BISHOP J. HILUKA
MUUNGANO wa nchi mbili za Tanganyika na Zanzibar uliozaa taifa jipya la Tanzania ulizaliwa Aprili 26, 1964 na hivyo Alhamisi ya
Aprili 26 mwaka huu muungano wetu umetimiza miaka 48. Nilishuhudia sherehe za Muungano
kupitia televisheni, na hali imeendelea kubainisha kuwa tunalazimisha
kusherehekea huku kukiwa na manung’uniko kutoka kwa wananchi na hata baadhi ya
viongozi wa kisiasa wakionekana ama kuupinga mfumo wa Muungano au kutoutaka
kabisa Muungano huu.
Wazanzibar wanalalamika
wamemezwa na Tanzania Bara, Watanzania Bara (Watanganyika) wanalalamika kuwa wameipoteza
Tanganyika yao na
wananyonywa kupitia mwamvuli wa Muungano wa Tanzania , lakini wachache katika serikali yetu wameapa kuwa
wataulinda muungano huu kwa nguvu zote!
Ni ajabu sana kuwa kila upande unalalamika! Inashangaza sana katika vuta nikuvute hii eti kuna kundi linasema litaulinda
Muungano kwa nguvu zote! Katika kuulinda huu Muungano kumekuwepo tafsiri ambayo
inahitaji ufafanuzi; kuulinda kwa nguvu zote maana yake nini?
Wafuatiliaji wa masuala ya
siasa wanaiona kauli ya kuulinda ni kuzuia watu wasiujadili. Kutoruhusu
uvunjike. Huku wengine (nikiwemo mimi) tukijiuliza, ya nini kuwa na muungano
bila kuujadili? Inafaa nini kuishi kwa mazoea? Na kwa faida ya nani? Huku Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akisema kuwa jambo pekee wanalopaswa wananchi kujadili
kuhusu Muungano ni kuuboresha! Inawezekanaje watu waboreshe kitu ambacho
hawajakubaliana umuhimu wake?
Rais amesahau kuwa Watanzania
walio wengi leo hii ni vijana waliozaliwa baada ya Muungano. Ingawa wamesoma
habari za Muungano katika vitabu vya historia lakini hawauelewi vyema, ndiyo
maana hata shamrashamra za serikali na wananchi juu ya Muungano zimeshuka siku
hizi. Tunachoshuhudia ni wananfunzi kulazimishwa kwenda kwenye sherehe hizi
bila ridhaa yao .
Hapa sijui kama kweli kuna nia ya dhati ya kuuboresha. Kutoujadili? Kutorusu uvunjike?
Hivi tunayafanya haya kwa faida ya nani? Wananchi ambao ndiyo wenye nchi yao wanataka kuandika upya historia yao tena kwa nyakati zao
lakini viongozi wanataka
kuwaenzi waasisi kinafiki! Nani mwenye nchi? Wananchi au viongozi?
Siandiki haya kwa kuwa
labda siutaki Muungano, hasha! Nautakia mema ndiyo maana napenda tukae mezani kuujadili,
tuangalie kasoro zote zilizopo na kuzirekebisha ili hatimaye tuingie kwenye Muungano
uliopata ridhaa za wananchi wa pande zote. Ni kufilisika kimawazo kudhani
kwamba anayehoji Muungano ana nia ya kuuvunja. Badala yake, ni kuchochea
mjadala mpana na wa kina kuhusu umuhimu wa Muungano. Hatutakuwa na muungano imara
kama viongozi wataendelea kutulazimisha bila kusikiliza
hoja na manung’uniko yetu.
Hata hivyo, kuvunjika kwa
muungano si jambo la ajabu, kama hatutaruhusu mijadala ya wazi tunaweza kuishia
walikoishia wengine. Tusidhani kuwa sisi tuna akili zaidi au tumebarikiwa zaidi
ya wengine. Tuna kipi cha ajabu? Kumbukumbu zangu zinanieleza kuwa mojawapo ya
waliokuwa nchi moja na kutengana ni Ethiopia iliyotengana na Eritrea, muungano
wa Senegambia ulishindikana kwa kuwa wananchi hawakushiriki na hatimaye walitengana
na kubaki nchi mbili za Senegal na Gambia, pia iliyokuwa Rwanda-Burundi ambayo
sasa ni nchi mbili za Rwanda na Burundi, India iliyogawanyika na kuzaa
Pakistan, na Pakistan ikazaa Bangladesh.
Inashangaza sana kuona kuwa kundi dogo linataka kubinafsisha mawazo
ya walio wengi, vijana na wasomi wa taifa hili wanashindwa kuhoji mambo kwa
mapana yake. Tunapaswa tujiulize, hivi kwa nini tuliungana? Huu si wakati tena
wa kuleta sababu dhaifu eti tunaleta umoja au eti kwa vile sisi ni ndugu. Mbona
hatuungani na Wakenya wakati nchi zote hizi zina undugu?
Kwa nini hatupewi nafasi ya
kuhoji nini sababu hasa ya muungano huu? Wenye majibu wote kwa sasa hawapo na
yaliyobaki ni majibu ya kufikirika tu, nafasi ya uongo ni kubwa. Bila majibu
haya, ni vigumu ni bora watu wakajadili na wakaja na aina ya muungano
wanaoutaka.
Hali ya mashaka inaugubika
Muungano huu, inatokana na kile kinachodaiwa kuwa kuundwa kwa Muungano wetu
kulikuwa siri na tangazo la kutiwa saini mkataba wa Muungano kati ya Rais wa
Tanganyika, Mwalimu Julius K. Nyerere, na Rais wa Zanzibar, Sheikh Abeid Amani
Karume, liliwashangaza watu kutoka pande zote za muungano; Bara na Visiwani.
Habari zinazidi kupasha
kuwa hali hii ilitokana na habari za Muungano kuwa za siri na watu wa pande
zote mbili za Muungano hawakushauriwa utadhani hawakuwa na haki yoyote ya
mustakabali wa nchi yao .
Ndiyo maana nafikiri
kuendelea kudhani kuwa kujadili jambo lolote linalohusu Muungano ni uhaini au
kuendelea kuyafumbia macho masuala ya Muungano tutakuwa tunajidanganya, kwani
kuficha au kudharau maradhi ni ugonjwa hatari, na ipo siku mauti itatuumbua.
Ukiuangalia Muungano wetu
kijuujuu utaona kuwa ni mfano mzuri sana wa maelewano kwa watu wa Bara la Afrika, lakini
chini kwa chini kunafuka moshi ambao ukiachwa hivi hivi bila kutafutiwa
ufumbuzi utakuja kujitokeza moto mkubwa ambao tunaweza kushindwa kuuzima na
hivyo matokeo yake hayatakuwa mazuri.
Kwa kuwa tupo katika
kipindi cha kuandika Katiba mpya, nadhani ni wakati mwafaka kila Mtanzania
aweke maslahi ya taifa mbele bila ushabiki, viongozi nao wawe mstari wa mbele
kuonesha njia na siyo kuwa na sauti ya mwisho juu ya Muungano.
Hofu za viongozi wetu
zinatoka wapi? Mbona Watanzania wengi kutoka pande zote zinazohusika na
Muungano, wanaonekana wazi hawapingi kuungana, kwani muungano kwao ni baraka.
Ila hiki kinachoitwa Kero za Muungano.
Kero hizi ni pamoja na
mfumo wa Muungano, ikiwa ni pamoja na wanaotaka muundo wa serikali mbili
uendelee, lakini wapo wanaosema uwe wa serikali moja na wapo wanaopendelea
mfumo wa shirikisho wa serikali tatu. Nadhani wote wanapaswa kusikilizwa, ikiwa
ni pamoja na sababu wanazotoa kama kweli tunataka kuuboresha Muungano. Muundo wa
Muungano, hata kama chama tawala kimekuwa kikidai kuwa sera yake ni ya
serikali mbili, linatakiwa liwe jambo litakaloamliwa na wananchi wenyewe
kupitia kura ya maoni.
Ukiangalia kwa makini
utagundua kuwa Muungano wetu uliundwa ukiwa zaidi na sura ya kisiasa na ulikuwa
wa mambo 11 kama ambavyo imekuwa ikielezwa, lakini sasa wapo
wanaosema yamefika 22 na wengine hudai ni zaidi ya 30. Kumekuwa na utata juu ya
kuongezeka mambo ya Muungano na viongozi wengine wanasema mengi yameongezwa
kinyemela.
Hata hili la ushirikiano wa
kimataifa halikuwa limejumuishwa katika orodha asili ya mambo ya Muungano na
ndiyo maana Zanzibar waliamua kujiunga na Jumuiya ya Nchi za Kiislamu
(OIC), kwa vile suala hili halikuwa la Muungano, hali iliyoutikisa Muungano na
kusababisha mzozo mkubwa.
Kero nyingine ni kuhusu
Rais wa Zanzibar aliyetakiwa moja kwa moja awe Makamu wa Rais wa serikali ya Muungano
kama Rais atatoka Bara, na pale Rais atakapotoka upande wa pili, yaani Zanzibar
mwenzake wa Bara awe Makamu wa Rais. Lakini hili limeondolewa bila ya kura ya
maoni, kwa hofu tu zisizo na maana yoyote
Miaka ya hivi karibuni
zimekuwa zinasikika kelele kutoka Zanzibar kutaka masuala ya uchimbaji na biashara ya mafuta
na bahari kuu yatolewe katika orodha ya Muungano, huku Mamlaka ya Kodi ya
Mapato pia ikilalamikiwa. Haya yanahitaji muungano kuhojiwa kwa uwazi ili
majibu ytaolewe. Kama kutakosekana majibu ya maana, itakuwa ni kazi bure
kutumia maneno makali kwani wananchi wataukataa.
No comments:
Post a Comment