Francois Hollande
Ufaransa
TAREHE 6 Mei 2012, Ufaransa
imempata rais mpya kupitia chama cha kisoshalisti, Francois Hollande, ambaye
amemshinda rais aliyekuwa madarakani akitarajia kupata kipindi kingine cha
uongozi, Nicolas Sarkozy, katika uchaguzi wa marudio uliofanyika mwishoni wa
juma lililopita.
Hollande anakuwa rais wa
kwanza wa kisoshalisti nchini Ufaransa kwa kipindi cha miaka 17; na amekuwa wa
kwanza kumshinda rais aliyetumika kwa muhula mmoja tu, tangu mwaka wa 1981.
Wasoshalisti wanasema kazi
ya mwanzo ni kufanya majadiliano tena juu ya sera za kiuchumi za Umoja wa
Ulaya. Punde baada ya kura za awali kuonesha matokeo, Rais Sarkozy alikiri kuwa
ameshindwa, na alimpigia simu Hollande kumtakia heri.
Historia yake
François Gérard Georges Hollande alizaliwa Agosti 12, 1954. Aliwahi kuwa katibu
wa kwanza wa chama cha Socialist cha Ufaransa kuanzia 1997 hadi 2008 na Naibu
wa Bunge la Ufaransa wa Jimbo la Corrèze 1 tangu mwaka 1997, na hapo awali
aliwakilisha kiti cha ubunge kuanzia 1988 hadi 1993. Alikuwa Meya wa jiji la Tulle
kuanzia mwaka 2001 hadi 2008, na alikuwa Rais wa Baraza Kuu la Corrèze kuanzia
2008 hadi 2012.
Maisha ya awali
Hollande alizaliwa katika eneo la Rouen, Seine-Maritime, Upper Normandy,
katika familia ya kati. Mama yake, Nicole Frédérique Marguerite Tribert
(1927-2009), alikuwa mfanyakazi wa jamii, na baba yake, Georges Gustave
Hollande, alikuwa daktari wa koo, pua na masikio ambaye "aliwahi mara moja
kugombea katika siasa za mitaa". Ubini wa "Hollande" "unaaminika
kutoka kwa mababu waliotoroka Holland (Netherlands) katika karne ya 16 na kuchukua
jina la nchi yao ya zamani." Hollande
alilelewa katika dhehebu la Katoliki.
Elimu
Alisoma katika shule ya Saint
Jean-Baptiste de La Salle, baadaye HEC Paris, shule ya utawala ya École, na Taasisi ya Mafunzo ya Siasa ya
Paris. Alimaliza mwaka 1980. Aliishi nchini Marekani katika majira ya joto ya
1974 alipokuwa mwanafunzi wa chuo kikuu. Mara baada ya kuhitimu, alifanya
kazi kama Diwani wa Mahakama ya Ukaguzi.
Kazi za mwanzo za kisiasa
Baada ya kazi za kujitolea kama mwanafunzi, François Mitterrand hatimaye alishindwa katika kampeni za uchaguzi
wa rais 1974, Hollande alijiunga na Chama cha Kisosholisti miaka mitano
baadaye. Haraka alionwa na Jacques Attali, mshauri mwandamizi wa Mitterrand,
ambaye alipanga Hollande agombee katika uchaguzi wa Bunge la Taifa la Ufaransa mwaka
1981 katika jimbo la Corrèze dhidi ya aliyekuja kuwa rais, Jacques Chirac.
Hollande alishindwa na
Chirac katika raundi ya kwanza, ingawa baadaye alikuwa Mshauri Maalum wa Rais
mpya Mitterrand, kabla ya kufanya kazi chini ya Max Gallo, msemaji wa serikali.
Baada ya kuwa Diwani wa Manispaa wa Ussel mwaka 1983, aligombea katika jimbo la
Corrèze kwa mara ya pili mwaka 1988, wakati huu alichaguliwa kuingia katika Bunge.
Katibu wa kwanza wa Chama cha Kisosholisti
Mwisho wa kipindi cha Mitterrand
madarakani ulivyokaribia, Chama cha Kisoshalisti kilipasuka kutokana na
mapambano ya makundi ndani ya chama, kila kundi likitaka kushawishi mwelekeo wa
chama. Hollande aliomba upatanisho ili chama kiungane nyuma ya Jacques Delors,
Rais wa Tume ya Ulaya, lakini Delors alitangaza nia yake ya kugombea Urais wa
Ufaransa mwaka 1995, na kusababisha Lionel Jospin kuanza upya mbio za uongozi
wa chama.
Jospin alimchagua Hollande
kuwa msemaji rasmi wa chama, na Hollande akagombea katika jimbo la Corrèze kwa
mara nyingine tena mwaka 1997, alifanikiwa kurudi katika Bunge. Mwaka huo,
Jospin akawa Waziri Mkuu wa Ufaransa, na Hollande akashinda na kuwa Katibu wa Kwanza wa chama cha Socialist wa Ufaransa, nafasi ambayo alishikilia kwa miaka
kumi na moja. Kwa sababu ya nafasi kubwa sana ya Chama cha kisoshalisti ndani ya Serikali ya
Ufaransa wakati wa kipindi hiki, nafasi ya Hollande iliwafanya baadhi kumuona kama "Makamu wa Waziri Mkuu". Hollande alichaguliwa kuwa Meya wa Tulle
mwaka 2001, alishikilia nafasi hiyo kwa miaka saba.
Kujiuzulu mara moja kwa
Jospin katika siasa kufuatia mshtuko wake wa kushindwa na mgombea Jean-Marie Le
Pen katika raundi ya kwanza ya uchaguzi wa rais mwaka 2002 kulimlazimisha
Hollande kutizamwa na umma wa chama kwa uchaguzi wa 2002 wa wabunge, ingawa aliweza
kuzuia kushindwa na alichaguliwa tena katika jimbo lake mwenyewe, Chama cha
Kisoshalisti kiliopoteza ushindi kitaifa.
Hatimaye mwenzi wake wa
ndani, Segolene Royal, alichaguliwa kuwakilisha Chama cha Kisosholisti katika
uchaguzi wa rais wa 2007, ambapo alipoteza kwa Nicolas Sarkozy. Hollande
alilaumiwa sana kwa kushindwa kwa Chama cha Kisoshalisti katika
uchaguzi wa 2007, na alitangaza kuwa hatagombea mhula mwingine kama Katibu wa Kwanza . Hollande alitangaza hadharani kumuunga mkono
Bertrand Delanoë, Meya wa Paris, ingawa ni Martine Aubry aliyefanikiwa kushinda
mwaka 2008.
Kufuatia kujiuzulu kwake kama Katibu Kwanza , Hollande mara moja alichaguliwa kuchukua nafasi ya
Jean-Pierre Dupont kama Rais wa Baraza
Kuu la Corrèze mwezi Aprili 2008, nafasi aliyoishika hadi anachaguliwa kuwa
rais.
Kufuatia kuchaguliwa kwake
tena kama Rais wa Baraza Kuu la Corrèze Machi 2011, Hollande
alitangaza kwamba atagombea katika uchaguzi ujao wa awali kuchagua mgombea wa
chama cha kisoshalisti wa urais. Kufuatia kukamatwa kwa Strauss-Kahn kwa tuhuma
za unyanyasaji wa kijinsia jijini New York Mei 2011, Hollande alionekana kuanza
kuongoza kura ya maoni. Nafasi yake kama mgombea ilianzishwa
na Strauss-Kahn aliposema hatatafuta nafasi ya uteuzi katika kinyang’anyiro
hicho. Baada ya mfululizo wa mijadala mwezi wote wa Septemba, Hollande aliongoza
katika kura katika duru ya kwanza iliyofanyika Oktoba 9 kwa asilimia 39 ya
kura, dhidi ya Martine Aubry, aliyekuwa wa pili kwa asilimia 30 ya kura.
Uchaguzi wa pili ulifanyika
Oktoba 16, 2011. Hollande alishinda kwa asilimia 56 ya kura kwa 43 za Aubry na
hivyo akawa mgombea rasmi wa chama cha kisoshalisti wa urais kwa mwaka 2012.
Baada ya matokeo ya awali, aliungwa mkono mara moja na wagombea wengine wa
chama kwa ajili ya uteuzi, ikiwa ni pamoja na Aubry, Arnaud Montebourg, Manuel
Valls na mgombea wa 2007, Segolene Royal.
Kampeni za urais za Hollande
zilisimamiwa na Pierre Moscovici na Stéphane Le foll, Mbunge ambaye pia ni Mbunge
wa Ulaya. Hollande alizindua kampeni zake rasmi na mkutano wa hadhara na hotuba
kubwa katika eneo la Le Bourget Januari 22, 2012, mbele ya watu 25,000.
Tarehe 26 Januari iliainisha
orodha kamili ya sera katika ilani yenye maazimio 60, ikiwa ni pamoja na
mgawanyo wa shughuli za rejareja kutoka biashara za uwekezaji za kibenki;
kupandisha kodi kwa makampuni makubwa, mabenki na matajiri; kutengeneza ajira za
kufundisha 60,000; kurudisha umri rasmi wa kustaafu kutoka 62 hadi 60; kuanzisha
ajira za ruzuku katika maeneo ya uhaba mkubwa wa ajira kwa vijana; kukuza zaidi
viwanda nchini Ufaransa kwa kujenga uwekezaji wa benki za umma; kupitisha ndoa
na haki za kuasili mtoto kwa wanandoa za jinsia moja, na kuwaondoa askari wa
Kifaransa nchini Afghanistan mwaka 2012. Februari 9, alielezea kwa kina sera
zake hasa kuhusiana na elimu katika hotuba kubwa katika eneo la Orleans .
Tarehe 15 Februari, Rais
Nicolas Sarkozy alitangaza kugombea kwa awamu ya pili na ya mwisho, akikosoa vikali
mapendekezo ya Hollande na kudai kuwa ataleta "maafa ya kiuchumi ndani ya
siku mbili baada ya kuchukua madaraka" kama akishinda.
Katika ziara yake ya kwanza
nje ya nchi kwa ajili ya kampeni zake, alitembelea Berlin, Ujerumani, Desemba
2011 kwenye mkutano wa Shirikisho wa Chama cha Kidemokrasi cha Kijamii, ambapo
alikutana na Sigmar Gabriel, Peer Steinbrueck, Frank-Walter Steinmeier na
Martin Schulz; pia alisafiri hadi Ubelgiji kabla ya kwenda Uingereza mwezi
Februari 2012, alikokutana na kiongozi wa upinzani, Ed Miliband, na hatimaye
Tunisia mwezi Mei 2012.
Duru ya kwanza ya uchaguzi
wa rais ilifanyika 22 Aprili. François Hollande aliongoza kwa asilimia 28.63 ya
kura, na kumkabili Nicolas Sarkozy katika duru ya pili. Katika mzunguko wa pili
Jumapili iliyopita ya Mei 6, 2012, François Hollande alichaguliwa kuwa Rais wa
Jamhuri ya Ufaransa kwa asilimia 51.7 ya kura.
Makala haya yameandaliwa na Bishop Hiluka kwa msaada
wa vyanzo mbalimbali vya habari vya kimataifa.
No comments:
Post a Comment