Jun 1, 2012

Tuwekane sawa; ni vazi au kitambaa cha taifa?


Ndesumbuka Merinyo, mwenyekiti wa kamati ya Vazi la Taifa na mjumbe wa Kamati hiyo


BISHOP HILUKA
Dar es Salaam

ZIMEKUWA zikitolewa hoja mbalimbali kuhusiana na hiki kinachoitwa vazi la taifa. Hoja ambazo zimekuwa zikiniacha na maswali kadhaa ambayo nimejaribu kuyauliza lakini hadi leo wahusika hawajajitokeza kuyatolea ufafanuzi, na hata pale walipofafanua walitoa hoja dhaifu ambazo binafsi bado hazijanishawishi kukiamini kile wanachokihubiri.

Mtaniwia radhi kama nitaonekana si mzalendo, lakini mimi pia nina mtazamo wangu katika jambo hili. Mwanzoni mwa mchakato nilidhani kinachotafutwa ni vazi la taifa, lakini siku chache hata kabla ya mdahalo mmoja uliorushwa na kituo cha televisheni cha ITV nilishangazwa kuanza kusikia kauli za wahusika wakuu wa mchakato huu kuhusu mwenendo mzima wa kupata kile kinachoitwa vazi la taifa. Wahusika hao, kwa nyakati tofauti walikuwa wakisikika kuongelea aina ya kitambaa, ubora wake na rangi gani inafaa!

Hapa bado pana mkanganyiko mkubwa, wanaposema eti kitambaa kitakuwa na ubora tofauti kulingana na hadhi ya mvaaji, wakitolea mfano wa wabunge, ambao wanaweza kuchagua suti waipendayo kutokana na kitambaa hicho! Kumbe mawazo yao yamejikita kwenye kitambaa na ubora wa kitambaa na si vazi kama dhana nzima ilivyoelezwa mwanzo! Je, kwa wananchi wengi, hususan vijijini ambao hawamudu bei za vitambaa madukani na kimbilio lao kubwa ni mitumba tunawaambia nini? Pia hapa sijajua, hoja ni vazi au kitambaa cha taifa?

Hata hivyo, vazi la taifa halitafutwi na halijawahi kutafutwa! Wamasai walitafutiwa na nani? Au hizo nchi zinazotolewa mfano; Ghana, Nigeria, Afrika Kusini au China hawajawahi kuwa na kamati ya kutafuta vazi. Kwanza si kweli kwamba wana mavazi ya taifa, hayo tunayodhani kuwa ni ya taifa ni mavazi yanayovaliwa na makabila makubwa. Nina wasiwasi kwamba tutatumia pesa nyingi katika kitu kisicho na tija kwa maana kuwa mwisho wa mchakato vazi halitakuwepo.

Nimekuwa sikubaliani na sababu zinatolewa eti vazi hili litazidisha uzalendo, litaleta maendeleo, litatangaza utamaduni, vivutio na utambulisho wa nchi! Nijuavyo, vazi la taifa kama ni utamaduni basi utamaduni hauundiwi mezani kama tunavyotaka kuaminishwa.

Ieleweke kuwa lengo la makala hii ni kutoa changamoto na kuibua mjadala zaidi katika kuangalia namna nzuri ya kurudisha maadili, uzalendo na kuutangaza utamaduni wetu katika kazi za sanaa na changamoto zinazotukabili juu ya namna ya kukuza au kudhibiti wimbi la mapokeo ya sanaa zinazokiuka mila, desturi na maadili yetu ya Ki-Tanzania, badala ya kufikiria kuwa kitambaa pekee kitatusaidia.

Hebu tujiulize ni nchi gani duniani ambayo kuendelea au kutokuendelea kwake kumetokana na kuwa ama kutokuwa na vazi la taifa? Je, ni kitu gani cha muhimu ambacho kama taifa tumekikosa kwa miaka 50 kwa sababu ya kutokuwa na kipande cha nguo kinachoitwa vazi la taifa? Ni kweli uzalendo umepungua nchini kwa sababu ya kukosa vazi la taifa? Je, vazi la taifa ni sawa na vazi la heshima ambalo ndicho kitu cha msingi sana kama tunaangalia udumishaji wa mila?

Nafikiri tuna changamoto nyingi ambazo hata tukileta hilo vazi haliwezi kuziondoa, tunapaswa kukabiliana na mmomonyoko wa maadili kwenye jamii yetu ambao unaletwa na utamaduni tunaoiga toka nje, huku wizara inayoratibu mchakato wa kitambaa kinachoitwa cha taifa ikiwa kimya na haijawahi kuunda kamati kuushughulikia. Tunashuhudia mmomonyoko mkubwa katika jamii hii, kupitia nyimbo za matusi, filamu na nyimbo za mapenzi au zisizo na asili yetu zilizonakili vitendo na maudhui ya jamii za nje. Je, wizara husika iko wapi katika hili?

Sanaa kama nguzo muhimu ya utamaduni hukua na pia hufa. Hivi sasa sanaa zetu zipo katika chumba cha wagonjwa mahututi na tusipochukua juhudi za ziada tutazika uasili wa sanaa zetu tulizoachiwa na wazee wetu zilizodumu kizazi hadi kizazi. Hili linazigusa sanaa zote kuanzia filamu, muziki, sanaa za maonesho na kazi za mikono. Ni kweli njia tunayoenda nayo katika kazi zetu za sanaa inatupeleka kwenye msingi wa waliotutangulia au tumepotea na wimbi la utandawazi? Je, hili vazi litasaidiaje kuzifanya sanaa zetu zisife?

Tuna tatizo kubwa la maadili katika sanaa na udhibiti wa kazi chafu, jambo ambalo limekuwa gumzo. Mbona wizara haijawahi kuandaa kamati ya kutafuta alama ya muziki wetu? Mbona haitafuti alama ya filamu au chanzo cha wasanii kuiga filamu zisizo na maadili? Au mbona ubunifu wa mitindo yetu ya kucheza muziki wetu na sanaa nyinginezo ni wa kuiga? Kwa nini vazi la taifa?

Nimewahi kusoma kwenye chapisho fulani kuwa fani ya muziki inaporomoka kwani wanamuziki walio wengi wamepotea njia kwa kutofuata miiko katika tungo zao, miundo, mitindo na maudhui kulingana na uasili, mila, desturi, mapokeo, historia na urithi tulioachiwa. Haya yote yakiwa yanaashiria kuporomoka kwa fani hii.

Kadri muda unavyozidi kwenda tunawapoteza wapiga ala kama ngoma, marimba, zeze, Saxophone na kadhalika, huku idadi lukuki ya waimbaji bandia wasio na msingi na kanuni za fani ya uimbaji na utunzi wakiongezeka na kusababisha muziki wetu kuchuja katika muda mfupi, hapo hapo teknolojia ikimaliza vipaji vya wapiga ala kwa kuwa kila ala siku hizi ipo studio kwenye mashine (computer). Mbona wizara haiundi kamati kunusuru hili?

Tumekuwa mahodari wa kushabikia sanaa za kutoka nje ya nchi. Kuanzia kwenye jamii hadi ngazi ya taifa, jambo linalotufanya kuwa wasindikizaji kwa kupokea sanaa na mitindo toka nje. Haya yanajitokeza katika fani za unenguaji, filamu, muziki wa injili na hata fani nyinginezo za sanaa. Bila kujua tumekuwa tunapandikiza mbegu mbaya katika jamii kwa kutopenda cha kwetu. Je, katika mazingira haya uzalendo na moyo wa kuipenda nchi utabadilishwaje na kitambaa tunachoita vazi la taifa?

Mwisho, tujiulize maswali haya; je, vipaumbele vyetu kama taifa ili kujiletea maendeleo na kudumisha maadili ni muhimu kuwa na vazi la Taifa leo? Tunapoangalia ubora na rangi ya vitambaa katika nchi hii ya wavaa mitumba, je, serikali kupitia wizara husika haikuona umuhimu wa kuunda kwanza tume ya kusaidia wakulima wa pamba ili pamba yao iwe katika kiwango bora badala ya kukimbilia kuunda tume ya kutafuta vazi la Taifa?

Je, kuna mkakati gani hadi sasa wa kuongeza thamani ya pamba yetu ili tuiuze kama malighafi nje ya nchi? Kwa nchi ambayo haina viwanda vya nguo, leo tunaunda tume ya kutafuta vazi la Taifa, hivi kama vazi hilo likipatikana ni kiwanda gani hapa nchini kitashona nguo hizo za vazi linaloitwa la Taifa? Au tutaanza tena mchakato wa kutafuta mzabuni wa kutushonea nguo katika nchi kama China, India, Pakistani na kwingineko?

Alamsiki…

No comments:

Post a Comment