Oct 26, 2011

WINSTON TUBMAN: Alihitilafiana na George Weah, sasa wanapeperusha bendera

 Winston Tubman

MONROVIA
Liberia

BAADA ya matokeo ya uchaguzi wa urais nchini Liberia duru ya kwanza kujulikana, vyama vya upinzani vya nchi hiyo viliwataka wafuasi wao wasiyatambue na wajumuike kwenye mhadhara mkubwa wa kupinga uchaguzi huo wa rais, ambao vyama hivyo vinasema kuwa umegubikwa na udanganyifu.

Wapinzani wa serikali wanasema kuwa wana ushahidi kuwa matokeo ya mwanzo ya uchaguzi huo yalibadilishwa wakati wa kuhesabu kura, ili kumpendelea rais wa sasa, Bibi Ellen Johnson Sirleaf. Hata hivyo, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya nchi hiyo, James Fromayan, alikanusha tuhuma hizo.

Matokeo hayo yalionesha kuwa rais wa nchi hiyo anayetetea kiti chake kwa mara ya pili, Ellen Johnson Sirleaf, aliongoza kwa kura chache, lakini hazikuwa zimetosha kumfanya Sirleaf aepuke duru ya pili ya upigaji kura, ambapo mgombea aliyeshika nafasi ya pili, Winston Tubman, ni kati ya wagombea waliodai kuwa kumepita udanganyifu kwenye uchaguzi huo.

Habari nyingine zenye utata zinaonesha kuwa kiongozi wa upinzani na mgombea urais nchini Liberia, Winston Tubman, wiki iliyopita alisafirishwa hadi nchini Ghana kwa ajili ya matibabu baada ya afya yake kuwa mbaya na kuanguka. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Ijumaa ya Oktoba 21, 2011 ilisema kuwa afya ya kiongozi huyo sio nzuri.

Chanzo kimoja kutoka katika Hospitali ya Umoja wa Mataifa ya nchini Liberia ambapo Tubman alikimbizwa mara baada ya kuanguka kwa sababu iliyosemwa kuwa alikuwa akisumbuliwa na malaria, kilisema kwamba kiongozi huyo wa upinzani alipelekwa nchini Ghana hasa kutokana na hali yake ya afya kuwa mbaya zaidi.

Tubman, ambaye anatarajiwa kushiriki katika uchaguzi wa marudio wa urais nchini Liberia akichuana na rais aliyeko madarakani, Ellen Johnson Sirleaf, katika uchaguzi utakaofanyika tena Novemba 8, 2011 kulingana na vyanzo mbalimbali vya habari, inasemekana kuwa alipelekwa mjini Accra, Ghana, Oktoba 20, 2011 mchana kwa kuzingatia ushauri kutoka kwa madaktari wake.

Lakini vyanzo vingine vya habari vinasema kuwa mgombea huyo wa CDC ana tatizo la shinikizo la damu linalomfanya ahitaji matibabu ya dharura.

Hata hivyo, Katibu Mkuu wa CDC, Acarous Musa Gray, alisema kwamba Tubman amekwenda nchini Ghana kwa ajili ya kufanya mashauriano na viongozi katika kanda hiyo ya Afrika Magharibi hasa kuhusiana na uchaguzi mkuu nchini Liberia.
“Tubman alikuwa akiumwa malaria tu kama mtu mwingine yeyote. Kwa sasa yupo katika nchi fulani katika kanda yetu ya Afrika Magharibi, akifanya mazungumzo juu ya hatma ya uchaguzi wa Liberia,” alisema Gray.

Wakati huohuo, habari kutoka gazeti moja la mjini Monrovia la New Dawn, ambalo lina tetesi kuwa kutokana na hali mbaya ya afya ya Tubman, chama chake cha CDC kinaangalia uwezekano wa kumsimamisha mgombea mwenza, George Weah Manneh, kuchukua nafasi yake katika uchaguzi huo unaosubiriwa kurudiwa wa rais.

Hata hivyo, waangalizi wa uchaguzi huo wanasema kuwa uwezekano huo wa George Weah kuchukua nafasi ya Tubman katika kinyang’anyiro hicho ni mdogo sana kwani kuna taarifa kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi tayari imeanza uchapishaji wa karatasi za kupigia kura.

Kabla ya kinyang’anyiro hicho, kulikuwa na tetesi za kutoelewana kati ya Tubman na George Weah kufuatia mzozo wa nani atakayebeba bendera ya CDC katika kinyang’anyiro cha urais, hata hivyo, Tubman alipitishwa na CDC kwa kura 111 kati ya 118 na kumuengua George Weah katika uwezekano wa kugombea nafasi hiyo.

Historia ya nchi ya Liberia

Nchi ya Liberia ni nchi iliyoko Afrika ya Magharibi ikiwa imepakana na nchi za Ivory Coast, Guinea, na Sierra Leone.

Liberia ni nchi iliyoundwa na makabila mbalimbali ya asili nchini humo na wahamiaji weusi toka Marekani. Wamarekani Weusi hawa walikuwa ni watumwa waliopata uhuru ambao kwa kushirikiana na chama cha American Colonization Society waliunda taifa hili na kutangaza uhuru wa nchi hiyo Julai 26, 1847.

Wamarekani Weusi hawa waliichukulia nchi hiyo kama nchi ya ahadi kutokana na asili yao kuwa ni Afrika ambako ndiko mababu zao walikotokea kabla ya kupelekwa utumwani Marekani. Hata hivyo, wahamiaji hawa waliendelea kujitambulisha kama Wamarekani na hawakujenga mahusiano ya karibu na wenyeji.

Alama za taifa hili (bendera, kaulimbiu, na nembo ya taifa) na hata muundo wa serikali vilikuwa vikionesha mahusiano ya karibu kati ya nchi hizi mbili; Liberia na Marekani. Liberia imekuwa katika vita ya wenyewe kwa wenyewe kati ya mwaka 1989-1996 na 1999-2003.

Historia ya Tubman

Winston A. Tubman amezaliwa mwaka 1941 nchini Liberia, ni mwanadiplomasia na mwanasiasa wa Liberia akiwa mmojawapo wa wahamiaji weusi toka Marekani, walioletwa nchini Liberia (Americo-Liberia descent). Tubman ni waziri wa zamani wa sheria wa Liberia na mwanadiplomasia wa taifa hilo ambaye kwa sasa ndiye kiongozi wa chama hicho kikuu cha upinzani cha Congress for Democratic Change (CDC).

Tubman alizaliwa katika eneo la kata ya Maryland katika mji wa Pleebo, ni mpwa wa William VS Tubman, aliyekuwa rais wa Liberia na aliyeitumikia nchi hiyo kwa muda mrefu zaidi kuliko marais wote wa nchi hiyo. Tubman ana shahada kutoka Shule ya Uchumi ya jijini London, Chuo Kikuu cha Cambridge kilichoko Uingereza na Chuo Kikuu cha Harvard cha nchini Marekani.

Tubman alianzisha kampuni yake ya sheria mwaka 1968 na aliwahi kuwa mshauri wa kisheria wa Wizara ya Mipango na Uchumi wakati wa serikali ya mjomba wake, William VS Tubman. Pia Tubman anasemekana kuwa na uzoefu mkubwa sana wa kazi katika Umoja wa Mataifa. Kazi yake ya kwanza kabisa ilikuwa ni katika Ofisi ya Sheria mwaka 1973.

Aliwahi kufanya kazi chini ya Rais Samuel Doe, akiwa Waziri wa Sheria kati ya mwaka 1982 hadi 1983. Tubman alisafiri kwenda Marekani mwaka 1990 kwa niaba ya Samuel Doe kwenda kujaribu kuishawishi serikali ya Marekani ikubali kuingilia kati katika vita vya kwanza vya Liberia vya wenyewe kwa wenyewe lakini hakufanikiwa. Na baadaye katika miaka ya karibuni alifanya kazi kama mwakilishi wa Katibu Mkuu na mkuu wa kisiasa katika Ofisi ya Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Somalia, kuanzia mwaka 2002 hadi 2005.

Kabla ya mwaka huu kupitishwa kuwa mgombea urais kupitia CDC, Tubman alishiriki katika uchaguzi wa Oktoba 11, 2005, akiwa mgombea wa urais kupitia chama chake cha zamamni cha National Democratic Party of Liberia (NDPL). Katika uchaguzi huo alishindwa kufurukuta ambapo alijikuta akiangukia pua katika duru ya kwanza tu, kwa kushika nafasi ya nne kwa kuambulia asilimia 9.2 ya kura zote zilizopigwa.

Mnamo tarehe 1 Mei, 2011, ndipo Tubman alichaguliwa kuwa mgombea urais kupitia Congress for Democratic Change katika uchaguzi wa mwaka huu ambao unatarajiwa kurudiwa katika duru ya pili mwezi Novemba, uchaguzi unaolalamikiwa na wagombea urais wa vyama vya upinzani akiwemo Tubman.

Katika uchaguzi wa mwaka huu, Tubman anagombea urais huku mgombea mwenza wake kupitia CDC akiwa ni George Weah, ambaye alishika nafasi ya pili katika uchaguzi wa mwaka 2005.

Makala haya yameandaliwa na Bishop Hiluka kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya habari vya kimataifa.

KUKITHIRI KWA RUSHWA: Rais Zuma awafukuza mawaziri waandamizi

Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma

PRETORIA
Afrika Kusini

KATIKA pekuapekua yangu nikitaka kujua mambo mbalimbali kupitia machapisho, hivi karibuni nilibahatika kuona kazi fulani ya waandishi wawili, Paul Holden na Hennie van Vuuren, walioandika na kuchapisha kazi yao: “The Devil in the Detail...”, wakimaanisha “Tazama kwa makini (serikali ya Mzee wa Afrika Kusini) ili umuone Shetani” na “...How the Arms Deal Changed Everything”.

Nilijitahidi kuperuzi lakini kuna kitu kimoja nikiri kuwa sikuwa nimekielewa au sikukitilia maanani wakati nikisoma; sikuweza kujua machapisho yao yalichapwa lini na walikuwa wakimmaanisha rais yupi kati ya huyu aliyepo sasa madarakani nchini humo (Jacob Zuma) au yule aliyepita (Thabo Mbeki). Hata hivyo, itoshe tu kusema kuwa ujumbe uliopo ni kuhusu kukithiri kwa rushwa nchini humo.

Maoni ya waandishi hao katika kitabu chao yanamaanisha kwamba vyombo vya dola vya nchi ya Afrika Kusini kwa sasa vinamilikiwa na watu binafsi walio karibu sana na rais wa nchi hiyo, watu hao wakijumuisha wafanyabiashara kadhaa wakubwa, wanasiasa na maofisa fulani wa jeshi.

Watu wote wamepewa vyeo vya juu na wote, kama kigezo cha kupewa vyeo hivyo wakiwa na historia tu ya ukaribu naye (Rais) binafsi, bila kuwa na uwezo maalum au ujuzi katika kazi husika.

Wakati wananchi wa kawaida, kwa maoni ya waandishi hao, wamekuwa hawanufaiki kabisa kadiri siku zinavyosonga mbele; na yote hii ilitokana na ununuzi wa silaha (Barani Ulaya) ulioambatana na madai ya kuwepo rushwa kwa viongozi wa ngazi za juu nchini humo. Yaani “vyombo vya dola ya Afrika Kusini vinazidi kugeuzwa kama viungo vya maiti anayeliwa na huyo (ibilisi wa wachache wenye kuendesha nchi kwa matakwa yao na ubinafsi)”.

Rushwa inazidi Afrika Kusini

Mnamo Julai 16, 2011, Chama kikuu cha wafanyakazi cha Afrika Kusini, kilionya kuwa rushwa nchini humo imezidi, na imefikia kiwango kikubwa cha kuweza hata kuigeuza nchi hiyo kuwa nchi isiyokuwa na nidhamu.

Msemaji wa Jumuiya ya wafanyakazi, COSATU, Patrick Cravan, alisema kuwa madai ya ufisadi na matumizi mabaya ya fedha za umma yanazidi kuongezeka nchini humo na kufikia kiwango cha kutisha. Wakati huohuo mashirika mengine, ambayo yanamuunga mkono Rais Jacob Zuma, yalipokea vema uamuzi wa serikali yake, wa kuanzisha uchunguzi kuhusu tuhuma mbalimbali za ufisadi ndani ya jeshi la polisi.

Msemaji huyo wa COSATU alisema kuwa suala hilo lazima lipewe uzito mkubwa na wakuu wa nchi: “Ikiwa hatuchukui hatua kali dhidi ya vitendo hivi, basi tutafikia hali ambapo wahalifu katika nchi hii wataweza kuiba mali ya taifa watakavyo, bila woga wala kufikishwa mahakamani.”

Rais Zuma awafukuza mawaziri wawili

Taarifa za hivi karibuni zinasema kuwa kutokana na kukithiri kwa rushwa Rais Jacob Zuma amechukua hatua ya kuwafukuza kazi mawaziri wawili, Waziri wa Serikali za Mitaa, Sicelo Shiceka, anayeshutumiwa kutumia fedha ambazo hazijaidhinishwa kisheria, na Waziri wa Kazi za Umma, Gwen Mahlangu-Nkabinde.

Rais huyo pia amemsimaisha kazi mkuu wa Jeshi la Polisi nchini humo, Jenerali Bheki Cele, ambaye pamoja na Bi Mahlangu-Nkabinde, wamehusishwa na madai ya kuuza majengo kinyume cha sheria. Viongozi wote watatu waliosimamishwa kazi wamekana kuhusika na kufanya jambo lolote kinyume cha sheria za nchi.

Mchunguzi maalum wa Afrika Kusini, aliyeteuliwa kuchunguza malalamiko dhidi ya maafisa hao wa serikali, alitoa wito kwa Rais Zuma kuwachukulia hatua kali. Lakini, Thuli Madonsela, mchunguzi maalum anayejulikana Afrika Kusini kama mwendesha mashtaka mkuu aligundua kuwa Shiceka alitumia zaidi ya dola za Marekani 68,000 (sawa na shilingi milioni 115 za Kitanzania) za serikali ya nchi hiyo kwa safari za kifahari na malipo ya hoteli bila idhini.

Gharama hizo ni pamoja na safari za kumtembelea mpenzi wake aliyekuwa amefungwa katika gereza moja nchini Switzerland kwa makosa ya kufanya magendo ya dawa za kulevya. Katika ripoti iliyotolewa mwezi uliopita, Bi Madonsela alisema kuwa vitendo vya Shiceka vilikuwa "kinyume cha sheria na matumizi mabaya ya madaraka, kukosa uaminifu kwa fedha za umma."

Alimshutumu pia kwa kusafiri nchi ya jirani ya Lesotho wakati akiwa likizo kutokana na kuumwa kwa gharama za walipa kodi wa nchi hiyo huku akitumia jina la uongo. Kwa wakati huo, Shiceka alikana madai hayo akisema "hayana msingi" na kuahidi kusafisha jina lake mahakamani. Alielezea kuwa baadhi ya gharama zake za hoteli ni kutokana na nyumba aliyopewa kuishi kutokana na wadhifa wake kujaa mbu.

Katika uchunguzi tofauti, Bi. Madonsela alibainisha kwamba Bi Mahlangu-Nkabinde na Jenerali Cele, mshirika mkuu wa Zuma, waliidhinisha mpango wa majengo yenye thamani ya mamilioni ya dola za Marekani kifisadi.

Rais Zuma alisema kuwa Jenerali Cele atasimamishwa kazi huku akilipwa mshahara wake wote, na uchunguzi ukiendelea dhidi yake. Rais huyo alisema kuwa uchunguzi huo utaongozwa na Jaji wa Mahakama ya Katiba, Yvonne Mokgoro.

Hata hivyo, Rais Zuma mwenyewe amewahi kukabiliwa na madai ya rushwa wakati alipokuwa makamu wa rais wa nchi hiyo, chini ya serikali ya Thabo Mbeki, lakini baadaye mashitaka dhidi yake yakatupiliwa mbali na mahakama. Sifa kubwa ya Rais Zuma ni kuaminika kwake kuwa msikilizaji zaidi wa matatizo ya masikini kuliko ilivyokuwa kwa rais aliyemtangulia, Thabo Mbeki, ambaye alikosolewa sana kutokana na kuhusudu zaidi biashara, sera za kiuchumi za kihafidhina – na kutumia mfumo wa kutoa maamuzi kutoka serikali kuu.

Baada ya kesi ya Zuma kufutwa na Mahakama Kuu katika mji wa Kusini-Mashariki wa Pietermaritzburg, alisafiri hadi Midrand, karibu na Johannesburg, ambako alipokelewa na wajumbe wa mkutano wa mwaka wa COSATU.

Lakini Jake Moloi, mtafiti mwandamizi katika Taasisi ya Mafunzo ya Usalama (ISS), yenye makao yake mjini Pretoria, alitoa taarifa yake ya kukumbusha kuwa matatizo ya kisheria ya makamu huyo wa rais wa zamani hayakuwa jambo la zamani.

"Ni mafanikio ya muda. Kuifuta kesi kutoka kwenye orodha ya mahakama kumeimarisha tu kibwagizo cha nyimbo za mashabiki wake," aliiambia IPS.

"Kwa upande wa Zuma, inaweza pia kuonekana kama tafu kubwa sana. Lakini bado wingu limetanda juu yake. Jaji mmoja tayari ameshamwelezea kama mwenye 'uhusiano wa rushwa' na mshauri wake wa zamani wa masuala ya fedha. Mtizamo huu una nafasi ya kubakia kwa muda mrefu," alisema Moloi.

Hata hivyo, uwezo wao wa kufuta madai ulitegemea nyaraka za dola zilizopatikana wakati wa upekuzi wa makazi ya Zuma na ofisi zake na mwanasheria wake – uhalali ambao ulipingwa mahakamani.

Kutokana na matokeo ya changamoto hizi, Jaji Herbert Msimang alitoa maamuzi kwamba waendesha mashitaka hawakutekeleza matakwa ya kisheria kwa wao kuonesha kuwa ushahidi muhimu ungepatikana hadi tarehe ya kuahirishwa kwa kesi hiyo.

Kwa upande wa kukosoa dola, alibainisha kuwa "uamuzi wa haraka" ulichukuliwa kumfungulia mashitaka Zuma, na pia kwamba "Utekelezaji wa uamuzi huo ulikuwa ni mwanzo wa mwisho… Hivyo kesi ya dola kuchechemea kutoka kwa janga moja hadi jingine."

Lakini, wakati uamuzi huo ulimwondoa Zuma kutoka kwenye mtego, bado haukuonesha mwisho wa mashitaka kumwandama katika siku zijazo: Waendesha mashitaka walitaka kumwingiza kwenye kitabu kuhusiana na jaribio la kutaka kupata rushwa ya mwaka ya dola za Marekani 70,000 kutoka kwa mshauri wake wa zamani wa masuala ya fedha, Schabir Shaik, kutoka kwa Kampuni ya silaha ya Kifaransa ya Thales – ili ailinde wakati wa mpango wa ununuzi wa silaha mwaka 1999.
Makala haya yameandaliwa na Bishop J. Hiluka kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya habari vya kimataifa.

Oct 19, 2011

EUGENE TERREBLANCHE: Athari za uhasama wa ubaguzi wa rangi zilichangia kifo chake

Eugene Terreblanche

VENTERSDORP,
Afrika Kusini

KESI inayowahusu wafanyakazi wa shambani wawili weusi, Chris Mahlangu, mwenye umri wa miaka 29 na kijana mmoja wa miaka 16 walioshtakiwa kwa kumpiga kiongozi wa Wazungu, Eugene Terreblanche, imeanza katika mahakama moja ya Afrika Kusini tangu wiki iliyopita ambapo wanakabiliwa na kesi ya mauaji na wizi.

Watu hao wawili walijisalimisha Polisi baada ya kukiri walikorofishana na muajiri wao kutokana na malipo. Mauaji hayo yaliyotokea mwaka 2010 yalionesha wazi uhasama wa ubaguzi wa rangi ambao bado upo Afrika Kusini, miaka 16 baada ya utawala wa wazungu wachache kumalizika.

Mara tu baada ya watu hao kukamatwa kulikuwa na mzozo kati ya Waafrika na Wazungu, wafuasi wa Terreblanche katika mji wa Kaskazini-Magharibi wa Ventersdorp, ambako ndiko kesi hii inakoendeshwa na imeshaahirishwa mara mbili.

Kwa mujibu wa taarifa, waandishi habari na familia ya Terreblanche wamekaa katika chumba kimoja na kufuatilia shughuli za mahakama kwa kutumia televisheni inayopitisha shughuli hizo moja kwa moja. Vyombo vya habari vimepigwa marufuku kuingia mahakamani kutokana na kuwa mmoja wa washtakiwa hao ni mtoto.

Historia yake

Eugène Ney Terre'Blanche alizaliwa 31 Januari 1941 na kufariki mnamo 3 Aprili 2010, alikuwa mwanachama wa zamani wa Chama cha Herstigte Nasionale nchini Afrika Kusini, ambaye alianzisha Weerstandsbeweging Afrikaner (AWB) wakati wa enzi ya ubaguzi wa rangi.

Katika miaka ya 1980 na miaka ya mwanzo ya 1990, alijulikana kwa kutishia uwepo wa vita vya wenyewe kwa wenyewe ili kudumisha utawala wa Wazungu wachache nchini Afrika Kusini. Baada ya nchi hiyo kuingia kwenye mpito wa demokrasia baada ya ubaguzi wa rangi, aliamsha upya misimamo yake na wito kwa wafuasi wake wa kushinikiza kuwepo kwa uhuru wa nchi huru ya Waafrikana, ambayo mara kwa mara aliitambulisha kama "Boerevolkstaat". Terre'Blanche aliongoza taasisi hiyo hadi kifo chake mwaka 2010.

Babu yake alipigana vita iliyoitwa “Waasi wa Rasi” kwa ajili ya Makaburu katika vita ya pili ya Makaburu, na baba yake alikuwa luteni kanali katika Jeshi la Afrika Kusini.

Babu yake ambaye aliitwa Terre'Blanche (jina lenye tafsiri ya 'ardhi ya weupe' au 'nchi ya weupe' kwa Kifaransa) aliyeitwa Estienne Terreblanche na alikuwa mkimbizi wa Kifaransa, kutoka jimbo la Toulon, ambaye aliwasili katika Rasi hiyo mwaka 1704, akikimbia mateso ya Waprotestanti nchini Ufaransa. Jina la Terreblanche kwa ujumla limebakia na herufi zake za awali ingawa wakati mwingine huandikwa Terre'Blanche, Terre Blanche, Terblanche au Terblans.
Alizaliwa eneo la mashambani katika mji wa Transvaal wa Ventersdorp, alihudhuria masomo katika shule za Laerskool Ventersdorp na Hoër Volkskool katika eneo la Potchefstroom, na kuingia Chuo Kikuu mwaka 1962. Wakati akiwa shule, alionesha tangu mwanzo mwelekeo wa mafunzo yake ya kisiasa kuanzisha taasisi ya kiutamaduni ya Jong Afrikanerharte (Moyo wa Waafrikana Vijana).
Alijiunga na Jeshi la Polisi la Afrika Kusini, na awali alitumikia katika eneo la Kusini Magharibi mwa Afrika (sasa Namibia), sehemu ambayo iliwekwa chini ya Afrika Kusini kwa mamlaka ya Umoja wa Mataifa baada ya Vita Kuu ya kwanza. Baada ya kurudi rasmi Afrika Kusini, alipanda na kuwa Afisa katika Kitengo Maalum, kilichoanzishwa na wajumbe wa Baraza la Mawaziri.
Kazi ya siasa

Siasa za Terre'Blanche zilitofautiana na sera za viongozi wakuu wa serikali ya weupe ya kibaguzi kwa kutaka kutambuliwa na kupewa ukuu jamii yake ya Waafrikana. Alisisitiza dhana ya Waafrikana/Makaburu kama jamii sawa ya kikabila pamoja na makabila ya asili ya Afrika Kusini. Pia alitaka uanzishwaji wa serikali ya Waafrikana ambayo itakuwa ikiongozwa na Waafrikana wenyewe katika eneo lote wanalolikalia.
Katika miaka ya 1960, Terre'Blanche alizidi kupinga kile alichokiita “sera huria” za BJ Vorster, aliyekuwa Waziri Mkuu wa Afrika Kusini. Baada ya miaka minne ya huduma katika SAP, alijiuzulu ili kujiingiza katika siasa, aligombea bila mafanikio nafasi katika ofisi za mitaa katika Heidelberg kama mjumbe wa Chama cha Nasionale.

Akiwa amechoshwa na njia iliyotumika katika ushiriki wa kisiasa, Terre'Blanche alianzisha Weerstandsbeweging Afrikaner ‘AWB’ (Vuguvugu la Waafrikana) katika eneo la Heidelberg mwaka 1973, awali ilikuwa ni chama cha siri. AWB kwanza ilionekana kwa umma baada ya wanachama wake kushtakiwa na kutozwa faini. Floors van Jaarsfeld, profesa wa historia ambaye alitoa hadharani maoni yake kwamba Siku ya Nadhiri (awali ikiitwa Siku ya Dingaan), siku ya mapumziko kwa ajili ya kumbukumbu ya ‘Vita ya Mto wa Damu’, haikuwa ni kitu zaidi ya tukio la kawaida na haina kumbukumbu yoyote halisi katika historia.

Ingawa Terre'Blanche baadaye alionesha majuto yake kuhusu tukio hilo alipokuwa akitoa ushahidi wake mbele ya Tume ya Ukweli na Maridhiano, alipendekeza kwamba imani yake kuhusiana na utakatifu wa Siku ya Nadhiri itafanya matendo yake yawe ya kueleweka zaidi. Katika miaka iliyofuata, hotuba ya Terre'Blanche katika mikusanyiko ya umma mara nyingi iliamsha vita ya Mto wa Damu, na ujuzi wake ulimwezesha sana kati ya mrengo wa kulia wa weupe nchini Afrika Kusini; AWB inadaiwa kuwa na wanachama 70,000 katika urefu wake.

Katika miaka ya 1980, Terre'Blanche aliendelea kujiwasilisha mwenyewe na AWB kama mbadala kwa wote, Chama cha National kinachoongoza serikali na Chama cha Conservative, na akabaki kambi inayopinga sera ya mageuzi ya PW Botha ya kuanzisha ziada, angalau tofauti kidogo, nafasi ya ubunge kwa ajili ya wasio wazungu, na haki ya kupiga kura kwa Chotara na Waafrika Kusini wenye asili ya India. Nguvu kubwa ya wafuasi ilipatikana katika jamii za vijijini ya Kaskazini ya Afrika Kusini, pamoja na wafuasi wachache katika maeneo ya mijini ambapo kwa kiasi kikubwa alizifuatilia za jamii ya Waafrikana wa kipato cha kati na chini.

Terre'Blanche aliona kuwa mwisho wa ubaguzi wa rangi ni kama kujisalimisha kwa Ukomunisti, na kutishia kuanzisha vita kamili vya wenyewe kwa wenyewe kama Rais FW de Klerk atakabidhi madaraka kwa Nelson Mandela na African National Congress. Wakati De Klerk akishughulikia mkutano katika mji wa Terre'Blanche wa Ventersdorp mwaka 1991, Terre'Blanche aliongoza maandamano, na mapambano ya Ventersdorp yalitokea baina ya AWB na polisi, na watu kadhaa kuuawa. Terre'Blanche alidai kuwa ni wakati tu aliposimama kati ya polisi na AWB na kudai kusitishwa mapigano ndipo vurugu zilipomalizika.

Machi 2008, AWB ilitangaza kurejesha upya chama cha siasa, akitoa mfano wa faraja ya umma. Sababu za kurudi zilihusishwa hasa kutokana na mashambulizi dhidi ya wakulima na biashara za jamii ya Makaburu, matatizo ya umeme, rushwa katika idara za serikali na uhalifu mkubwa. Aprili 2008, Terre'Blanche alikuwa msemaji katika mikutano kadhaa ya kampeni ya AWB, iliyojumuisha Vryburg, Middelburg, Mpumalanga na Pretoria.

Alikuwa akitoa wito wa “Jamhuri huru ya Waafrikana”, na aliapa kupeleka kampeni yake kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Umoja wa Mataifa mjini The Hague katika jitihada za kupata alichohitaji. Alitetea ardhi kubwa iliyonunuliwa kutoka kwa kabila la Swaziland katika sehemu ya Mashariki ya Jamhuri ya Afrika ya Kusini, kutoka Kaskazini mwa Wazulu Natal, na sehemu nyingine ambayo imekuwa makazi ya Voortrekkers. Juni 2008, ilitangazwa kuwa tawi la vijana wa AWB litazinduliwa na Terre'Blanche kama mwanzilishi wake.
Septemba 2009 alihutubia mkutano wa siku 3 uliohudhuriwa na Waafrikana 300 waliokuwa na lengo la kuendeleza mkakati wa “Ukombozi wa makaburu”.

Tarehe 17 Juni 2001, Terre'Blanche alihukumiwa kifungo cha miaka sita gerezani, ambapo alitumikia miaka mitatu, kwa kumshambulia mfanyakazi wa kituo cha petroli na jaribio la mauaji ya askari wa usalama mwaka 1996. Alikanusha madai yote na alisisitiza kuwa hana hatia. Wakati alipokuwa gerezani, mmoja wa wazungu watatu waliokuwa gerezani Rooigrond karibu Mafikeng, alidai kuwa Mkristo aliyezaliwa mara ya pili.

Terre'Blanche was released on 11 June 2004 [ 46 ] and the AWB website claims these court cases and other scandals involving him were fabricated by the "Black Government and the left wing media". [ 12 ] Terre'Blanche alitolewa tarehe 11 Juni 2004 na tovuti ya AWB ilidai kuwa kesi hizi na kashfa nyingine zilizomshirikisha zilikuwa za kutungwa na “Serikali ya Weusi na vyombo vya habari vya mrengo wa kushoto.”

Tarehe 3 Aprili 2010, alipigwa na kukatwakatwa hadi kufa katika shamba lake na wafanyakazi wawili, kutokana na madai ya mshahara. Wafuasi wa Terre'Blanche wanasema kwamba mauaji hayo ni sehemu ya mkakati mkubwa wa kupambana na weupe “mauaji ya shamba” nchini Afrika Kusini.

Makala haya yameandaliwa na Bishop Hiluka kwa msaada wa mashirika mbalimbali ya habari ya kimataifa.

Oct 12, 2011

Uchaguzi wa Igunga na haja ya Katiba mpya, Tume huru

 Mbunge mteule wa Igunga, Dk. Kafumu akipongezwa

 Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya uchaguzi,
Rajabu Kiravu

BISHOP J. HILUKA
Dar es Salaam

UCHAGUZI mdogo wa hivi karibuni katika jimbo la Igunga, ambapo mgombea ubunge wa Chama Cha Mapinduzi, CCM, Dk. Dalaly Peter Kafumu, ameibuka mshindi wa kinyang’anyiro hicho umeendelea kuonesha kuwa mazingira ya uchaguzi hapa nchini bado si shirikishi kwa vyama visivyoshika dola, na kwamba vyama vya upinzani vilivyoshiriki uchaguzi huo na chaguzi nyingine, vinaingia kwenye uchaguzi kwa hofu tu ya kumsusia nguruwe shamba na wala sio kushinda, ingawa kwa baadhi ya vyama kama Chadema au CUF vilionesha kuwa na nafasi nzuri ya kushinda.

Uchaguzi wa Igunga ambao kwa kiasi kikubwa ulitawaliwa na vitisho na fujo huku viongozi wengine wakipanda jukwaani na bastola, umeendelea kuonesha kuwepo mapungufu mbalimbali katika mfumo mzima wa namna tunavyoendesha chaguzi zetu, hasa tangu tulipoingia kwenye mfumo wa vyama vingi mwaka 1992.

Mfumo unaotumika sasa kuendesha uchaguzi umekuwa ukilalamikiwa sana na vyama vya upinzani hasa uwepo wa wasimamizi wote wa uchaguzi, tangu mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), mpaka wasimamizi wa majimbo na kata ni watumishi wa serikali ama wateule wa rais ambaye wakati huohuo yeye mwenyewe na chama chake wanashiriki katika uchaguzi huo. Ndiyo maana, kwa mfano, kwenye uchaguzi wa Igunga watendaji wa vijiji wametuhumiwa kugawa mahindi kuwashawishi wapiga kura wamchague mgombea wa chama tawala, na tuhuma za ununuzi wa shahada.

Hapa naomba ieleweke kuwa siandiki makala hii kwa kuwa labda ninashabikia chama fulani hasha, mimi si mmoja wa wale ambao hudhani kuwa ili demokrasia ionekane imefanya kazi basi ni lazima chama cha upinzani kishinde. Nimeamua kuandika haya kutokana na mazingira ya chaguzi zetu (ambayo hayafichiki) tangu tulipoanza mfumo huu wa vyama vingi ambapo imekuwa ikionekana dhahiri kuwa chama tawala kimekuwa kikibebwa.

Mazingira haya ndiyo yanayosababisha watu wengi kukata tamaa na ndiyo sababu ya walio wengi kutokwenda kupiga kura, hasa pale wanapohisi kuwa mtu watakayemchagua (ambaye hatokani na chama tawala) hatapita kwa kuwa matokeo yatachakachuliwa, ingawa ukiangalia kwa undani utagundua kuwepo pia sababu nyingine inayowakatisha tamaa, kama kampeni za uchaguzi kutawaliwa na vitisho vya kila aina kwa washiriki wa uchaguzi na viongozi wa siasa.
Mfano hadi uchaguzi wa tatu tangu kuanza mfumo wa vyama vingi mwaka 2005, wananchi walio wengi walionekana kuwa bado wana imani na mfumo, lakini mwaka jana ikawa tofauti kabisa ambapo walionesha jinsi walivyokatishwa tamaa na mfumo uliopo, hasa serikali ya awamu ya nne.

Katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana ambao ni wa nne tangu mfumo wa vyama vingi, idadi ya wapiga kura ilipungua sana katika kiwango cha kushangaza mno, kwani hesabu za waliojiandikisha unapolinganisha na waliojitokeza kupiga kura, inaonekana kuna tatizo kubwa katika mfumo wetu ambalo linahitaji ufumbuzi wa haraka. Ufumbuzi huo si mwingine bali Katiba mpya na Tume huru ya uchaguzi.

Serikali ya awamu ya nne iliingia baada ya uchaguzi wa mwaka 2005, wananchi waliojiandikisha kupiga kura wakati huo walikuwa 16,407,318 na waliopiga kura walikuwa 11,365,477 ambao ni takriban asilimia 70 ya watu waliojiandikisha.

Lakini mwaka jana, kwa mujibu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), ni watu 20,137,303 waliojiandikisha lakini waliopiga kura ni 8,398,394 tu ambao ni sawa na asilimia 42.64 tu ya watu wote waliostahili kupiga kura!

Kwa hali hii ni kwamba imani ya watu kwa serikali iliyopo madarakani imepungua mno, na hili si jambo la kishabiki kwani hata ukiangalia katika chaguzi zilizotangulia kabla na baada ya mfumo wa vyama vingi utagundua kuwa wananchi wengi walikuwa na imani na serikali yao. Mwaka 1965 waliopiga kura walikuwa asilimia 77.1 ya walioandikishwa. Mwaka 1970 walikuwa asilimia 72.2, mwaka 1975 asilimia 81.7. Mwaka 1980 asilimia 75, mwaka 1985 asilimia 75 na 1990 walikuwa asilimia 74.4.

Baada ya kuingia mfumo wa vyama vingi mwaka 1992 na uchaguzi wa kwanza katika mfumo wa vyama vingi mwaka 1995, waliopiga kura walikuwa asilimia 76.7 ya waliojiandikisha, mwaka 2000 waliongezeka na kuwa asilimia 84.4, ambapo mwaka 2005 walipungua kidogo na kuwa asilimia 72.4.

Tatizo lilizidi mwaka 2010 kutokana na mfumo tulionao ambapo ni asilimia 42.64 tu ya waliojiandikisha ndiyo waliopiga kura. Na hapa panaonekana kuwepo tatizo kubwa ambalo linapaswa kuangaliwa kwa umakini sana bila ushabiki.

Hali hii imedhihirika hata katika uchaguzi mdogo wa Igunga kwa idadi ndogo ya watu walijitokeza kupiga kura, ambapo ni watu 53,672 tu ambao ni sawa na asilimia 31.3 tu ya watu 171,019 waliojiandikisha ndiyo waliopiga kura.

Katika chaguzi zote zilizotangulia kabla ya 2010 hatujawahi kuwa chini ya asilimia 70 ya wapiga kura waliojiandikisha. Je, kwa nini sasa hali hii inajitokeza tena kwa kiwango cha chini mno? Sababu hasa ni nini?

Je, si kweli kwamba mfumo uliopo ndiyo chanzo cha idadi ya watu wanaopaswa kupiga kura kupungua? Je, kwa nini serikali ambayo mwaka 2005 ilionekana kukubalika mno kwa kupata kura zaidi ya milioni 9, miaka mitano tu katika uchaguzi uliofuata ikaambulia kura milioni 5 tu ambazo ni tofauti ya kura takriban milioni nne wakati idadi ya waliojiandikisha kupiga kura ikiwa imeongezeka? Kwa kweli hili siyo jambo la kujivunia kabisa.


PEDRO VERONA PIRES: Kaachia madaraka Agosti na kanyakua tuzo Oktoba

 Pedro Rodriguez Pires

PRAIA
Cape Verde

KAMATI ya taasisi ya Mo Ibrahim mjini London imemtangaza aliyekuwa rais wa Cape Verde, Pedro Rodriguez Pires, kuwa mshindi wa tuzo ya utawala bora, kutokana na mafanikio yake katika kuleta demokrasia, uimara na neema katika visiwa hivyo.

Kamati hiyo imesema katika tangazo lake mwanzoni mwa wiki hii mjini London kwamba, katika uongozi wa Pedro Pires wa miaka 10 katika visiwa vya Cape Verde (Rasi ya Verde), kwenye pwani ya Magharibi mwa Afrika, Pedro Verona Pires, aliweka msingi wa kuwaondoa wananchi wake 200,000 kutoka kwenye umasikini.

Kutokana na utawala wake bora, Pires alitambulika duniani kwa sera zake za kutekeleza haki za binadamu. Kamati hiyo ya Mo Ibrahim inayoshughulikia zawadi hiyo ilisema kuwa Pires, aliyeachia madaraka mwezi Agosti, amesaidia sana kuifanya nchi hiyo kuwa "yenye demokrasia, utulivu na kustawi zaidi".

Tuzo hiyo inatakaiwa kutolewa kila mwaka kwa kiongozi anayechaguliwa kidemokrasia na kuondoka madarakani kwa hiari. Lakini hapajakuwa na mshindi kwa miaka miwili iliyopita, na kamati hiyo ilisema kuwa hakukuwa na mgombea aliyestahili kupokea tuzo hiyo katika kipindi hicho.

Tuzo hiyo ya dola za Marekani milioni tano, inayotolewa kwa zaidi ya miaka 10, ni zawadi yenye thamani kubwa duniani inayotolewa kwa mtu binafsi. Washindi wa awali wa tuzo hiyo ni aliyekuwa rais wa Botswana, Festus Mogae na wa Msumbiji, Joaquim Chissano.

Kabla ya kumpa tuzo hiyo wanakamati wa Mo Ibrahim wametilia maanani kwamba Rais huyo mstaafu, Pedro Rodriguez Pires, alilikataa wazo la kuibadilisha katiba ili kumwezesha kugombea urais tena. Mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 77 ameutumia muda wa miaka 50 wa maisha yake katika shughuli za kisiasa.

Rais huyo mstaafu aliuweka msingi uliokigeuza kisiwa chake cha Cape Verde kuwa na mfano wa demokrasia, uimara wa kisiasa na neema. Katika maelezo yaliyotolewa mjini London na Kamati ya Mo Ibrahim wanakamati wametilia maanani kwamba kisiwa cha Rasi ya Verde ni mfano wa mafanikio ya kiuchumi, kijamii na kisiasa barani Afrika.

Pedro aliyatetea maadili ya ubinadamu kama alivyosema baada ya kutangazwa mshindi wa Tuzo ya Mo Ibrahim, katika harakati zake za kisiasa alikuwa na kaulimbiu ya maneno matatu - Kazi, Ukweli na Utiifu".

Historia ya Pires

Pedro Pires Verona Rodrigues alizaliwa Aprili 29, 1934, katika kisiwa cha Cape Verde na alisoma kwenye shule ya msingi na ya sekondari katika kisiwa hicho kabla ya kwenda kwenye Chuo Kikuu cha Lisbon nchini Ureno mnamo mwaka 1956. Lakini kabla ya kuhitimu shahada yake, aliitwa ili kulitumikia jeshi la Ureno kama afisa wa kikosi cha anga.

Lakini mnamo mwaka 1961 pamoja na vijana wengine wa Kiafrika aliondoka Ureno kimya kimya, na kujiunga na chama cha ukombozi wa Guinea na Cape Verde, PAIGC kilichokuwa kinaongozwa na Amilcar Cabral mpigania uhuru jarabati.

Alifanya bidii ya kuwahamasisha vijana wa nchi yake kwa ajili ya harakati za ukombozi. Mnamo mwaka 1974 Pires aliuongoza ujumbe wa chama chake cha PAIGC kwenye mazungumzo na serikali ya Ureno juu ya kuleta uhuru wa Cape Verde. Na tarehe 5 ya mwezi wa Julai mwaka 1975 Cape Verde alitangaza uhuru wake.

Hata hivyo Pires amekuwa Rais wa Cape Verde kuanzia Machi 2001 hadi Septemba 2011. Kabla ya kuwa Rais, alikuwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo kuanzia 1975 na aliutumikia wadhifa huo kwa muda wa miaka 16 hadi 1991, kabla ya kuwa Rais mwaka 2001.

Baadaye mwaka huohuo wa 1991 aliamua kugombea katika uchaguzi uliofanyika kwa mara ya kwanza katika kisiwa chake cha Cape Verde kwa njia za kidemokrasia, baada ya chama tawala cha African Party for the Independence of Cape Verde (PAICV) kuamua kuruhusu demokrasia ya vyama vingi mnamo Februari 1990, lakini alishindwa.

Mwaka mmoja kabla mnamo 1990, Pires alikuwa amechukua nafasi ya Rais Aristides Pereira kama Katibu Mkuu wa PAICV mwezi Agosti 1990. Hata hivyo, katika wakati huu chama chake cha PAICV kilipoteza nafasi katika uchaguzi wa vyama vingi wa rais na wabunge uliofanyika mapema mwaka 1991 na Pedro akabaki kuwa mpinzani.

Katika mkutano wa chama mnamo Agosti 1993, nafasi ya Katibu Mkuu iliyokuwa ikishikiliwa na Pires ilichukuliwa na Aristides Lima, baada ya yeye kuchaguliwa kuwa Rais wa chama. Kama mgombea aliyepitishwa na chama kwa nafasi ya urais mnamo Septemba 1997, kwenye mkutano wa chama, alikabiliwa na José Maria Neves na kumshinda kwa asilimia 68 ya kura. Aliamua kujiuzulu nafasi ya urais wa PAICV mwaka 2000 katika maandalizi yake kwa ajili ya uchaguzi wa urais katika mwaka uliokuwa ukifuata na alikuwa akikabiliwa na Neves. Alitangaza rasmi nia yake ya kugombea urais wa Cape Verde tarehe 5 Septemba, 2000.

Pires alikuwa mgombea kupitia PAICV katika uchaguzi wa rais wa Februari 2001, akimshinda Waziri Mkuu wa zamani, Carlos Veiga, wa Movement for Democracy (MpD) katika raundi ya pili kwa kura 17 tu. Pires alichukua madaraka mnamo Machi 22; chama cha MpD kiligomea uzinduzi wake, kikisema kuwa uchaguzi ulikuwa umefunikwa na "mchakato usiokuwa wa uwazi".

Baada ya kuwa Rais, Pires alimteua Neves kuwa Waziri Mkuu. Aligombea tena katika awamu ya pili katika uchaguzi wa rais uliofanyika tarehe 12 Februari 2006 na kumshinda tena Veiga, safari hii alishinda katika raundi ya kwanza tu kwa kiwango cha asilimia 51 kwa asilimia 49 alizopata mpinzani wake.

Mwezi Mei mwaka 2008, alitoa tahadhari kuwa kulikuwa na safari ndefu katika kuundwa kwa Umoja wa Mataifa ya Afrika, yeye akipendekeza kwamba ushirikiano wa kikanda utangulizwe kabla ya muungano wa bara nzima. Alihudhuria Mkutano wa Kimataifa wa Tokyo wa Maendeleo ya Afrika (TICAD-IV) kwa wakati huu.

Nchi ya Cape Verde

Cape Verde ni nchi ya visiwa katika Bahari ya Atlantiki mbele ya pwani ya Afrika ya Magharibi. Umbali wake na Senegal ni kilomita 460. Eneo la visiwa vyake 15 (funguvisiwa) lina ukubwa wa kilomita za mraba 4,033.

Mji mkuu wa nchi hiyo ni Praia uliopo katika kisiwa cha Santiago. Visiwa vyake vinavyounda nchi ya Cape Verde vipo jumla ya visiwa 15 ambavyo vipo katika vikundi viwili:
  • Visiwa "juu ya upepo" (Barlavento): Santo Antao, Sao Vicente, Sao Nicolau, Sal, Boa Vista na visiwa visivyokaliwa na watu vya Santa Luzia, Branco na Razo.
  • Visiwa "chini ya upepo" (Sotavento) ni pamoja na Maio, Santiago, Fogo, Brava na visiwa visivyo na watu vya Ilheus Secos ou do Rombo.

Miji mikubwa zaidi ni (sensa ya mwaka 2005): Praia (wakazi 113,364), Mindelo (wakazi 70,611), Santa Maria (wakazi 17,231), Pedra Badejo (wakazi 9,488) na Sao Filipe (wakazi 8,189).

Hadi kufika kwa Wareno funguvisiwa vya Cape Verde havikuwa na watu. Wareno walianzisha mashamba ya miwa na kuleta watumwa kutoka bara la Afrika. Cape Verde ilikuwa pia kituo muhimu cha biashara ya watumwa kati ya Afrika na Amerika. Wahamiaji kutoka Ulaya walikuwa pamoja na Wayahudi Wareno waliokataliwa kukaa kwao Ureno. Idadi kubwa ya wakazi wa visiwa hivi ni chotara kati ya Waafrika na Wareno.

Makala haya yameandaliwa na Bishop Hiluka kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya habari vya kimataifa.

Oct 7, 2011

DK. GUY SCOTT: Mzungu wa Zambia na msomi aliyeukwaa umakamu wa Rais

 Dk. Guy Scott

LUSAKA
Zambia

RAIS wa Zambia, Michael Sata, amefanya kile ambacho mtu yeyote mpenda maendeleo anapaswa kukiunga mkono, hasa pale alipoteua mawaziri sita katika baraza lake la mawaziri wenye sifa bila kujali itikadi zao, wanaotoka chama kilichokuwa kikitawala cha MMD ambacho ni chama pinzani kwa sasa. Kadhalika amempa cheo cha umakamu wa Rais kada wa chama chake cha Patriotic Front (PF), Dk. Guy Scott, mwenye asili ya Uingereza.

Hakika Rais Sata ametoa funzo kubwa kwa wanaodhani kuwa Ikulu ni ya wateule fulani tu na kwamba, haiwezekani hata siku moja watu wengine kuingia au kufanya kazi na watu wenye itikadi tofauti na wao, kuwa sasa inawezekana.

Mawaziri hao kutoka MMD ni pamoja na E. C. Lungu, aliyeteuliwa kuwa Naibu Waziri katika ofisi ya Makamu wa Rais, S.S Zulu aliyeteuliwa kuwa Waziri wa Sheria, G. B. Mwamba, anayekuwa Waziri wa Ulinzi na A. B. Chikwanda, Waziri wa Fedha.

Wengine ni C. Kambwili, aliyeteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na K. Sakeni aliyeteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani. Baraza hilo lilitangazwa siku 63 toka baraza lililopita kuvunjwa na rais wa zamani, Rupia Banda, alipotangaza tarehe ya uchaguzi mkuu.

Historia ya Scott

Dk. Guy Scott amezaliwa 1 Juni 1944, katika eneo la Livingstone. Amepata elimu yake katika eneo la Rhodesia ya Kusini (sasa Zimbabwe) na Uingereza katika Chuo Kikuu cha Cambridge na Chuo Kikuu cha Sussex, ambako alipata shahada ya uchumi na PhD katika utambuzi sayansi.

Dk. Scott ni mwanasiasa wa Zambia ambaye ameoa na anaishi jijini Lusaka.

Mafanikio katika taaluma
Baada ya kufuzu katika Chuo Kikuu cha Cambridge mwaka 1965, alijiunga na serikali ya Jamhuri ya Zambia ambapo aliajiriwa katika Wizara ya Fedha kama afisa mipango. Pia alikuwa naibu mhariri wa Biashara na Uchumi wa Afrika Mashariki na Kati katika kipindi hiki.
Mwaka 1970, Scott aliacha kazi ya serikali na kuwa mjasiriamali ambapo alianzisha mashamba, mradi wa kilimo cha biashara, ambayo aliwekeza katika mazao ya thamani kubwa kama vile umwagiliaji wa ngano, stroberi, na aina mbalimbali ya mboga mboga za msimu.

Mwaka 1978, alishiriki katika kuanzisha kampuni ya Mpongwe Development pamoja na Shirika la Maendeleo ya Jumuiya ya Madola. Baada ya hapo aliendelea kushiriki katika kutoa elimu na utafiti katika Chuo Kikuu cha Oxford katika miaka ya 1980.

Kazi ya siasa

Mwaka 1990, Scott alijiunga na kazi ya siasa kwa kujiunga na chama cha Movement for Multi-Party Democracy (MMD), ambapo alichaguliwa kutumikia nafasi ya Mwenyekiti wa kamati ya kilimo katika mkataba wa kwanza. Ushiriki wake katika siasa za Zambia ulitokana na marehemu baba yake ambaye alikuwa mshirika wa uanzishwaji wa taifa la Zambia na mwanzilishi wa magazeti yaliyopinga serikali ya kikoloni ikiwa ni pamoja na African Mail, ambalo sasa linajulikana kama Zambia Daily Mail. Katika miaka ya 1950, baba yake alikuwa mbunge wa kujitegemea wa shirikisho kupitia jimbo la Lusaka.

Scott aliteuliwa kuwa mgombea wa MMD wa jimbo la Mpika katika Bunge wakati wa uchaguzi mkuu wa 1991. Alichaguliwa na baadaye kuteuliwa kuwa Waziri wa Kilimo, Chakula na Uvuvi. Alifanya mageuzi kadhaa ya sera na alikuwa na jukumu la kusimamia hali ya maendeleo ya chakula baada ya "ukame wa karne" kati ya Januari na Februari 1992. Hakukuwa na hifadhi ya mahindi nchini Zambia wala kusini mwa Afrika, hivyo alikuwa na mipango ya dharura ya kuagiza kutoka nje ya nchi na kuyaleta Zambia kupitia reli na barabara.

Mwaka 1996, alijitoa MMD na kuunda chama cha Lima pamoja na Ben Kapita, aliyekuwa rais wa ZNFU. Aliandaa mpango wa muungano kati ya Chama cha Lima na vyama vingine ikiwa ni pamoja na ZADECO cha Dean Mungomba na kuunda ZAP.

Hata hivyo, baadaye alijitoa ZAP na kuelekeza nguvu zake kwenye kampuni yake ya ushauri wa kilimo. Mwaka 2001, alijiunga na Patriotic Front na kurejea kwenye siasa. Alirejea Bungeni alipochaguliwa kuwa mbunge wa Lusaka Kati katika uchaguzi mkuu wa 2006. Guy Scott pia alipanda hadi nafasi ya Makamu wa Rais wa Patriotic Front.

Na baada ya uchaguzi wa rais wa Zambia uliofanyika tarehe 20 Septemba 2011, na matokeo ya mwisho yaliyotolewa tarehe 23 Septemba kuonesha mgombea wa Patriotic Front, Michael Sata, kushinda kwa asilimia 43 ya kura dhidi ya asilimia 36 alizopata mgombea wa MMD na rais aliyemaliza muda wake, Rupiah Banda, Scott Guy aliapishwa kuwa Makamu wa Rais mnamo 29 Septemba 2011.

Makala imeandaliwa na Bishop Hiluka kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya habari vya kimataifa.


HERMAN KOJO: Mjasiriamali wa Ghana anayefananishwa na Bill Gates

 Herman Kojo Chinery-Hesse

ACCRA
Ghana

MFANYABIASHARA wa Ghana, Herman Kojo Chinery-Hesse, hujulikana kama Bill Gates wa Ghana, na amekuwa wa kwanza kutajwa katika mfululizo maalum wa vipindi vya shirika la utangazaji la Uingereza la BBC kama ndoto ya Afrika inayoangaza kati ya wajasiriamali wa bara hilo.
Kampuni ambayo Chinery-Hesse aliibuni kwa ushirika miongo miwili iliyopita, SOFTtribe Limited, huenda ikawa haijajitanua duniani kama ile kampuni ya Microsoft lakini imeimarika na kuwa mojawapo wa mashirika makubwa ya programu za kompyuta katika Afrika ya Magharibi.

Chinery-Hesse alisamehe fursa ya kujiendeleza kimaisha nchini Marekani alikosoma au Uingereza ambako aliwahi kufanya kazi kwa miaka michache, na badala yake kuamua kuanzisha biashara nchini Ghana.

Alianza kuandika programu za kompyuta chumbani alikolala katika nyumba ya wazazi wake katika wakati ambapo sio watu wengi walitambua umuhimu wa mapinduzi ya kompyuta barani Afrika.

Kampuni yake hatimaye ikaanza kuunda programu za kompyuta za uongozi wa biashara na sasa ina zaidi ya wateja 250, yakiwemo mashirika kadhaa ya kimataifa kama vile Ford Foundation, Nestle, na Unilever. SOFTtribe Limited pia ni mshirika wa maendeleo wa kampuni ya Microsoft katika kanda.

"Imekuwa kama burudani. Si rahisi kusema haiwezekani. Sidhani kuwa mimi ni mtu mwenye kipaji. Nadhani mtu yeyote anaweza kufanya hayo awe makini na awe tayari kusubiri miaka. Mbinu niliyotumia ni kwamba nilijihusisha katika biashara nikiwa sitarajii kuwa tajiri katika kipindi cha miaka 2," Chinery-Hesse aliliambia shirika la BBC.

"Wakati fulani kwa kipindi cha miezi sita kampuni yetu haikupokea hundi zozote na ilitulazimu kugawana kiasi kidogo cha pesa tulizokuwa nazo. Kulikuwa na nyakati ambapo hatukuwa na fedha zozote kulipa mishahara wakati tulipokuwa na madeni."

Kwa maoni yake miongoni mwa vitu viwili muhimu katika biashara ni ustahamilivu na uaminifu.
"Katika biashara yoyote; lazima uamini kwamba inanufaisha kote kote. Mtu anayenunua lazima anufaike na wewe pia lazima unufaike, la sivyo haitaendelea."

Hapana shaka mojawapo ya sababu za kufanikiwa kampuni yake ni kwamba kuanzia mapema sana aliamua kubuni programu ya kompyuta ambayo imetengenezwa mahsusi kwa mazingira ya bara la Afrika.
"Nadhani kuna fursa kubwa sana barani Afrika, hali ya umasikini mkubwa, kuna mengi ambayo hayakufanywa; lakini hii si sayansi ngumu, ukiwa na nidhamu usiogope kujitosa," Chinery-Hesse anawaambia wengine wanaozingatia kuwa wajasiriamali.

"Inawezekana, na nadhani ingewapasa watu wengine kufanya hivyo, na kama hatutajichukulia hatua, basi wageni watakuja Afrika kama tunavyoona na watafanya wakitakacho."

Makala hii imeandaliwa na Bishop Hiluka kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya habari