Sep 21, 2011

MICHAEL SATA: Tishio la Rais Rupiah Banda wa Zambia katika nafasi ya urais

 Michael Sata

LUSAKA
Zambia

UCHAGUZI mkuu wa Zambia umefanyika Jumanne (Septemba 20) huku ukiacha homa na joto la uchaguzi katika kila pembe ya nchi hiyo. Michael Sata, kiongozi wa chama cha upinzani cha Patriotic Front (PF) na Rais Rupiah Banda wa chama tawala cha Movement for Multiparty Democracy (MMD) wamechuana vikali katika kinyang'anyiro cha kuwania urais wa nchi hiyo. Kumekuwa na milolongo mirefu nje ya vituo vya kupigia kura wakati Wazambia walipokuwa wanapiga kura katika kinyanganyiro kikali zaidi katika historia ya uchaguzi nchini Zambia.

Pia ziliripotiwa taarifa za kuchelewa kwa shughuli hiyo na kuwepo kwa ghasia lakini wachunguzi wa uchaguzi wamesema utaratibu mzima wa upigaji kura umekuwa mzuri. Tangu uchaguzi wa mwaka 2008, watu wengine, ikiwa ni zaidi ya milioni moja wamejiandikisha kuwa wapigaji kura, wengi wao ni vijana ambao hawana ajira. Bei ya juu ya madini ya shaba imeimarisha ukuaji wa uchumi wa Zambia lakini wananchi wa kawaida wanasema hawajapata faida yoyote kutokana na ukuaji huo.

Maelfu ya Polisi walipelekwa sehemu mbalimbali ili kuepusha ghasia na uuzaji wa shoka na vifaa vingine ambavyo vina uwezo wa kutumika kama silaha umepigwa marufuku katika kipindi hiki cha uchaguzi.

Watu milioni 5.2 walitarajiwa kupiga kura, hii ikiwa ni idadi kubwa zaidi ya watu waliojiandikisha kuwa wapiga kura katika uchaguzi wa Rais, wabunge na wawakilishi wa serikali za mitaa. Upigaji kura ulianza saa kumi na mbili asubuhi saa za Zambia na kumalizika saa kumi na mbili jioni ambapo wakati makala hii ikiandaliwa matokeo yalikuwa hayajaanza kutoka.

Chunguzi za maoni zilizofanywa kuhusiana na nafasi ya kushinda urais aliyonayo kila mgombea zilitoa matokeo yenye kutofautiana. Tawi la vijana la chama tawala liliamini kuwa Rais Rupiah Banda angeibuka mshindi katika uchaguzi huo wakati ambapo uchunguzi mwingine uliofanywa unaonesha kuwa Michael Sata angeshinda kwa asilimia 55 ya kura.

Sata aliyekuwa mwanachama wa chama tawala cha zamani cha UNIP cha kiongozi wa harakati za uhuru wa Zambia, Dk. Kenneth Kaunda, lakini aliamua kukihama chama hicho na kujiunga na chama kipya cha MMD ambacho kilichuana na UNIP katika uchaguzi wa rais wa mwaka 1990. Katika uchaguzi huo, Fredrick Chiluba, aliyewania kiti hicho kwa tiketi ya MMD aliibuka mshindi na kubaki madarakani kwa muda wa muongo mzima.

Hata hivyo, katika uchaguzi wa mwaka 2001 kinyume na matarajio ya Michael Sata, viongozi wa MMD walimteua Levy Mwanawasa badala yake kuwa mgombea urais katika uchaguzi wa rais kitendo ambacho kilimfanya Sata aamue kukihama chama hicho pia na kuunda chama chake cha Patriotic Front. Katika uchaguzi wa rais wa mwaka 2006 Sata alijitosa kwenye kinyang'anyiro hicho lakini alishindwa na Mwanawasa.

Mwaka 2008 Rais wa wakati huo wa Zambia, Levy Mwanawasa, alifariki dunia na kupelekea kuitishwa uchaguzi wa kabla ya wakati ambapo mara hiyo Michael Sata alichuana na Rupiah Banda. Ingawa Banda alitangazwa mshindi kwa kujipatia asilimia 40 ya kura akimshinda Sata kwa kura 35,000 tu, lakini Sata aliyepata asilimia 38 alidai kuwa matokea ya uchaguzi huo yalichakachuliwa. Hali hii ilisababisha ghasia kubwa ambazo zilizochochewa na baadhi ya wafuasi wa upinzani katika ngome zao za mijini.

Historia yake

Michael Chilufya Sata amezaliwa mwaka 1937 ba kabla ya kuanzisha chama chake cha Patriotic Front, Sata alikuwa waziri katika serikali ya Chiluba iliyoongozwa na Movement for Multiparty Democracy (MMD). Kama kiongozi wa chama cha upinzani cha Patriotic Front (PF), Sata, maarufu kama "King Cobra", amejitokeza kama mgombea urais na mpinzani katika kipindi cha marehemu Rais Levy Mwanawasa katika uchaguzi wa rais 2006, lakini alishindwa.

Miaka ya mwanzo

Michael Sata alizaliwa na kukulia katika eneo la Mpika, Mkoa wa Kaskazini. Alifanya kazi kama afisa wa polisi, afisa katika shirika la reli na mfanyakazi wa vyama vya wafanyakazi na biashara wakati wa utawala wa kikoloni. Sata alianza kushiriki kikamilifu katika siasa za Rhodesia ya Kaskazini ya wakati huo, mwaka 1963. Alifanya kazi kwa njia yake kupitia ngazi mbalimbali wakati wa chama tawala cha United National Independence Party (UNIP), na akawa kiongozi wa Lusaka mwaka 1985.

Kama kiongozi alijijengea jina kama mtu wa utekelezaji kwa mbinu mbalimbali. Alisafisha mitaa, alitia viraka barabara na kujenga madaraja katika mji. Baadaye alikuja kuwa Mbunge wa jimbo la Kabwata katika Lusaka. Ingawa alikuwa karibu na aliyekuwa Rais wa wakati huo, Kenneth Kaunda, aliamua kuwa mbali kutokana na mtindo wa kidikteta wa Kaunda na kisha alijiondoa kabisa katika chama cha UNIP na kujiunga na chama cha Movement for Multiparty Democracy (MMD) wakati wa kampeni za vyama vingi vya siasa mwaka 1991.
Baada ya Frederick Chiluba kumshinda Kaunda mwaka 1991, Sata alikuwa mmoja wa watu waliotambulika sana nchini Zambia. Chini ya chama cha MMD, alikuwa waziri wa serikali za mitaa, kazi na, afya ambapo, anajigamba, "mageuzi yake yameleta mfumo bora wa afya".

Mwaka 1995, aliteuliwa kuwa waziri asiye na wizara maalum, katibu wa maandalizi wa taifa katika chama wakati ambao mtindo wake wa kisiasa ulielezewa kama "unazidi kuchukiza".
Kuanziasha Patriotic Front

Mwaka 2001, rais wa wakati huo wa Zambia, Fredrick Chiluba alimteua Levy Mwanawasa kama mgombea wa MMD katika uchaguzi wa 2001. Katika kuchanganyikiwa, Sata alijiondoa MMD na kuanzisha chama kipya, Patriotic Front (PF). Aligombea katika uchaguzi wa 2001 lakini hakufanya vyema - chama chake kiliambulia kiti kimoja tu katika Bunge. Sata alikubali kushindwa na akaendelea na kampeni.

Sata aligombea tena uchaguzi wa rais wa Septemba 2006 kama mshindani aliyetumia umasikini katika sera ya mageuzi ya kiuchumi ya Mwanawasa. Sata wakati wote alitoa hotuba za kudhihaki. Katika tukio moja la kampeni, Sata alirarua kabichi mbele ya wafuasi wake. Kabichi hiyo ilimaanisha kigugumizi cha hotuba ya Mwanawasa, ambayo ni matokeo ya kujeruhiwa katika ajali ya 1992 ya gari.

Pia alimshutumu Mwanawasa kwa "kuiuza" Zambia kwa maslahi ya kimataifa, na katika tukio moja, aliifananisha Hong Kong kama nchi na Taiwan kama taifa huru. Kama majibu, China, ambayo ni mwekezaji katika shaba ya Zambia, ilitishia kukata mahusiano na Zambia kama akichaguliwa.

Matokeo ya uchaguzi wa awali yalimpa Sata ushindi, lakini matokeo zaidi yalimweka Mwanawasa katika nafasi ya kwanza na kumsukuma Sata nafasi ya tatu. Matokeo ya Muda ya kura kutoka majimbo 120 kati ya 150 yalihesabiwa na kumweka Mwanawasa juu zaidi ya asilimia 42 ya kura; Hakainde Hichilema asilimia 28; na Michael Sata asilimia 27. Wafuasi wa upinzani walipopata habari kwamba Sata yupo nafasi ya tatu, maandamano yalizuka mjini Lusaka. Oktoba 2, Tume ya Uchaguzi ya Zambia ilitangaza kuwa Mwanawasa alikuwa mshindi rasmi wa uchaguzi, na Sata katika nafasi ya pili kwa kuwa na asilimia 29.

Sata alikamatwa mnamo Desemba 2006, akituhumiwa kutoa tangazo la uongo la mali zake alipoomba kuwania urais mwezi Agosti, pamoja na mashtaka mengine. Alihojiwa na polisi na kutolewa kwa dhamana. Angepatikana na hatia, angefungwa kifungo jela miaka miwili. Kwa hatia hiyo, hangeruhusiwa pia kushikilia madaraka katika ofisi ya umma. Sata alisema madai dhidi yake yalikuwa ya kisiasa, na aliyakana mahakamani. Desemba 14, mashtaka yalifutwa na madai kuwa tamko la mali halikufanywa chini ya kiapo.

Mnamo Machi 15, 2007, Sata alifukuzwa Malawi muda mfupi baada ya kuwasili. Sata alisema kwamba alikwenda kukutana na wafanyabiashara, na alidai serikali ya Zambia inaeneza uongo kuwa alikuwa Malawi kumsaidia rais wa zamani wa nchi hiyo, Bakili Muluzi. Serikali ya Zambia ilikana, wakati serikali ya Malawi haikutoa maelezo yoyote. Aprili 6, mwanasheria wa Sata alisema kwamba alifungua kesi dhidi ya serikali ya Malawi kwa kukiuka haki ya mteja wake.

Baada ya kupoteza pasipoti yake jijini London mwishoni mwa 2007, Sata alipata nyingine, hata hivyo, Novemba 10, 2007, Waziri wa Mambo ya Ndani, Ronnie Shikapwashya, alisitisha pasipoti ya Sata kwa muda kwa sababu hakufuata taratibu muhimu na kuthibitisha kwamba alihitaji pasipoti mpya.

Sata alipata mshtuko wa moyo Aprili 25, 2008 na alihamishiwa Hospitali ya Milpark ya mjini Johannesburg, Afrika Kusini, ambapo alisemwa kuwa katika hali njema mwezi Aprili 26. Alipatanishwa na Rais Mwanawasa Mei 2008.

Kifo cha Mwanawasa na uchaguzi 2008

Baada ya Mwanawasa kupata kiharusi na kulazwa hospitali nchini Ufaransa, Sata alihoji rasmi afya ya Mwanawasa Julai 15, 2008 na kutoa mwito wa timu ya madaktari kupelekwa na Baraza la Mawaziri kumchunguza Mwanawasa, timu hii ingefichua hali halisi ya Mwanawasa. Mwanawasa alifariki dunia Agosti 2008. Agosti 25, Sata alipojaribu kuhudhuria mazishi ya Mwanawasa huko Chipata katika Jimbo la Mashariki, Maureen Mwanawasa, mjane wa Mwanawasa, aliamuru Sata aondoke, akisema kwamba alitumia tukio hilo kisiasa na kwamba hakuwahi kupatana na familia ya Mwanawasa. Sata, aliyeondolewa kutoka eneo hilo na usalama, alisema kwamba alikwenda pale kumuomboleza Mwanawasa na kwamba alikuwa na nia ya kuusindikiza mwili, alisisitiza kwamba upatanisho wake na Mwanawasa mwenyewe ulitosha kuhalalisha uwepo wake. Pia alisema kuwa Maureen Mwanawasa hakumtendea sawa.

Makala hii imeandaliwa na Bishop Hiluka kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya habari.


No comments:

Post a Comment