Feb 17, 2011

Tunahitaji madaraka kwa watu na Afrika mpya

Joseph-Desire Mobutu
 
Rais Muammar Gaddafi wa Libya
 
 Teodoro Obiang Nguema Mbasogo wa Equatorial Guinea

BISHOP J. HILUKA
Dar es Salaam

KILICHOTOKEA Tunisia, na sasa Misri ni kiashirio tu kwamba Afrika sasa imeamka kutoka kwenye usingizi wa ukandamizwaji wa wanyonge, wananchi wameamua kujiunga na harakati za kutafuta maisha bora. Wanadai demokrasia ya kweli, wanaandamana dhidi ya ufisadi na wanatilia nguvu zaidi maridhiano. Jamii yenye mwamko imejitokeza inayoweza kubadilisha hali.

Wakati umefika sasa kwa viongozi wa nchi za Afrika kubadilisha mfumo wanaotumia kututawala kwani muda wa ufisadi na wanasiasa madikteta unakaribia mwisho. Licha ya matukio kadhaa ya kukatisha tamaa, watu wameanza kudai mengi kutoka kwa viongozi wao. Wanadai uwajibikaji na demokrasia ya kweli kwa wanasiasa na serikali zao, huku mashirika ya ndani na asasi zisizo za kiserikali zikisaidia kufanya sauti zao zisikike.

Bara la Afrika ndilo bara linaloongoza kwa marais wake kushika madaraka kwa muda mrefu kuliko mabara yote duniani. Viongozi wa Afrika wamekuwa na tabia ya kubadilisha katiba ili wachaguliwe tena baada ya muda wao wa uongozi unapomalizika kikatiba. Wasipochanguliwa hutumia jeuri na mabavu.

Hivi Waafrika tumelogwa au kitu gani? Kwa nini viongozi wa Kiafrika wanapoingia madarakani wanang'ang'ania utadhani wana hakimiliki ya kutawala? Hebu angalia mfano mdogo hapa chini:

Joseph-Desire Mobutu aliyejiita baadaye Mobutu Sese Seko, rais wa zamani wa Zaire (sasa DR Congo) alishika madaraka kwa miaka 32, aliingia madarakani mwaka 1965 hadi alipopinduliwa mwaka 1997, na baadaye kufia uhamishoni tarehe 7 Septemba, 1997.
 
Omar Bongo, rais wa zamaniwa Gabon alikaa madaraka kwa miaka 42, alishika madaraka Novemba 1967 na ndiye aliyekaa madarakani muda mrefu zaidi kuliko wote, kabla hajafa mwaka 2009 na madaraka kurithishwa na mwanaye, Ali Ben Bongo.

Rais Muammar Gaddafi wa Libya yupo madarakani kwa miaka 41, aliingia madarakani mwaka 1969 kwa njia ya mtutu, baada ya kusaidiwa na jeshi. Inasemekana ana mpango wa kumrithisha mwanaye madaraka atakapostaafu.

Rais wa Angola, Jose Eduardo Dos Santos yupo madarakani kwa miaka 34, aliingia madarakani mwaka 1976 hadi leo bado anang'ang'ana.

Rais Teodoro Obiang Nguema Mbasogo wa Equatorial Guinea, ambaye hivi karibuni amechaguliwa kuwa mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU) aliingia madarakani mwaka 1979 hadi sasa amekuwa aking'ang'ania madaraka kwa miaka 31.

Rais Denis Sassou Nguesso wa Jamhuri ya Congo, huyu aliingia madarakani mwaka 1979 kwa mapinduzi lakini wakati wa mfumo wa vyama vingi alipoteza urais mwaka 1992 dhidi ya Pascal Lissouba. Alifanikiwa kurudi maradakani mwaka 1997 na kubaki hadi sasa.

Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe amekaa madarakani miaka 30, aliingia madarakani mwaka 1980 baada ya nchi hiyo kupata uhuru. Mpaka sasa anaendelea kuongoza taifa hilo linalokabiliwa na hali mbaya ya uchumi na alikataa kuachia madaraka hata pale ilipothibitishwa kwamba kashindwa na Tsvangirai.

Rais Hosni Mubarak wa Misri ana miaka 30 madarakani, aliingia madarakani mwaka 1981 na ametawala hadi sasa anapokabiliwa na maandamano ya wananchi kutaka kumng'oa.

Rais wa Cameroon, Paul Biya, ana miaka 28 madarakani, aliingia madarakani 1982 akichukuwa nafasi ya mtangulizi wake, Ahmadou Ahidjo.


Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda, ana miaka 25 madarakani, aliingia madarakani mwaka 1986 baada ya mapambano makali ya msituni. Amekuwa bingwa wa kubadilisha katiba ili aendelee kutawala na mwaka huu 2011 anagombea tena.

Zine al-Abiden Ben aliyekuwa rais wa Tunusia na kung'olewa hivi karibuni kwa maandamano ya wananchi, aliingia madarakani mwaka 1987 na kudumu madarakani kwa miaka 23.

Rais Omar Al-Bashir wa Sudan aliingia madaraka kwa mapinduzi mwaka 1989, hadi sasa akiwa amekaa madarakani kwa miaka 21 bado kang'ang'ania madaraka.

Frederick Chiluba, rais wa zamani wa Zambia aliyeingia madarakani mwaka 1992, baada ya miaka yake kumi hapo mwaka 2002, alipendekeza kufuta kifungu cha katiba ambacho kinamkataza kugombea tena awamu ya tatu lakini alikumbana na upinzani mkubwa.

Rais Idris Derby aliyekuwa mkuu wa majeshi, aliingia madarakani mwaka 1990 akimng’oa rasi Hissene Habre na kujitangaza rais wa Chad hadi sasa.

Hata hapa Tanzania tumeshuhudia pale Salmin Amour, rais wa zamani wa Zanzibar aliyeingia madarakani mwaka 1990 alipotaka kubadilisha kifungu cha katiba mwaka 2000 kilichomzuia kugombea tena awamu ya tatu, lakini akakumbana na upinzani mkali ulioongozwa na rais aliyemaliza muda wake hivi karibuni, Aman Abeid Karume.

Rais Yahya Jameh wa Gambia aliingia madarakani kwa mapinduzi mwaka 1994 na ameendelea kubaki madarakani hadi sasa.

Rais Mwai Kibaki wa Kenya, aliingia madarakani mwaka 2002, japo hajakaa muda mrefu lakini anaendelea kuongoza baada ya kukataa kuachia madaraka hata pale ilipoonekana kuwa kashindwa na Raila Odinga na kusababisha mauaji ya maelfu ya Wakenya na wengine kukosa makazi.

Hali hii imeendelea hata huko Ivory Coast, baada ya Laurent Gbagbo aliyeshindwa uchaguzi na Alassane Ouatara, lakini akajitangaza rais. Hivi hali hii itaendelea kwenye bara hili hadi lini?

Viongozi wa nchi za Afrika pamoja na kumshutumu Gbagbo lakini wengi wao wanakosa ujasiri wa kumkabili kwa kuwa ni waroho wa madaraka na uongozi wao una utata. Naridhishwa na maamuzi ya Umoja wa Afrika ya kutafuta ufumbuzi wa mgogoro wa kisiasa nchini Ivory Coast kati ya Rais Laurent Gbagbo na Alassane Ouattara kwa kuiteua Tanzania na nchi za Mauritania, Nigeria na Afrika Kusini, zitakazoungana na Burkina Faso kushughulikia mgogoro huo, lakini naipinga Chad, kwa kuwa rais wake, Idris Derby anakosa sifa za kumfanya kuwa mpatanishi.

Jeuri ya sasa ya viongozi wa Kiafrika inatokana na ukweli kwamba wanachama wa AU hushindwa kutafuta njia nyingine mbadala ya kumaliza migogoro ya uchaguzi na kuishia kuhimiza mgawanyo wa madaraka, kitendo kinachoendekeza uchafuzi wa uchaguzi huru na wa haki, kwa kuwa tu itakuwepo nafasi kwa vyama tawala kufanya mazungumzo ya usuluhishi yatakayowezesha kupatikana ufumbuzi kwa kugawana madaraka.

Yaani ukiweza kuingia madarakani kwa mtutu wa bunduki au kwa ubabe wowote ni ruksa. Ukitumia mbinu nyingine za “kisayansi” hakuna shaka ili mradi uwe mwepesi wa kushawishi na kuitisha mazungumzo yatakayozaa mgawano wa madaraka kwa wapinzani wakubwa. Hali hii itatupeleka wapi? 
 
Hii imeonekana Kenya ambako inaaminika kuwa ndiyo jaribio la kwanza la mbinu hii, ilipoonekana inawezekana, Zimbabwe ikafuatia ambapo AU ilibariki Mugabe akae na wapinzani wake na kufikia maafikiano kama ilivyokuwa Kenya. Hii inamaanisha aliyeibiwa anagawana na mwizi kilicho chake!

SOURCE: KULIKONI

No comments:

Post a Comment