Jun 1, 2012

AHMED SHAFIK: Kusuka au kunyoa urais wa Misri



Ahmed Shafik


CAIRO,
Misri

HALI ni tete nchini Misri kwa mgombea mmoja wa urais. Waandamanaji nchini humo wameshambulia makao makuu ya mgombea huyo wa urais, Ahmed Shafik, mjini Cairo. Ahmed Shafik anashutumiwa kuunga mkono utawala wa zamani wa Hosni Mubarak, madai ambayo yeye na wafuasi wake wanakanusha vikali.

Uvamizi huo umetokea muda mfupi baada ya tume ya uchaguzi kuthibitisha kuwa uchaguzi wa marudio utafanyika mwezi huu kati ya Ahmed Shafik, ambaye aliwahi kuwa waziri mkuu wa zamani katika utawala wa Rais Hosni Mubarak, na Mohamed Mursi wa chama cha Muslim Brotherhood.

Hakuna aliyedai kuhusika na mashambulio hayo. Mwandishi wa Shirika la Utangazaji la Uingereza, BBC, katika eneo la tukio alisema kuwa jengo liliwaka moto kidogo, lakini halikupata uharibifu mkubwa.

Waandamanaji wapatao elfu moja wanaliokuwa wanapinga matokeo ya uchaguzi huo pia walikusanyika katika medani ya Tahrir.

Wakati hayo yakijiri, wagombea urais wawili walioshindwa katika duru ya kwanza ya uchaguzi nchini humo pia wametaka baadhi ya kura zihesabiwe tena, wakidai kuwa kulitokea udanganyifu.

Afisa mmoja wa polisi aliwashutumu baadhi ya wenzake, kwamba waligawa kadi 900,000 za utambulishi, bila ya kutaja kazi yao, ili wapate kupiga kura. Inasemekana kuwa katika uchaguzi nchini humo, wanajeshi hawaruhusiwi kabisa kupiga kura.

Msemaji wa kiongozi wa mrengo wa kushoto aliyeshika nafasi ya tatu katika duru ya kwanza, Hamdeen Sabahi, alisema kuwa wangekata rufaa Jumapili, ili kuzuwia duru ya pili ya uchaguzi wa urais.

Waziri wa zamani wa mashauri ya nchi za nje, Amr Moussa, aliyemaliza akiwa wa tano, alimsihi afisa wa mashtaka kufanya uchunguzi. Kwa matokeo ya hadi sasa, duru ya pili ya uchaguzi itakuwa kati ya Ahmed Shafik, waziri mkuu wa mwisho wa Hosni Mubarak, na Mohamed Mursi wa chama cha Muslim Brotherhood.

Historia ya Shafik

Ahmed Mohamed Shafik alizaliwa Novemba 1941, ni mwanasiasa wa Misri. Aliwahi kuwa kamanda mwandamizi katika Jeshi la Anga la Misri na baadaye alifanya kazi kama Waziri Mkuu wa Misri kati ya Januari 31, 2011 na Machi 3, 2011, kipindi cha siku 33 tu.

Baada ya kazi ya anga kama rubani wa mapigano, kamanda wa tawi na kituo cha kijeshi, Ahmed Shafik alikuwa Kamanda wa Jeshi la Anga la Misri kuanzia 1996 hadi 2002, na kufikia daraja la jemadari wa anga. Baada ya hapo alifanya kazi katika serikali kwenye nafasi ya Waziri wa Usafiri wa Anga kuanzia mwaka 2002 hadi 2011.

Aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu na Rais Hosni Mubarak mnamo Januari 31, 2011, katika kukabiliana na Mapinduzi ya Misri ya mwaka 2011, na hivyo kumfanya kuwa Waziri Mkuu wa mwisho kutumikia nafasi hiyo chini ya utawala wa Hosni Mubarak. Alikaa kwenye nafasi hiyo kwa mwezi mmoja tu, akajiuzulu mnamo Machi 3, 2011, siku moja baada ya kipindi cha mahojiano kilichozua utata kwenye kituo cha televisheni ambapo alishutumiwa na mwandishi maarufu wa vitabu nchini Misri ya kuendeleza utawala wa Mubarak.

Maisha ya awali

Shafik alizaliwa katika jiji la Cairo mwezi Novemba, 1941. Baada ya kufuzu mafunzo yake katika Chuo cha Anga cha Misri mwaka 1961, alijiunga na Jeshi la Anga la Misri (EAF) akiwa na umri wa miaka 20. Baadaye katika kazi yake, alipata shahada yake ya uzamili katika Sayansi ya Jeshi, Nishani ya Juu ya Vita kutoka Chuo cha Kijeshi cha Nasser, Nishani ya Pamoja ya Kijeshi kutoka Chuo cha Juu cha Vita jijini Paris, Nishani ya ulinzi wa Taifa kutoka katika Chuo cha Kijeshi cha Nasser na shahada ya uzamivu (Ph.D.) katika "Mkakati wa Taifa wa Anga". Jemadari wa Anga, Ahmed Shafik, alipata medali za juu na uhalali wakati wa utumishi wake.

Kazi ya kijeshi

Kama afisa wa jeshi kijana, Shafik aliwahi kuwa rubani mpiganaji na baadaye aliteuliwa kuwa kamanda wa kikosi cha jeshi la anga. Wakati wa Vita ya msuguano kati ya 1967 na 1970, Shafik alijikuta akiwa anafanya zaidi kazi kama Kamanda mwenye majukumu mengi katika kikosi cha anga. Baadaye akawa kamanda wa kikosi cha jeshi la anga.

Mwaka wa vita vya Oktoba 1973, Shafik alikuwa rubani mpiganaji mwandamizi chini ya uongozi wa Hosni Mubarak. Inaaminika kwamba Shafik alizidondosha ndege mbili za Israel wakati wa vita mnamo tarehe 14 Oktoba, 1973.

Mwaka 1984 Shafik aliteuliwa kuwa mwambata wa kijeshi katika ubalozi wa Misri nchini Roma. Aliendelea katika nafasi hii hadi mwaka 1986. katika kipindi cha kuanzia 1988 hadi 1991, Shafik alifanya kazi katika nafasi kadhaa andamizi za kijeshi kabla ya kuteuliwa kuwa Kamanda wa Idara ya Uendeshaji wa Anga.

Mwezi Septemba 1991, Shafik aliteuliwa kuwa Mkuu wa Utumishi wa Jeshi la Anga, akishikilia nafasi hii hadi mwezi Aprili 1996, alipokuwa Kamanda wa Kikosi cha Anga cha jeshi la Misri. Mwaka 2002, baada ya kujiuzulu kutoka huduma za kijeshi, aliteuliwa kuwa Waziri wa Usafiri wa Anga na nafasi yake ilichukuliwa na na mkuu wake wa utumishi, Jemadari wa Anga Magdy Galali Sharawi.

Uteuzi wa Waziri Mkuu na Kujiuzulu

Katika kipindi cha vuguvugu la Mapinduzi ya Misri ya mwaka 2011, Shafik aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu mnamo Januari 29. Hata hivyo, Uwaziri Mkuu wake ulikuwa wa muda mfupi mno, ulidumu kwa kipindi cha mwezi mmoja tu na siku chache, baada ya kujiuzulu mnamo Machi 3 kutokana na shinikizo kutoka kwa waandamanaji na upinzani.

Walikuwa walipinga Shafik kuwa Waziri Mkuu, baada ya kuonekana kama mmoja wa walinzi wa zamani wa Mubarak. Shafik alidaiwa kuwa alikuwa ni mjumbe wa Baraza Kuu la Vikosi vya Jeshi ambavyo vilichukua madaraka baada ya kuondoka kwa Mubarak mnamo Februari 11, 2011. nafasi ya Shafik ilichukuliwa na Essam Sharaf baada ya kujiuzulu.

Shafik alijiuzulu nafasi ya Waziri Mkuu siku moja baada ya mahojiano yaliyozua utata kwenye kituo cha ONTV (Misri) ambapo alikuwa anakabiliwa na Alaa Al Aswany, mwandishi maarufu wa vitabu nchini Misri aliyeandika ‘The Yacoubian Building’, kwenye kipindi cha majadiliano cha Baladna bel Masry. Al Aswany alimkosoa vikali Shafik wakati matangazo hayo yakirushwa, akiwakilisha moja ya vipindi vya kwanza vya ukosoaji katika televisheni rasmi ya umma katika historia ya serikali ya Misri.

Katika hatua moja, Al Aswany alisema kuhusu Shafik, "kama mtoto wako alikuwa mmoja wa wale waliokimbia na magari ya polisi, usingeweza kubaki kimya kama hiyo." Al Aswany alimtuhumu zaidi Shafik ya kuwa bado anaendeleza utawala ambao Jihadi ya Wamisri imeupindua, na kwamba alikuwa hafai kuwakilisha Wamisri katika zama za baada ya mapinduzi.

Makala haya yameandaliwa na Bishop Hiluka kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya habari vya kimataifa.

No comments:

Post a Comment