Jim Yong Kim
Marekani
BODI ya Benki ya Dunia
imemchagua mwanazuoni wa Marekani, Jim Yong Kim, kuwa rais wa Benki hiyo. Hii
ni licha ya shinikizo kutaka nafasi hiyo kumuendea raia asiye Mmarekani. Dk.
Kim ni mtaalamu wa Afya akiwa na uzoefu wa nchi zinazoendelea.
Kim alikuwa akipambana na
Waziri wa fedha wa Nigeria Ngozi Okonjo-Iweala. Waziri huyo aliungwa mkono na
nchi kadhaa zinazoendelea. Hata hivyo alikabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa
wajumbe wanaopiga kura ambao wengi hutoka Ulaya na Marekani.
Rais wa sasa, Robert
Zoellick, anamaliza mhula wake wa miaka mitano hapo mwezi Juni.
Historia yake
Jim Yong Kim amezaliwa tarehe
8 Desemba 1959, ni daktari Mmarekani mwenye asili ya Korea na Rais wa 17 wa Chuo cha Dartmouth . Zamani alikuwa Mwenyekiti wa Idara ya Afya na Tiba
ya Jamii katika Shule ya Tiba ya Harvard, na alikuwa mmoja wa waanzilishi na mkurugenzi
mtendaji wa Taasisi ya Washirika Katika Afya (PIH). Machi 2, 2009, Kim aliteuliwa
kuwa rais wa Chuo cha Dartmouth .
Kim pia ni Mmareka wa kwanza mwenye asilia ya Asia kushika nafasi ya rais katika taasisi ya Ivy League.
Machi 23, 2012, Rais Barack
Obama alitangaza kuwa Marekani itamteua Kim kama Rais wa Benki ya Dunia ajaye. Aprili 16, Kim alichaguliwa kuwa rais na
ataanza kazi Julai 1.
Alizaliwa jijini Seoul , Korea ya Kusini, Jim Yong Kim na familia yake walihamia Marekani
akiwa na umri wa miaka mitano na kukulia Muscatine , katika Jimbo la Iowa . Baba yake alifundisha somo la afya ya meno na kinywa
katika Chuo Kikuu cha Iowa ,
wakati mama yake alipata shahada yake ya uzamivu (Ph.D.) katika falsafa. Kim alipata
masomo ya juu katika shule ya Muscatine . Baada ya mwaka mmoja na nusu katika Chuo Kikuu cha
Iowa , alihamishiwa Chuo Kikuu cha Brown, ambapo alihitimu
shahada ya kwanza mwaka 1982. Alihitimu shahada ya udaktari kutoka Shule ya
Tiba ya Harvard mwaka 1991, na shahada ya uzamivu (Ph.D.) kutoka Chuo Kikuu cha
Harvard, Idara ya anthropolojia (elimu ya binaadamu), mwaka 1993.
Kazi
Jim Yong Kim, pamoja na
Paul Farmer, Todd McCormack, Thomas J. White na Ophelia Dahl, walianzisha Taasisi
ya Washirika Katika Afya (PIH) mwaka 1987. Shirika lililenga katika mpango wa huduma
za afya ya jamii nchini Haiti , ambao ulilenga kutoa tiba kulingana na mahitaji ya
ndani na mafunzo ya jamii kuyatekeleza. Mwanzoni mwa miaka ya 1990, mpango wa Haiti ulihudumia watu zaidi ya 100,000. Ni mafanikio ya
ajabu kutibu magonjwa ya kuambukiza kwa gharama nafuu, wakitumia dola 150 na 200
kutibu wagonjwa wa kifua kikuu majumbani mwao, matibabu ambayo yangegharimu dola
15,000 hadi 20,000 katika hospitali nchini Marekani. Kim alikuwa mtu muhimu
katika kubuni itifaki ya matibabu na kukata mikataba kwa bei nafuu, na ufanisi
zaidi.
Mwaka 2003 Kim alijiunga na
Shirika la Afya Duniani (WHO) kama mshauri wa mkurugenzi mkuu. Mwezi Machi 2004,
aliteuliwa kuwa mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani wa idara ya VVU/UKIMWI,
baada ya kuonesha mafanikio katika mipango ya kupambana na ugonjwa huo kupitia
taasisi ya PIH. Dk. Kim alisimamia kazi zote za Shirika la Afya Duniani
kuhusiana na VVU/UKIMWI, akilenga mpango wa kusaidia nchi zinazoendelea
kuongeza matibabu yao , kuzuia, na mipango ya huduma.
Kuanzia mwaka 1993, Dk. Kim
alikuwa mhadhiri katika Shule ya Tiba ya Harvard, hatimaye akawa profesa katika
tiba, tiba ya jamii na haki za binadamu. Alipoondoka mwaka 2009, Kim alishikilia
cheo cha mwenyekiti wa Idara ya Afya na Tiba ya Jamii, Mkuu wa Idara ya Global
Health Equity katika Hospitali ya Brigham na Wanawake, na Mkurugenzi wa Kituo
cha François Xavier Bagnoud wa Afya na Haki za Binadamu katika Shule ya Afya ya
Umma ya Harvard.
Katika miongo yake miwili
ya kazi aliboresha afya katika nchi zinazoendelea, Kim amekuwa akishiriki
katika jitihada kadhaa ya utafiti na kitaaluma. Katika miaka ya karibuni, Kim ameongoza
maendeleo mapya akilenga katika kuboresha utekelezaji na utoaji wa shughuli za
afya katika jamii maskini duniani kote.
Akiwa Harvard, Kim alichapisha
makala mbalimbali kwa ajili ya majarida ya kitaaluma na kisayansi, ikiwa ni pamoja
na New England Journal of Medicine, Lancet, Science, na mengineyo,
na kuchangia katika vitabu kadhaa. Mtaalam wa kifua kikuu, Kim pia alikuwa
mwenyekiti au mjumbe katika kamati kadhaa katika sera ya kimataifa ya TB.
Machi 2009, Kim alikuwa
Rais wa 17 wa Chuo cha Dartmouth ,
akiwa Mmarekani wa kwanza mwenye asili ya Asia kushika madaraka ya urais katika taasisi ya Ivy League. Kim amesimamia
maendeleo ya programu kadhaa ya kiubunifu katika Chuo cha Dartmouth , akitumia uzoefu wake wa zamani katika huduma za
afya na masuala ya kimataifa. Januari 2010, Kim alisaidia wanafunzi wenzake wa Dartmouth na kitivo kupitia taasisi aliyoianzisha, Taasisi ya
Washirika Katika Afya, na mashirika mengine, kukabiliana na tetemeko kubwa la
ardhi nchini Haiti , na kuanzisha taasisi ya Dartmouth Haiti Response. Mpango huo ulisababisha
upatikanaji wa zaidi ya dola milioni 1 katika michango, utoaji wa tani 18 ya
vifaa tiba na wataalamu wa afya 25 wa kujitolea nchini Haiti , pamoja na mamia ya wanafunzi wa kujitolea.
Aprili 2010, Kim alizindua Mradi
wa Kitaifa wa Chuo katika Uboreshaji wa Afya (NCHIP), ambao huzileta pamoja taasisi
za kitaalam kuendeleza mbinu za kushughulikia masuala ya afya ya mwanafunzi. Mradi
ulizindua programu yake, jitihada za kukabiliana na ulevi, mwezi Aprili 2011.
Mei 2010, Kim alisaidia upatikanaji dola milioni 35 kuanzisha Kituo cha Dartmouth kwa ajili ya Huduma ya Afya na Sayansi. Kituo kilianzisha
uwanja mpya wa mafunzo ya utafiti, kukuza ushirikiano wa kimataifa kati ya
watafiti na madaktari, kutekeleza, na kuweka mipango mipya ya ubora wa huduma
kwa gharama nafuu. Mwaka 2012, kufuatia wasiwasi mkubwa na juhudi za Kim
kushughulikia unyanyasaji wa kijinsia chuoni, Dartmouth ilirithi hatua mpya ya chuo ya kuwaelimisha
wanafunzi juu ya umuhimu wa kuingilia uangalizi katika kesi za kushambuliwa
kingono kama sehemu ya Mpango wa Uelewa wa Unyanyasaji wa
Kingono.
Mwaka 2011, Kim alikosolewa
kutokana na kukataa kutoa bajeti ya chuo, na hivyo kusababisha sehemu ya azimio
kwa kitivo kudai maelezo zaidi. Kim akajibu kwa kutoa ripoti kubwa ya ziada juu
ya bajeti na kufanya mkutano wa hadhara na kitivo ambao baadaye walionesha
kuridhika na majibu. Hata hivyo, Kim hakushughulikia ombi la Mkutano wa
Wanafunzi walioomba kupata taarifa juu ya bajeti yote inayozidi dola 10,000.
Mwaka 2011, wahariri wachache walionekana katika gazeti la wanafunzi la Dartmouth wakionesha kutoridhika na urais wa Kim, na mmoja akamuelezea
Kim kama "asiye na umaarufu miongoni mwa wanafunzi wengi siku hizi." Uongozi
wake pia umekosolewa kutokana na kashfa ya udhalilishaji, ambayo ilisababisha
mashitaka dhidi ya udugu na kuundwa kwa kikosi kazi cha kushughulikia kashfa;
na kukiwa na maoni kutoka kwa baadhi ya kuwa Kim hakutumia muda wa kutosha chuoni.
Machi 23, 2012, Rais wa
Marekani, Barack Obama alitangaza uteuzi wake wa Jim Yong Kim kuwa rais wa
Benki ya Dunia. Siku hiyohiyo Jim Yong Kim alituma barua akihutubia Jumuiya ya Dartmouth akisema kuwa nafasi ilikuwa ni "moja ya
taasisi muhimu zaidi ya kupambana na umaskini na kutoa msaada kwa nchi zinazoendelea
katika dunia ya leo. Baada ya kutafakari sana , nimekubali uteuzi huu kwa huduma ya kitaifa na
kimataifa "na kwamba" kama nitachaguliwa,
Bodi yetu itachukua hatua zinazofaa ili kuhakikisha mwendelezo wa uongozi na
utafiti. Kwa sasa, nabakia kuwa rais wa Dartmouth ". Aprili
16, 2012, Benki ya Dunia ilimchagua rasmi Kim kuwa rais wake ajaye.
Maisha binafsi
Kim, amemuoa Younsook Lim,
daktari wa watoto katika Hospitali ya Watoto ya Boston , wana watoto wawili, Thomas, ambaye alizaliwa mwaka
2000, na wa pili aliyezaliwa Februari 27, 2009, siku chache kabla ya kutangazwa
kwa urais wa Kim katika Chuo cha Dartmouth . Anashiriki kikamilifu katika aina mbalimbali za
michezo, ikiwa ni pamoja na mpira wa kikapu, volleyball, tennis, na golf.
Makala haya yameandaliwa na Bishop Hiluka kwa msaada
wa vyanzo mbalimbali vya kimataifa.
No comments:
Post a Comment