Feb 17, 2011

Sekondari za Kata: Maji tumeyavulia nguo hatuna budi kuyaoga

 Sekondari ya Kata

 Wanafunzi wa sekondari za kata

BISHOP J. HILUKA
Dar es Salaam

NIMESIKILIZA kwa makini hoja mbalimbali za Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wakati wakiijadili hotuba ya Rais Jakaya Kikwete, wengi wao wameongelea suala la sekondari za kata kwa hoja tofauti, wale wa chama tawala (CCM) wakiziunga mkono na kuisifu Serikali ya Awamu ya Nne kwa kuzianzisha shule hizo wakati wale wa Kambi ya Upinzani wamezibeza.

Kwa mtu yeyote aliye makini, matokeo ya mtihani wa form four mwaka jana yametoa picha halisi ya taifa tunalojenga japo wanasiasa wa chama tawala wanataka tuamini kuwa nchi inafanya vizuri katika sekta ya elimu. Hawa wenzetu nadhani wapo bize kujifikiria wao wenyewe na chama chao, watakavyoweza kubaki madarakani, milele na milele, badala ya kuifikiria nchi na wananchi kwa jumla.

Nawaomba viongozi wa kisiasa waache kutoa maamuzi ya kielimu yasiyokuwa na tija kwa kuwa tu wanataka kujinufaisha kisiasa wao binafsi na vyama vyao. Maamuzi ya kisiasa yasiyokuwa na tija ni pamoja na kupingana hata na tafiti zinazoonesha hali halisi ya elimu nchini.

Tungependa kusikia hoja zao kuhusu nini kifanyike? Je, tuanze upya? Tuanzie wapi na tufanye nini? Hii ni hatari inayotokea tunapoamua kuongozwa na fikra za wanasiasa na kubeza maoni ya kitaalam.
Ni hawa hawa wanasiasa kwa sababu wanazojua wao walipiga marufuku mitihani ya kitaifa ya darasa la nne na kidato cha pili! Katika elimu ya msingi kwa mfano, watoto wanamaliza shule bila ya kuzijua stadi muhimu za kusoma, kuandika na kuhesabu. Mtihani wa darasa la nne ulikuwa ni kipimo cha uelewa wa mwanafunzi kama anajua kusoma, kuandika na kuhesabu.
Hizi ndizo stadi za msingi anazopaswa kuzijua kila mwanafunzi. Lakini wanasiasa wetu wamefuta mtihani huu, hivyo kila mtoto hivi sasa ana uwezo wa kumaliza darasa la saba hata kama hajui kusoma. Na imedhihirika kuwa hata wanafunzi wasiojua kusoma na kuandika huchaguliwa kusoma katika sekondari za kata.
Hata kwa sekondari, matokeo ya kidato cha nne yaliyotoka hivi karibuni yamedhihirisha athari ya kuupiga marufuku mtihani wa kidato cha pili. Sijui wanasiasa wetu wamefanya hivi kwa faida ya nani?

Ukiangalia matokeo ya kidato cha nne ya mwaka jana, utagundua kwamba robo tatu ya wahitimu katika shule za sekondari za kata zilizojengwa kidhaifu na kuwekwa kidhaifu bila walimu bora, vitabu, na maabara, wahitimu wake wamepata zero "0".

Serikali ya Awamu ya Nne, imewahi kukiri kwamba ilikurupuka katika ujenzi wa sekondari za kata ambazo kwa asilimia kubwa zimekosa sifa za kupokea wanafunzi, zina upungufu wa walimu na vitabu.

Haya yalisemwa mwaka 2008, na aliyekuwa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Ludovic Mwananzila, wakati wa mahafali ya tatu ya kidato cha sita katika Shule ya Sekondari ya St Matthews, Wilaya ya Mkuranga, mkoani Pwani.
Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal, wakati huo akiwa Mgombea Mwenza wa Urais kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), aliwataka wananchi wa mkoa wa Tabora kuwapuuza wanaotoa kauli za bezo dhidi ya mpango wa serikali kujenga shule za sekondari za kata.

Alisema kuwa asilimia zaidi ya 50 ya wanafunzi wanaofaulu na kuingia vyuo vikuu kwa sasa wanatoka katika shule za kata. Eti wanapatikana baada ya mpango mzuri wa serikali ya CCM kuamua kujenga shule hizi.

Nilishangazwa na kauli toka kwa kiongozi msomi kama huyo kwa kutotambua kuwa waliomaliza kidato cha nne mwaka jana 2010 ndio Form Four wa kwanza katika shule za kata, na ndio tumepata 'gradutes' wa kwanza ambao zaidi ya asilimia 80 ya wanafunzi wa shule hizi wamefeli. Sasa hao wanaoingia vyuo vikuu ni wa sekondari zipi za kata? Tunatoa takwimu za uongo kwa faida ya nani?
Tukubali au tusikubali tayari sekondari za kata zipo na hatuna namna ya kuziondoa, zimepokea wanafunzi ambao ni wadogo zetu na watoto wetu na sidhani kama tunahitaji ushabiki wa kisiasa kuzijadili wakati vijana wetu wanasoma, tuangalie tutakavyosaidia kuziboresha.

Bila kuwekeza kwa dhati katika ubora wa elimu tutakuwa tunapalilia ufa mkubwa uliopo kati ya wenye nacho (wanaosomesha watoto wao shule bora zenye gharama) na wasio nacho (wanaosomesha watoto shule hizi za kata).

Tusipindishe mambo kwani kushuka kwa ufaulu wa kidato cha nne kumetokana na uhaba wa walimu hasa kwa shule za kata. Sababu nyingine ni pamoja na ukosefu wa maabara shuleni, maktaba, vifaa vya kufundishia na kujifunzia, ukosefu wa makazi bora na motisha kwa walimu.

Nakubaliana na mtu mmoja aliyewahi kusema kuwa hili ni janga la kitaifa, taifa lisilokuwa na wajuzi ni taifa la vibarua na makuli, kwa takwimu ya zaidi ya asilimia 80 ya watahiniwa wote kufeli na kuingia kwenye kundi la vibarua na makuli au hata vibaka na majambazi. Ni aibu kwa rais, ni aibu kwa waziri, ni aibu kwa wazazi... ni aibu kwa mfumo mzima wa utawala.

Inasikitisha sana kuona Wizara ya Elimu imekuwa wizara ya majaribio ya sera, kila waziri anakuja na msimamo wake. Halafu cha kushangaza mara wanapoanza kutekeleza mikakati hiyo ukiwapinga wanakuwa wakali kama pilipili na wa kwanza kukanusha.

Kwa hakika hii ni aibu kubwa, tumeonesha kukosa umakini katika maamuzi ya serikali. Cha kushangaza maofisa wanaohusika kuishauri serikali katika masuala ya elimu na mengine wana elimu nzuri tu, tatizo ni wataalam ambao ni watumwa wa wanasiasa.

Wapo watendaji wengi tu pale Makao Makuu ya Wizara ya Elimu ambao japo hawakubaliani na mambo mengi ambayo serikali (wanasiasa) wanayashinikiza katika suala la maendeleo ya elimu, wanalazimika kuyakubali.

Tunawaomba wanasiasa kuacha kukurupuka kutaka kufanya mambo kwa haraka na kwa muda mfupi, ili wapate kujinadi, wakati muafaka ufikapo, kwa shabaha ya kubaki madarakani kwa sifa zisizomnufaisha mtu mwingine katika jamii. Nadhani ni uchu wa madaraka tu unaoleta ukurupukaji huu. Kwa nini tunakosa mpango wa muda mrefu?

Kama tunaendeleza ushabiki wa kisiasa na kulumbana kuhusu ujenzi wa shule za sekondari za kata, ambazo maendeleo yake hayakupangwa kisayansi, tunawezaje kuanza kuzungumzia kujenga dispensari katika kila kata wakati hili la sekondari halijafanikiwa? Hivi tunaitakia mema nchi hii kweli?
Tumeshalaumu sana, tumeshasema sana, tumejisifia sana, sasa ni muda muafaka wa kujadili haya bila ushabiki, kama mambo yakiendelea kama yalivyo, basi tutajikuta tuna pengo kubwa la wananchi/vijana wasio na ujuzi (elimu ya kutosha) kwenye nyanja mbalimbali wakati wa uundwaji wa Shirikisho la Afrika Mashariki.
Alamsiki

SOURCE: KULIKONI

No comments:

Post a Comment