Joshua Nassari (Chadema) na Sioi Sumari (CCM)
BISHOP HILUKA
KESHOKUTWA Jumapili, tarehe
mosi, Watanzania wenzetu wa Jimbo la Arumeru watakuwa na zoezi muhimu la
kisiasa, kumchagua Mbunge wao. Hivyo huu ni wakati muhimu na muafaka kwa wananchi
wa Arumeru kutafakari kwa makini tunu na maadili ya kiongozi bora kabla ya
kuingia kwenye chumba cha upigaji kura.
Natoa wito kwa wana-Arumeru
kuchagua kiongozi ‘muadilifu’ bila kujali anatoka chama gani au kina nani
wanampigia debe, kwani mwisho wa siku wananchi watabaki na mbunge wao huku
chama na wapiga debe (ambao wanatoka nje ya jimbo) watakuwa wameondoka zao na
kuwaachia matatizo yao .
Kabla hatujasonga mbele
kwanza tujiulize dhana ya maadili, maana yake ni nini? Kwa mujibu wa Padre
Hurbert Akhweso, Mtalaam katika masuala ya Maadili, katika moja ya machapisho
yake amewahi kuandika kuwa: maadili ni wema wa mwenendo au tendo la mtu; ni
kule kuhukumiwa kwa mwenendo wa mtu kuwa ni mwema, au tendo la kibinadamu kuwa
ni jema. Mwenendo au tendo la mtu ni jema vinapolingana na hadhi yake
kibinadamu, yaani vinapoakisi utu wake. Hapa tunasema mtu huyu ni mwadilifu, au
tendo hili ni adilifu.
Na mwenendo wa mtu au
matendo yake vinapokuwa kinyume na hadhi yake ya kibinadamu, yaani kinyume cha
utu wake, tunahukumu kuwa ni mabaya, na huo ni ukosefu wa uadilifu. Kwa kifupi,
uadilifu ni wema wa mwenendo au tendo la kibinadamu, na ukosefu wa uadilifu ni
ubaya wa mwenendo au tendo la kibinadamu. Maadili pia ni taaluma juu ya kanuni
zinazohukumu mwenendo na matendo ya mtu kulingana na UTU wake.
Hivyo kwa kutumia kipawa cha
akili binadamu hutafuta, kung’amua na kufahamu ukweli, naamini wananchi wa
Arumeru wataweza kufahamu au kujua ni kiongozi yupi anayewafaa, na watawaweza kufahamu
au kujua jambo lililo la kweli wakati huu wa kampeni zilizotawaliwa na porojo,
kashfa kwa watu binafsi badala ya sera na ahadi zisizotekelezeka jambo ambalo
haliwasaidii wana Arumeru kutatua matatizo yao.
Ieleweke kuwa mtu
anapojiuliza kama jambo fulani ni la ‘kweli au la,’ au kama ‘lipo au halipo,’ anatumia kipawa cha akili, na akili inapokosa
ukweli, huwa na mahangaiko makubwa na maswali mengi; lakini inapopata ukweli,
hutulia kwa kuwa imeridhika.
Chakula kikuu cha akili ni
ukweli, hivyo kila mmoja anao wajibu wa kuilisha akili yake kwa kutafuta ukweli
daima, yaani, kujifunza na kuzitafakari hoja za wagombea na wapiga debe wao
kabla ya keshokutwa kupiga kura.
Wananchi wa Arumeru ni
vyema wakaongozwa na utashi katika kupiga kura. Utashi ni kipawa
kinachotuwezesha kuona jambo fulani kuwa ni jema. Na jambo lililo jema ni lile
ambalo akili imethibitisha kuwa ni la kweli.
Kinachonishangaza hadi sasa
wakati huu wa kuelekea mwisho wa kampeni kabla ya uchaguzi jimboni Arumeru ni
malumbano yasiyo na tija kwa wananchi wa jimbo hilo, tena yakiwahusisha
viongozi wenye heshima kubwa katika taifa hili lakini wanaotoka nje ya jimbo
hilo, kitendo ninachokitafsiri kama kufirisika kisiasa.
Huu ndiyo ulikuwa wakati
muafaka kwa wananchi kutafakari kwa kina na kujua ni nani anayewafaa, mwenye
maadili ya kweli, mwenye dhamira ya kweli kuwaondoa katika matatizo yao, bila
kujali propaganda za wakubwa fulani ambao baada ya uchaguzi wataondoka zao na
kuwaachia wananchi mbunge ambaye kama atakuwa ‘garasa’ watoto wa mjini wanasema
kuwa itakuwa “imekula kwao”.
Jambo la msingi la
kuangalia hapo ni kiongozi mwadilifu na mwenye maadili. Tukumbuke kuwa kule
kuumbwa na utu (yaani, kuwa mtu), ndiko kunakomdai mtu kuwa mwadilifu, madai
ambayo hawezi kuyakataa maadam ni mtu. Kuwa au kutenda kinyume na utu ni kujishusha
hadhi na kuwa sawa na, au hata kuwa chini ya wanyama.
Hivyo keshokutwa wagombea
(na vyama vyao) baada ya kunadi sera zao na kuahidi mambo mengi, itakuwa ni
zamu ya Mpiga kura mwadilifu ambaye ameshasikiliza kwa makini na kupima hoja za
wagombea wote kwa kadiri ya ufahamu wake na kubaini ukweli na kuridhisha utashi
wake, kupiga kura.
Wananchi wa Arumeru
wasifanye makosa kumchagua kiongozi asiye mwadilifu kwa kuwa anatoka chama
fulani au wakubwa fulani waliwaambia eti huyo ndiye anayefaa. Wachague kwa kuzingatia
sheria ya maumbile ya kimaadili ili baadaye wasije wakajutia kwa hii miaka
mitatu iliyobakia kabla ya uchaguzi mkuu hapo 2015.
Kwa luga nyingine,
ninawaasa wana-Arumeru keshokutwa msichague Chama bali mtu ambaye ni mwadilifu
na mwenye uwezo wa kushirikiana nanyi katika kutatua ama kupunguza kero zenu
ambazo kubwa tumeambiwa ni suala la ardhi inayokaliwa na ‘wawekezaji’ wachache,
maji safi na salama na kupanda kwa gharama za maisha.
Alamsiki...
No comments:
Post a Comment