HIVI karibuni wanajeshi nchini
Mali waliupindua uongozi wa nchi hiyo uliokuwa chini ya
Amadou Touman Toure. Kadhalika waasi wanaoongozwa na Watuareg wamezidi kuteka
maeneo mengine ya nchi hiyo na wamesonga mbele katika maeneo ya Kaskazini ya Mali , eneo kubwa wanalodai liwe huru.
Hali ya wasiwasi inazidi
kuongezeka kuhusu harakati za makundi ya wapiganaji wa Kiislamu Kaskazini ya Mali baada ya waasi hao wanaoongozwa na Watuareg
kuyateka maeneo makuu ya eneo hilo wiki iliyopita.
Waasi hao wakiongozwa na
makamanda Watuareg wameteka maeneo zaidi katika mkoa wa kati wa Mopti kwa
mujibu wa wakazi wa eneo hilo .
Wameingia katika mji mdogo wa Hombori ulio kilometa 300 Kaskazini mwa mji mkuu
wa mkoa wa Mopte bila ya mapigano yoyote.
Awali walisema mji wa
Homboni hauko katika eneo la Azawad wanalodai liwe huru. Hakuna ishara yoyote kama watasonga mbele kuelekea Kusini. Wapiganaji wa kundi la Waislamu la
Ansar Eddine wameanza kutekeleza kanuni za sheria za Kiislamu katika miji mikuu
mitatu iliyotekwa na waasi mwishoni mwa wiki iliyopita.
Taarifa kutoka Kidal Gao na
Timbuktu zanaeleza kuwa wapiganaji wa Ansar Edinne
walishambulia baa zinazouza pombe na kupiga marufuku kucheza muziki wa nchi za
Magharibi katika vituo vya redio. Shirika la Utamaduni la umoja wa mataifa
limeelezea wasiwasi wao kuwa maeneo ya kale katika Timbuktu huenda yakaharibiwa na uasi huo.
Hata hivyo, kiongozi wa Mali aliyepinduliwa, Toure, japo hajulikani yuko wapi, amenukuliwa
akisema yuko huru na salama kabisa. Toure amekanusha habari kuwa anashikiliwa
na wanajeshi ambao siku ya tarehe 22 walipindua serikali yake.
Kupinduliwa kwa Rais huyo
wa Mali kulitokea kukiwa kumesalia wiki tano peke yake ili
uchaguzi mkuu ufanywe. Lakini mara tu baada ya kumtimua madarakani Rais Toure,
Baraza la Jeshi linaloongoza nchi lilitangaza kuahirishwa kwa uchaguzi huo kwa
muda usiojulikana.
Katika taarifa yake fupi
kwa njia ya simu kwa shirika la habari la AFP Toure alisema lililo muhimu kwa wakati huu ni kufahamisha watu kuwa
yuko huru wala hazuiliwi kama inavyodaiwa.
“Nafuatilia kwa makini sana yale yote yanayotokea nchini. Kwa moyo wangu wote
nataka amani na demokrasia”, Toure alisema.
Historia yake
Amadou Toumani Touré amezaliwa
tarehe 4 Novemba 1948. Alikuwa Rais wa Mali kuanzia 2002 hadi 2012. Alimwangusha Rais Moussa
Traoré katika mapinduzi ya kijeshi ya Machi 1991 na kuongoza serikali ya mpito
kwa mwaka mzima kabla ya uchaguzi wa vyama vingi; alikabidhi madaraka kwa
mamlaka za kiraia mnamo Juni 1992.
Miaka kumi baadaye, baada
ya kustaafu kutoka katika jeshi, aliingia katika siasa kama raia na kushindi uchaguzi wa urais wa mwaka 2002. Alichaguliwa tena kirahisi
mwaka 2007 kwa muhula wa pili na wa mwisho. Miezi tu kabla ya kuachia ngazi
kufuatia uchaguzi uliopangwa kufanyika, wanajeshi wa Mali wenye kinyongo walipindua nchi na hivyo kumlazimisha
aende mafichoni
Maisha ya awali
Amadou Toumani Touré
alizaliwa tarehe 4 Novemba 1948, katika eneo la Mopti, ambako alihudhuria masomo
ya shule ya msingi. Kati ya 1966 na 1969, alihudhuria masomo ya sekondari
katika shule ya Badalabougou iliyopo Bamako ili aje kuwa mwalimu. Hatimaye, alijiunga na jeshi
na kujiunga na chuo cha Kijeshi cha Kati. Akiwa mmoja wa wanaanga, alipanda
haraka akipitia safu na kozi mbalimbali za mafunzo katika Umoja wa Kisovieti na
Ufaransa, na kuwa kamanda wa kikosi cha parachute Commandos mwaka 1984.
Siasa na kazi ya kijeshi
Mwezi Machi mwaka 1991,
baada ya ukandamizaji wa kutumia nguvu wa maandamano dhidi ya serikali, Toure alishiriki
katika mapinduzi yaliyoelekezwa dhidi ya Rais Moussa Traoré, na kuwa kiongozi
wa Kamati ya Mpito kwa ajili ya Ustawi ya Watu na kiongozi wa nchi katika
jitihada ya kamati ya mpito kuipeleka serikali ya nchi hiyo kwenye demokrasia.
Aliandaa mkutano wa kitaifa
kati ya Julai 29 na Agosti 13, 1991 kuandaa Katiba ya Mali na kufanyika kwa uchaguzi wa wabunge na rais wa
mwaka 1992. Baada ya matokeo ya uchaguzi kujulikana, Toure alikabidhi madaraka
kwa rais mpya aliyechaguliwa, Alpha Oumar Konaré. Kutokana na kuondoka kwake madarakani
kwa hiari, alipata jina la utani la "Askari wa Demokrasia."
Juni 2001, Toure alifanya
kazi kama mjumbe maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan , wa Jamhuri ya Afrika, baada ya jaribio la mapinduzi lililoshindwa
nchini humo.
June 2002, Mwezi Septemba
2001, aliomba na kustaafu kutoka jeshi, akaingia katika siasa kama mgombea katika uchaguzi wa mwaka 2002. Katika duru ya kwanza ya kupiga
kura, alikuwa wa kwanza kwa asilimia 28.71 ya kura, wakati katika raundi ya
pili alishinda kwa asilimia 64.35 ya kura, akimshinda mgombea wa ADEMA, waziri
wa zamani wa baraza la mawaziri, Soumaïla Cissé, ambaye alipata asilimia 35.65.
Touré aliapishwa tarehe 8 Juni 2002.
Urais wake umekuwa ukitazamwa
na waangalizi wa mambo kama si wa kawaida, kwa sehemu kutokana na ukweli kwamba
si mwanachama wa chama chochote cha siasa na kwamba amekusanya wanachama wote
kutoka vyama vyote vya kisiasa nchini humo katika serikali yake. Kufuatia
uchaguzi wake wa 2002, aliwateua Ahmed Mohamed AG Hamani kama Waziri Mkuu, lakini tarehe 28 Aprili 2004, nafasi yake ilichukuliwa na
Ousmane Issoufi Maiga, ambaye naye kwa upande alilirithiwa na Modibo Sidibé tarehe
28 Septemba 2007.
Touré pia alianzishwa shirika
la watoto lililoitwa Fondation pour l'enfance - jina lililokuwa likitumiwa pia
shirika kama hilo lililoundwa
na Danielle Mitterrand, mke wa rais wa Ufaransa, François Mitterand. Shirika
hili hivi karibuni limekuwa likisimamiwa na mke wa Rais Toure, Lobbo Traore, akiliongoza
kama wakala wa Touré.
Touré alitangaza mnamo 27
Machi 2007, kuwa angegombea kwa awamu ya pili katika uchaguzi wa rais wa Aprili
2007. Kwa mujibu wa matokeo ya mwisho yaliyotangaza tarehe 12 Mei, Toure
alishinda uchaguzi kwa asilimia 71.20 ya kura. Mpinzani mkuu, Rais wa Bunge,
Ibrahima Boubacar Keïta, aliambulia asilimia 19.15; Chama cha Front for
Democracy and the Republic; umoja huo ikiwa ni pamoja na Keïta na wagombea
wengine watatu, waliyakataa matokeo rasmi. Waangalizi wa Nje, hata hivyo, waliukubali
uchaguzi kama huru na wa haki. Touré akaapishwa kwa muhula wake
wa pili kama Rais tarehe 8 Juni 2007, katika sherehe iliyohudhuriwa
na marais wengine saba ya Afrika.
Kutokana na katiba ya Mali , ambayo inataja vipindi viwili vya urais, Toure
alithibitisha katika mkutano wa vyombo vya habari tarehe 12 Juni 2011, kwamba hataweza
kusimama katika uchaguzi wa rais wa 2012 .
Mapinduzi ya kijeshi 2012
Kwa miezi kadhaa mwaka huu,
wanajeshi wa Mali wameipinga serikali ya Touré na kufanya uasi katika eneo la Kaskazini
mwa Mali . Tarehe 21 Machi, askari walifanya jaribio la
mapinduzi baada ya kuteka maeneo kadhaa Bamako , ikiwa ni pamoja na ukumbi wa rais, makao makuu ya
televisheni ya nchi, na baadhi ya kambi za kijeshi. Kisha wakaanzisha mamlaka
ya awali ya kiserikali, Kamati ya Taifa ya Matengenezo ya Demokrasia na Nchi
(CNRDR), na kutangaza kwamba wameuangusha utawala wa Touré, kwa shutuma kuwa serikali
yake ilitawaliwa na uzembe. Touré hakufungwa gerezani na waasi.
Mahali alipo Touré kwa sasa
hapajulikani na wanejeshi hao wanaotawala nchi (CNRDR) hawajaonesha kuwa yupo
chini ya ulinzi wao.
Makala haya yameandaliwa na Bishop Hiluka kwa msaada
wa vyanzo mbalimbali vya habari vya kimataifa.
No comments:
Post a Comment