Dioncounda Traore
WAKUU wa serikali nchini Mali wamesema kuwa Rais wa Mpito wa nchi hiyo,
Dioncounda Traore, amepelekwa eneo salama baada ya kupigwa hadi kuzirai na
mamia ya waandamanaji nchini humo.
Mamia ya waandamanaji
walimshambulia Rais Traoure wakipinga mkataba ulioafikiwa na Tume ya kiuchumi
ya nchi za Magharibi mwa Afrika, ECOWAS, ambapo Traoure ataendelea kutawala kwa
hadi mwaka mmoja badala ya siku 40 pekee zilizokubaliwa miezi miwili iliyopita.
Mwandishi wa Shirika la
Utangazaji la Uingereza, BBC, amesema kuwa shambulio hilo litawashtua wanadiplomasia waliokuwa wakifanya kila
juhudi kurejesha amani na utangamano nchini humo. Muda wa kuongoza aliopewa
kiongozi huyo, Djouncounda Traore, ulitarajiwa kukamilika Jumatatu.
Lakini viongozi wa nchi za
Magharibi mwa Afrika, waliafikia mkataba na kiongozi wa mapinduzi, Kapteni
Amadou Sanogo, kwamba Traore asalie mamlakani ili aweze kuongoza harakati za
uchaguzi na kumaliza harakati za waasi wa Tuareg.
Mkataba huo pia ulijumuisha
mpango wa kukubalia Sanogo atajwe kama kiongozi wa
zamani alipwe mshahara wa rais na apewe nyumba ya kifahari.
Mapinduzi hayo pamoja na
harakati za waasi kuteka maeneo ya Kaskazini mwa Mali , yamesababisha maelfu ya watu kutoroka makwao. Mashirika
ya misaada wanasema wana wasiwasi mkubwa kuhusu hali ya kibinadamu nchini Mali nchi ambayo pia inakumbwa na baa la njaa.
Mwandishi wa Shirika la
Utangazaji la Uingereza, BBC, mjini Bamako , Martin Vogl amesema kuwa wanajeshi waliwaruhusu
baadhi ya waandamanji kuingia katika ikulu ya rais ingawa rais huyo wa mpito
hakuwepo wakati huo.
Historia yake
Dioncounda Traoré amezaliwa
tarehe 23 Februari, 1942, ni mwanasiasa wa Mali ambaye amekuwa Rais wa Mali katika kipicha cha muda mfupi tangu mwezi Aprili
mwaka 2012. Amekuwa Rais wa Bunge la Mali tangu mwezi Septemba 2007, na Rais wa chama cha
kisiasa kinachojulikana kama Alliance
for Democracy in Mali-African Party for Solidarity and Justice (ADEMA-PASJ)
tangu mwaka 2000. Pia alikuwa Rais wa Alliance for Democracy and Progress (ADP), muungano wa vyama
ambavyo viliunga mkono uchaguzi wa marudio wa Rais Amadou Toumani Touré mwaka
2007.
Kazi ya siasa
Traoré alizaliwa katika
eneo la Kati. Baada ya kusoma nje ya nchi katika Umoja wa Kisovyeti, katika
Chuo Kikuu cha Algiers, na katika Chuo Kikuu cha Nice, alifundisha nchini Mali
katika Chuo cha Walimu (ENSUP) kati ya 1977 na 1980. Kisha alikamatwa kwa kujishughulisha
na harakati za mambo ya muungano wa vyama vya kibiashara na kupelekwa Ménaka
kaskazini mwa Mali .
Baada ya hapo, akawa
mkurugenzi mkuu wa Shule ya Taifa ya Uhandisi. Alishiriki katika mapambano kwa
ajili ya demokrasia ambayo yalisababisha kuangushwa kwa Rais Moussa Traoré mnamo
Machi 1991. Alikuwa mwanachama mwanzilishi wa ADEMA, na katika mkutano wake wa
Katiba, uliofanyika mnamo Mei 25 na 26 mwaka 1991, alichaguliwa kuwa Makamu wa
Pili wa Rais wa ADEMA, wakati Alpha Oumar Konaré alichaguliwa kuwa Rais wa
chama hicho na Mohamed Lamine Traoré alichaguliwa kuwa Makamu wake wa kwanza wa
Rais.
Baada ya Konaré kuchaguliwa
kuwa Rais wa Mali katika uchaguzi wa rais wa mwaka 1992, Traoré aliteuliwa kuwa Waziri
wa Utumishi wa Umma, Kazi, na Utawala mnamo tarehe 9 Juni 1992, katika serikali
ya kwanza chini ya rais wa Konaré. Baadaye aliteuliwa kuwa Waziri wa Nchi kwa
ajili ya Ulinzi mnamao tarehe 16 Aprili 1993, ameshika nafasi hiyo hadi alipokuwa
Waziri wa Nchi kwa ajili ya Mambo ya Nje mnamo tarehe 25 Oktoba 1994. Katika
mkutano wa kwanza wa ADEMA wa kawaida, uliofanyika Septemba 1994, Traoré
alichaguliwa kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa chama hicho, wakati Ibrahim Boubacar
Keïta alichaguliwa kuwa Rais wake.
Alichaguliwa kuwa Naibu
katika Bunge akitokea Nara mwaka 1997 na kujiuzulu nafasi yake ya Waziri wa
Mambo ya Nje mnamo tarehe 24 Agosti 1997 ili kuchukua kiti chake cha ubunge.
Katika Bunge, akawa Rais wa Kundi la Wabunge wa ADEMA, kufuatia kujiuzulu kwa
Keïta katika nafasi ya Urais wa ADEMA mnamo Oktoba 2000, Traoré alichaguliwa
kuwa Rais wa ADEMA kwa mara ya kwanza katika Mkutano wa chama wa dharula,
uliofanyika Novemba 25 hadi 28, 2000. Katika uchaguzi wa mwaka 2002 wa bunge, Traore
alishindwa katika jimbo la Nara
na kupoteza kiti chake.
Katika uchaguzi wa wabunge mnamo
Julai 2007, Traoré aligombea tena katika akiwemo orodha ya ADEMA katika jimbo
la Nara , ambapo viti vitatu vilikuwa hatarini. Katika
raundi ya kwanza, orodha yake ilishinda kwa asilimia 39.59 ya kura, na katika
raundi ya pili ilishinda kwa asilimia 58.41 ya kura. Wakati Bunge jipya la
taifa lilipofanya mkutano wake wa kwanza tarehe 3 Septemba 2007, Traoré
alichaguliwa kuwa Rais wa Bunge, akipata kura 111 dhidi ya kura 31 za Mountaga
Tall wa National Congress for Democratic Initiative (CNID), mwanachama mwingine
wa ADP.
Kufuatia mapinduzi ya
kijeshi mnamo Machi 2012, ambayo yalisababisha kuwekwa vikwazo vya kiuchumi na
Jumuiya ya Kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) dhidi ya Mali, mpango
huo, ulioandaliwa katika nchi ya Burkina Faso na Rais Blaise Compaoré chini ya
mwamvuli wa ECOWAS, ulisainiwa tarehe 6 Aprili 2012 ambao ulitarajiwa kuona
mkuu wa serikali hiyo ya kijeshi, Kapteni Amadou Sanogo, akiachia madaraka kwa
Dioncounda Traoré ili ashikilie madaraka ya urais katika serikali ya mpito hadi
uchaguzi utakapofanyika. Traoré alikuwa ameondoka nchini humo kufuatia
mapinduzi ya kijeshi, lakini alirudi mnamo Aprili 7.
Traoré aliapishwa kuwa Rais
katika sherehe iliyofanyika mnamo tarehe 12 Mei 2012. Aliahidi "kufanya
vita" juu ya uasi wa Tuareg katika upande wa kaskazini mwa Mali isipokuwa kama wataachia udhibiti
wa miji ya kaskazini mwa Mali na kutangaza kuwa ni nchi ya Azawad.
Shambulio la Mei 2012
Tarehe 21 Mei 2012, askari
waliruhusu kundi la waandamanaji wanaounga mkono mapinduzi ndani ya ofisi ya Traoré
katika mji wa Bamako . Waandamanaji, ambao walikuwa wamebeba jeneza likiwa
limeandikwa kimasikhara jina la Traoré juu yake, wakamshambuliwa, hadi akapoteza
fahamu. Alipelekwa katika Hospitali ya Point G lakini hakuwa na fahamu wakati akipelekwa
hapo, inaonekana alikwa anaosumbuliwa na majeraha ya kichwa. Waandamanaji
watatu waliuawa na wengine kujeruhiwa wakati wana usalama wa Traoré walipowafyatulia
risasi.
Makala haya yameandaliwa na Bishop Hiluka kwa msaada
wa vyanzo mbalimbali vya habari vya kimataifa.
No comments:
Post a Comment