Jun 1, 2012

ABDULLAH SENUSSI: Jasusi na shemeji wa Kanali Gaddafi anayehusishwa na uhalifu wa kivita

Abdullah Sanussi


Mauritania

TAARIFA za vyombo vya habari vya kimataifa imeikariri Serikali ya Libya kusisitiza kuwa ina uwezo wa kumfanyia kesi mkuu wa zamani wa usalama, Abdullah Sanussi, na imeomba arejeshwe nyumbani. Kumetolewa wito kuwa Sanussi apelekwe Mahakama ya Jinai ya Kimataifa, ICC, mjini Hague au Ufaransa, ambako ameshtakiwa kwa ugaidi.

Ingawa hakuna picha zilotolewa za Abdullah Sanussi tangu kuarifiwa kuwa amekamatwa nchini Mauritania, wakuu wa Libya wanasema wana hakika kuwa ametekwa, na wameomba kuwa arejeshwe nyumbani.

Mkuu huyo wa ujasusi wa Kanali Gaddafi, anakabiliwa na mashtaka kadhaa, pamoja na yale yanayohusu mauaji. Serikali ya mpito ya Libya ina hamu kuwa arejeshwe nyumbani kufikishwa mahakamani haraka.

Lakini kuna wasiwasi, kwa sababu serikali kuu ya Libya bado haina nguvu, na bado hakuna mfumo wa sheria unaoweza kufanya kesi ya al-Sanussi au viongozi wengine wa zamani wa utawala wa Gaddafi.

Ufaransa imeshasema kuwa itapenda kumpata al Sanussi kwa sababu ya kuhusika kwake na shambulio la bomu kwenye ndege ya Ufaransa mwaka wa 1989.

Pia kuna wito mwengine kuwa mwanasiasa huyo apelekwe ICC, ambako anakabiliwa na mashtaka ya kushiriki kwenye shughuli za kufyeka upinzani wa Libya mwaka jana.

Wakuu wa Mauritania bado hawakusema vipi watajibu maombi hayo, na inaweza kuchukua muda kabla ya afisa huyo kurejeshwa nyumbani - afisa aliyechukiwa na kuogopwa kabisa nchini mwake.

Historia yake

Abdullah Senussi amezaliwa tarehe 5 Desemba, mwaka 1949. Raia huyu wa Libya alikuwa mkuu wa upelelezi na shemeji wa aliyekuwa rais wa Libya, Kanali Muammar Gaddafi. Alikuwa amemuowa shemeji wa Kanali Gaddafi.

Maafisa wa polisi wa Kiskochi wana mpango wa kumhoji al-Senussi kuhusu uhusiano wake na mabomu yaliyoripua Lockerbie, wakiongeza matarajio ya kuibua kesi ya pili kuhusu shambulio la Lockerbie.

Kwa mujibu wa gazeti la The Guardian la Uigereza, al-Senussi alikuwa na sifa ya ukatili tangu miaka ya 1970. Katika miaka ya 1980 alikuwa mkuu wa usalama wa ndani nchini Libya, katika kipindi ambacho wapinzani wengi wa Gaddafi waliuawa. Baadaye, alielezewa kama mkuu wa upelelezi wa kijeshi, lakini haijawekwa wazi kama kweli aliwahi kuwa na cheo hicho.

Mwaka 1999 alikutwa na hatia wakati akiwa hayupo mahakamani nchini Ufaransa kwa kushiriki kwake katika shambulio la bomu 1989 katika ndege ya abiria iliyokuwa ikiruka Niger ambalo lilisababisha vifo vya watu 170. Walibya wanaamini kuwa hawezi kukwepa tuhuma za mauaji ya wafungwa 1,200 katika jela ya Abu Salim mwaka 1996. Pia anadhaniwa kuwa nyuma ya mauaji ya mwaka 2003 ya mrithi wa ufalme wa Saudi Arabia, Prince Abdullah.

Mtandao wa Ubalozi wa Marekani umemuelezea al-Senussi kama msiri wa Gaddafi ambaye alifanya "mipango yake mingi ya matibabu". Wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Libya vya 2011, al-Senussi alilaumiwa kwa kuchochea mauaji katika mji wa Benghazi na kuajiri mamluki wa kigeni. Aliaminika kuwa na maslahi makubwa ya kibiashara katika Libya.

Tarehe 1 Machi 2011, gazeti la Libya la Quryna lilitoa taarifa kwamba Gaddafi alimfukuza kazi al-Senussi.

Tarehe 16 Mei 2011, mwendesha mashitaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai alitangaza kuwa anatafuta kibali cha kukamatwa kwa Abdullah Senussi kwa madai ya uhalifu dhidi ya binadamu.

Tarehe 21 Julai 2011, vyanzo vya upinzani nchini Libya vilidai kuwa Senussi alikuwa ameuawa katika shambulizi lililofanywa na waasi wenye silaha katika jiji la Tripoli, hata hivyo, saa chache baadaye vyanzo hivyo kukanusha madai yao yaliyotolewa kabla na hata baadhi wakasema kuwa huenda alikuwa amejeruhiwa tu.

Tarehe 30 Agosti 2011, kulikuwa na taarifa kuwa watoto wote wawili; wa Senussi, Mohammed Abdullah al-Senussi, na wa Kanali Muammar Gaddafi, Khamis, waliuawa wakati wa mapigano na vikosi vya NATO na NTC katika eneo la Tarhuna. Mnamo mwezi Oktoba, kituo cha televisheni cha Arrai, mtandao uliokuwa ukimuunga mkono Kanali Gaddafi nchini Syria ulithibitisha kuwa Mohammed Senussi na Khamis Gaddafi walikuwa wameuawa tarehe 29 Agosti.

Tarehe 20 Oktoba, Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Niger, Mohammad Bazoum, aliliambia shirika la habari la Reuters kwamba alikuwa kakimbilia Niger. Hata hivyo, mpiganaji wa Libya baadaye aliliambia gazeti la The Guardian kwamba waasi walikuwa wanashikilia watu wengine watatu ambao walikuwa katika msafara wa Gaddafi wakati alipouawa na kwamba aliamini kuwa mmoja wao alikuwa Senussi.

Watu wengine wawili walitambuliwa kama mwana wa Gaddafi aliyeuawa, Mutassim na mmoja wa makamanda wake wa kijeshi, Mansour Dhao, ambaye alikuwa bado hai na kuthibitisha utambulisho wake, pamoja na maelezo ya kifo cha mtoto wa Gaddafi, kwa shirika la Haki za Binadamu wakati wakiwa katika hospitali hiyo; Dhao awali alidhaniwa kuwa alikuwa kakimbilia Niger.

Hata hivyo, baadaye zilisikika taarifa kwamba Senussi katoka katika maficho yake nchini Niger kumsaidia Saif al-Islam Gaddafi ili atoroke kutoka nchini Libya. Senussi aliripotiwa kuwa alitekwa nyara tarehe 20 Novemba karibu na mji wa Sabha. Baadaye ilitolewa taarifa ya kwamba angeweza kuchukuliwa hadi Tripoli kujibu mashtaka ya uhalifu dhidi ya binadamu, kwa mujibu wa Baraza la Mpito la Taifa.

Hata hivyo, mwendesha mashitaka mkuu wa ICC, Luis Moreno Ocampo, alionesha wazi kuwa na shaka kama kweli Senussi alikuwa kakamatwa. Waziri wa Ulinzi wa Libya, Osama Jweli, pia alisema kuwa hakuna ushahidi wa Senussi kuwa alikuwa katekwa. Mnamo tarehe 4 Desemba 2011, Abdullah Nakir, afisa wa Libya, alikiambia chombo cha habari cha Al Arabiya kwamba Senussi alikamatwa na alikuwa akihojiwa kuhusu kituo cha siri cha nyuklia ambacho Gaddafi alikuwa akikiendesha, lakini alikiri kwamba serikali ya Libya haikuweza kutoa picha yoyote ya yeye akiwa chini ya ulinzi.

Tarehe 17 Machi 2012, taarifa za vyombo vya habari zilisema kuwa Senussi ametiwa mbaroni katika uwanja wa ndege wa Nouakchott katika nchi ya Mauritania. Serikali ya Libya inaelezwa kutoa ombi la kumtaka al-Senussi apelekwe nchini Libya kwa mahojiano.

Makala haya yameandaliwa na Bishop Hiluka kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya habari vya kimataifa.

1 comment:

  1. Wynn Hotel & Casino - Mapyro
    Get 제천 출장마사지 directions, reviews and information for Wynn Hotel & Casino in Las 대구광역 출장샵 Vegas, NV. Location: 목포 출장안마 3131 South Flamingo Road, Las 목포 출장마사지 Vegas, NV 순천 출장안마 89109. (702) 770-9960.

    ReplyDelete