 Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na 
Ustawi wa Jamii, Blandina Nyoni


 Samaki aina ya Mackerel

BISHOP J. HILUKA
Dar es Salaam

HII taarifa kuhusu samaki wenye sumu imetushtua na kutuogofya watu wengi. Kwanza niliposikia kwa mara ya kwanza nilidhani ni mzaha, lakini baada ya kusikia tangazo la tahadhari likitolewa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, kuwataka wananchi washiriki msako kuhusu kusambazwa kwa zaidi ya kilo 1,000 za samaki wenye sumu sehemu mbalimbali za nchi, nilijikuta nikichanganyikiwa.

Ndiyo nilichanganyikiwa! Nilichanganyikiwa kwa kuwa familia yangu wanapenda sana kula samaki, si hivyo tu bali hata hii taarifa ya wizara iliyotolewa Jumatatu wiki hii jijini Dar es Salaam, imeeleza kuwa samaki hao ni sehemu tu ya tani takriban 125 (kilo 124,992) zilizoingizwa nchini kutoka Japan, na kwamba Serikali imeanza msako mkali kuwatafuta samaki hao, lakini ikaonesha wasiwasi kwamba juhudi hizo huenda zisizae matunda kwa kuwa sehemu ya shehena hiyo imeshaingia sokoni!

Mpaka hapa tayari kila atakayesoma makala yangu ataelewa kwa nini nilichanganyikiwa. Hapa ninajaribu kuyaangalia majaaliwa ya Watanzania waliokwishakula na watakaokula samaki hawa. Uchunguzi wa awali unaonesha kuwa samaki hao tayari wameingizwa katika masoko ya Dar es Salaam na Morogoro.

Taarifa hiyo ilisema kuwa athari za sumu inayohofiwa kuwapo kwenye samaki hao ni ya mionzi ya nyuklia ambayo kimsingi hujitokeza taratibu katika mwili wa binadamu.

Taarifa hiyo iliendelea kueleza kuwa samaki hao aina ya 'Mackerel' waliingizwa nchini na kampuni ya
Alphakrust Ltd ya Dar es Salaam kutoka kampuni ya Kaneyama Corporation ya Chiba, Japan. Samaki hao walisafirishwa kupitia Bandari ya Yokohama, Japan na kuingia nchini kupitia Bandari ya Dar es Salaam, na inaonesha waliingizwa baada ya kukidhi masharti ya kisheria na taratibu zilizowekwa!

Hapa kuna maswali ya kujiuliza; masharti ya kisheria na taratibu zipi zilizozingatiwa katika kuingiza samaki hao? Hivi hadi lini nchi yetu itaendelea kufanywa dampo la bidhaa mbovu? Eti samaki hao waliruhusiwa kuingizwa nchini kwa kibali cha TFDA namba TFDA11/F/IPER/0896, cha Julai 11 2011. Je, ni kweli hakuna viashiria vya rushwa katika sakata hili?

Inaeleweka wazi kuwa samaki na mboga zitokazo Japan zimechafuliwa na mionzi ya nyuklia, na inasikitisha sana kuona watu wanaagiza vyakula 'vya baharini' kutoka Japan kwa wakati huu, huku Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) ikiruhusu ziingizwe nchini. Inamaana tumeshindwa hata kutumia busara tu ya binadamu wa kawaida?

Hapa sielewi, hili ombi la Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kuwaomba wananchi kutoa ushirikiano kwa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Idara za Afya za Mikoa ya Dar es Salaam na Morogoro na Jeshi la Polisi, ili samaki waliobaki wapatikane ni nini kama si kiini macho? Ushirikiano upi inautaka mamlaka iliyosababisha uzembe na wala hatuoni wahusika kuwajibika? Kwa nini wahusika wasiwajibike kwanza?

Taarifa ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Blandina Nyoni, ilisema kuwa hadi kufikia Jumapili asubuhi, kiasi cha samaki wenye uzito wa tani 123.673, kati ya tani 124.992 walioingizwa nchini, walipatikana na kuzuiliwa katika maghala ya kampuni ya Alphakrust Ltd. Nyoni alisema wizara yake iliiagiza TFDA kuchukua hatua za haraka za kuzuia usambazaji wa samaki hao hadi uchunguzi utakapokamilika.

Hivi kama Japan yenyewe imepiga marufuku samaki hao kusambazwa kwenye maeneo mengine ya nchi yao, iweje sisi bila hata wasiwasi tunaingiza bidhaa kutoka mji huo? Kama balaa hilo la mionzi lingetokea nchini mwetu hata pini tusingeweza kuuza nje, hivi tunawaogopa hawa wakubwa mpaka kiasi cha kuweka rehani maisha yetu kiasi hiki? Haya yamefanywa kwa maslahi ya nani ili kuwaua Watanzania?

Kama wahusika hawatawajibika na serikali haitachukua hatua katika kuwawajibisha waliohusika na sakata hili sisi wananchi hatutaielewa kabisa serikali yetu! Itabidi tuelezwe serikali ipo kwa maslahi ya raia wa nchi ipi kama si raia wake; Watanzania?

Kwa mujibu wa nyaraka za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), mzigo huo ulifika Bandari ya Dar es Salaam tarehe 18 Julai, 2011. Wizara ilipata taarifa siku ya Jumamosi kwamba samaki hao wanahisiwa kuchafuliwa na mionzi ya nyuklia iliyotokea huko Japan, mwezi Machi, 2011.

Hakuna asiyejua kuwa mionzi ya nyuklia ina athari kubwa sana kwa afya ya jamii. Dalili za awali zinafanana na za mtu anayefanyiwa tiba ya mionzi kwa kansa: kichefuchefu na uchovu, kisha kutapika. Baada ya hapo mtu hupoteza nywele na kuharisha.

Lakini kama mfiduo (exposure) ni mkubwa, hatua ya pili kwa ujumla ni uharibifu wa utando wa matumbo, kuhara sana kunakosababisha upungufu wa maji mwilini, baadaye uharibifu kwenye mfumo wa neva kunakosababisha kupoteza fahamu, na hatimaye kifo.

Je, tuliowaamini kutuongoza haya ndiyo malipo yao kwetu? Kwa nini wahusika wasiwajibike kwa (uzembe?) walioufanya kama si kitu kidogo kimetumika kuruhusu samaki hawa waingizwe nchini?

Mungu ibariki Tanzania...

BINGU WA MUTHARIKA: Atwishwa zigo la lawama baada ya wafadhili kujitoa kuisaidia Malawi

 Bingu wa Mutharika

 Prof. Peter Mutharika

LILONGWE
Malawi

LICHA ya kukabiliwa na changamoto nyingi, Rais Bingu wa Mutharika wa Malawi amemteua mkuu mpya wa jeshi, siku mbili baada ya waandamanaji 18 kuuawa, pale polisi walipofyatua risasi na moshi wa kutoa machozi, ili kuzima maandamano sehemu mbalimbali za nchi.

Brigadier-Jenerali Henry Odillo amechukua nafasi ya Jenerali Marko Chiziko, ambaye mkataba wake wa ajira umemalizika. Nchi sasa ni shwari lakini viongozi wa maandamano, wameonya kuwa watafanya maandamano mengine iwapo rais hatozungumza nao.

Maafisa wa matitabu kutoka hospitali moja nchini Malawi wanasema kuwa kwa uchache watu 18 wameuawa katika ghasia za maandamano nchini humo. Jeshi lilipelekwa katika mji mkuu wa Lilongwe, wakati ambapo maandamano yalikuwa yamerejelewa katika miji jirani. Msemaji wa polisi alithibitisha kifo kimoja tu lakini maafisa kutoka hospitali wakasema watu wanane wameuawa.

Waandamanaji walighadhabika kwa kuongezwa kwa bei za bidhaa na vilevile na Rais Bingu wa Mutharika. Rais wa Mutharika alilihutubia taifa na kusema yuko tayari kwa mazungumzo na wapinzani na makundi ya kiraia.

Makundi ya kiraia yalioandaa maandamano hayo yamesema kuwa Malawi inakabiliwa na mzozo mbaya zaidi wa kiuchumi tangu kupatikana uhuru miaka 47 iliyopita. Serikali hivi karibuni iliidhinisha bajeti ya kubana matumizi na kuongeza kodi ili kupunguza kutegemea misaada baada ya wafadhili wengi kukatiza misaada yao kwa Malawi.

Kufuatia hatua ya nchi ya Uingereza kutangaza kutotoa msaada wa fedha kusaidia bajeti ya nchi ya Malawi, upinzani nchini humo umemtupia lawama rais Bingu wa Mutharika kuifikisha nchi hiyo hapo ilipo. Msemaji wa chama cha Malawi Congress Party, Nancy Tembo, amesema kuwa serikali ilifanya maamuzi yenye hasira kuvunja uhusiano wa kibalozi na nchi ya Uingereza wakati akijua fika nchi hiyo inategemea kwa kiasi kikubwa msaada wa nchi hiyo.

Miezi michache iliyopita rais Mutharika alitangaza kusitisha uhusiano wa kibalozi na nchi ya uingereza kufuatia matamshi ya balozi wake nchini humo ya kukosoa utendaji wa serikali yake. Wafadhili wameishutumu Malawi kwa kufuja uchumi na kukosa kuzingatia haki za binadamu. Maandamano hayo yamefanyika katika miji mingi lakini vifo vimetokea katika mji wa Mzuzu kilomita 300 Kaskazini mwa Lilongwe.

Siku ya Alhamisi wiki iliyopita msemaji wa mfuko wa kuchangia maendeleo wa serikali ya Uingereza alitangaza mfuko huo kusitisha msaada wa kifedha wa zaidi ya euro milioni 19 kwenye bajeti ya serikali ya malawi kwa kile kilichotokea.

Wabunge wa upinzani nchini humo wameishutumu serikali yao wakitaka iombe radhi kwa nchi ya Uingereza ili kuweza kupatiwa fedha hizo ambazo nchi ya Uingereza ndio mshirika mkubwa wa bajeti ya nchi hiyo.

Askofu Maurice Munthali, naibu katibu mkuu wa kanisa la Kipresbyteri aliyekwenda katika chumba cha kuhifadhia maiti kutambua waliouawa alisema wote waliokufa wanaonesha walipigwa risasi, jambo ambalo limethibitishwa na wauguzi. Askofu huyo alisema pia baadhi ya wale walio hospitali hawakushiriki katika maandamano bali walijikuta katikati ya vurugu hizo.

Mashambulio
Taarifa zaidi zasema kuwa mali ya Waziri mmoja wa serikali imeshambuliwa na waandamanaji katika mji huo. Baadhi ya waandamanaji hao wanaomtaka Rais Bingu wa Mutharika ajiuzulu. Polisi nao wametumia gesi za kutoa machozi mjini Lilongwe kuwatawanya waandamanaji na vilevile wameweka vizuizi kuwazuia watu kuingia katika mji huo.

Mmiliki wa radio moja ya kibinafsi nchini humo, Alaudin Osman, aliliambia Shirika la Habari la Uingereza (BBC) kuwa ameagizwa na vyombo vya utawala kutopeperusha matangazo ya moja kwa moja kwa kuwa inadaiwa yanachochoea kinachoendelea hivi sasa.

Malawi ni mojawapo ya nchi masikini zaidi ulimwenguni ambapo asilimia 75 ya idadi ya watu nchini humo hutumia chini ya dola moja katika matumizi yao ya kila siku.

Historia yake

Bingu wa Mutharika amezaliwa 24 Februari 1934. Ni mwanauchumi, mwanasiasa, na Rais wa aasa wa Malawi. Aliingia madarakani mnamo Mei 24, 2004, baada ya kushinda uchaguzi wa urais.

Kwa msaada wa Rais Bakili Muluzi, Mutharika alishinda uchaguzi wa 2004 kama mgombea wa United Democratic Front (UDF), akaimega UDF (ambayo imebakia chini ya utawala wa Muluzi) mwezi Februari mwaka 2005, hata hivyo, kutokana na kutokubaliana juu yake kuhusu kampeni ya kupambana na rushwa. Kisha alianzisha chama kipya, Democratic Progressive Party (DPP), lakini hakuwa na wingi wa wabunge kwa muhula wake wote wa kwanza. Alishinda awamu ya pili katika uchaguzi wa Mei 2009, na pia kupata wabunge wengi.

Maisha binafsi

Alizaliwa akiwa Brightson Webster Ryson Thom katika eneo la Thyolo, kilomita 30 kutoka mji mkuu wa kibiashara wa Malawi, Blantyre. Aliamua kulitumia jina la familia la Mutharika na kujipa jina la kwanza la Bingu katika miaka ya 1960 wakati Umoja wa Afrika ulipokuwa ukifanya kazi ya ukombozi katika bara hili.

Baadaye aliongeza kiambishi cha 'wa' kati ya majina yake ili kuficha utambulisho wake ili kuukwepa usalama wa taifa wa Hastings Kamuzu Banda, hata kama hakuwa mpinzani wa kisiasa wa Banda.

Muda mfupi baada ya Mgogoro wa Baraza la Mawaziri mwaka 1964, Mutharika alikuwa mmoja wa Wamalawi 32 waliochaguliwa na Banda kusafiri kwenda India kwa udhamini wa Indira Gandhi kwa masomo ya diploma ya muda mfupi (fast track). Alipokuwa India, Mutharika alipata shahada yake ya Uchumi.

Maisha ya kifamilia

ETHEL MUTHARIKA:
Amemuoa Ethel Mutharika Zvauya, mwanamke wa asili ya Zimbabwe, ambaye aliwahi kuwa sababu ya kuleta utulivu katika kipindi cha kwanza cha siasa za Bingu kati ya 2004 na wakati wa kufariki kwake. Mutharika na Ethel walikuwa na watoto wanne pamoja. Baada ya kusumbuliwa muda mrefu na kansa ambayo ilimpeleka Ufaransa na Afrika Kusini kutafuta tiba, mke wa Mutharika alifariki Mei 28, 2007. Siku ya maombolezo ilitangazwa kwa ajili yake mnamo Januari 22, 2010.

CALLISTA MUTHARIKA (CHAPOLA-CHIMOMBO):
Baadaye mwaka 2010, Mutharika alitangaza mipango ya kuoana na Callista Chapola-Chimombo, Waziri wa zamani wa Utalii ambaye aliyekuwa na miaka 50. Wawili hao walioana mwaka 2010 katika harusi iliyogharimu milioni 200 pesa za Malawi kwenye Uwanja wa Civo mjini Lilongwe. Harusi ilifadhiliwa kwa gharama ya umma.

PETER MUTHARIKA:
Ni ndugu wa Mutharika, profesa wa sheria katika Chuo Kikuu cha Washington mjini St Louis. Mei mwaka 2009, alichaguliwa kwenye Bunge la Malawi, na Aliteuliwa kwenye Baraza la Mawaziri la Malawi kama Waziri wa Sheria na Mambo ya Katiba. Kwa sasa ni Waziri wa Elimu. Mutharika anamuandaa mdogo wake kuchukua urais, na Peter anatarajiwa kwa kiasi kikubwa kuwa mgombea kupitia DPP katika uchaguzi wa 2014.

Elimu

Mutharika alikuwa mtoto wa mwalimu mkuu wa shule ya msingi. Alipata elimu India katika Chuo cha Biashara cha Shri Ram, Chuo Kikuu cha Delhi, ambapo alipata shahada ya Uchumi. kisha alisoma na kufuzu shahada ya uzamili katika uchumi. Baadaye akapata shahada ya uzamivu katika Uchumi na Maendeleo kutoka Pacific Western University.


Kazi na siasa

Mutharika aliwahi kuhudumia katika asasi za kiraia na alitumia muda katika serikali ya Zambia. Mwaka 1978, alijiungana na Umoja wa Mataifa, ambapo hatimaye akawa Mkurugenzi wa Biashara na Fedha wa Maendeleo ya Afrika. Mwaka 1991 alichaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa Soko la Pamoja la Mashariki na Kusini mwa Afrika (COMESA), kanda yenye nchi 20.

Baada ya Banda kulazimishwa kuanisha vyama vingi, Mutharika nadaiwa kuwa mmoja wa waanzilishi wa UDF, chama kilichoshinda uchaguzi wa kwanza wa Malawi wa vyama vingi mwaka 1994. Mutharika wakati huo alikuwa msaidizi wa kiongozi wa UDF, Rais Bakili Muluzi, lakini akawa mkosoaji wa sera za Muluzi za uchumi, na kuondoka UDF.

Alianzisha United Party (UP) mwaka 1997 na kushindana na Muluzi bila mafanikio katika uchaguzi wa 1999, akiambulia chini ya asilimia 1 ya kura. Mutharika aliifuta UP na kurudi UDF baada ya kuteuliwa naibu gavana wa Benki Kuu ya Malawi. Aliteuliwa kuwa Waziri wa Uchumi, Mipango na Maendeleo mwaka 2002, na baadaye kuteuliwa na Muluzi kama mrithi wake.

Makala haya yameandaliwa na Bishop J. Hiluka kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya habari vya kimataifa

Jul 20, 2011

Miaka 50 ya uhuru na nadharia ya Mkukuta ya kupunguza umasikini

 Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo (kulia), 
akichati na Katibu Mkuu wake, Ramadhan Khijah (katikati) 
pamoja na Naibu Katibu Ofisi ya Rais Tume ya Mipango, 
Clifford Tandari mara baada ya uzinduzi wa mchakato 
wa majadiliano ya Mpango wa Kukuza Uchumi na Kuondoa 
Umaskini Tanzania (Mkukuta).
 
 
 Rais Jakaya Kikwete
 
BISHOP J. HILUKA
Dar es Salaam

MKUKUTA ni neno lililojipatia umaarufu mkubwa katika jamii ya Tanzania toka mpango huo ulipozinduliwa mwaka 2005. Ni neno maarufu ingawa Watanzania wengi hata hawajui ni kitu gani au kirefu chake, na limekuzwa zaidi na wanasiasa, hasa wa chama tawala, CCM.

Hata hivyo kirefu cha Mkukuta ambacho ni Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini Tanzania, bado kinatuwia vigumu wengi wetu kuelewa mkakati huo unatekelezwa namna gani. Mkakati wa kwanza wa kupunguza umasikini ulizinduliwa mnamo Oktoba 2000 na kutekelezwa kuanzia 2005 hadi 2010. Hivi sasa tuna Mkukuta Awamu ya Pili.
Mojawapo ya eneo ambalo Mkukuta ulipaswa kujikita ni kwenye ukuaji wa uchumi na kupunguza umasikini wa kipato kwa wanawake na wanaume wa maeneo ya vijijini wanaoishi chini ya mstari wa umasikini wapungue toka asilimia 38.6 hadi asilimia 14.

Kupungua kwa umasikini kutatokana tu na wakazi wa maeneo ya vijijini ambao wengi wao ni wakulima wadogo endapo watajengewa uwezo wa kuongeza tija na kupata faida ndani na nje ya sekta ya kilimo. Kuwezesha kutafuta masoko ya uhakika ya bidhaa za kilimo. Kuwajengea uwezo wa kuongeza thamani mazao wazalishayo ili waweze kupata faida.

Tukiwa tunaelekea miaka 50 tangu tujipatie uhuru toka kwa Waingereza, huku tukiwa kwenye awamu ya pili ya mpango huu wa Mkukuta baada ya awamu yake ya kwanza kufika mwisho wake mwaka jana 2010, umasikini wa Watanzania bado uko pale pale na umeendelea kukita mizizi hasa maeneo ya vijijini, ingawa serikali inajigamba kuwa uchumi wa nchi unakua.

Umasikini wa kipato vijijini unachangiwa na wakulima kuendesha kilimo cha kujikimu kwa kutegemea mvua, uzalishaji duni, nguvukazi haba na vitendea kazi duni ingawaje huduma za kilimo cha umwagiliaji zinaonesha kuanza kukua lakini wananchi wengi hawatumii kutokana na ubunifu mdogo.

Mitaji na fursa finyu ya kupata mikopo ni changamoto kwa wakazi wengi wa vijijini. Hata maeneo ya mijini ambayo tatizo lilionekana sio kubwa sana ukilinganisha na maeneo ya vijijini hali ni mbaya vilevile.

Nakubali kuwa yapo maeneo ambayo wananchi wake hawahitaji fedha kwa ajili ya mitaji ya kuongeza kipato lakini wanakabiliwa na umasikini wa kipato kutokana na sheria ambazo kama zingerekebishwa zingeweza kuwajengea mazingira mazuri ya kuinua hali za maisha yao.

Nadhani kila kitu kipo wazi kuwa malengo ya serikali ya kupunguza umaskini hadi kufikia mwaka huu ambapo nchi yetu itaadhimisha miaka hamsini ya uhuru, kupitia mpango huu wa Mkukuta yameonesha kushindwa kabisa na maisha ya Watanzania yanazidi kuwa magumu.

Ingawa takwimu zinaonesha kuwa uchumi umekuwa ukikua kwa wastani wa asilimia saba miaka ya karibuni (nadhani kwa kanuni ya 'Head in the oven and legs in the freeze, the average is comfortable'), lakini hakuna unafuu wowote kwa wananchi wa kawaida.

Hata Malengo ya Mpango wa Milenia (MDGs) kupunguza umaskini kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2015 hayatafikiwa kwa kuwa uchumi wetu bado umeendelea kuwa tegemezi kwa kiwango kikubwa, na sasa tuna hili balaa kubwa lisiloonesha dalili zozote za kumalizika pamoja na serikali kujigamba kupata tiba yake; janga la umeme ambalo mimi hupenda kuliita 'mgawo wa giza'.

Ni aibu kubwa kwa nchi hii inayojisifu kufikia miaka 50 ya uhuru huku ikiwa bado inashindwa kujitegemea kwenye bajeti yake, ikikumbwa na janga la mgawo wa giza na matatizo lukuki. Bajeti yetu kila mara imekuwa haina jipya kwa kuwa haijabainisha njia za kutengeneza utajiri mpya kama vile kuongeza viwanda vya uzalishaji mali na kuwekeza nguvu kubwa kwenye kilimo ili kiwe na tija.

Vipaumbele vya serikali kila mara vinaonekana ni vya bajeti dhaifu na ya kivivu ambayo hata mimi nisiye mchumi naweza kuiandika hata nikikurupushwa usingizini.

Sioni kabisa kipaumbele cha uhakika katika sekta ya elimu ambayo ndiyo inaweza kuwa njia kuu ya kukuza uchumi na serikali yetu imeishia kujenga shule za kata, ambazo ukijaribu kuzikosoa utaiona hasira ya watawala watakaokuona kama msaliti wa maendeleo.

Shule hizi nyingi hazina walimu na zimeishia kuwa vijiwe vya wasichana kupata mimba kwa kuwa wanafika shuleni na kukaa bila kufundishwa.

Pia kwa hili la wabunge bila kujali itikadi zao kuikataa bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini ni uthibitisho tosha kuwa miaka hamsini baada ya uhuru, bila nishati ya uhakika Mkukuta ni sawa na porojo kwa kuwa hakuna kinachoweza kufanyika. Ukosefu wa nishati ya uhakika ni kiashirio kwamba Watanzania wasitarajie faraja yoyote.

Tanzania ingefanikiwa katika mpango huu endapo kama ingeharakisha kutekeleza mpango wa kuanzisha vitambulisho vya taifa, baada ya sheria hiyo kupitishwa na Bunge mwaka 1986.

Vitambulisho hivyo vingesaidia katika mfumo wa utambuzi wa wananchi wake na kurahisisha kazi ya kuwajua walipa kodi wote na hivyo mzigo huo kubebwa na wachache kiasi kwamba lazima nchi kama hiyo itembeze bakuli katika kutekeleza bajeti yake.

Mungu ibariki Tanzania

NELSON MANDELA: Nembo ya demokrasia duniani atimiza miaka 93 ya kuzaliwa

 Mzee Nelson Mandela

 Mzee Nelson Mandela katika sherehe yake ya kutimiza miaka 93 ya kuzaliwa, hapa akiwa na famila

AFRIKA KUSINI

MWANZO wa wiki hii, Jumatatu ya Julai 18, Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Nelson Mandela, alitimiza miaka 93 tangu azaliwe. Mandela, hata hivyo, kwa sasa ni mnyonge kiafya na yuko chini ya uangalizi wa karibu kutoka kwa madakatari kwa muda wa saa 24. Hii ni tangu atoke hospitali mwezi Januari pale alipolazwa baada ya kuugua.

Lakini hali hii haijawazuia raia wa Afrika Kusini na watu wengi duniani kumtakia kheri njema wakati alipokuwa akisheherekea miaka 93 tangu azaliwe. Kuadhimisha siku hii, wimbo maalum umetungwa kwa heshima yake.

Raia wa Afrika Kusini waliweka historia ambapo yamkini watu milioni 12 waliimba wimbo huo kwa wakati mmoja. Shirika la utangazaji nchini humo (SABC) pamoja na idara ya elimu walifanya mapango kuwa ifikiapo saa mbili asubuhi, wanafaunzi katika shule zote nchini humo wawe wanauimba wimbo huo maalum uliotungwa kwa heshima ya Madiba.

Siku ya kuzaliwa kwa Nelson Mandela, rais wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini ni mojawapo ya siku ya kimataifa iliyoorodheshwa na Umoja wa Mataifa. Nchini Afrika Kusini kila mtu alipaswa kujitolea dakika 67 za muda wake kufanya huduma za kijamii.

Viongozi mbalimbali duniani wamemtumia salamu za kheri njema mzee Mandela wakiongozwa na Rais Barack Obama wa Marekani, ambaye alisema kuwa Mandela ni nembo ya demokrasia na haki duniani na amemshukuru kwa kujitolea maisha yake kwa huduma ya jamii. Kiongozi huyo wa Marekani amesema Mandela ataacha urithi wa busara, nguvu na fadhila nyingi.

Historia yake

Nelson Rolihlahla Mandela au Madiba kama anavyojulikana kwa jina la utani, alizaliwa katika Jimbo la Transkei, Afrika Kusini Julai 18, 1918. Baba yake alikuwa ni Chifu Henry Mandela, wa kabila la Tembu. Ni rais wa kwanza aliyechaguliwa kidemokrasia nchini Afrika Kusini. Alikuwa mwanasheria na mwanachama wa ANC aliyepinga siasa za Ubaguzi wa rangi katika Afrika Kusini.

Nelson Mandela ni wa nasaba inayotoka tawi la cadet la Thembu, ambalo linatawala katika mkoa wa Transkei, Jimbo la Cape ya Mashariki nchini Afrika Kusini. Alizaliwa katika kijiji kidogo cha Mvezo, ambacho kipo katika wilaya ya Umtata.

Wakati Mandela alipokuwa na miaka tisa, baba yake alifariki kwa kifua kikuu, na Jongintaba, aliyekaimu utawala kwa muda akawa mlezi wake.

Mandela alipata elimu yake katika Chuo Kikuu cha Fort Hare na Chuo Kikuu cha Witwatersrand na kuhitimu katika sheria mwaka 1942. Alijiunga na African National Congress (ANC) mwaka 1944 na kushiriki katika upinzani dhidi ya sera za chama tawala cha National Party ya ubaguzi wa rangi baada ya 1948.
Baada ya ushindi wa chama cha Makaburu cha National Party katika uchaguzi wa 1948, chama ambacho kiliunga mkono sera ya ubaguzi wa rangi, Mandela alianza kushiriki kikamilifu katika siasa. Awali, Mandela na watu wengine 150 walikamatwa tarehe 5 Desemba 1956 na kushtakiwa kwa uhaini, aliachiwa huru mwaka 1961.

Kutoka 1952 hadi 1959, daraja jipya la wanaharakati weusi lililojulikana kama Africanists lilivuruga shughuli za ANC katika makazi duni, na kutaka hatua kali zaidi dhidi ya utawala wa National Party.

Uongozi wa ANC chini ya Albert Luthuli, Oliver Tambo na Walter Sisulu waliona si tu kwamba Africanists walikuwa wanasonga kwa kasi lakini pia walitoa changamoto kwa uongozi wao. Uongozi wa ANC uliimarisha nafasi yao kwa njia ya muungano na vyama vya siasa vya Weupe wachache, Machotara, na Waasia katika jaribio la kutaka uwakilishi mpana zaidi ya ule wa Africanists.

Africanists waliudharau Mkataba wa Uhuru wa 1955 katika Mkutano wa Kliptown wa mkataba wa wanachama wa ANC 100,000 wenye nguvu ya kupiga kura moja katika muungano.

Baada ya kupigwa marufuku kwa ANC mwaka 1960, Nelson Mandela alitaka kuanzishwa tawi la jeshi ndani ya ANC. Mwezi Juni 1961, mtendaji wa ANC alilikubali pendekezo lake juu ya matumizi ya mbinu za vurugu na walikubaliana kwamba wanachama waliotaka kujihusisha wenyewe katika kampeni ya Mandela hawatazuiwa kufanya hivyo na ANC. Hii ilisababisha kuundwa kwa Umkhonto we Sizwe. Mandela alikamatwa mwaka 1962 na kuhukumiwa kifungo cha miaka mitano pamoja na kazi ngumu.

Mwaka 1963, wakati viongozi wenzake wengi wa ANC na Umkhonto we Sizwe walipokamatwa, Mandela aliletwa kujibu mashtaka yao kwa kupanga njama za kuipindua serikali. Juni 12, 1964, washitakiwa wanane, ikiwa ni pamoja na Mandela, walihukumiwa kifungo cha maisha. Kutoka 1964 hadi 1982, aliwekwa kizuizini katika gereza la Robben Island, nje ya Cape Town; baada ya hapo, alikuwa katika Gereza la Pollsmoor.

Katika miaka yake gerezani, sifa ya Nelson Mandela ilikua kwa kasi. Alikubaliwa sana kama kiongozi muhimu zaidi mweusi nchini Afrika Kusini na akawa mtu muhimu mwenye nguvu ya upinzani kama harakati za kupambana na ubaguzi wa rangi. Mara kwa mara alikataa kukubaliana au kubadili msimamo wake wa kisiasa ili aachiwe.

Kwa kutumia mbinu za Mahatma Gandhi, Mandela hatimaye alifanikiwa kwa ajili ya vizazi vya wanaharakati wa Afrika Kusini dhidi ya ubaguzi wa rangi. Baadaye alishiriki katika mkutano tarehe 29-30 Januari, 2007, uliofanyika New Delhi kuadhimisha kumbukumbu ya miaka 100 ya Gandhi kuanzisha satyagraha (upinzani usio wa vurugu) nchini Afrika Kusini.

Tarehe 2 Februari 1990, Rais wa nchi hiyo, Fredreck W de Klerk aliachana na amri ya kupiga marufuku shughuli za ANC na vyama vingine vya kupambana na ubaguzi wa rangi, na kutangaza kuwa Mandela muda mfupi atafunguliwa kutoka gerezani. Mandela ilitolewa kutoka gereza la Victor Verster Februari 11, 1990. Tukio hilo lilitangazwa moja kwa moja duniani kote.

Kufuatia kuachiliwa kwake kutoka gerezani, Mandela akarudi kwenye uongozi wa ANC na, kati ya 1990 na 1994, alikiongoza chama katika mazungumzo ya vyama vingi ambayo yalisababisha uchaguzi wa kwanza nchini humo usio wa ubaguzi wa rangi.

Mwaka 1990 alianzisha sera ya maridhiano. Yeye mwenyewe kwa moyo wote alijiimarisha katika maisha yake ya kazi na kujitahidi kufikia malengo ya yeye na wengine yaliyowekwa gerezani karibu miongo minne kabla. Mwaka 1991, katika mkutano wa kwanza wa kitaifa wa ANC uliofanyika ndani ya Afrika Kusini baada ya uanzishwaji wake kupigwa marufuku mwaka 1960, Mandela alichaguliwa kuwa Rais wa ANC wakati rafiki yake wa muda mrefu, Oliver Tambo, kuwa Mwenyekiti wa Taifa wa chama. Mwaka wa 1993, pamoja na Frederick de Klerk, alikuwa mshindi wa Tuzo ya Nobel ya Amani.

Mandela anakumbukwa kwa ushujaa wake, uzalendo wake na kutanguliza mbele maslahi ya wengi kuliko ya kwake. Hata aliposhika madaraka ya kuongoza taifa hilo lenye uchumi borea zaidi kuliko mengine Afrika, hakutaka kung’ang’ania madarakani kama walivyo wenzake akina Robert Mugabe wa Zimbabwe. Alitoka madarakani huku wananchi bado wakimpenda na kuwapisha wengine. Je, viongozi wengi wa Afrika ni akina nani wanafuata nyayo zake?
Makala haya yameandaliwa na Bishop J. Hiluka kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya habari.

Jul 14, 2011

FILAMU NYINGINE: Bunge la rusha jiwe gizani ukisikia mmh jua limempata!

 Jengo la Bunge

Wabunge wakiwa kwenye kikao

Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki (EAC), 
Samuel Sitta

 Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa

BISHOP J. HILUKA
Dar es Salaam

HAKIKA haya yanayoendelea ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano ni kama maigizo ingawa ndiyo hali halisi inayoendelea kwenye vikao vya bunge letu (tukufu?) mjini Dodoma, ambapo kumekuwepo hali ya kutofautiana kihoja na kimawazo kiasi cha kufikia hatua ya kuporomosheana vijembe na kejeli hizi na zile, tena zikiwa zinatoka kwa watu ambao wanaheshimika mno ndani ya jamii.

Hakika kile kinachoendelea huko bungeni hakina tofauti na ule upinzani uliokuwepo kwenye bendi zetu za muziki wakati ule; Extra Bongo walipokuwa wakiimba kibwagizo chao kwamba 'zama za kurusha jiwe kwenye giza na ukisika mmmh… ujue limempata', ambapo mwanamuziki mwingine, Muumini Mwinjuma alipingana nao na kuimba kuwa 'unaporusha mawe kuwa mwangalifu usije ukampiga mkweo...'

Hali hii pia inanikumbusha simulizi ninazosikia kila mara kuhusu wenyeji wa mikoa ambayo uwindaji ni moja ya shughuli zao kuu za kila siku. Simulizi ambazo zimekuwa zikisema kuwa wawindaji hawa wamekuwa na msemo usemao, "Ukirusha mshale usiku mawindoni, ukasikia chwiiii! Chwiii! Jua umempata mnyama.”

Hali hii ni dhahiri kabisa kuwa ipo katika vikao vya bunge linaloendelea mjini Dodoma. Ambapo wabunge wa Kambi ya Upinzani Bungeni wamekuwa wakirusha mishale (wakitoa hoja kali) ambazo zimekuwa zikiwatikisa sana mawaziri na wabunge wa chama tawala kiasi cha kuomba muongozo wa spika kila mara.

Mfano ni ile hoja ya ufisadi na mafisadi katika akaunti ya EPA ilipotolewa kwa mara ya kwanza katika bunge lililopita, wabunge wa chama tawala wakiongozwa na spika wa wakati huo wakazomea. Spika akasema kuwa hayo ni majungu. Lakini baada ya muda ukweli ukajulikana.

Hali kadhalika hoja ya posho iliyoibuka katika bunge hili linaloendelea imekwisha wainua takribani mawaziri wote na wabunge wengi wa chama tawala, ambapo wamesimama kupinga hoja hiyo kwa nguvu zao zote.

Katika kikao cha Jumanne wiki hii, Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi), alipokuwa akichangia katika hotuba ya Wizara ya Afya alisema kwa kunukuu kauli ya Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere kuwa 'serikali corrupt haiwezi kukusanya kodi', yeye akisema kwamba serikali ya Rais Kikwete ni legelege kwa vile imeshindwa kukusanya kodi, kauli iliyosababisha mawaziri zaidi ya watatu kuomba mwongozo wa mwenyekiti.

Hata alipotakiwa na kiti cha mwenyekiti, Jenista Mhagama, kufuta kauli hiyo, Kafulila alikataa na kusisitiza kwamba yuko tayari kufia msimamo huo ambao ni mchungu kwa watu fulani (serikali na wabunge wa CCM), ndipo Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki (EAC), Samuel Sitta, alipoamua kusimama kutuliza mzozo huo. Alisimama na kuwasihi wabunge wa CCM kuwa watulivu, kwani wapinzani kazi yao ni kubeza kila kitu kinachofanywa na serikali.

“Wabunge wa upinzani kazi yao ni kubeza kila kitu kinachofanywa na serikali, lakini sisi tutahukumiwa na wananchi. Siku zote wapinzani mambo yao ni ya unafikinafiki,” alisema Sitta na kuibua zogo zaidi.

Nitatoa mfano, baadhi yao wanadai posho za vikao ni kuwaibia wananchi, lakini wapo baadhi yao walichukua posho hizo miaka mitano iliyopita. Warejeshe posho hizo ndiyo wananchi watawaelewa… na wataendelea kuwa wapinzani,” alisema.

Hata hivyo, maelezo ya Sitta hayakuweza kuzima mzozo uliokuwapo kwani wabunge wengi wa upinzani walisimama wakitaka mwongozo wa mwenyekiti, lakini mwenyekiti aliahirisha Bunge kutokana na muda wa kikao kwisha.

Majibu ya Sitta ambaye amekuwa kiongozi wa shughuli za Bunge akikaimu nafasi ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, yalikuja wakati akitoa ufafanuzi wa kauli iliyoibua zogo hayakuwafurahisha wabunge wa kambi ya upinzani.
Wapinzani waliona kana kwamba kuwaita wafaniki ni lugha yenye kuudhi pia, kinyume cha kanuni za Bunge.

Kurusha mawe pia kumefanywa na Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa alipoirushia jiwe serikali ambayo yeye pia aliwahi kuwa Waziri Mkuu wake kabla hajajiuzulu kwa kashfa ya Richmond. Haukupita muda tukasikia mmhhh! Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kujaribu kukwepa jiwe la Lowassa na kisha Samuel Sitta naye wiki iliyopita akatumia nafasi hiyo kumjibu Lowassa.

Hata hivyo, imesemwa kuwa hata Makamu wa Kwanza wa Rais wa serikali ya umoja ya Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, pia amevipongeza vyama vya Chadema na NCCR-Mageuzi kwa hoja ya posho waliyoisimamia kidete, hadi kieleweke.

Katika hili imeonesha wazi kuwa wabunge wa kambi ya upinzani safari hii wana shabaha kwa kulenga ipasavyo mishale na mikuki yao, maana kila wanapolenga ama kutupa mawe tunasikia mmmh ama chwiii. Maana kila jiwe walilotupa, mkuki na mshale waliourusha umeonekana kuleta majibu hata kama bado wanayarusha gizani.

Hoja zao zinatuingia sisi tunaosikia kwamba zina mantiki lakini mshangao ni wenzao wa CCM ambao kinachoonekana ni kwamba wameacha jukumu lao la kuisimamia serikali na kuwa watu wa kuibeba, nadhanai wakijiona ni mawaziri watarajiwa!

Mimi ninawahamasisha wapinzani waendelee kurusha mawe gizani kwani yanawapata na sisi tunaona, hata kama ikipigwa kura wao wanashinda lakini wanaondoka na majeraha. Majeraha haya yatakapowazidi, watakufa na hapo bila shaka umma wa Watanzania utanufaika na uwepo wa hili Bunge.

Alamsiki...

Jul 13, 2011

PROF. JOHN ATTA MILLS: Apambana na kumgaragaza mke wa bosi wake wa zamani ndani ya chama

 John Atta Mills

 Nana Konadu Rawlings

ACCRA
Ghana

RAIS wa Ghana, John Atta Mills amechaguliwa tena kuibeba bendera ya chama tawala cha National Democratic Congress (NDC) nchini Ghana katika uchaguzi mkuu wa rais utakaofanyika mwakani.

Rais Atta Mills ambaye alikuwa akipambana katika kinyang'anyiro cha kuwania nafasi hiyo kupitia chama chake kwenye uchaguzi wa mwaka ujao na mke wa aliyekuwa kiongozi wa Ghana, Jerry Rawlings, alijinyakulia asilimia 97 ya kura zilizopigwa kwenye uchaguzi wa chama hicho mwanzoni mwa wiki hii.

Mke wa Jerry Rawlings, Nana Konadu Rawlings, ndiye aliyekuwa mpinzani wake wa pekee. Baada ya ushindi huo, Atta Mills amesema kuwa huu ndiyo mwanzo wa kinyang'anyiro cha mwaka ujao na kuwataka wafuasi wake kuendelea kukiunga mkono chama hicho tawala. Rais huyo wa sasa wa nchi hiyo ya Magharibi mwa Afrika anatazamiwa kuchuana na Nana Akufo Addo wa chama kikuu cha upinzani cha NPP katika uchaguzi mkuu ujao, utakaofanyika Desemba mwaka kesho, 2012.

Historia yake
John Evans Atta Mills alizaliwa Julai 21, 1944. Aliingia madarakani Januari 7, 2009, baada ya kumshinda mgombea wa kilichokuwa chama tawala, Nana Akufo-Addo kwa asilimia 50.23 ya kura dhidi ya asilimia 49.77 alizopata mpinzani wake katika uchaguzi wa Rais uliofanyika mwaka 2008. Alikuwa Makamu wa Rais kuanzia 1997 hadi 2001, chini ya Rais Jerry Rawlings, na aligombea bila mafanikio katika uchaguzi wa rais wa mwaka 2000 na 2004 kama mgombea wa chama cha National Democratic Congress (NDC).

Maisha ya awali na elimu

Mills alizaliwa katika eneo la Tarkwa, eneo lililoko katika Mkoa wa Magharibi wa Ghana. Alielimishwa katika shule ya Achimota, ambapo alihitimu Advanced Level Certificate mwaka 1963, na baadaye elimu ya juu katika Chuo Kikuu cha Ghana, Legon, ambapo alihitimu shahada na cheti cha taalamu katika sheria mwaka 1967.

Wakati akisoma kiwango cha udaktari katika Sheria katika Shule ya Oriental and African Studies (SOAS) ya Chuo Kikuu cha London, Mills alikuwa amechaguliwa ugenini, kama msomi wa Fulbright katika Chuo cha Sheria cha Stanford huko Marekani.

Mills alihitimu masomo yake ya udaktari SOAS, baada ya kukamilisha makala yake (Thesis) katika eneo la ushuru na maendeleo ya kiuchumi.

Kazi ya uhadhiri

Mills alianza kazi ya kufundisha (uhadhiri) katika Kitivo cha Sheria katika Chuo Kikuu cha Ghana, Legon. Alikaa karibu miaka ishirini na mitano akifundisha katika Legon na taasisi nyingine za elimu ya juu, na akapanda cheo kuanzia mhadhiri, mhadhiri mkuu na Profesa, na ni mjumbe katika bodi na kamati mbalimbali.

Zaidi ya hayo, alisafiri kutembelea duniani kote kama mhadhiri na profesa katika taasisi ya elimu kama vile LSE, na kufafanua utafiti wake na majarida katika mikutano mbali mbali.

Mills ametunga machapisho kadhaa, kama vile:Taxation of Periodical or Deferred Payments arising from the Sale of Fixed Capital (1974) na Exemption of Dividends from Income taxation: A critical Appraisal (1977) Katika: Review of Ghana Law, 1997, 9: 1, pg.38-47.

Mengine ni Report of the Tax Review Commission, Ghana, parts 1,2&3 (1977), Ghana's Income Tax laws and the Investor. ( iliyochapishwa na Chuo Kikuu cha Ghana), na Ghana's new investment code: an appraisal (1993) Katika: University of Ghana Law Journal, 1993, vol. 18, pg.1-29.
Amewahi kushikilia nafasi za mtahini katika taasisi kadhaa zenye uhusiano na fedha taasisi nchini Ghana, ikiwa ni pamoja na Taasisi ya Wahasibu, Taasisi ya wafanyakazi wa Benki, na Tume ya ushuru ya Ghana.

Mchango katika michezo

Amechangia katika shirika la Ghana la Hockey, Shirika la kitaifa la Michezo nchini Ghana, na klabu ya Accra Heart of Oak. Hufurahia sana michezo ya Hoki na kuogelea, na huchezea mara kwa mara timu ya taifa ya Hockey (ni mwanachama wa timu ya Hockey Veterans).

Makamu wa Rais wa Ghana

Katika uzinduzi wa uchaguzi wa kwanza wa Rais mwaka 1992, National Convention Party (NCP) kiliunda muungano na National Democratic Congress (NDC). Mwenyekiti wa zamani wa Baraza la Taifa la Muda la Ulinzi (PNDC) na kiongozi wa Ghana, Jerry John Rawlings alimchagua kiongozi wa NCP, Kow Nkensen Arkaah, kuwa mgombea mwenza kwa ajili ya Umakamu wa Rais. Baada ya kuchaguliwa katika uchaguzi wa 1992, Arkaah alishikilia madaraka hayo kati ya 1992-1996.

Hata hivyo, tarehe 29 Januari 1996, NCP kilivunja muungano na NDC, kikaungana na People's Convention Party (PCP) na kuunda chama kipya cha Convention People's Party (chama cha siasa cha zamani kilichopigwa marufuku cha Rais wa kwanza wa Ghana, Kwame Nkrumah). Hivyo, katika mgawanyiko huo mchungu, Arkaah alisimama kama mgombea wa CPP iliyozaliwa upya katika Uchaguzi wa 1996 dhidi ya Rais Rawlings.

Rawlings alimchagua Mills kwa nafasi iliyokuwa wazi ya Makamu wa Rais katika jitihada zake za kuchaguliwa tena kwa muhula wa pili katika Uchaguzi wa Rais wa Ghana 1996. Rawlings alichaguliwa tena katika muhula wake wa pili kuwa rais, na Mills akawa Makamu wa Rais wa Ghana kati ya mwaka 1996 hadi 2000.

Urais

Desemba ya 2002 John Atta Mills alichaguliwa na chama chake kuwa mbeba bendera ya chama na kuwaongoza katika uchaguzi wa mwaka, baada ya Rais Rawlings ambaye katiba ilimzuia kuendelea kuwa rais. Hata hivyo alishindwa na mwanasiasa mkongwe, John Agyekum Kufuor, ambaye alikuwa kugombea wa NPP. Kufuor alikuwa mbunge wa zamani wakati wa utawala wa Waziri Mkuu Kofi A. Busia wa Progress Party katika kipindi chake cha utawala cha 1969-1971 na aliwahi kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje.

Tarehe 21 Desemba 2006, Mills alichaguliwa tena na NDC kuwa mgombea wake kwa ajili ya uchaguzi wa rais wa 2008 kwa jumla ya asilimia 81.4 (kura 1,362), akiwashinda kwa mbali wapinzani wake, Ekwow Spio-Garbrah, Alhaji Mahama Iddrisu, na Eddie Anna. Mwaka 2008, alichaguliwa kuwa rais wa Ghana, baada ya uchaguzi wa pande tatu.

Shughuli na miradi mingine

Mills amehusika katika shughuli na miradi mbalimbali kama vile:
  • Mwanachama wa soko la hisa la Ghana
  • Bodi ya Wadhamini, Mines Trust
  • Mjumbe wa Kamati ya usimamizi, Utawala wa ushuru ya Wataalam, Umoja wa Mataifa Kikundi cha Wataalam katika Ushirikiano wa Kimataifa katika Masuala ya ushuru, na Umoja wa Mataifa Mradi wa Sheria na Idadi ya Watu
  • Masomo juu kukodesha vifaa nchini Ghana
  • Kitabu kiandalizi juu ya ushuru ya Mapato ya Ghana
  • Mapitio ya Mkataba na Uingereza wa ushuru
  • Mwaka 1988, John Evans Atta Mills akawa kaimu Kamishna wa Mapato ya Ndani ya Humuma ya Ghana na aliteuliwa kamishna mwezi Septemba 1996.
  • Mwaka 1997, Profesa Mills alipata cheo kingine muhimu tarehe 7 Januari 1997, alipoapa kama Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Ghana.
  • Katika 2002, Prof Mills alikuwa kutembelea Liu kama msomi mtalii katika Kituo cha Masomo ya Maswala ya Dunia, Chuo Kikuu cha British Columbia, Kanada.
  • Mnamo Desemba 2002, John Evans Atta Mills alichaguliwa na chama chake kuwa kiongozi na akawaongoza katika uchaguzi wa 2004.

Maisha binafsi

Rais Mills amemuoa Ernestina Naadu Mills, mkufunzi na wana watoto wawili; Sam Kofi Mills, mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka 19, na Ruby Addo, binti.

Ni rafiki mzuri wa Mchungaji TB Joshua wa The Synagogue, Kanisa la mataifa yote mjini Lagos, Nigeria na hutembelea kanisa lake mara kwa mara. Alisema kufuatia uzinduzi wake kwamba TB Joshua alitabiri kwamba kungekuwa na uchaguzi wa tatu, matokeo yangetolewa Januari, na angeweza kuibuka mshindi.

Makala haya yameandaliwa na Bishop J. Hiluka kwa msaada wa mashirika mbalimbali ya habari ya kimataifa.

Jul 6, 2011

Takwimu za unywaji maziwa na madhara ya uchakachuaji

 Baadhi ya wanafunzi wa shule mbalimbali za msingi 
za Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam 
wakiandamana kwenye barabara ya Kawawa 
kuadhimisha kilele cha wiki ya uhamasishaji 
unywaji wa maziwa.
 
BISHOP J. HILUKA
Dar es Salaam

WIKI hii nimesoma habari kuhusu taarifa ya Bodi ya Maziwa nchini (TDB), kwamba wastani wa Watanzania kunywa maziwa unaongezeka na imewaomba kujenga utamaduni wa kunywa maziwa kwa wingi ili kujenga afya zao.

Akizungumza kwenye maonesho ya kimataifa ya Sabasaba katika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam, Meneja Masoko wa bodi hiyo, Dk. Mayasa Simba, alisema bodi hiyo imeendelea kuhamasisha unywaji wa maziwa na hadi sasa wastani wa mtu mmoja kunywa maziwa umefikia lita 43 kwa mwaka ingawa Shirika la Afya duniani (WHO) linapendekeza wastani wa lita 200 kila mwaka kwa kila mtu.

Alisema kuwa bodi hiyo imeendelea na mikakati ya kuhamasisha unywaji wa maziwa kuanzia shuleni, kwenye maonesho kama Sabasaba na Wiki ya Maziwa ambapo bidhaa mbalimbali zitokanazo na maziwa zimekuwa zikioneshwa.

Na kaulimbiu ya bodi hiyo ni “Maziwa ya Tanzania kwa afya na utajiri”, hivyo itaendelea kuwaeleza Watanzania kuwa kuna bidhaa nyingi zitokanazo na maziwa tofauti na mtazamo wa baadhi ya watu.

Taarifa hiyo iliendelea kusema kuwa kwenye maziwa kunapatikana bidhaa nyingi kama vile jibini, yoghurt, siagi na samli na maziwa yanaweza kutumika kupikia wali na vyakula mbalimbali na kujenga afya za Watanzania.

Na mwisho habari hizo zilibainisha kuwa Bodi ya Maziwa kwa kushirikiana na Wizara ya Mifugo na wadau mbalimbali wanaandaa andiko kwa ajili ya mpango wa unywaji wa maziwa shuleni, hali ambayo itajenga utamaduni wa watoto kupenda kunywa maziwa.

Hivi karibuni niliandika makala kuhusu unywaji wa maziwa na jinsi Watanzania wanavyokatishwa tamaa na mambo fulanifulani. Imekuwa ikisemwa kuwa Watanzania hatuna utamaduni wa kunywa maziwa, huku wenzetu wa Kenya ndio wanaosemwa kuongoza kwa kunywa maziwa wakifuatiwa na Uganda na Rwanda ingawaje sisi tumejaaliwa kuwa na mifugo wengi ambao wangetosheleza mahitaji yetu ya vyakula hivyo.

Napenda nisisitize tena kuwa mimi ni mmoja wa watu wanaopenda sana wanywe maziwa, lakini kutokunywa maziwa hakumaanishi kwambwa hatupendi bali kinachotukatisha tamaa ni kwamba maziwa mengi yanayouzwa si maziwa halisi, kwa kuwa wafugaji tayari huwa wamekwishayachakachua kwa kuongeza maji ili yawe mengi.

Na haiishii hapo tu kwani yakishafika kwa wafanyabiashara nao hupenda kuchukua maziwa hayo kiasi kidogo na kuchanganya na maziwa ya unga au wakati mwingine hata unga wa ngano, kisha wanatia mafuta kidogo ili kupata utando wa mafuta juu yake.

Maziwa ya moto yanayouzwa kwenye vibanda vingi jijini Dar es Salaam, pindi ukiyatia mdomoni huwezi kuisikia ile radha ya maziwa, na pia huwa yana utando wa mafuta ambao si wa kawaida hasa kwa mtu anayeyafahamu vizuri maziwa halisi.

Lengo la wafanyabiashara kuamua kuchakachua maziwa ni ili wapate faida kubwa bila kujua kwamba wanajiharibia soko na wakati huohuo kuhatarisha afya za watumiaji kwani hata hayo maji wanayotumia kuchakachua sidhani kama ni maji salama.

Sababu nyingine inayosababisha Watanzania kuonekana kuwa hawapendi kunywa maziwa ni kutokana na kuendelea kwa umasikini na hali ngumu ya kiuchumi katika ngazi za kifamilia na kitaifa, hali hii imefanya afya za wananchi ziendelee kuwa hatarini kutokana na ugumu wa maisha na hivyo kufanya hata baadhi ya vyakula muhimu ikiwemo maziwa kuwa anasa kwa Mtanzania wa kawaida.

Kauli mbalimbali zinazotolewa na baadhi ya viongozi na watafiti kwamba eti Watanzania wafundishwe (waelimishwe) kuhusu umuhimu wa kula nyama, mayai na kunywa maziwa, kwangu mimi nahisi kama hiki ni kichekesho cha mwaka!

Ni kichekesho kwa kuwa sidhani kama kuna Mtanzania asiyejua umuhimu wa vyakula hivyo kwa mwili wa binadamu au asiyependa kula na kunywa vizuri!

Wanapodai kuwa tuelimishwe, wanatuelimisha katika lipi wakati tuna kliniki zimejaa nchini takriban kila kijiji, ni nani ambaye hajawahi kufundishwa au ambaye mama yake hajafundishwa umuhimu wa vyakula hivyo?

Inaposemwa kuwa Watanzania hawanywi maziwa, hawali nyama na mayai sio kwa sababu hawana elimu ya umuhimu wa lishe hiyo bali hawana imani na maziwa yanayouzwa na wafanyabiashara wetu na pia hali ya kiuchumi haiwaruhusu kufanya hivyo!

Maziwa pekee yanayoonekana kuaminika miongoni mwa jamii zetu au kuwa halisi ni yale yanayosindikwa viwandani ambayo hata hivyo kwa hali halisi ya kiuchumi ya Watanzania wengi ni sawa na anasa kuyanunua.

Nawashauri wahusika hawa wangeangalia njia nzuri ya kujirekebisha kwa kunyoosheana kidole kwa kujiharibia soko kwa kuchakachua maziwa. Lakini pia ni jukumu la Serikali kupitia Bodi ya Maziwa na Wizara ya Mifugo kuchukua hatua na kuangalia jinsi ya kudhibiti uchakachuaji huu ili kulinda afya za Watanzania na kwa kufanya hivyo, biashara hiyo itakuwa kubwa na hata Serikali itapata mapato kupitia kodi.

Alamsiki.

HUGO CHAVEZ: Kiboko ya Marekani aliyekwenda kuugulia kwa rafiki zake Cuba

Rais a Venezuela, Hugo Chavez

CARACAS
Venezuela

RAIS wa Venezuela, Hugo Chavez, wiki hii aliwahutubia maelfu ya watu mjini Caracas baada ya kutoka kupata matibabu ya saratani nchini Cuba. Wafuasi wa Rais Chavez walimshangilia kwa wingi alipowaonesha bendera ya Venezuela kutoka kwenye ghorofa ya kasri lake na kusema kuwa afya yake itaimarika.

Chavez, mwenye umri wa miaka 56, amekuwa nchini Cuba tangu Juni 8, alikofanyiwa upasuaji kuondoa uvimbe uliokuwa na vimelea vya saratani. Chavez ni rafiki mkubwa baba wa taifa wa Cuba, Fidel Castro na mtu ambaye huwa anaonekana mwiba kwa kuipasha Marekani kuacha eubabe.

Chavez, mtu mkakamavu na mwenye hotuba ndefu lakini zisizochosha alisema hatoweza kushiriki katika sherehe za kuadhimisha miaka 200 ya uhuru wa Venezuela kutoka kwa Uhispania siku ya Jumanne.

Lakini alisema kuwa atafuatilia sherehe hizo akiwa kwenye kasri ya rais. Akiwa amevaa magwanda yake ya kijeshi na kofia nyekundu, Chavez kwanza aliongoza umati huo kuimba wimbo wa taifa wa Venezuela.
"Nimerudi," alisema akiwashukuru wale wanaomuunga mkono. "Hii ndiyo dawa bora kwa ugonjwa wowote ule." Akisimama bila kusaidiwa, Chavez alizungumza kwa muda wa dakika 30 bila kuangalia popote. Maelfu ya wafuasi waliokuwa wamevaa mavazi mekundu walisema: "Hapana! Chavez haondoki!"

Awali, Chavez alisema amekuwa "na wakati mgumu" nchini Cuba lakini kwamba sasa anaendelea kupata nafuu. Chavez, ambaye ameiongoza Venezuela kwa miaka 12 na hata kunusurika jaribio la mapinduzi mwaka 2002, aliambia Televisheni ya taifa kuwa ana utaratibu kamili wa matibabu, "anatumia dawa, anatakiwa kupumzika, na kula vyakula maalum".

Mapema kulikuwa na uvumi kuhusu hali ya afya ya Chavez baada ya kuondoka Venezuela zaidi ya wiki tatu huku kila mtu akisema lake.Lakini maafisa walichosema ni kufanyiwa upasuaji.

Historia yake

Hugo Rafael Chavez Frias alizaliwa Julai 28, 1954. Alishika madaraka ya kuiongoza Venezuela mwaka 1999. Kufuatia itikadi yake ya kisiasa ya Kibolivarian na "Usoshalisti wa karne ya 21", amelenga katika kutekeleza mageuzi ya usoshalisti katika nchi kama sehemu ya mradi wa kijamii inayojulikana kama Mapinduzi ya Wabolivia, ambayo yameshuhudia utekelezaji mpya wa katiba, demokrasia shirikishi na kutaifisha viwanda kadhaa muhimu.
Alizaliwa Sabaneta, Barinas, akawa afisa kazi jeshini, na baada ya kutoridhika na mfumo wa siasa za Venezuela ambao aliuona kama wa rushwa na sio wakidemokrasia, alianzisha Vuguvugu la siri la Mapinduzi ya Kibolivarian-200 (MBR-200) katika miaka ya 1980 ili kuipindua serikali.

Baada ya tukio la kidemokrasia serikali ya Rais Carlos Perez Andres aliamuru ukandamizaji mkali wa maandamano dhidi ya kupunguzwa matumizi, Chávez aliongoza MBR-200 katika mapinduzi yaliyoshindwa dhidi ya serikali mwaka 1992, ambapo aliishia kufungwa jela.

Alipotoka gerezani baada ya miaka miwili, alianzisha chama cha siasa, Fifth Republic Movement, na alichaguliwa kuwa rais wa Venezuela mwaka 1998. Hatimaye alipendekeza katiba mpya ambayo iliongeza haki kwa makundi yaliyotengwa na ilibadilisha utaratibu wa serikali ya Venezuela, na alichaguliwa tena mwaka 2000. 
 

Wakati wa muhula wake wa pili wa urais, alianzisha mfumo wa Misheni ya Kibolivarian, Halmashauri za Kijamii na vyama vya ushirika vinavyosimamiwa na wafanyakazi, wakati pia alitaifisha viwanda mbalimbali muhimu kwa maslahi ya taifa. Wapinzani wakati huohuo, walionesha hofu kwamba alikuwa akiumomonyoa uwakilishi wa kidemokrasia na kujiongezea mamlaka, walijaribu kumwondoa madarakani kwa njia zote kupitia mapinduzi ya kijeshi yaliyoshindwa mwaka 2002 na kura ya maoni ya kukumbukwa mwaka 2003. 
 

Alichaguliwa tena mwaka 2006, kufuatia kuanzisha chama kipya cha siasa, United Socialist Party of Venezuela (PSUV), mwaka 2007.
anajulikana kama mkosoaji wa ubepari na hasa uliberali wa kisasa, Chávez amekuwa mpinzani maarufu wa sera za kigeni za Marekani. Akifungamana mwenyewe na serikali ya ujamaa ya Fidel na kisha Raul Castrol ya Cuba, ya Evo Morales wa Bolivia, na ya Rafael Correa wa Ecuador. Urais wake unaonekana kama sehemu ya “mrengo wa kushoto” ukiisafisha Amerika ya Kusini.

Amekuwa anaunga mkono ushirikiano wa Amerika Kusini na Caribbean na alikuwa mtu muhimu katika kuanzisha ushirikiano wa kanda nzima; Umoja wa Mataifa ya Amerika Kusini, Muungano wa Wabolivia kwa ajili ya Waamerika, Benki Kuu ya Kusini, na mtandao wa televisheni wa kikanda, TeleSur. Ushawishi wake wa kisiasa katika Amerika ya Kusini ulimfanya jarida la Time kumuweka katika orodha ya watu 100 wenye ushawishi mkubwa zaidi duniani katika miaka ya 2005 na 2006.

Maisha ya awali: 1954-1970

Hugo Chávez alizaliwa katika nyumba ya upande wa bibi yake mzaa baba, Rosa Inéz Chávez (aliyefariki 1982), kwenye kibanda cha matope cha vyumba-vitatu iliyoko kijiji cha Sabeneta, Jimbo la Barinas.

Wazazi wake, Hugo de los Reyes Chavez na Elena Frias de Chavez, walikuwa walimu – wa tabaka la chini kati - waliokuwa wakiishi katika kijiji kidogo cha Los Rastrojos, na kabla ya kuzaliwa Hugo walikuwa tayari na mtoto mmoja, Adan Chavez, na baada ya Hugo walipata watoto wengine watano zaidi, ingawa mmoja wao, Enzo, alikufa kwenye umri wa miezi sita. Familia ya Chávez ilikuwa ya mchanganyiko wa asili ya Amerindia, Afro-Venezuela, na Kihispania. 
 

Waliishi katika umaskini, hasa Hugo na ndugu yake Adan waliishi na bibi yao Rosa, ambaye baadae Hugo alimuelezea kuwa "binadamu safi... mwenye upendo, mwema." Alikuwa mcha Mungu, Mkatoliki, na Hugo mwenyewe alilelewa katika imani, kijana wa madhabahu ya kanisa la mtaa. Chávez alijua kwamba yeye na ndugu yake "tulikuwa maskini sana lakini watoto wenye furaha sana", na kwamba "Kwa upande wa (Rosa) bibi, nilijua unyenyekevu, umaskini, maumivu, na wakati mwingine kutokuwa na kitu chochote cha kula. Nikaona ukosefu wa haki katika dunia hii."

Mafunzo ya Kijeshi: 1971–1975

Akiwa na miaka kumi na saba, aliamua kwenda kusoma katika Chuo cha Sayansi ya Jeshi cha Venezuela mjini Caracas, baadaye alisema kwamba "nilijihisi kama samaki katika maji. Kama nimegundua sehemu ya kiini cha maisha, wito wangu wa kweli." Katika Chuo, alikuwa mwanachama wa daraja la kwanza aliyefuata mitaala ya marekebisho inayojulikana kama Mpango wa Andres Bello. Mpango huu uliwekwa na kundi la maendeleo, maafisa wa kijeshi walioamini mabadiliko yanahitajika katika jeshi.


Kazi ya awali ya kijeshi: 1976-1981

Wakati wa sherehe za kijeshi mwaka 1976. Baada ya kuhitimu, Chavez alikuwa afisa wa mawasiliano katika kitengo cha kupambana na uasi katika Jimbo la Barinas, ingawa uasi wa Marxist-Leninist ambapo jeshi lilitumwa kupambana ulikuwa umetokomezwa katika jimbo, ukitoa muda mwingi wa kitengo. Chávez mwenyewe alicheza katika timu ya baseball, aliandika makala kwenye gazeti. Katika hatua moja alikuta fasihi iliyofichwa ya ki-Marxist iliyokuwa katika gari iliyotelekezwa imejawa mashimo ya risasi. 
 

Inaonekana kilikuwa mali ya wapiganaji wa miaka mingi kabla, aliendelea kusoma vitabu hivi, ambayo ni pamoja na vile vyenye nadharia kama hiyo vya Karl Marx, Vladimir Lenin na Mao Zedong, lakini kazi aliyoipenda sana ni iliyopewa jina la Times wa Ezequiel Zamora, iliyoandikwa karne ya 19. Vitabu hivi vilimshawishi Chávez kuona haja ya mrengo wa kushoto katika serikali ya Venezuela, baadaye alisema kwamba "Kwa wakati huo nilikuwa na miaka 21 au 22, nilijiona kuwa mtu wa mrengo wa kushoto."

Kazi ya jeshi na MBR-200: 1982-1991

Miaka mitano baada ya kuianzisha ELPV, Chávez alianzisha mapambano mapya ya siri ndani ya jeshi, EBR-200, baadaye aliiboresha MBR-200. Akivutiwa na viongozi watatu wa Venezuela aliowahusudu sana, Ezequiel Zamora (1817-1860), Simon Bolivar (1783-1830) na Simon Rodriguez (1769-1854), watu hawa wa kihistoria walijulikana kama "mizizi mitatu ya mti" wa MBR-200. 
 

Baadaye alielezea msingi wa kundi hilo, Chávez alisema kuwa na "mfumo wa Bolivarian ulioanzishwa haukuwa na malengo ya kisiasa... malengo yake yalikuwa ya ndani. Juhudi zake zilielekezwa katika mahali pa kwanza pa kujifunza historia ya jeshi la Venezuela kama chanzo chetu wenyewe cha mafundisho ya kijeshi, ambacho hakikuwepo." 
 

Hata hivyo, alitumaini kwamba MBR-200 itatawala kisiasa, na mawazo yake kisiasa wakati huo, alisema kuwa "huu mti (wa Bolívar, Zamora na Rodríguez) unatakiwa kuwa mduara, unatakiwa kukubali kila aina ya mawazo, kutoka upande wa kulia, kutoka kushoto, kutoka mabaki ya kiitikadi ya wale wa zamani wa mifumo wa kibepari na kikomunusti."

Makala haya yameandaliwa na Bishop J. Hiluka kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya habari.