Apr 5, 2011

Tunahitaji kongamano kuhusu ulemavu na virusi vya Ukimwi

Walemavu ni moja ya makundi ya watu waliotengwa kijamii, kisiasa, kitamaduni na kiuchumi


BISHOP J. HILUKA
Dar es Salaam

NIMEKUWA nikiona matangazo yanayotolewa kwa kutumia mchezo wa kuigiza kwenye vituo vya televisheni kuhusu dhana iliyojengeka kuwa watu wenye ulemavu hawana maambukizo ya Virusi vya Ukimwi, na hivyo kuwafanya wanaume wakwale kuwakimbilia.

Mwanzoni sikuwa nikiyachukulia matangazo haya kwa uzito mkubwa kwa kudhani kuwa zilikuwa ni fikra tu, lakini hivi majuzi nimegundua kuwa walioyatengeneza hawakufanya makosa baada ya mimi mwenyewe kusikia kauli za aina hiyo mitaani ninakoishi.

Ilianza kama hivi; nilikuwa nikipita eneo fulani nikabahatika kusikia mazungumzo ya vijana kadhaa yaliyonivutia kiasi cha kusimama kusikiliza, walikuwa wakiongea kuwa sasa ukimwi siyo tishio tena baada ya kupatikana kwa dawa ya ukimwi huko Loliondo, huku wengine wakijaribu kutahadharisha kuwa dawa hiyo bado haijathibitishwa kutibu ukimwi hivyo wasibweteke kwa kufanya ngono zembe wakitegemea kwenda Loliondo kupata kikombe cha babu.

Kijana mmoja aliyekuwa kimya muda mwingi aliibuka na kusema ndiyo maana yeye hataki wanawake wengine, amekuwa akiwafuata wanawake wenye ulemavu kwa kuwa hawana virusi vya ukimwi. Kwa kweli kauli yake ilinitisha sana, nikaamua kuwakabili kwa nia ya kuwaelimisha. Nashukuru Mungu kwani hatimaye walinielewa.

Kwa kweli jamii yetu bado ina uelewa tofauti kuhusiana na watu wenye ulemavu kitendo kinachopelekea kampeni za ugonjwa huu hatari kubaki kuwa ndoto. Kama taifa, nadhani tunahitaji Kongamano la wazi kuhusu Ulemavu na Virusi vya Ukimwi ili kuielimisha jamii kuhusiana na ugonjwa huu.

Kongamano hili lihusishe Mashirika ya Walemavu, Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (Tacaids), Serikali na mashirika ya umma yanayojishughulisha na walemavu ama yanayofanya kazi kwa niaba ya watu wenye ulemavu, mashirika wafadhili na mashirika ya kimaendeleo.

Kongamano la aina hii ni muhimu hasa tukitambua ukweli kwamba, maambukizi na kuenea kwa Virusi vya Ukimwi yamefikia viwango vya juu katika makundi ya watu waliotengwa kijamii, kisiasa, kitamaduni na kiuchumi, wakijumuisha watu wenye ulemavu, na ambao wameendelea kutengwa katika mikakati ya mipango ya kitaifa kuhusu Virusi vya Ukimwi nchini.

Tufanye hivi tukitambua umuhimu wa kusawazisha maswala ya ulemavu kama kiungo muhimu cha mikakati husika ili kupata maendeleo ya kudumu.

Vyombo vya kitaifa na kimataifa kuhusu Haki za Kibinadamu kama vile Sheria ya Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Kibinadamu na Makubaliano ya Kimataifa kuhusu Haki za Kibinadamu vinakubaliana kwamba kila mtu ana haki ya uhuru uliowekwa katika vyombo hivi, bila ubaguzi wa aina yoyote.

Pia jamii ielimishwe kanuni na malengo ya Makubaliano ya Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Watu wenye Ulemavu ya mwaka 2006, Azimio la Masharti kuhusu Virusi vya Ukimwi na Ukimwi - lililoafikiwa katika Kikao Maalum cha Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Virusi vya Ukimwi na Ukimwi mwaka 2001 na Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDG).

Licha ya vyombo hivi na juhudi zote za mataifa mengi wanachama wa Umoja wa Mataifa ambayo yameweka sahihi, watu wenye ulemavu wanaendelea kukumbana na vikwazo katika hali yao ya kutaka kushiriki kama watu wengine katika jamii huku haki zao zikiendelea kukiukwa kila mahali duniani, Tanzania ikiwa mojawapo.

Watu wenye ulemavu wanapaswa kuwa na nafasi ya kushiriki kikamilifu katika shughuli zote za maamuzi kuhusu sera na mipango, ikijumuisha zile zinazowahusu wao moja kwa moja; na umuhimu wa kufikia mazingira mwafaka ya kimaumbile, kisiasa, kijamii, kiuchumi na kitamaduni, kwa afya, elimu, habari na mawasiliano ili kuwezesha watu wenye ulemavu kufurahikia haki zote za kibinadamu na uhuru wote muhimu.

Ieleweke kuwa watoto; vijana na wanawake wenye ulemavu mara nyingi ndiyo watu walio katika hatari kubwa, ya kuumizwa ama kudhulumiwa, kutojaliwa, ama kuchukuliwa vibaya, kutendwa mabaya au kunyanyaswa wakiwa nyumbani ama nje ya nyumba.

Kongamano hilo litaisaidia serikali yetu kutambua baadhi ya mambo na kuujumuisha ulemavu katika mipango yake yote kama suala la jumla katika mikakati yote ya kupunguza umaskini na ya maendeleo.

Kongamano pia litasaidia kwa Mashirika ya Umma yanayohusiana na majukumu ya mikutano inayohusiana na Virusi vya Ukimwi kuwafanya walemavu kuwa wanachama na hivyo kuwashirikisha kikamilifu.

Litasaidia kutekeleza hatua za kulinda na kuimarisha haki hizo, mahitaji, usiri na utu wa watu wenye ulemavu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi na ambao ni wanachama wao. Litasaidia ushiriki katika kuunda sera kuhusu ulemavu na Virusi vya Ukimwi na Ukimwi
katika viwango vyote.

Mifumo ya Taifa ya ufuatiliaji na tathmini na ile ya uchunguzi wa idadi ya watu iliyopo ijumuishe viashirio maalum vya watu walio na ulemavu lakini ambavyo havijatambuliwa vyema, vinavyopaswa kutumiwa katika malengo ya mipango.

Mikakati ya Habari, Elimu na Mawasiliano katika viwango vyote ihakikishe inatoa habari, elimu na mawasiliano yanayoweza kufikiwa na watu wenye ulemavu wa kiakili, kukua, kimaumbile na ule wa milango ya hisi. Vituo vyote vinavyotoa huduma za utunzaji viweze kutoa habari za kina na mawaidha ya siri kwa watu hao.

Kongamano pia litasaidia kukuza na kuhimiza nafasi sawa kwa watu wenye ulemavu ili waweze kujifunza mafunzo ya kutoa ushauri nasaha na ya utunzaji (kama ya VCT na watoa ushauri nasaha waaminifu, na watunzaji wa nyumbani).

Ni wakati sasa wa kulisaidia kundi hili katika jamii yetu kwa mustakabali wa maendeleo ya nchi.

Naomba kuwasilisha.

No comments:

Post a Comment