PARIS
JAJI ambaye alikuwa anasikiliza kesi ya tuhuma za ubakaji iliyokuwa inamkabili Mkurugenzi wa zamani wa Shirika la Fedha Duniani IMF, Dominique Strauss-Kahn, ametupilia mbali mashtaka hayo na hivyo kumuacha huru kigogo huyo.
Jaji Michael Obus alilazimika kuitupilia mbali kesi hiyo baada ya waendesha mashtaka kuwasilisha pendekezo la kufutwa kwa mashtaka hayo wakiamini hayana ukweli wowote na yalikuwa na lengo la kumchafua tu.
Baada ya Jaji Obus kutoa uamuzi huo ndipo Mwanasheria wa Strauss-Kahn, Benjamin Brafman, akachukua nafasi hii kuzungumza na waandishi wa habari ambapo alisema umma ulikosea kutokana na kuchukua hatua ya kuhukumu.
Naye Mwanasheria wa Nafissatou Diallo, Kenneth Thompson ametoa malalamiko kwa mahakama kwa hatua yake ya kutupilia mbali ombi lake la kuletwa kwa mwendesha mashtaka mwingine ambaye angesimamia kesi hiyo.
Strauss-Kahn mwenyewe baada ya kufutiwa mashtaka yaliyokuwa yanamkabili alimshuru mkewe pamoja na familia yake kwa kuwa naye pamoja kwenye kipindi kigumu cha kukabiliwa na tuhuma.
Hata hivyo, inasemekana kuwa Wafaransa wengi wanamuheshimu sana mwanasiasa huyu mwenye mwendo wa madaha, ambaye ni mashuhuri kwa jina la mkato la DSK. Mwenyewe amewahi kusema kwamba ana udhaifu katika mambo matatu: pesa, wanawake na uyahudi wake.
Upande mmoja wa familia ya Dominiques Strauss-Kahn ni Mayahudi wenye asili ya Morocco, nchi ya Kaskazini mwa Afrika na iliyokuja kuwa miongoni mwa makoloni ya Hispania.
Dominique Gaston Andre Strauss-Kahn alizaliwa Aprili 25, 1949 katika eneo la Neuilly Sur-Sein, karibu na mji mkuu wa Paris, Ufaransa. Amekulia Morocco kabla ya kuhamia Monaco na kusomea baadaye mjini Paris.
Mara nyingi akijulikana katika vyombo vya habari kama DSK, ni Profesa wa kiuchumi wa Ufaransa, mwanasheria, na mwanasiasa, na mwanachama wa Chama cha Kisoshalisti cha mrengo wa kushoto. Amekuwa pia akiwika katika jukwaa la kisiasa nchini Ufaransa kwa miongo miwili sasa.
Strauss-Kahn alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Fedha Duniani (IMF) tangu tarehe 28 Septemba 2007, kwa msaada wa Rais Nicolas Sarkozy, na ametumikia katika nafasi hiyo hadi alipojiuzulu tarehe 18 Mei 2011.
Mei 2011, Strauss-Kahn alikamatwa katika mji wa New York na kushtakiwa kwa unyanyasaji wa kijinsia wa mfanyakazi wa hoteli aliyeingia chumbani kwake, lakini mashitaka yote yalifutwa baadaye kwa ombi la upande wa mashtaka. Strauss-Kahn alikana mashtaka yote. Mwanasheria wa Wilaya ya New York aliondoa mashtaka tarehe 22 Agosti 2011, kutokana na upande wa mlalamikaji kushindwa kuthibitisha, na mahakama ilikubali.
Strauss-Kahn au DSK, kama ulivyo umaarufu wake kwenye siasa za Ufaransa, alifuata nyayo za wazee wake na kuelemea mrengo wa kushoto. Alijiunga mapema na Chama cha Kisoshialisti ambacho mnamo mwaka 1971 kilikuwa nguvu muhimu ya mrengo wa kushoto uliokuwa ukiongozwa na Francois Mitterand.
Katika miaka ya ’80 na ’90 alikabidhiwa nyadhifa tofauti za kisiasa, hadi mnamo mwaka 1997 alipochaguliwa kuwa Waziri wa Uchumi, Fedha na Viwanda.
Yeye ndiye aliyetandika misingi ya Ufaransa kuweza kujiunga na sarafu ya euro. Wengi wanakiri kwamba Strauss-Kahn alifanikiwa kuunganisha mawazo yakinifu ya kiuchumi na yale ya ujamaa wa kidemokrasia. Kwa mfano, yeye ndiye aliyepunguza muda wa kufanya kazi kwa wiki na wakati huo huo kuanzisha utaratibu wa kubinafsishwa mashirika ya serikali.
Mnamo mwaka 1999, Strauss-Kahn alijiuzulu kwa tuhuma za kuhusika na rushwa, ingawa baadaye alitakaswa na tuhuma hizo. Baada ya kujizulu, DSK alikuwa akijishughulisha zaidi na kazi yake ya kusomesha kwenye vyuo vikuu.
Miongoni mwa mengineyo, alikabidhiwa jukumu la kusimamia chuo kikuu mashuhuri cha Institut d’Etudes Politiques (IEP), ambako binafsi ndiko alikosomea. Wakati huo huo akateuliwa kuwa mshauri wa Shirika la Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo barani Ulaya (OECD).
Staruss-Kahn alirejea katika jukwaa la kisiasa mwaka 2001 na kuongoza kampeni ya uchaguzi ya Lionel Jospin mnamo mwaka 2002 alipopigania kuwa rais wa Ufaransa.
Akiwa mbunge, Strauss-Kahn alipigania sana masuala yanayohusu Ulaya na kuunga mkono ushirikiano kati ya Ujerumani na Ufaransa kama injini ya Umoja wa Ulaya. Yeye alikuwa miongoni mwa wale waliokuwa wakiunga mkono katiba ya Umoja wa Ulaya iliyokataliwa na Ufaransa mnamo mwaka 2005.
Magazeti ya Ufaransa yakiandika taarifa za kashfa ya Strauss-Kahn; baada ya kukaa kwenye upande wa upinzani kwa miaka kadhaa, Strauss-Kahn akajitokeza kutaka kupigania kiti cha rais mwaka 2006 kwa tiketi ya chama chake cha Kisoshalisti cha mrengo wa kushoto, lakini alishindwa na Ségolène Royal. Wakati huo, Strauss-Kahn alikuwa akifikiria umuhimu wa kuunda chama kipya cha mrengo wa kushoto.
Lakini kabla ya kufanya hivyo, akajikuta anateuliwa kuwa mkuu wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), akiwa amependekezwa na mpinzani wake wa kisiasa, Rais Nicolas Sarkozy.
Lakini mara tu baada ya kuchaguliwa kuongoza shirika hilo, IMF ikakafanya uchunguzi dhidi ya kiongozi wake mpya. Lengo lilikuwa kutaka kujua ikiwa bosi huyo alitumia vibaya madaraka yake na kumpendelea mtaalamu wa kike wa kiuchumi, Piroska Nagy.
Naggy, ambaye alisemekana kuwa na uhusiano na Strauss-Kahn, alikubali kupokea fidia mnamo Agusti mwaka 2008 na kuacha kazi yake kutoka IMF.
Baada ya Straúss-Kahn kuomba radhi wakati ule, baraza la shughuli za utawala likapiga kura kwa sauti moja kumruhusu kuendelea na kazi yake. Uchunguzi haukutoa ushahidi wowote wa madai ya kutumia vibaya madaraka yake.
Februari mwaka 2010, Strauss Kahn alisema katika mahojiano ya radio kwamba anaweza kuamua kutetea kiti cha rais kwa tiketi ya Chama cha Kisoshalisti dhidi ya Rais Sarkozy wa kutoka chama tawala cha UMP na, kwa hivyo, kuachana na IMF kabla ya wakati wake kumalizika.
Maisha binafsi
Strauss-Kahn amemuoa mwandishi habari na mtangazaji wa televisheni, Anne Sinclair, tangu mwaka 1991. Ana watoto wanne wa kike kutoka ndoa zake mbili za mwanzo, mmoja kati yao ni kwa mke wake wa pili, Brigitte Guillemette, aliyemuoa mwaka 1984.
Ukiacha lugha yake ya Kifaransa, anazungumza pia kwa ufasaha Kiingereza na Kijerumani na pia ana ujuzi mzuri wa Kihispania na Kiarabu.
Nafasi muhimu alizoshika
- Waziri wa Viwanda na Biashara ya Nje, 1991-1993.
- Waziri wa Fedha, Uchumi na Viwanda, 1997-1999 (kujiuzulu).
- Mbunge wa Bunge la Ufaransa kupitia Val d'Oise, 1986-1991 (na waziri 1991), akachaguliwa tena 1997, kisha akawa waziri 2001-2007 (alijiuzulu baada ya kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa IMF 2007).
- Alichaguliwa tena miaka ya 1986, 1988, 1997, 2001, 2002, 2007.
- Diwani wa Mkoa wa Ile-de-France, 1998-2001 (kujiuzulu).
- Meya wa Sarcelles, 1995-1997 (kujiuzulu).
- Naibu meya wa Sarcelles, 1997-2007 (alijiuzulu baada ya kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa IMF 2007), akachaguliwa tena mwaka 2001.
- Diwani wa manispaa ya Sarcelles, 1989-2007 (alijiuzulu baada ya kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa IMF 2007), alichaguliwa tena 1995, 2001.
- Rais wa jamii wa Agglomeration katika Val de France, 2002-2007 (alijiuzulu baada ya kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa IMF 2007).
- Mwanachama wa jumuiya ya Agglomeration wa Val de France, 2002-2007 (alijiuzulu baada ya kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa IMF 2007).
- Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Fedha Duniani, 2007-2011 (alijiuzulu kwa tuhuma za shambulio la ngono).
Makala hii imeandaliwa na Bishop J. Hiluka kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya habari vya kimataifa
No comments:
Post a Comment