Nov 30, 2011

KATIBA MPYA Wakati muafaka kuliangalia suala la walemavu kwa mapana zaidi

 walemavu hawahitaji hisani bali wanahitaji fursa

BISHOP HILUKA
Dar es Salaam

TAKWIMU za Shirika la Afya la Dunia (WHO) zinaonesha kuwa angalau asilimia 10 ya watu wote duniani wana ulemavu wa aina fulani. Kuna aina nyingi za ulemavu, ikiwa ni pamoja na ule wa Kimwili (Physical Disability), Kiakili (Mental Disability), Ulemavu wa ngozi (Albino), Uziwi, Wasioona na kadhalika.

Ulemavu unaweza kumpata mtu kwa kuzaliwa au katika maisha kwa ajali au ugonjwa. Leo hii mtu yoyote mzima anaweza kupata ulemavu wakati wowote kwa ajali au ugonjwa! Kuwa mzima ni bahati tu – hakuna anayeweza kukwepa jambo hili!

Ingawa Katiba tuliyonayo inasema wazi kuwa ni wajibu wa Serikali kuwahudumia watu wenye mahitaji maalumu kama walemavu na wazee - kwa maana kwamba huduma kwao ni wajibu na siyo msaada - lakini hali imekuwa tofauti kabisa, kwani mara nyingi walemavu huwa wanapata huduma toka Mashirika ya dini na vyama vyao vya hiari vya kutetea haki zao, huku serikali ikionekana kuyaachia mashirika hayo ya dini jukumu hili muhimu.

Hata ukitaka kuangalia kwa undani kuhusu tafsiri sahihi ya Mlemavu, utagundua kuwa tayari imeshapindishwa na kupunguzwa (sijui kwa maslahi ya nani) kuwa zaidi suala la fursa finyu ya kupata ajira pekee, badala ya kuliangalia suala hili katika uwanja mzima wa maisha kwa ujumla kama ilivyo katika maana halisi ya ulemavu.

Kwa kuwa tafsiri halisi ya Mlemavu imepindishwa, basi hata sera, mikakati na hata utekelezaji wake navyo vimekuwa hivyo hivyo, jambo ambalo si haki na hatuwasaidii watu wenye ulemavu japo kwenye katiba yetu inatamkwa hivyo.

Kwa mujibu wa 'tafsiri halisi' ya neno ulemavu, hata tunaojidhani si walemavu bado twaweza walemavu, japo si walemavu wa viungo, ubongo wala wa ngozi, lakini tutakuwa walemavu katika namna nyingine: Walemavu wa Kisiasa (Political Disability). Wakati tukifikiria kuanza mchakato wa kujadili katiba mpya tunapaswa kwanza kujivua ulemavu huu wa kisiasa ‘Political Disability’ ndipo tuweze kuchangia maoni yetu katika katiba mpya ili kuwasaidia wenzetu wenye mahitaji maalum.

Huu ni muda muafaka wa kuachana na dhana potofu kwamba ulemavu ni ugonjwa; hii inatokana na Serikali ya Tanzania kuratibu huduma za walemavu kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii. Nimekuwa najiuliza swali hili bila majibu; kwa nini Wizara ya Afya?

Kwa nini masuala ya walemavu tumeamua kuyaweka Wizara ya Afya, hii ni sawa na kuchukulia kuwa Walemavu ni watu wagonjwa wanaohitaji matibabu! Uratibu wa huduma za walemavu kabla ya kupelekwa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, walihudumiwa na Wizara ya Kazi, Vijana na Michezo.

Nadhani mtizamo wetu katika suala hili unaangukia kwenye ile jinsi ya “Medical model” katika kuuangalia ulemavu. Mtizamo huu unaoangalia ulemavu kama ugonjwa, na walemavu kama watu wanaohitaji matibabu ili waweze kupona pamoja na kusaidiwa, ni mtizamo uliopotoshwa sana. Tunasahau kuwa walemavu hawahitaji hisani bali wanahitaji fursa (opportunity) ili waweze kujikwamua, na ieleweke kuwa wengine wao ni wazuri katika kazi kuliko hata sisi watu wazima.

Nadhani si vibaya wakati tukijadili Katiba mpya tukaangalia mifano ya Afrika Kusini ambao wameweka Kurugenzi (Directorate) ya watu wenye ulemavu chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais, na Malawi ambao wana Waziri anayeshughulikia masuala ya Walemavu. Kwetu sisi si vibaya kama masuala ya walemavu tutaamua kuyaweka chini ya ofisi ya Raisi, Makamu wa Rais au Ofisi ya Waziri Mkuu.

Katika katiba mpya tuwe na sera zitakazoweka mikakati madhubuti ya kuwajali walemavu kwani suala la ulemavu ni suala mtambuka linalohusisha kila Wizara. Hapa panahitaji zaidi utashi wa kisiasa. Tujaribu kufikiria kuingiza katika Katiba sheria itakayozitaka Wizara zote kuwa na 'Disability desk'. Kama imewezekana kwenye suala la 'Jenda' kwa nini isiwezekane kwa watu wenye ulemavu?
Naomba kutoa hoja...

ETIENNE TSHISEKEDI: Mwanasiasa mwenye matatizo ya kiafya wa DRC asiyechuja

 Etienne Tshisekedi wa Mulumba

KINSHASA
Congo

UPIGAJI kura katika uchaguzi mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), ulifanyika mapema wiki hii. Uchaguzi huo wa rais na wabunge ni wa pili kufanyika nchini humo baada ya kumalizika kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe miaka minane iliyopita.

Hata hivyo muda wa upigaji kura uliongezwa na kuingia siku ya pili katika baadhi ya maeneo sehemu ambazo upigaji huo haukufanyika siku ya Jumatatu. Maafisa wa uchaguzi walisema kuongeza muda huo kuliathiri takriban watu 400 katika nchi hiyo kubwa yenye vituo vya kupigia kura 63,000.

Mbali na hatua hiyo kuchukua muda mrefu, upigaji kura huo uligubikwa na vurugu huku vituo vya kupigia kura vikishambuliwa na watu wenye silaha na wapiga kura wenye hasira. Ni uchaguzi wa pili tangu kumalizika kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe miaka minane iliyopita, ambapo watu milioni nne walifariki dunia.

Wote wawili rais Joseph Kabila, mwenye umri wa miaka, 40, ambaye amekuwa madarakani kwa miaka 10, na kiongozi wa upinzani mkongwe, Etienne Tshisekedi, mwenye miaka, 78, wamesema wanaamini watashinda. Tshisekedi amemshutumu Bw Kabila kwa kupanga kuutia hila uchaguzi.

Historia ya Tshiseked

Etienne Tshisekedi wa Mulumba amezaliwa 14 Desemba 1932, ni mwanasheria, mwanasiasa, na kiongozi wa chama cha UDPS. Alikuwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo (wakati ikiitwa Zaire) mara tatu: 1991, 1992-1993, na 1997.

Tshisekedi alizaliwa pale Luluabourg (sasa inaitwa Kananga), Kasai mwaka 1932, akiwa ni mwana wa Alexis Mulumba na mke wake Agnès Kabena. Anatokea katika kabila la Luba. Alihitimu stashahada (diploma) mwaka 1961 katika Shule ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Lovanium cha Léopoldville (sasa Kinshasa). Aliwahi kufanya kazia katika serikali ya Mobutu katika nafasi mbalimbali kwenye miaka ya 1960 na 1970.
Kwa sasa ndiye mpinzani mkuu wa Rais Kabila katika Uchaguzi wa wa Rais nchini Kongo. Tshisekedi alitoa taarifa mnamo Novemba 2011 akijitangaza kuwa Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Kazi ya siasa
Mwaka 1960, Tshisekedi, aliyekuwa kamishina msaidizi katika Chuo cha Mobutu cha Makamishna, alishiriki katika mazungumzo kati ya Léopoldsville, Élisabethville na Bakwanga kuhusu makabidhiano ya Patrice Lumumba (ambaye alikuwa chini ya ulinzi wa Mobutu) aidha kwa Moise Tshombe au Albert Kalonji ili kumuondoa Lumumba.

Muda mfupi kabla ya Krismasi, Tshisekedi alimtumia taarifa ya kidiplomasia Albert Kalonji ambapo alijadili makabidhiano ya wafungwa wengine wa kisiasa na jinsi watakavyopokea adhabu ya kifo. Mapema Mukamba, kamishina wa Kalonji, alielezea kwa undani kile ambacho kingemtokea Lumumba kama Albert Kalonji atajiingiza kwenye uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasia wa uwaziri mkuu wa Kongo mkuu: "Lumumba Patrice atahamishiwa Bakwanga na kwenye mji huo angeuawa na kukatwa katika vipande vidogo ambavyo kila m-Luba angekuwa na uwezo wa kula nyama yake."
Taarifa ifuatayo, ilivuja kutoka kwa Mobutu kwenye magazeti ya Kongo katika miaka ya 1990, na ilitumwa na Tshisekedi mnamo Desemba 1960 na ilisomeka kama ifuatavyo:
BARAZA LA MAWAZIRI LA WIZARA YA SHERIA
N°1.399/ETSH/ ME/CAB.
Mtukufu Mfalme wa Kasai Kusini "Mulopwe"
Kwa Bakwanga
Nawasilisha heshima yangu kwako Mtukufu kwamba sasa yule chura (akimaanisha Patrice Lumumba aliyewekwa jela na Mobutu) amezingatiwa, jitihada ya Timu yetu bado inatafakari katika imani yote kuhusu washirika wake wa zamani ili kuzuia uendelevu wa kazi yake ya uharibifu. Hivi karibuni, serikali yako mtukufu wa enzi itamilki maluteni muhimu wa chura ambao ni Pierre Elengesa, Jean-Pierre Finant, Emmanuel Nzuzi, Christophe Muzungu, Joseph Mbuyi ili kuwafanya wakabiliane na adhabu itakayokuwa ya mfano. Ni katika njia hii ya kufanya kazi tutasaidia vita unavyopigana. Kwa heshima yangu yote Mtukufu…

Naibu Kamishna wa Haki
E. TSHISEKEDI E. TSHISEKEDI
Mnamo Februari 9, 1961, wafungwa 6 wa kisiasa ambao Tshisekedi aliwamaanisha walisafirishwa kwenda Bakwanga, eneo lililo chini ya udhibiti wa Albert Kalonji kukutana na kile kilichoelezwa kabla na Mukamba. Wafungwa hao 6 wa kisiasa walikuwa: Jean-Pierre Finant, Jacques Fataki, Pierre Elengesa, Camille Yangara, Emmanuel Nzuzi na Christophe Muzungu.”
Mwaka 1980 Tshisekedi aliondolewa kwenye serikali ya Mobutu na kutupwa gerezani kwa ukosoaji. Baada ya hapo akaendelea kutupwa ndani mara kwa mara na serikali zote mbili, ya Mobutu na Laurent Kabila. Mwaka 1989 wakati bado serikali ikiwa chini ya Mobutu, kesi kadhaa za kuzuiliwa kwake zilitambuliwa kuwa ni kinyume cha sheria na Kamati ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa.

Tarehe 15 Februari 1982 alianzisha chama cha UDPS, ambacho bado anaendelea kukiongoza. Chama kimeendelea kuwa maarufu miongoni mwa watu wa kabila la Tshisekedi la wa Kasai na lengo lake kuu ni kuwa na mabadiliko yasiyokuwa na ghasia kuelekea utawala wa kidemokrasia. Kwa mujibu wa Thomas Luhaka wa MLC, nguvu kubwa ya UDPS na viongozi wake ni uhusiano wa karibu na watu wenye ushawishi mkubwa katika vyombo vya habari nchini humo ikiwa ni pamoja na “Le Potentiel,” “Le Phare,” na “La Tempete des Tropiques”.

Hili lilithibitishwa na balozi wa Marekani nchini Kongo, Roger Meece, ambaye alidai "Le Phare" na "La Temptete" kimsingi yanahusiana na UDPS. [12] Katika mtandao, balozi Meece pia aliandika kwamba ingawa wanachama UDPS hupenda kutaja "demokrasia", "maadili ya jamhuri" na "utawala wa sheria", UDPS kama chama cha siasa kipo mbali na demokrasia na kwamba msimamo wake ni kupambana na hata kukiuka mikataba ya kisiasa.

Tshisekedi aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu mara tatu tofauti. Mara ya kwanza alidumu kwa mwezi mmoja tu (Septemba 29, 1991 - 1 Novemba 1991), ya pili kwa muda wa miezi saba (15 Agosti 1992 - 18 Machi 1993). Mara zote, Tshisekedi alilalamika kwamba alizuiwa kufanya kazi vizuri na Mobutu. Awamu ya tatu, ilikuwa wakati vikosi vya waasi vya Laurent Kabila vilipokuwa vikiandamana Kinshasa, alidumu kwa wiki tu (2 Aprili 1997 - Aprili 9, 1997) na alikosa tena ushirikiano kutoka kwa Mobutu. Mwezi mmoja baadaye Laurent Kabila alimuondoa madarakani Mobutu.

Uchaguzi wa 2011

Katika mkutano wa UPDS mwezi Aprili, 2009, wajumbe bila kupingwa waliamua kuwa chama kitashiriki katika uchaguzi wa 2011 na Tshisekedi atakuwa mgombea wake wa urais. Agosti 2011, Tshisekedi alitangaza kutaka majadiliano na vyama vingine vya upinzani ili kuunda juhudi za pamoja dhidi ya rais anayemaliza muda wake, Joseph Kabila. Hii ni mara ya kwanza ya Tshisekedi kugombea urais wa nchi hiyo tangu kuanzisha chama cha upinzani cha kwanza mwaka 1982.

Tshisekedi anayekaribia miaka themanini afya yake ni mbaya. Katika muongo uliopita alifanyiwa mfululizo matibabu ya nchini Afrika Kusini na Ubelgiji. Akitokea Afrika Kusini, Tshisekedi ana matatizo ya kutembea kwa sababu uwezo wake wa kuona umeshuka kwa kiasi kikubwa. Masamba pia alisema kwamba uwezo wa akili wa Tshisekedi umepungua. Kwa sababu ya afya yake mbaya, pia mara chache amekuwa akionekana kwa umma. Mukamba alisema kuwa Tshisekedi “hatamaliza miaka miwili” katika harakati. Waangalizi wengi wa kujitegemea wanakubaliana kwamba Tshisekedi akifa, UDPS itaanguka, lakini kwa yu hai wanachama wa UDPS watajaribu kumtumia kwa vyovyote iwezekanavyo.

Makala haya yameandaliwa na Bishop Hiluka kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya habari vya kimataifa

Nov 28, 2011

Mnigeria aongoza kwa utajiri Afrika, Tanzania haina kati ya 40

*Afrika Kusini ina matajiri wengi zaidi

Aliko Dangote akiwa ndani ya boti ya kifahari

JARIDA la Forbes ambalo huwa linachapisha orodha ya watu matajiri duniani, wiki iliyopita lilichapisha orodha ya kwanza ya watu matajiri Barani Afrika. Wa kwanza katika matajiri hao ni mfanyabiashara kutoka Nigeria, Aliko Dangote, ambaye anamiliki kampuni za saruji na utajiri wake unazidi dola za Kimarekani bilioni 10.Orodha hiyo iliyotolewa na jarida hilo la Forbes ina majina ya watu 40 tajiri zaidi barani Afrika ambapo utajiri wa hao wote kwa pamoja unafikia zaidi ya dola bilioni 65. katika orodha hiyo Nicky Oppenheimer (Dola 6.5 bilioni), mwenyekiti wa kampuni ya madini ya almasi nchini Afrika Kusini, De Beers, anashika nafasi ya pili.


Wengine walio katika nafasi 10 za kwanza ni Naseef Sawiris wa Misri (dola 4.75 bilioni), Johann Lupert wa Afrika Kusini (dola 4.7 bilioni), Mike Adenuga wa Nigeria (dola 4.3 bilioni), Miloud Chaabi wa Morocco (dola 3 bilioni), Naguib Sawiris wa Misri (dola 2.9 bilioni), Christoffel Wiese wa Afrika Kusini (dola 2.7 bilioni), Onsi sawiris wa Misri (dola 2.6 bilioni), na anayeshika namba kumi ni Patrice Motsepe wa Afrika Kusini (dola 2.5 bilioni).


Idadi ya matajiri 40 na nchi wanazotoka, ni kama ifuatavyo; Afrika Kusini (16), Misri (9), Nigeria (8), Morocco (5), Kenya (2) na Zimbabwe mmoja. Tanzania haina tajiri hata mmoja katika orodha ya matajiri 40 wa Bara la Afrika wakati Kenya ina wawili ambao ni pamoja na Uhuru Kenyatta anayeshika nafasi ya 26 kwa utajiri barani Afrika na Chris Kirubi wa 31.


Dangote ni nani?


Aliko Dangote alizaliwa 10 Aprili, 1957, ni mfanyabiashara wa nchini Nigeria ambaye anamiliki muungano wa makampuni yanayojulikana kama Dangote Group, ambayo yana shughuli katika nchi ya Nigeria na nchi nyingine kadhaa za Afrika Magharibi. Msaidizi huyo tajiri wa Rais wa zamani, Olusegun Obasanjo, na chama tawala cha People's Democratic Party (PDP), Dangote, huendesha biashara ya bidhaa nchini Nigeria kupitia kampuni yake na anafahamiana na wanasiasa wengi.


Akiwa na wastani wa thamani wa karibu dola bilioni 2.5, alihesabiwa na Forbes kama mmoja wa watu wenye asili ya Kiafrika walio matajiri zaidi, nyuma ya Mohammed Al Amoudi (dola bilioni 9.0) na Oprah Winfrey (dola bilioni 2.7). 


Dangote ni mwanzilishi na rais wa Dangote Group. Kwa kutajwa kwake katika orodha ya watu tajiri duniani anasema "Nadhani kuwa nilipaswa kupimwa na jarida la Forbes kwanza kabla sijaweza kuwa (kuitwa) mtu tajiri zaidi katika Afrika,” anasema Dangote. "Lakini, unajua, nina starehe." 


Aliwekwa katika nafasi ya kwanza nchini Nigeria katika orodha ya Forbes ya mwaka 2008 ya watu tajiri zaidi duniani akikadiriwa kuwa na utajiri unaofikia dola bilioni 3.3.


Mwanzo


Alizaliwa katika mji wa Kano, babu yake, marehemu Alhaji Sanusi Dantata alimpa mtaji mdogo wa kuanza biashara yake, na ilikuwa desturi wakati huo. Kwa hiyo, akaanza biashara katika mji wa Kano mwaka 1977 akiuza bidhaa na vifaa vya ujenzi. Alhaji Aliko Dangote alihamia Lagos mwezi Juni 1977 na kuendelea na biashara ya saruji na bidhaa nyingine. Akitiwa moyo na mafanikio makubwa na kuongezeka kwa shughuli za biashara, alianzisha kampuni mbili mwaka 1981.  kampuni hizi na nyingine zilizofuata sasa zikaunda muungano unaojulikana kama Dangote Group.


Wasifu wa Biashara


Dangote Group, ina thamani ya Naira (pesa ya Nigeria) trilioni nyingi na iliyosambaa katika nchi za Benin, Ghana, Nigeria na Togo. 


Biashara za Dangote ni pamoja na usindikaji wa chakula, utengenezaji saruji na kusafirisha mizigo. Dangote Group inatawala soko la sukari nchini Nigeria, kwani yeye ndiye msambazaji mkubwa zaidi wa sukari nchini humo katika makampuni ya vinywaji laini, watengenezaji pombe na watengenezaji peremende. 


Dangote Group imekua kutoka katika kampuni ya biashara hadi kuwa kundi kubwa zaidi la Viwanda nchini Nigeria, pamoja na kiwanda cha kusafishia sukari cha Dangote (kampuni iliyo na pesa zaidi katika Soko la Hisa la Nigeria, yenye thamani ya zaidi ya dola bilioni 3 na usawa wa Aliko Dangote umefika dola bilioni 2), kiwanda kikubwa zaidi barani Afrika cha kutengeneza simenti: Obajana Cement, na Kiwanda cha Unga cha Dangote miongoni mwa viwanda vingi.


Dangote aliwahi kujihusisha kwa sehemu kubwa katika kufadhili kampeni za Olusegun Obasanjo wakati wa awamu ya pili katika uchaguzi wa mwaka 2003, ambapo alichangia zaidi ya Naira milioni 200 (dola milioni 2). 


Alichangia Naira 50 milioni (dola milioni 0.5) akitumia kikundi cha “Marafiki wa Obasanjo na Atiku” (Friends of Obasanjo and Atiku), na akachangia Naira 200 milioni (dola milioni 2) kwa hifadhi ya vitabu ya Rais. Zawadi hizi zenye utata kwa wanachama wa chama tawala cha People's Democratic Party zimechangia wasiwasi juu ya ufisadi licha kampeni za kupambana na rushwa zilizoongozwa na Obasanjo katika kipindi chake cha pili cha uongozi.


Kama mfanyabiashara asiye mfuasi mwenye ari wa chama na aliyevunja ukabila, amekuwa mwema kwa vyama mbalimbali vya kisiasa, mashirika ya kidini na taasisi za utamaduni. Mbali ya kutoa ajira kwa wahitimu wasomi wa matabaka na makabila tofauti, amepunguza kiwango cha uhalifu kwa kushirikisha vijana wanaohitimu shule katika maeneo ya usafiri, ufungashaji vitu na usalama miongoni mwa mengi.


Inaweza kuwa ni wazo sahihi kusema kwamba kila Mnigeria ameshasikia jina lake kwa sababu ya matokeo ya biashara yake. Bidhaa zake zinatumika katika familia nyingi nchini kote. Hata wale wasiotumia bidhaa zake watakuwa wamekosa tu kwa bahati mbaya. Dangote anapatikana katika bidhaa mbalimbali zinazouzwa nje ya nchi, zinazoagizwa toka nje, mali za viwandani, mashambani na uhisani. Haya yote yameunganishwa pamoja katika kile kinachojulikana kama Dangote Group. 


Kwa masuala yake kama Rais na Mtendaji Mkuu, Aliko Dangote ni mtu mnyenyekevu. Mtazamo wa uwekezaji wake umeegemea zaidi kwenye chakula, mavazi na makazi. 


Dangote Group inaagiza tani 400,000 za sukari kwa mwaka ambazo zinachangia asilimia 70 ya mahitaji ya jumla ya nchi na ni muuzaji mkubwa wa bidhaa kwa wazalishaji wa Coca Cola, Pepsi Cola na Seven-Up nchini Nigeria. Inaagiza tani 200,000 za mchele kila mwaka, na kuagiza nje tani nyingi za saruji na mbolea na vifaa vya ujenzi.


Dangote Group pia inaagiza samaki na inamiliki meli tatu kubwa za uvuvi zilizoidhinishwa kwa ajili ya uvuvi na uwezo wa 5,000 MT. Dangote Group inauza nje pamba, kakao, korosho, mbegu za ufuta, tangawizi na ubani wa Kiarabu katika nchi kadhaa.


Shughuli


Dangote Group leo inashiriki katika aina mbalimbali ya viwanda na ina mauzo ya juu. Viwanda vya nguo vya Dangote na Nigeria Plc, ambavyo vinazalisha zaidi ya mita 120,000 za nguo zilizokamilika kila siku. Dangote inamiliki jineri katika eneo la Kankawa, Jimbo la Katsina yenye uwezo wa kuzalisha 30,000 MT za mbegu za pamba kwa mwaka.


Kiwanda cha kusafishia sukari katika bandari ya Apapa, Lagos ambacho ni kikubwa zaidi katika Afrika na cha tatu kwa ukubwa duniani chenye uwezo wa kuzalisha tani 700,000 za sukari iliyosafishwa kwa mwaka. Pia ina uwezo wa kuzalisha tani 100,000 nyingine za sukari katika kiwanda cha Hadeja katika Jimbo la Jigawa. 


Mbali na kuwekeza katika Kampuni ya Taifa ya Chumvi ya Nigeria katika eneo la Ota, Jimbo la Ogun Nchi, pia Dangote ana viwanda vya chumvi katika eneo la Apapa na Calabar, kiwanda cha mifuko ya plastiki ambacho kinazalisha mifuko inayohitajika kwa ajili ya bidhaa zake, zaidi ya matera 600 kwa ajili ya mtandao wa usambazaji na bidhaa zilizokusudiwa kuuzwa nje pia husafirishwa kwa kutumia kifuko hiyo kwenda bandarini. 


Dangote Group ina wafanyakazi 12,000. Mafanikio ya biashara za Alhaji Aliko Dangote yanaweza kuwa yamechangiwa na sababu mbalimbali. Anaonekana kuwa na upeo mkubwa. Tofauti na baadhi ya watu, msaidizi wake binafsi ni wa kutoka kabila la Yoruba wakati Mkuu wake wa Mambo ya mashirikiano ni Mkristo kutoka Jimbo la Delta. 


Kama mjasiriamali, mwenye elimu ya kawaida, amethibitisha kuwa mafanikio ya biashara yanaweza kuchangiwa na dhamira, uaminifu na uvumilivu, na si lazima uwe umepata shahada kutoka Harvard au Oxford au umefuzu daraja la kwanza la taaluma. Badala ya kuficha fedha zake katika mabenki ya nje, jambo ambalo ni la kawaida la ulaghai na uporaji wa mali za umma, Dangote amewekeza katika sekta ya uzalishaji wa uchumi wa Nigeria.


Makala haya yameandaliwa na Bishop Hiluka kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya habari vya kimataifa.

Nov 16, 2011

Tutatatua migogoro yetu kwa mitutu ya bunduki hadi lini?

 Askari wa kutuliza ghasia wakiwa tayari kuwakabili 
wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam

 Picha hii inaonesha matokeo ya vurugu jijini Mbeya

BISHOP HILUKA
Dar es Salaam

IMEKUWA ni kawaida kuona ama kusikia polisi wakiwashambulia kwa risasi za moto na mabomu wananchi waliogoma, wanaoandamana, wanafunzi wa vyuo vikuu waliogoma, wafanyabiashara ndogondogo wasioridhishwa na taratibu za watawala, wananchi wanaoishi maeneo ya migodi wanaodai haki zao huku wakiwa hawaridhishwi na ‘uporaji’ wa urithi wao huo, na migogoro mingine mingi katika sehemu tofauti za nchi.

Matukio ya aina hii katika nchi hii yamekuwa ni ya kawaida na hayajaanza leo, yamekuwa yakitokea mara kwa mara katika sehemu kadhaa nchini, hasa katika miji mikubwa. Na mara zote kumekuwepo taarifa za watu ama kujeruhiwa au taarifa za mauaji ya watu kadhaa.

Matukio haya yametamalaki kila pembe ya nchi yetu, kuanzia kwenye maeneo ya migodi, vyuo vikuu, hadi kwenye maeneo ya wafanyabiashara ndogondogo maarufu kwa jina la machinga.

Kwa hali inavyoonekana, Serikali haioni tena umuhimu wala haja ya kutafuta suluhu kwa kufanya mazungumzo na makundi mbalimbali ya kiraia na kijamii inapotokea pande hizo mbili zinapotofautiana, na imeamua kutumia njia inayodhani inafaa 'ya mitutu ya bunduki na mabomu' kwa kutumia vikosi vyake vya ulinzi kama njia muafaka ya utatuzi wa migogoro inayojitokeza!

Kibaya zaidi ni kwamba, mauaji haya yanazidi kujitokeza katika Serikali ambayo imejivika joho la utawala bora na kudai kuwa imebobea na kuitekeleza dhana ya utawala bora kwa vitendo.

Wakati huko nyuma ingeliwezekana watu kujiuzulu kwa mauaji na manyanyaso kwa wananchi kama ilivyotokea kwa Ali Hassan Mwinyi akiwa waziri, siku hizi hata polisi wanapodhihirika kutumia nguvu kubwa ambayo haikuhitajika katika kuua wananchi hakuna hatua wanazochukuliwa.

Nakubaliana kabisa na kauli ya Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Yuda Thadeus Ruwa-Inchi, wa Kanisa Katoliki, pale alipowataka viongozi wa serikali kutambua kuwa amani na usalama haviwezi kulindwa wala kudumishwa kwa kutumia nguvu kubwa za jeshi na matumizi ya silaha kali, bali ni kwa kila kiongozi kuwatendea haki watu wake.

Mfano hivi karibuni, katika kipindi cha siku saba tu kumekuwepo matukio yaliyowahusisha polisi na wananchi ambapo polisi walitumia risasi za moto na mabomu hata pale ambapo hakukuwa na haja ya kufanya hivyo.

Hapa jijini Dar es Salaam, polisi waliwatia nguvuni wanafunzi 46 wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa kuandamana kuishinikiza Serikali kuwapa wenzao 1,000 mikopo ya elimu ya juu. Kabla ya kuwakamata, polisi walitumia mabomu na kutoa vipigo kwa wanafunzi hao waliokuwa wanaelekea sehemu za Ubungo kupeleka ujumbe huo kwa wananchi.

Eneo hilo la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam liligeuka uwanja wa mapambano baina ya jeshi la polisi na wanafunzi wa chuo hicho walioandamana kushinikiza kupatiwa mikopo ya elimu. Hata hivyo, vurugu hizo zilisababisha shughuli zote za chuo hicho kusimama kwa saa kadhaa.

Kuna picha fulani niliiona ambayo kwa kweli haikunipendeza kabisa, ambapo askari wawili wa kiume walionekana kumdhalilisha mwanafunzi wa kike, huku wenzao saba wakiwa wameelekeza mitutu ya bunduki kwa mwanafunzi huyo!

Jijini Arusha polisi walikuwa katika mapambano makali na viongozi na wafuasi wa Chadema waliowatia mbaroni na kuwafungulia mashtaka kwa tuhuma za kufanya mkusanyiko kinyume cha sheria na kukataa kutii amri halali ya polisi.

Na huko Mbeya, risasi na mabomu vilitawala sehemu kubwa ya jiji hilo na kusababisha kifo cha mtu mmoja na kujeruhi watu kadhaa. Vurugu hizo zilitokana na operesheni iliyofanywa na askari wa Jiji la Mbeya iliyokuwa na lengo la kuwaondoa wafanyabiashara wadogo (Wamachinga) katika mitaa ya jiji hilo. Katika vurugu hizo, watu 235 walikamatwa na polisi.

Mapambano hayo yaliyoanza majira ya saa 2.30 asubuhi katika maeneo ya Mwanjelwa na kusambaa kwa kasi katika mitaa mingi ya jiji hilo, yalisababisha kufungwa kwa barabara zote na hakukuwa na gari linaloingia ama kutoka katikati ya jiji.

Polisi zaidi wakiwa na silaha waliwasili na kuanza kuwashambulia wananchi kwa risasi bila kujali kama ni mfanyabiashara ama watembea kwa miguu. Katika mapambano hayo, mtu mmoja Abel Mwalukali, alipigwa risasi katika mkono wake wa kulia uliovunjika vibaya, na kukimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mbeya kwa matibabu. Pia kuna taarifa ya watu wengine kupigwa risasi za moto na kujeruhiwa.

Lakini pamoja na mapambano hayo, vurugu hizo zilizoendelea bila kukoma na jeshi la polisi kwa kushirikiana na JKT kambi ya Itete hawakufanikiwa kutuliza ghasia hizo. Pongezi za pekee ni kwa Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi, maarufu kama Sugu kwa kuacha kikao cha Bunge mjini Dodoma na kwenda mjini Mbeya ambako alifanikiwa kuzima vurugu hizo kwa njia ya kidiplomasia.

Kwa kweli Sugu ametoa somo kubwa sana kwa viongozi wa Serikali na vyombo vyake vya ulinzi na usalama kuwa, wananchi wanahitaji kiongozi anayewasikiliza na kutafuta suluhisho la matatizo yao, na kamwe migogoro haiwezi kuzimwa kwa mitutu ya bunduki.

Alamsiki.

MFALME MSWATI III: Akumbana na shinikizo la mabadiliko nchini Swaziland

 Mflame Mswati III

SWAZILAND

KIONGOZI mwandamizi wa Kianglikana wa Swaziland, Askofu Meshack Mabuza, ametoa wito kwa mfalme Mswati III kuachia madaraka ya kisiasa ili kuipa nafasi serikali ya kidemokrasia.

Askofu Mabuza aliliambia shirika la habari la Uingereza, BBC kwamba mfumo wa serikali wa "mambo ya kale" umeiingiza nchi katika mgogoro mzito wa fedha na uchumi. Mfalme Mswati, mwenye wake 13, ni kiongozi pekee mwenye kushikilia mamlaka yote ya nchi Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Anashutumiwa kwa kiasi kikubwa kuhusishwa na ufisadi, lakini akaahirisha sherehe zake za kufikisha miaka 25 madarakani mwaka huu kutokana na msukosuko wa fedha nchini humo.

Mpaka sasa Swaziland imekataa kupokea mkopo wa dola za Marekani milioni 355 kutoka Afrika Kusini kuisaidia kulipa gharama mbalimbali, baada ya Pretoria kuitaka nchi hiyo kufanya mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi.

Askofu Mabuza, askofu wa Kianglikana wa Swaziland, aliiambia BBC kuwa matatizo ya Swaziland hayatokwisha iwapo uongozi huyo utaendelea kuwepo madarakani.

Alisema, "Jawabu kwa hakika litatokana na mabadiliko ya uongozi wa serikali ya kiutamaduni, kikabaila, na mambo ya kale."

"Lazima ibadilishwe na uongozi wa kidemokrasia wa vyama vingi."

Taarifa ya serikali iliyoonekana kabla ya kutolewa rasmi - iliyotiwa saini na mhasibu anayekaimu, AF Mabila - ilisema malipo ya mishahara ya wafanyakazi wa serikali ya Novemba yamesogezwa hadi Desemba.

Msemaji wa serikali, Percy Simelane, aliiambia BBC kuwa Baraza la Mawaziri limekuwa likijadili suala hilo tangu Jumamosi, lakini mpaka sasa hamna muafaka wowote uliofikiwa.

Serikali imesema mgogoro wake wa fedha umesababishwa na msukosuko wa uchumi duniani na kuporomoka kwa mapato ya uongozi huo kutoka umoja wa ushuru wa forodha wa Kusini mwa Afrika (Sacu), kufuatia makubaliano mapya ya ushuru wa forodha mwingi.

Lakini askofu Mabuza, anayetarajiwa kuachia madaraka mwezi ujao, alisema hivyo ni "visababu".

Alisema, "Matatizo ya kiuchumi yalikuwepo hata kabla ya kuporomoka kwa uchumi wa dunia kwa sababu imekuwa kama hakuna ukuaji wa kiuchumi."

"Nchi hii imefika hatua ya kuporomoka kabisa."

Kumekuwa pia na wasiwasi kuwa hospitali za taifa zinaweza kuishiwa na dawa za kufubaza ukimwi ARVs kutokana na upungufu wa fedha. Swaziland, yenye jumla ya watu milioni 1.2, ni miongoni mwa nchi zenye idadi kubwa ya walioathirika na ukimwi duniani.

Takriban watu 230,000 wanaishi na virusi vya ukimwi, ambapo 65,000 wanategemea hospitali za taifa kuwapa dawa hizo za ARV.

Vyama vya kisiasa vinazuiwa Swaziland, ambapo Mfalme Mswati amekuwa madarakani tangu mwaka 1986.

Wakosoaji wanaishutumu familia hiyo ya kifalme kwa kuwa na matumizi makubwa kupita kiasi, licha ya idadi kubwa ya watu wake kuishi maisha ya kimaskini.

Msukosuko wa kiuchumi umechochea maandamano dhidi ya uongozi wa mfalme Mswati, lakini wachambuzi wamesema ufalme huo bado unapewa heshima kubwa na Waswaziland wengi wanaothamini mila na desturi zao.

Historia ya Mswati III

Mswati III amezaliwa Makhosetive Dlamini mnamo Aprili 19, 1968. Mwaka 1986, alimrithi baba yake, Sobhuza II, kama mkuu wa ufalme huo wa Kusini mwa Afrika. Anachukuliwa kuwa mfalme mmoja wa wafalme wa mwisho kabisa duniani, kuwa na mamlaka ya kuteua Waziri Mkuu wa nchi, baraza la mawaziri, na mahakama. Hata hivyo, ana wajibu wa kiwango fulani kwa mila za Swaziland na hana mamlaka ya kuchagua mrithi wake.

Mswati III anajulikana kwa tabia yake ya anasa na ndoa ya mitala, na amekuwa akikosolewa nje ya nchi kwa kutafuta maslahi yake binafsi kwa gharama ya nchi yake, moja ya mataifa maskini zaidi dunia. Mwaka 2001 alijaribu kukabiliana na janga la UKIMWI kwa kutaja usafi wa ibada, 'umchwasho', unaopiga marufuku wanawake chini ya umri wa miaka 18 kufanya ngono. Ndani ya Swaziland, Mswati anaheshimiwa kama mtu maarufu. Hata hivyo, sera zake na aina ya maisha yalisababisha maandamano ya ndani na kukosolewa kimataifa.

Maisha ya awali

Yeye ni mmoja wa watoto wengi wa mfalme Sobhuza II (aliyekuwa na wake 70, watoto 210 na wakati wa kifo chake aliacha wajukuu 1000). Alizaliwa katika Hospitali ya Kumbukumbu ya Raleigh Fitkin, miezi minne kabla Swaziland haijapata uhuru kutoka Uingereza. Waliporuhusiwa kutoka hospitali na mama yake, wakaenda kuishi katika moja ya makazi ya mfalme Sobhuza Etjeni karibu na Masundwini Palace. Jina lake la kuzaliwa lilikuwa Makhosetive (Mfalme wa Mataifa).
Akiwa vijana, alihudhuria Shule ya Msingi ya Masundwini na Shule ya Lozitha. Alifanya mtihani wa kumaliza elimu ya Msingi mnamo Desemba 1982 na kupata daraja la kwanza na kupata tuzo katika masomo ya Hisabati na Kiingereza. Alijihusisha zaidi katika ulinzi wa kifalme, na kuwa kijana wa kwanza kujiunga na Jeshi la Umbutfo la Swaziland (USDF).

Mfalme Sobhuza II alipofariki mwaka 1982, Halmashauri Kuu ya Taifa (Liqoqo) ilimchaguwa kijana mwenye umri wa miaka 14, Makhosetive (Mswati III), kuwa mfalme ajaye. Kwa miaka minne iliyofuata wake wawili wa marehemu mfalme Sobhuza II, Malkia Dzeliwe Shongwe (1982-1983) na Malkia Ntombi Tfwala (1983-1986), walitumikia wakati mfalme mtarajiwa akiendelea na elimu yake nchini Uingereza, shule ya Sherborne, kabla ya kuitwa nyumbani kuchukua madaraka.

Mfalme

Alitambulishwa kama Crown Prince mwezi Septemba 1983 na alitawazwa ufalme Aprili 25, 1986, akiwa na umri wa miaka 18 na siku 6, na hivyo kumfanya kuwa mfalme mwenye umri mdogo kutawala hadi kuibuka kwa Mfalme Jigme Khesar Namgyel Wangchuck wa Bhutan mnamo Desemba 14, 2006; pia alikuwa kiongozi mdogo wa nchi hadi alipoibuka Joseph Kabila kuchukua madaraka mnamo Januari 26, 2001, nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Mfalme na mama yake, aliyepachikwa jina la Indlovukazi (Tembo Mkuu wa Kike), kutawala kwa pamoja.

Mwaka 2004, Mswati alianzisha katiba mpya ambayo inaruhusu uhuru wa kusema na mkutano kwa vyombo vya habari na umma, lakini wakibakia katika mfumo wa jadi 'Tinkhundla'. Ingawa Amnesty International waliikosoa katiba mpya kuwa duni katika mambo fulani, waandishi wa habari wa Swaziland waliuambia mikutano wa vyombo vya habari vya Kanda (MISA), kwamba wao wako huru kuripoti kama watakavyo.

Katika jitihada za kukabiliana na VVU na UKIMWI mwaka 2001, mfalme alitumia mamlaka yake ya jadi kuomba muda wa kuheshimu usafi wa ibada (umcwasho), ambao huwatia moyo mabinti wote wa Swaziland kujiepusha na mahusiano ya kimapenzi kwa miaka mitano. Ibada hii inapiga marufuku mahusiano ya kimapenzi kwa Waswazi chini ya miaka 18 kuanzia Septemba 9, 2001 na 19 Agosti 2005, lakini miezi miwili tu baada ya kupiga marufuku, yeye mwenyewe alivunja amri hii kwa kuoa msichana wa miaka 17, aliyekuja kuwa mke wake 13. Kama desturi, alitozwa faini ya ng'ombe, ambayo aliipa.

Mali

Mswati amekuwa akikosolewa kwa maisha yake, hasa na vyombo vya habari. Kufuatia upinzani wa ununuzi wake wa magari ya kifahari, ikiwa ni pamoja na gari la anasa la dola 500,000, alipiga marufuku kupigwa picha magari yake. Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa zamani wa Ofisi ya mfalme, manunuzi yalikuwa binafsi na mfalme wa Swaziland anapata mshahara mkubwa kama Mkuu wa Nchi, ana uwekezaji ndani na nje ya nchi na anamiliki kiasi kisichojulikana cha hisa katika makampuni mbalimbali ndani ya Swaziland.

Kwa mujibu wa jarida la Forbes la 2009, orodha ya wafalme matajiri duniani, mfalme Mswati ana mali yenye thamani ya dola za Marekani Million 200. Hii haijumuishi jumla ya dola 10 bilioni ambazo baba yake mfalme Sobhuza II, aliziweka kwenye mfuko kwa ajili ya taifa la Swaziland wakati wa utawala wake, ambapo Mswati III ni mdhamini.

Makala haya yameandalia na Bishop Hiluka kwa msaada wa vyombo mbalimbali vya habari vya kimataifa.

Nov 14, 2011

DK CONRAD MURRAY: Daktari bingwa anayekabiliwa na kifungo kwa kumuua Michael Jackson bila kukusudia

Dk. Conrad Murray

LOS ANGELES
Marekani

WIKI hii, daktari binafsi wa aliyekuwa Mfalme wa Pop duniani, Michael Jakson, Dk. Conrad Murray, amekutwa na hatia ya kosa la mauaji bila kukusudia na mahakama moja mjini Los Angeles, Marekani, ambapo Baraza la wazee wa mahakama - wanaume saba na wanawake watano - walichukua siku mbili kujadili kesi na kufikia hukumu hiyo.

Michael Jackson alifariki Juni 25 mwaka 2009 kutokana na kuzidisha kipimo cha dawa ya usingizi. Na inasemwa kuwa Murray, 58, anaweza kukabiliwa na adhabu ya kwenda gerezani miaka minne na kupoteza leseni yake ya utabibu.

Wanasheria wa Dk. Murray walisema kuwa Michael Jackson alijidunga mwenyewe dawa hiyo wakati daktari wake akiwa nje ya chumba. Dk. Murray alipelekwa rumande baada ya kukutwa na hatia hadi wakati atakaposomewa adhabu yake, inayotarajiwa kutolewa Novemba 29.

Akielezea uamuzi wake, jaji alisema Dk. Murray kwa sasa ni mhalifu aliyekutwa na hatia na kwa kuwa anafahamiana na watu nje ya jimbo la California, inamaanisha hakuna uhakika kuwa daktari huyo ataweza kubakia bila kutoka katika jimbo hilo.

Dk. Murray alibaki kimya mahakamani hapo wakati hukumu ikisomwa. Baraza la wazee - lililoundwa na wazungu sita, Mmarekani mweusi mmoja na Wamarekani watano wenye asili ya Hispania - walijadili shauri hilo kuanzia Ijumaa hadi Jumatatu asubuhi.

Katika hoja za mwisho mahakamani siku ya Alhamisi, upande wa mashtaka ulisema Dk. Murray alisababisha kifo cha nyota huyo kutokana na uzembe, na hivyo kuwanyima watoto wa Jackson haki ya kuwa na baba.

Upande wa utetezi ulihoji kuwa Jackson alikuwa amejizoesha kutumia dawa, kitu ambacho kilisababisha kifo chake kutokana na kujipa kiwango kikubwa cha dawa huku daktari wake akiwa nje ya chumba katika jumba alilokuwa amekodi nyota huyo mjini Los Angeles.

Historia ya Murray

Dk. Conrad Murray ni daktari bingwa wa moyo (Cardiologist) na daktari binafsi. Alizaliwa Februari 19, 1953, katika eneo la St Andrews, Grenada. Alihamia Marekani mwaka 1980. Mwaka 1999, alianzisha kituo binafsi cha mazoezi. Michael Jackson alimwajiri kama daktari binafsi kwa ajili ya ziara ya tamasha lake mwaka 2009. Mwezi Juni 2009, Jackson alikufa kwa kuzidisha kiwango cha dawa. Dk Conrad ameshtakiwa kwa kuua bila kukusudia (manslaughter involuntary).

Maisha ya mwanzo na Mafunzo ya Utabibu

Daktari huyu ambaye amekumbana na utata wa kifo cha Mfalme wa Pop mnamo Juni 2009, hakutoka kwenye familia yenye fedha. Pamoja na mama yake Milta kutumia muda wake nchini Trinidad na Tobago akitafuta kazi nzuri yenye kulipa, Murray aliishi na bibi na babu yake wa upande wa mama, wakulima wa Kigrenada. Maisha ya familia yake iliyovunjika yalizungukwa na kukosekana kabisa kwa baba yake, Rawle Andrews, daktari wa eneo la Houston ambaye, hadi kifo chake mwaka 2001, alilenga kazi yake zaidi katika kutoa huduma ya matibabu kwa maskini. Conrad hakuwahi kukutana na baba yake hadi alipokuwa na miaka 25.

Alipofikisha miaka saba, Murray alihamishiwa nchini Trinidad na Tobago kuishi na mama yake, ambapo alipata uraia na kumaliza shule ya sekondari. Kama mama yake, Murray aliamua kufanya ili awe na maisha bora, alionesha kupendelea kufanya kazi kwa bidii katika umri mdogo. Baada ya shule ya sekondari alijitolea kufanya kazi kama mwalimu katika shule ya msingi Trinidad, uzoefu alioupata ulimfanya kufanya kazi kama karani wa forodha na bima ili kujilipia ada yamasomo yake ya elimu ya chuo. Katika umri wa miaka 19 alinunua nyumba yake ya kwanza, halafu baadaye akaiuza kwa faida ili pesa zimsaide katika masomo yake ya chuo kikuu nchini Marekani.

Mwaka 1980, miaka miwili baada ya kutembelea Houston kwa mara ya kwanza na kupata nafasi ya kujitambulisha mwenyewe kwa baba yake, Conrad akarudi Texas kujiandikisha katika Chuo Kikuu cha Texas Kusini, ambapo katika miaka mitatu tu alihitimu shahada ya sayansi ya tiba na baiolojia. Kuanzia hapo, alifuata nyayo za baba yake na kuhudhuria Chuo cha Tiba cha Mmarekani-Mweusi Meharry kilichopo Nashville, Tennessee.

Baada ya kufuzu Maharre, Murray alijiunga na mafunzo ya ziada katika Kliniki ya Mayo jimbo la Minnesota na kisha kukamilika makazi yake katika Chuo Kikuu cha Tiba cha Loma Linda Medical huko California. Kisha mafunzo mengine yalifuata; alisoma Cardiology (magonjwa ya moyo) katika Chuo Kikuu cha Arizona, na kurudi California, ambako hatimaye akafanya kazi kama mkurugenzi mwenza katika mpango wa kimataifa wa mafunzo ya magonjwa ya moyo katika Hospitali ya Kumbukumbu ya Sharp katika eneo la San Diego.
Kazi ya Tiba huko Las Vegas

Mwaka 1999, Dk Murray aliondoka California kwa mara ya pili na kuanza kivyake, akafungua kituo binafsi cha mazoezi katika eneo la Las Vegas. Akiiweka ofisi yake mashariki mwa mji, akifuata tena nyayo za baba yake – alikusudia si tu kutumikia utajiri wa mji, lakini mafanikio yake pia. Mwaka 2006, Murray alipanua wigo wake na kurudi katika mji ambapo baba yake alijitengenezea jina lake, akafungua Taasisi ya Moyo iliyoitwa ‘Acres Homes Heart and Vascular Institute’.
"Tumekuwa na bahati ya kuwa na Dk Murray na kliniki hiyo katika jamii hii," mgonjwa wa Houston, Ruby Mosley, aliliambia jalida moja. "Kuna wagonjwa wengi, wengi mno wanaomshukuru Mungu kwamba mtu huyu yupo hapa kwa ajili yao."

Wale ambao wamekuwa na mahusiano ya kifedha na daktari, hata hivyo, wanaweza kujisikia vinginevyo. Wasiolipa madeni, kesi za kisheria, na wenye madai ya kodi wamefuata maisha ya Dk Murray. Zaidi ya dola 400,000 katika hukumu ya mahakama peke yake zilitolewa dhidi ya kazi yake huko Las Vegas, na mwezi Desemba 2008 Murray, ambaye ana idadi isiyojulikana ya watoto, aliamriwa kutoa 3,700 kwa ajili ya malipo ya mtoto.

Kumtibu Mfalme wa Pop
Ukweli, ilikuwa ni hali ya madeni ya Dk Murray iliyoanzisha kufanya kazi na uhusiano wake Michael Jackson. Watu hawa wawili walikutana kwa mara ya kwanza mwaka 2006 wakati mwanamuziki huyo, alipozuru mara kwa mara Las Vegas, aliwasiliana na Dk Murray kuhusu kumtibu mmoja wa watoto wake kutokana na matatizo yasiyojulikana. Taarifa zinaonesha kwamba watu hao wawili wakawa marafiki na, Jackson alipoanza mipango ya ziara yake ya tamasha la 2009, alimuajiri Dk Murray kuwa daktari wake binafsi kwa mshahara wa dola 150,000 kwa mwezi.
Dhamira ya Jackson kumleta Murray, ingawa, yawezekana haikuhusiana na urafiki na zaidi ilihusiana na matatizo ya Jackson mwenyewe kuhusiana na tiba. Kufuatia kifo cha Jackson, polisi waligundua vyeti vya dawa zaidi ya 20 ndani ya nyumba yake ya kukodi ya Holmby Hills, ikiwa ni pamoja na methadone, fentanyl, percocet, dilaudid, na vicodin.

Pamoja na yote, Jackson aliathiriwa na tatizo la kukosa usingizi (Insomniac) na alisukumwa kutumia propofol na anesthetic, ili zimsaidie kupumzika. Pamoja na mchanganyiko wa dawa nyingine, Jackson alipenda kulala, mara nyingi alipendelea kuchanganya dawa na kuzifanya "maziwa" yake au "kinywaji cha kulalia." Lakini ilikuwa ni propofol aliyoonekana kuipenda hasa. Cherilyn Lee, muuguzi na mtaalam wa lishe aliyesajiliwa ambaye Jackson alimuajiri, aliiambia ABC News kwamba mwimbaji huyo alimwomba amnunulie dawa nyingi zaidi za kutumia. Muuguzi huyo alikataa.

Kifo cha Michael Jackson

Dk Murray, hata hivyo, alikuwa ni suala jingine. Wakati nyaraka za mahakama zilionesha hakuwahi kumnunulia dawa Jackson, katika kipindi cha wiki sita alizofanya kazi kwake, daktari huyo alimtundikia maji (intravenous drip) yenye mchanganyiko wa propofol - licha ya wasiwasi wake kwamba Jackson anaweza kuwa mwathirika wa dawa za kulevya.

Hiyo ilikuwa tarehe 25 Juni, 2009, wakati Jackson, akiwa amechoka na mazoezi ya muda mrefu katika Kituo cha Staples, Los Angeles, alikokwenda usiku wa manane, alirudi nyumbani na kujaribu kupata mapumziko. Alitumia njia iliyotumiwa mara kwa mara na Murray kwa mteja wake kumtundikia maji (IV) ili kuingiza propofol. Dk Murray pia alimpa Jackson lorazepam, dawa za kuondoa wasiwasi, na midazolam, dawa ya kulegeza misuli.

Kwa mujibu wa kumbukumbu, daktari alimwacha Jackson kwa dakika chache na kwenda bafuni. Aliporudi alimkuta Jackson akiwa na mapigo dhaifu ya moyo na alishindwa kupumua. Inasemekana, Murray mara moja alianza kutumia CPR kumfufua Jackson. Aidha, katika kile ambacho kimeongeza zaidi utata, Dk Murray pia aliongeza dawa nyingine ya kulevya, flumazenil, ili kujaribu kukabiliana na dawa ambazo tayari zilikuwa kwenye mzunguko wa damu katika mwili wa Michael Jackson. Baadhi ya wataalam wamesema kuwa matumizi ya dawa aliyoongeza Murray yanaweza kuwa ndiyo yaliyozidisha matatizo ya propofol mwilini.

Makala haya yameandaliwa na Bishop Hiluka kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya habari vya kimataifa.

Nov 2, 2011

Ni kweli malengo ya Mkukuta yanafikiwa?

 

 Picha zinazowaonesha wakazi wa vijijini ambao
wanapaswa kukwamuliwa kupitia Mkukuta
 
BISHOP HILUKA
Dar es Salaam

MKUKUTA ni neno maarufu katika jamii ya Tanzania toka ulipozinduliwa mwaka 2005. Kirefu chake kikiwa ni Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini Tanzania. Hivi sasa tuna Mkukuta II ambao umeboreshwa kutoka katika Mkakati wa kwanza wa kupunguza umaskini uliozinduliwa Oktoba mwaka 2000 na kutekelezwa kuanzia 2005 hadi 2010.

Malengo ya Mkukuta yamejikita katika ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini wa kipato, ambapo eneo hili lina malengo sita likiwemo la kupunguza umaskini wa kipato kwa wanawake na wanaume wa maeneo ya vijijini.

Kwamba wakazi wa maeneo hayo ambao wengi wao ni wakulima wadogo watajengewa uwezo wa kuongeza tija na kupata faida ndani na nje ya sekta ya kilimo. Wakiwezeshwa kutafuta masoko ya uhakika ya bidhaa za kilimo na kujengewa uwezo wa kuongeza thamani mazao wazalishayo ili waweze kupata faida.

Pia ilibuniwa kuwa wakazi wa sehemu hizo wajengewe uwezo wa kutumia raslimali zinazowazunguka ili kuongeza michango inayotokana na wanyama pori, misitu na uvuvi katika vipato vya jumuiya za vijijini.

Ukweli sioni juhudi za kivitendo zaidi ya nadharia katika kukamilisha malengo ya Mkukuta, sioni viongozi wakihamasisha wakulima vijijini kuzalisha mazao yenye faida kubwa na kuongeza upatikanaji wa nyenzo za kilimo na matumizi sahihi ya teknolojia sambamba na mbinu za usimamizi wa mavuno katika kaya za vijijini na kukuza miradi inayoongeza thamani katika kilimo, uvuvi mifugo na bidhaa za misituni.

Sioni watendaji wakitoa mafunzo ya stadi za maisha na ujasiriamali kwa watu wa vijijini hususani wanawake na vijana, kwani kundi hili ndio limekuwa likiathirika sana na hivyo wengi wao hukimbilia mijini wakidhani kuna unafuu na wengi wanaokosa elimu hiyo hupunjwa mazao na hivyo kubaki katika hali ya umaskini. Elimu ya ujasiriamali na mitaji ndiyo suluhisho pekee la kuwakwamua.

Ninachoona ni kukosekana miundombinu; barabara na umeme imekuwa kiwazo kikubwa cha juhudi za kujikwamua kiuchumi kwa wakazi wengi wa vijijini. Barabara zisizounganika zinakwaza usafirishaji wa mazao na kupata tija kwa wakati muafaka. Mazao mengi huozea mashambani hasa wakati wa msimu wa matunda

Pia wakulima wameendelea kuendesha kilimo cha kujikimu miaka yote kwa kutegemea mvua, uzalishaji ni duni, nguvu kazi ni haba na vitendea kazi ni duni. Hata zile pesa zilizowahi kutolewa na serikali wakati fulani katika kila mkoa, maarufu kama mabilioni ya JK, hazikuwasaidia walengwa na inasemwa kulikuwa na ugumu mkubwa wa kuzipata kutokana na masharti magumu ambayo walalahoi wasingeyaweza.

Kumekuwa na fursa finyu ya kupata mitaji na mikopo kwa wakazi wengi wa vijijini. Kupanda kwa bei ya mafuta ya taa, huku umeme na gesi vikiwa ni anasa kwa wananchi wa kawaida wa Tanzania, na kukosekana njia mbadala ya kupunguza matumizi halisi ya nishati ya kupikia ni changamoto kwa wengi katika kufikia malengo ya Mkukuta.

Mambo haya ndiyo sababu ya kuwa na asilimia moja tu ya watu, tena wenye asili ya mabara ya nje kumiliki uchumi wa Tanzania. Hii ni hatari kubwa, zaidi ya asilimia 90 ya uchumi wa Tanzania kuendelea kumilikiwa na wageni, huku kukiwa na kilio kikubwa cha Watanzania wazawa, kutaka wajengewe mazingira mazuri ya uwezeshaji ili kumiliki uchumi wa nchi yao kupitia migodi mikubwa ya madini na maeneo nyeti ya kiuchumi!

Tangu uhuru Watanzania wengi hawajawahi kushiriki kikamilifu katika kumiliki uchumi wa nchi yao. Uchumi wa nchi umeendelea kutawaliwa na wageni wakishirikiana na Watanzania wachache. Inashangaza sana kuona tuna ardhi nzuri, tuna madini na rasilimali kibao lakini tunaendelea kuwa masikini wa kutupwa, tukitegemea misaada ya wahisani ili kuendesha maisha yetu!

Huduma za jamii; elimu na afya zimedorora mno, shule za serikali zimebaki majengo tu, walimu hawatoshi, vitendea kazi kwa walimu havitoshi na zana za kujifunzia kwa wanafunzi havikidhi mahitaji halisi, madawati hayatoshi na hivyo watoto wengi wanakaa chini wakati wakisoma, na michango na ada sasa ni kero na vikwazo kwa watoto wengi kupata elimu.

Shule za serikali zimekuwa kama biashara, ada na michango inaanzia shule za msingi mpaka Chuo Kikuu. Ubaguzi katika elimu umekuwa rasmi, kwani kuna shule za matajiri na zile za watoto wa masikini, shule za matajiri zikiwa na huduma zote muhimu na za kisasa, wakati zile za walalahoi ziko hoi bin taaban.

Watoto wengi wa masikini sasa hawaendi shule na hivyo kusababisha kuongezeka kwa idadi ya watu wasiojua kusoma na kuandika, jambo linaloongeza umasikini miongoni mwa Watanzania, ambapo sasa inakadiriwa kuwa wananchi karibu asilimia 30 hawajui kusoma wala kuandika.

Hospitali na zahanati za serikali sasa si mahali pa kuokoa maisha ya watu bali ni mahali pa kufia ndiyo maana wakati fulani watu waliona tegemeo pekee la kupata tiba ni Loliondo kwa Babu, na wakubwa wanakwenda India kwani hospitalini hakuna dawa na huduma zingine muhimu za matibabu.

Mkukuta hauwezi kufanikiwa kama Serikali itaendelea kuwa tegemezi, bajeti ya serikali kutegemea misaada na mikopo kutoka kwa wageni kwa asilimia 35, na hivyo kusababisha manyanyaso na kuingiliwa kwa uhuru wetu kwa kupangiwa mambo ya kufanya na hawa wanaojiita wawekezaji. Hatuwezi kufanikiwa katika Mkukuta kwa mfumo huu, vinginevyo tutakuwa tunadanganyana.


ANDERS RASMUSSEN: Mkuu wa Nato aliyepata msukosuko kutokana na katuni ya Muhammad

 Anders Fogh Rasmussen

TRIPOLI
Libya

MKUU wa Umoja wa Kujihami wa nchi za Mharibi (Nato), Anders Fogh Rasmussen, amesema majeshi yake yamefanya kazi nzuri kusaidia Libya wakati wa mapinduzi anayoita ya kiraia dhidi ya hayati Kanali Muammar Gaddafi.

Rasmussen ameyasema hayo akiwa katika jiji la Tripoli kuhitimisha rasmi ujumbe wa Nato nchini Libya. Amesema Nato ingeweza kusaidia utawala mpya wa Libya kwa ulinzi na mageuzi kuelekea demokrasia iwapo wangeombwa.

Vikosi vya Nato vikifanya kazi chini ya amri ya Baraza la Umoja wa Mataifa kuwalinda raia vilianza harakati zake mwezi Machi wakati vikosi vya Gaddafi vilipoamua kupambana na waandamanaji. Ujumbe wa Nato umekamilisha rasmi kazi zake Libya dakika moja kabla ya kuingia saa sita usiku ya Jumatatu kwa saa za Libya.

Rasmussen alisema wamefanya mazungumzo na viongozi wa NTC akiwemo mwenyekiti Mustafa Abdul Jalil, kuhusu hatma ya Libya katika siku zijazo na mwelekeo wa mageuzi ya kidemokrasia.

"Mmechukua hatua kubadilisha historia na hatma yenu. Nasi tumewalinda. Pamoja tumefanikiwa. Libya hatimaye iko huru, kuanzia Benghazi hadi Brega, Misrata hadi kwenye milima ya Nafusa na Tripoli.

"Nchi nyingi za Kiarabu watatufahamu na kutuamini, wengi walifanya kazi pamoja kuwalinda ninyi. Ni matumaini yangu kuwa Libya yenye uhuru, demokrasia itajiunga nasi kama washirika siku moja lakini hilo ni uamuzi wenu. Hatma ya Libya sasa iko mikononi mwenu,” alisema.

Historia yake

Anders Fogh Rasmussen alizaliwa Januari 26, 1953, katika eneo la Ginnerup, Jutland, kwa mkulima Soren Rasmussen na Marie Rasmussen (nee Fogh). Ni mwanasiasa wa Denmark, na Katibu Mkuu wa 12 na wa sasa wa Nato. Rasmussen aliwahi kuwa Waziri Mkuu wa Denmark kuanzia Novemba 27, 2001 hadi 5 Aprili 2009.

Rasmussen alikuwa kiongozi wa chama cha Liberal (Venstre), na aliongoza muungano wa mrengo wa kulia na chama cha Conservative ambacho kilichukua madaraka mwaka 2001, na kushinda mara ya pili na ya tatu mnamo Februari 2005 na Novemba 2007. Serikali ya Rasmussen ilitegemea kuungwa mkono na Chama cha Watu wa Denmark (Danish People's Party), kufuatana na mapokeo ya serikali ya Wadanish wachache.

Katika kazi yake ya mwanzo, Rasmussen alikuwa mkosoaji wa hali ya ustawi, akiandika kitabu; Kutoka Serikali ya Jamii Hadi Serikali Ndogo mwaka 1993, ambapo alitetea mageuzi ya kina ya Denmark na mfumo wa ustawi wa jamii pamoja na uliberali. Hata hivyo, miaka ya 1990, maoni yake yalibadilika. Chini ya serikali ya Rasmussen, baadhi ya kodi zilipunguzwa, lakini muungano wa washirika wa Conservative ulirudia kudai punguzo la zaidi kwa ushuru na kodi ya kiwango kisichozidi asilimia 50.

Rasmussen alitekeleza mageuzi ya kiutawala kupunguza idadi ya manispaa (kommuner) na badala yake kuanzisha wilaya kumi na tatu (amter) na mikoa mitano. Rasmussen alitambua jambo hili kama “mageuzi makubwa katika miaka thelathini”. Hana uhusiano wowote na mtangulizi wake, Poul Nyrup Rasmussen, au mrithi wake, Lars Lokke Rasmussen; kufanana kwa majina yao ya mwisho ni jambo la kawaida nchini Denmark.

Amesomea lugha na masomo ya kijamii kutoka Shule ya Viborg Cathedral, 1969 – 1972, na Uchumi katika Chuo Kikuu cha Aarhus ambapo alifuzu mwaka 1978. Amekuwa akishiriki katika siasa karibu maisha yake yote na ameandika vitabu kadhaa kuhusu kodi na muundo wa serikali. Rasmussen na mkewe, Anne-Mette, aliyezaliwa 1958, wameoana mwaka 1978 na wana watoto watatu: Henrik (amezaliwa 1979), Maria (amezaliwa 1981) na Christina (amezaliwa 1984).

Alishikilia nafasi mbalimbali katika serikali na upinzani katika kazi yake, alishinda kwa mara ya kwanza kuingia katika bunge la Denmark kupitia Folketing mwaka 1978. Kwa ujumla, Rasmussen anapendelea katika ubinafsishaji na kupunguza ukubwa wa serikali. Hasa, hupenda kupunguza kodi na serikali kutoingilia katika ushirika na masuala ya mtu binafsi nk. Mwaka 1993 alipewa tuzo ya Adam Smith, na jamii ya Libertas, kutokana na yeye kuandika 'Kutoka Serikali ya Jamii Hadi Serikali Ndogo'.
Kuanzia 1987 hadi 1990 alikuwa Waziri wa Kodi na kuanzia 1990 akawa Waziri wa Uchumi na Kodi katika serikali ya Conservative iliyoongozwa na Poul Schlüter. Mwaka 1992 alijiuzulu nafasi yake ya uwaziri baada ya ripoti kutoka tume ya uchunguzi iliyoamua kwamba aliitolea Folketing (Bunge) taarifa zisizo sahihi na kamilifu kuhusu uamuzi wake wa kuahirisha malipo ya bili kadhaa za Regnecentralen na Kommunedata kutoka kwenye mahesabu ya mwaka. Rasmussen hakukubaliana na matokeo ya tume, lakini alikabiliwa na tishio la hoja ya kutokuwa na imani, aliamua kujiuzulu kwa hiari yake.

Uchaguzi wa 2001
Chama chake cha Kiliberali kilishinda katika uchaguzi wa Novemba 2001, kikiishinda serikali ya chama cha Social Democratic ya Poul Nyrup Rasmussen, na kumuwezesha kuunda Baraza lake la Mawaziri la kwanza. Uchaguzi huo ulileta mabadiliko makubwa katika siasa za Denmark. Ilikuwa ni mara ya kwanza tangu 1920 kwa Chama cha Social Democratic kupoteza nafasi yake kama chama kikuu katika Bunge.

Waziri Mkuu wa Denmark

Baada ya kuwa Waziri Mkuu, Rasmussen alijiweka mbali na maandiko yake ya awali na kutangaza kifo cha uliberali wa kisasa wakati wa uchaguzi wa kitaifa wa 2005. Alionekana kuvutiwa na mafanikio ya awali ya Tony Blair, Rasmussen sasa alionekana zaidi kupendelea nadharia ya Anthony Giddens na njia yake ya tatu. Kulikuwa na majadiliano katika jamii ya Libertas ya kutangua tuzo ya Rasmussen kama matokeo ya hili, ingawa haikutokea.

Serikali yake pia ilitunga hatua ngumu iliyoundwa kupunguza idadi ya wahamiaji kuingia Denmark, hasa wanaokimbilia kumo kutafuta makazi au kwa njia ya kupanga ndoa. Hata hivyo, serikali ya Rasmussen ilitegemea msaada wa Dansk Folkeparti, na ilikuwa vigumu kuchora mstari ulio sawa wa kugawa kati ya itikadi ya Rasmussen na siasa za serikali yake kutokana na maafikiano na Dansk Folkeparti.

Urais wa EU 2002

Rasmussen alishikilia nafasi ya urais wa kupokezana wa Umoja wa Ulaya kuanzia Julai hadi Desemba 2002, wakati ambao alijitolea kuunga mkono ajenda ya EU na kanuni elekezi ya mafundisho ya Ellemann-Jensen.

Wakati wa urais wa EU, alihusika katika tukio la kichunguzi na aliyekuwa Waziri Mkuu wa Italia, Silvio Berlusconi. Katika mkutano wa pamoja na waandishi wa habari Oktoba 4, 2002, Silvio Berlusconi alisema: “Rasmussen ni waziri mkuu handsome kuliko wote barani Ulaya. Nadhani nitamtambulisha kwa mke wangu kwa sababu yeye ni mzuri zaidi kuliko Cacciari”. Massimo Cacciari ni mwanafalsafa wa Italia na mwanasiasa mpinzani wa Berlusconi, na baadhi ya magazeti ya udaku yamewahi kuandika uvumi kuhusu madai ya uhusiano kati yake na mke wa pili wa Berlusconi, Veronica Lario. Rasmussen alishangazwa na kauli hii na Berlusconi haraka akamwambia angemwelewesha baadaye.

Ndoa za mashoga

Vyama vya wanandoa mashoga vimekuwepo kisheria nchini Denmark tangu 1989. Januari 2004, Rasmussen alisema imani yake kwamba mashoga wanapaswa kuoana katika sherehe za kidini, ambazo kwa sasa haziruhusiwi katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri la Denmark, lakini alisema ni lazima jumuiya za kidini ziamue kama kufanya sherehe kwa ajili ya wapenzi mashoga.

Uchaguzi wa 2005
Januari 18, 2005 Rasmussen aliitisha uchaguzi wa Februari 8, 2005. Alichelewesha wito huo kwa wiki kadhaa kwa sababu ya tetemeko la Bahari ya Hindi 2004 lililoua Wadanish kadhaa. Serikali yake imekuwa ikikosolewa na Wadanish wachache kwa kile walichodhani yalikuwa majibu mepesi ya mgogoro huo, ingawa walio wengi waliipongeza serikali kwa kukabiliana na maafa.

Ingawa waliounga mkono chama chake walipungua kutoka uchaguzi wa 2001, na kusababisha kupoteza viti vinne, Venstre ilikuwa na uwezo wa kudumisha umoja wake baada ya uchaguzi kwa njia ya mafanikio na vyama vingine, na 18 Februari, Rasmussen aliunda Baraza lake la Mawaziri la pili. Rasmussen ndiye mwanasiasa aliyewahi kupata "kura binafsi" nyingi kuliko mwanasiasa yeyote katika Bunge la Denmark, (kura 61,792).

Katuni ya Muhammad
Mgogoro mkubwa katika kipindi cha siasa za Rasmussen kinahusiana na katuni iliyochapishwa katika Jyllands-Poste, gazeti kubwa la Denmark. Septemba 2005, gazeti lilichapisha ukurasa mzima katuni 12 zikionesha tafsiri mbalimbali ya Muhammad, ikiwa ni pamoja na moja ambayo Muhammad alionekana na bomu katika kilemba chake. Baadhi ya shule za dini ya Kiislamu hazikuruhusu picha ya tafsiri ya Muhammad. Baadhi ya Waislamu waliiona katuni hiyo ni ya kukera.

Rasmussen alikataa ombi la mabalozi 11 wa nchi za Mashariki ya Kati kujadili suala hilo. Rasmussen ameuelezea utata huo kama mgogoro mkubwa zaidi wa kimataifa kwa Denmark tangu Vita Kuu ya Pili. Alinukuliwa baadaye akisema, “alikuwa na mashaka kwamba katuni ilionekana kwa baadhi ya Waislamu kama jaribio la Denmark kuwatusi au kukosa heshima dhidi ya Uislamu au Muhammad.”

Baada ya kuthibitishwa kama Katibu Mkuu wa Nato, Rasmussen alitangaza kujiuzulu uwaziri Mkuu wa Denmark tarehe 5 Aprili 2009.

Makala haya yameandaliwa na Bishop Hiluka kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya habari vya kimataifa.