Mshindi wa ubunge Jimbo la Arumeru, Joshua Nassari
BISHOP HILUKA
Naamini kuwa kwa sasa
uchaguzi umepita na wahusika wanafanya tathmini ya yaliyotokea, lakini binafsi umeniacha
na maswali ambayo sina majibu yake na ninadhani Tume ya Taifa ya uchaguzi (Nec)
inapaswa kutafuta majibu ili kutuondolea shaka hii, kwani naamini si mimi peke
yangu mwenye shaka.
Natumaini kuwa hivi sasa Tume
ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) watakuwa wameanza kufanya tathmini ya utendaji wa chombo
hicho katika muktadha wa usimamizi wa sheria, kanuni, taratibu, maadili ya
uchaguzi na mwenendo mzima wa uchaguzi huo.
Tukiachana na kasoro kadhaa
zilizojitokeza katika uchaguzi wa Arumeru na hata katika chaguzi zingine
zilizoambatana na huo za udiwani katika maeneo kadhaa ya nchi, mojawapo ya
kasoro hizo ilihusu uvunjifu wa amani na kusababisha wabunge wawili wa Chadema
kucharangwa mapanga katika mkesha wa uchaguzi wa diwani katika Kata ya Kirumba,
jijini Mwanza.
Ninachokikusudia hapa ni kuieleza
hii kasoro ya idadi ya watu waliojiandikisha kupiga kura kuwa kubwa mno ikilinganisha
na idadi ya watu wanaojitokeza kupiga kura.
Inaonekana kuwa suala hili
la takwimu katika idadi ya wapiga kura walioandikishwa katika daftari la kudumu
la wapiga kura limekuwa ni tatizo sugu nchini. Mi’ nadhani kazi kubwa
inayoikabili Nec kwa sasa ni kuhakiki upya Daftari hili la Kudumu la Wapiga kura
ambalo naamini limesababisha wananchi wengi kutokuwa na imani na chaguzi
zinazosimamiwa na kuendeshwa na tume hiyo.
Takwimu hizi ni jinamizi linalousumbua
mfumo mzima wa uchaguzi katika nchi yetu kwani sidhani kama Nec yenyewe wana uhakika na idadi ya wapiga kura walioorodheshwa
katika daftari hilo .
Wakati wa uchaguzi Mkuu wa
mwaka 2010 nilianza kuingiwa shaka pale ilipokuwa ikitajwa kuwa idadi ya wapiga
kura katika daftari la kudumu ilikuwa ni watu milioni 20,137,303, na hata baada
ya uchaguzi kauli kubadilika na kuwa watu milioni 19! Hii ikiambatana na idadi
ndogo ya watu milioni 8,626,283 tu sawa na asilimia 42.84 waliojitokeza kupiga
kura katika uchaguzi huo.
Nilianza kupata wasiwasi
hasa baada ya kusoma chapisho lenye takwimu zinazochapishwa na majarida ya
kimataifa, kuwa Tanzania , Afrika na nchi zinazoendelea duniani zinaonesha
watu wenye umri kati ya siku moja hadi chini ya miaka 18 ni kati ya asilimia 65
hadi 70.
Wenye umri wa kuanzia miaka
18 na kuendelea ni kati ya asilimia 30 hadi 35. Na ikasisitizwa kuwa haijapata
kutokea katika nchi yoyote ya dunia ya tatu ikiwemo Tanzania kukuta idadi ya watu waliojiandikisha kupiga kura
ikazidi asilimia 25 ya idadi ya wananchi katika nchi husika.
Lakini mwaka 2010, Tanzania iliyo katika kundi hili la nchi za dunia ya tatu, eti
ikawa na idadi ya watu waliojiandikisha kupiga kura karibu asilimia 55 ya
wananchi wake! Hii ilikuwa ni rekodi ya aina yake na ilipaswa kuingizwa kama maajabu kwenye kitabu cha kumbukumbu za dunia, Guinness Book
Encyclopedia.
Lakini hili la Arumeru
limenifanya nione kuwa hapa kuna kiini macho kuhusu idadi ya watu katika daftari
la wapiga kura, kwani naamini kuwa wakazi wa Jimbo la Arumeru walikuwa wamehamasika
mno katika uchaguzi huu, na hata vyama vilivyochuana, hususan CCM na Chadema
vilikuwa vikiwahamasisha na kuwahimiza kujitokeza kupiga kura siku ya tarehe
Mosi Aprili. Cha ajabu bado tumesikia yaleyale ya idadi ndogo ya wapiga kura
ikilinganishwa na waliojiandikisha!
Ni watu 60,699 tu waliopiga
kura kati ya watu 127,455 waliojiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga
kura kwa mujibu wa Nec. Hapa kuna maswali mengi kuliko majibu.
Kwa nini Nec haifanyi
uhakiki kila mwaka kujua ni wangapi waliofariki au kuhama kutoka sehemu moja
kwenda nyingine? Hivi haioni kuwa kutofanya hivyo ni kuiminya demokrasia? Nasmea
kuiminya demokrasia kwa kuwa ikumbukwe pia kuna vijana wengi ambao mwaka 2010 (miaka
miwili nyuma) hawakuwa wametimiza miaka 18 inayowaruhusu kupiga kura kwa mujibu
wa sheria lakini mwaka jana na hata mwaka huu wametimiza umri wa kupiga kura.
Hivyo walikuwa na haki ya kupiga kura katika chaguzi ndogo lakini wamenyimwa
fursa hii. Hivi hali hii inaendelea hadi lini?
Naomba kuwasilisha.
No comments:
Post a Comment