Charles Ekerege, Mkurugenzi Mkuu wa TBS
Machinjio ya ng'ombe
BISHOP HILUKA
MAJUZI nilikutana na dokezo
moja kutoka kwa Profesa Mbele alilolitoa kwenye blogu yake, kuwa ufisadi ndiyo
dini inayoenea kwa kasi nchini Tanzania . Kwangu mimi hii ilikuwa ni habari kubwa mno. Japo
ilikuwa ni kama dokezo tu (fupi mno) la kawaida, lakini ilinifanya
kufikiria kwa kina huku nikilinganisha na hiki kinachoendelea kutokea nchini
mwetu. Kwa kifupi nakubaliana na Profesa Mbele kuhusu hilo .
Profesa Mbele aliandika
hivi: “Mara kwa mara ninawasikia watu wakiongelea suala la dini inayoenea kwa
kasi kuliko zote Tanzania , Afrika au duniani kwa ujumla. Kila mtu ana mtazamo
wake. Wengine wanatoa pia takwimu, ambazo sijui kama ni za kweli au ndoto. Ni mchezo wa kuringiana nani zaidi kwa kutumia
takwimu, wakati dini ni suala la mtu binafsi. Wala hutaingia ahera kwa msingi
kuwa dini yako hapa duniani ilikuwa na wafuasi wengi kuliko dini nyingine.
“Kwa mtazamo wangu, dini
inayoenea kwa kasi kuliko zote Tanzania ni ufisadi na ushirikina. Ufisadi na ushirikina huo
unaendelea kushamiri kiasi kwamba unajitokeza hata kwenye nyumba za ibada za
dini mbalimbali. Hebu tutafakari hilo .”
Ni maneno machache lakini
yaliyobeba ujumbe mkubwa mno na unaweza kuyaelezea kwa kurasa zaidi ya elfu
moja. Binafsi nadhani kuenea kwa dini (ufisadi) hii kumesababishwa na nchi hii kuitupa
misingi iliyoongozwa na Azimio la Arusha, kufumbia macho vitendo vya rushwa na kukubali
wafanyabiashara ambao wengi wao historia zao binafsi katika suala zima la uadilifu
zinafahamika waziwazi ndani ya jamii na zimekuwa zinatiliwa shaka sana kupewa nafasi kwenye vyama vya siasa, hasa chama
tawala.
Wafanyabiashara hawa wakubwa
wenye kashfa mbalimbali za kuhujumu Taifa wamekuwa wakijitokeza kugombania
nafasi mbalimbali za kisiasa, wanapokosa huwa wanaamua kupandikiza watu wao
katika uongozi ili kuhakikisha dili zao na biashara zao zinakaa sawa.
Kinyume na ilivyokuwa katika
awamu ya kwanza na kipindi cha kwanza (1985-90) cha awamu ya pili ya uongozi wa
nchi hii, uongozi wa Tanzania kwa sasa si dhamana tena kama tulivyokuwa tukifundishwa shuleni kwamba 'cheo ni dhamana'. Uongozi
sasa hivi umegeuka kuwa njia ya kumfanya mtu mambo yake yamnyookee, uongozi
umekuwa biashara 'bab kubwa' isiyo na hasara. Zamani uongozi ulikuwa ni mzigo
lakini siku hizi uongozi ni ‘kuula’ kwa maana ya dhiki kutoweka kabisa.
Kuenea kwa dini hii ni
matokeo ya wimbi la wafanyabiashara kujiingiza kwenye siasa na kuviteka vyama huku
wakipandikiza watu wao kwenye uongozi. Inashangaa hata pale wataalamu wa fani
tofauti wanapoacha fani zao na kukimbilia kwenye siasa. Hebu fikiria maprofesa,
madaktari, wahandisi, na wataalamu wa fani mbalimbali wanaacha kazi zao
walizosomea na kupigania kwenda kusinzia bungeni au kwenye mikutano ya
halmashauri!
Wafanyabiashara hawa wana
nguvu kubwa sana ndani ya vyama na hata serikalini, ndiyo maana sasa
tunashuhudia wakisamehewa kodi kila mwaka huku ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu
wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2009/10 aliyoitoa hivi karibuni ikionesha
kwamba katika kipindi hicho misamaha ilifikia shilingi trilioni 1.2 (asilimia
18 ya bajeti yote ya serikali).
Kibaya zaidi, mawaziri na
wabunge wetu ni miongoni mwa vigogo wanaojinufaisha na Sheria ya Msamaha wa
Kodi kinyume cha taratibu. Orodha ya majina ya watu waliosamahewa kodi na
Serikali katika mwaka wa fedha 2009/2010 inaonesha majina ya baadhi ya
mawaziri, wabunge na wakuu wa taasisi za Serikali wakiwa wamenufaika na
misamaha hiyo.
Viongozi hawa wameshiriki katika kuidhinisha shilingi bilioni 31 kununua
bidhaa kwa matumizi ya Serikali pasipo kutolewa ufafanuzi, shilingi bilioni 8 kutumika
bila kufuata utaratibu maalumu na shilingi milioni 143 kutumiwa na serikali
kulipa mishahara kwa wafanyakazi hewa, watoro na waliostaafu! Yaliyomo kwenye
ripoti hiyo yanasikitisha na kutisha sana.
Matokeo ya kushamiri kwa dini hii yamesababisha wataalamu wa wanyama, afisa
afya na watendaji wa majinchio ya Vingunguti jijini Dar es Salaam kuruhusu
kuletwa utumbo na nyama iliyooza na kuuzwa kwa wananchi, kitendo kilichovuka
hata mipaka ya ubinadamu!
Ni nani atabisha kwamba dini hii haina nguvu na haijaenea nchini? Hata
kama nchi inanuka rushwa na ufisadi, lakini ndiyo iwe kwa kiwango cha namna
hii? Kwa hali ya kawaida, haihitaji kuwa msomi sana kubaini kuwa bidhaa ya
kuoza kama ile italeta madhara makubwa sana kwa watu na pengine hata ndugu wa
karibu wa wahusika.
Hii pia haina tofauti na ile habari Shirika la Viwango Nchini (TBS)
kuruhusu bidhaa feki zitumike nchini. Tukubali au tukatae, hii ni dini
inayoenea kwa kasi kutokana na kukumbatia rushwa, kuruhusu wafanyabiashara
watawale mfumo wa uongozi kwa kupandikiza watu wao, na kutochukuliwa hatua
thabiti kwa wanaobainika kufanya ‘madudu’.
Kushamiri kwa dini hii kumesababisha pia kuwapo habari kuwa vibali
bandia 480 vimetolewa na kuidhinishwa na kigogo mmoja wa Idara ya uhamiaji
mkoani Kilimanjaro. Vibali hivyo vimeisababishia Serikali hasara ya Sh 231
milioni. Serikali pia ilipata hasara ya Sh 86 milioni kutokana na vibali vingine
bandia 84 vilivyokamatwa mwaka jana katika kiwanda kimoja wilayani Mwanga, huku
kinara mkuu akidaiwa kuwa uraiani.
Hayo na mengine mengi yanatufanya tuamini kuwa sasa hii ndiyo dini
iliyoshamiri nchini. Ni kipi kitatufanya tusiamini kuwa dini hii ndiyo
inayoenea kwa kasi nchini?
No comments:
Post a Comment