May 11, 2011

MAMADOU TANDJA: Rais wa zamani Niger aliyeonja joto ya jiwe sasa kupata ahueni

 Mamadou Tandja

NIAMEY
Niger

MAHAKAMA ya Rufaa nchini Niger Jumanne wiki hii imeamuru kuachiliwa huru kwa rais wa zamani wa nchi hiyo, Mamadou Tandja, aliyepinduliwa mwezi Februari 2010. Tandja aliyekuwa madarakani kwa miaka 10, anatuhumiwa kwa matumizi mabaya ya fedha za umma.

Viongozi wa mapinduzi hayo walikasirishwa baada ya Tandja kuwania uongozi tena kwa kipindi kingine cha tatu. Mwezi uliopita, uongozi huo wa kijeshi ulikabidhi rasmi utawala kwa kiongozi wa upinzani wa siku nyingi, Mahamadou Issoufou, aliyeshinda uchaguzi wa marudio mwezi Machi.

Katika mzunguko wa kwanza mwezi Januari, Tandja aliondolewa kutoka kwenye nyumba aliyowekwa kizuizini na kupelekwa gerezani. "Mashtaka yote na kesi dhidi ya Mamadou Tandja yamefutwa," mmoja wa wanasheria wake, Souley Oumarou, aliliambia shirika la Habari la AFP siku ya Jumanne wiki hii.

Hata hivyo, mwandishi wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) nchini Niger, Idy Baraou alisema kuwa Tandja alikuwa anatuhumiwa kwa ubadhirifu wa fedha za serikali kiasi cha dola milioni moja. Alikuwa pia anahusishwa na ufisadi wa zabuni ya mbolea yenye gharama kati ya dola milioni 9 na milioni 10.

Katiba mpya ya Niger imepunguza madaraka ya Marais na kuweka kikomo cha urais kuwa miaka kumi.

Historia yake:
Luteni Kanali mstaafu Mamadou Tandja (tamka Mamaduu Tanja), alizaliwa mwaka 1938. Ni mwanasiasa ambaye alikuwa rais wa Niger kuanzia 1999 hadi 2010. Alikuwa Rais wa chama cha National Movement of the Development Society (MNSD) kuanzia 1991 hadi 1999 na bila mafanikio alijaribu kuwania urais akiwa mgombea kupitia MNSD mwaka 1993 na 1996 kabla ya kuchaguliwa kwa mara ya kwanza mwaka 1999. Wakati akiwa Rais wa Niger, alikuwa pia Mwenyekiti wa Jumuia ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi (Ecowas) kuanzia 2005 hadi 2007.

Tandja ni mchanganyiko wa makabila ya Fula na Kanuri. Ameweka historia ya kuwa Rais wa kwanza wa Niger ambaye si wa kutoka kabila la Hausa au Djerma.

Kufuatia mgogoro wa kikatiba wa mwaka 2009, ambao ulisababishwa na jitihada za Tandja kutaka kubaki madarakani kwa zaidi ya muda wake, alipinduliwa na jeshi katika mapinduzi yaliyofanyika mwezi Februari 2010.

Mapinduzi ya 1974:
Tandja aliyezaliwa katika eneo la Maine-Soroa, nchini Niger, alishiriki katika mapinduzi ya 1974 yaliyomuingiza madarakani Seyni Kountche, alikuwa mwanachama wa Halmashauri Kuu ya Jeshi.

Mwaka 1976 akawa msimamizi wa Maradi kabla ya kuteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani Septemba 10, 1979; alikaa katika nafasi hiyo mpaka ilipokabidhiwa kwa Kountche mwenyewe, Agosti 31, 1981. Kisha akawa Msimamizi wa Tahoua kuanzia 1981 hadi Machi 1988, Balozi katika nchi ya Nigeria kuanzia Juni 1988 hadi Machi 1990 na Waziri wa Mambo ya Ndani kwa mara nyingine kuanzia Machi 1990 hadi Machi 1991.

Mwaka 1991, Tandja aliibuka kuwa kiongozi wa kundi moja kati ya makundi mawili yenye nguvu katika chama tawala, MNSD na katika mkutano wa chama uliofanyika Novemba 1991, alichaguliwa kuwa Rais wa MNSD. Tandja alipokea uongozi wa chama kutoka kwa mpinzani wake, Moumouni Adamou Djermakoye na kuonekana kama ishara ya kumalizika kwa utawala wa kabila la Zarma (Djerma) la Djermakoye.

Uchaguzi wa 1993:
Tandja aliwania urais katika uchaguzi mkuu wa 1993, na kuwa wa kwanza katika duru ya kwanza mwezi Februari kwa asilimia 34.22 ya kura, lakini alipoteza nafasi hiyo kwa Mahamane Ousmane katika duru ya pili mwezi Machi, kwa kupata asilimia 45.58 ya kura. Tandja alikubali matokeo na kumpongeza Ousmane.

Tandja alishiriki katika maandamano ya upinzani dhidi ya serikali ya Muungano wa Majeshi ya Mabadiliko Aprili 16, mwaka 1994 na alikamatwa pamoja na watu wengine 90. Ousmane alipinduliwa katika mapinduzi ya kijeshi yakiongozwa na Ibrahim Bare Mainasara Januari 27, 1996.

Uchaguzi wa 1996:
Chini ya uongozi wa Mainassara, uchaguzi mpya wa rais ulifanyika tarehe 7 na 8 Julai, 1996, ambapo Tandja aligombea tena na kuwa wa tatu kwa kuambulia asilimia 15.65 ya kura, nyuma ya Mainassara aliyepata asilimia 52 na Ousmane mwenye asilimia 20, kwa mujibu na matokeo rasmi.

Katika siku ya pili ya kupiga kura alikamatwa na kuwekwa chini ya ulinzi pamoja na wagombea wengine watatu wa upinzani kwa wiki mbili. Kufuatia maandamano ya kidemokrasia tarehe 11 Januari 1997, Tandja alikamatwa pamoja na Ousmane na aliyekuwa Waziri Mkuu, Mahamadou Issoufou na kushikiliwa mpaka 23 Januari.

Uchaguzi wa 1999:
Aprili 1999, Mainassara aliuawa na serikali ya kijeshi na Meja Daouda Malam Wanke kuchukua madaraka. Baraza la majeshi liliahidi kurejea kwa demokrasia ndani ya mwaka, na uchaguzi ulifanyika Oktoba na Novemba. Tandja alishinda uchaguzi wa rais, kwa asilimia 32 ya kura, katika duru ya kwanza, na asilimia 59.89 katika duru ya pili, na kumshinda Issoufou.

Tandja aliungwa mkono na Ousmane katika duru ya pili ya uchaguzi. MNSD pia kilishinda viti vingi katika uchaguzi wa bunge mwezi Novemba, 1999 na Tandja mwenyewe alichaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo la Diffa kupiti MNSD, ingawa kutokana na nafasi yake ya Urais, nafasi yake ya ubunge ilijazwa na mbadala wake, Nassourou Samaila. Alichukua rasmi madaraka ya Rais mwezi Disemba 22, 1999. Alimteua Hama Amadou kuwa Waziri Mkuu Januari 2000.

Niger ilikuwa na madeni makubwa na haikupata misaada yoyote toka nje kutokana na mapinduzi ya 1996. Tandja alilenga katika maendeleo ya kiuchumi, mazungumzo na vyama vya wafanyakazi katika utumishi wa umma na wahisani wa kigeni. Wengi hawakukubaliana na hatua ya Tandja kutaka kupunguza matumizi ya serikali.

Mwaka 2001, wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Niamey walifanya maandamano ya nguvu dhidi ya serikali kupunguza fedha zao. Julai 31, 2002, baadhi ya askari katika eneo la Diffa walianza uasi wakidai malipo na kuboresha hali ya maisha; uasi ulienea hadi Niamey siku chache baadaye. Wafuasi wake waliwashinda waasi na kurejeshwa kwa amani 9 Agosti.

Uchaguzi wa 2004:
Tandja aligombea tena mwaka 2004. Katika duru ya kwanza alishika nafasi ya kwanza kwa asilimia 40.7 ya kura, huku wapinzani wake watano wakigawana zilizobakia. Kama 1999, Mahamadou Issoufou alishika nafasi ya pili, na kushiriki katika duru ya pili na Tandja hapo Disemba 4.

Tandja alichaguliwa kwa asilimia 65.53 ya kura, na Issoufou kuambulia asilimia 34.47. Wagombea wote wanne walioshindwa raundi ya kwanza walimuunga mkono Tandja katika raundi ya pili. Aliapishwa kwa muhula wa pili 21 Desemba katika hafla iliyofanyika Uwanja wa Jenerali Seyni Kountche mjini Niamey, iliyohudhuriwa na marais sita wa nchi za Afrika.

Ingawa kulikuwa na uvumi juu ya uwezekano wa mabadiliko ya katiba ili kumwezesha kuwania tena urais mwaka 2009, alisema katika mahojiano na gazeti la Le Monde, yaliyochapishwa 6 Oktoba 2007, alikusudia kuachia ngazi baada ya muhula wake wa pili. Hata hivyo, Disemba 21, 2008, mkutano mkubwa ulifanyika mbele ya jengo la Bunge la Taifa mjini Niamey uliotoa wito wa kuongeza muda wa miaka mitatu kwa Tandja, ili amalize utawala wake Disemba 22, 2012.

Kulingana na pendekezo la wafuasi wake - ambalo pia lilipendekeza kuendeleza mamlaka ya Bunge na taasisi nyingine kwa miaka mitatu kwa kile kilichosemwa kuwa kwa manufaa na maendeleo ya Niger. Waziri Mkuu, Seyni Oumarou alikuwa miongoni mwa washiriki wa mkutano huo. Upinzani ulipinga pendekezo hilo, na maandamano makubwa yalifanyika mjini Niamey siku chache baadaye. Disemba 30, mashirika 20 yasiyo ya kiserikali na vyama, ikiwa ni pamoja na Shirikisho la Kidemokrasia la Wafanyakazi wa Niger (CDTN), walianzisha upinzani, na walitoa wito kwa Tandja kuacha mpango huo.

Mgogoro wa kikatiba 2009:
Katika uchaguzi wa 2009, harakati ya rasimu ya Rais Tandja kugombea awamu ya tatu ilitolewa. Wakiongozwa na mtu muhimu wa MNSD nje ya serikali, kikundi hicho kilichukua kaulimbiu ya Tandja ya 2004, “Tazartche”: neno la Kihausa lenye maana ya “mwendelezo”.

Kupitia mikutano kadhaa ya kampeni za umma iliyofadhiliwa na kuhudhuriwa sana mwishoni mwa 2008, Rais alibaki kimya katika wito wa kumtaka abaki madarakani. Katiba ya 1999 ilieleza ugumu wa kuongoza kwa zaidi ya vipindi viwili (Ibara ya 36), na marekebisho yake kutokuwa halali kwa njia yoyote (Ibara ya 136). Waziri Mkuu Seyni Oumarou alielezea 22 Januari kwamba ratiba ya uchaguzi iliyopangwa itafuatwa na uchaguzi kufanyika kabla ya mwisho wa 2009. Mwezi Machi, wakati wa mikutano yake na Rais wa Ufaransa, Sarkozy, Tandja alisema kuwa hatafuti kuongeza muda wa tatu wa kuongoza.

Mei 2009, alipoulizwa na waandishi wa habari wakati wa ziara yake ya Agadez kuanza mazungumzo ya amani na waasi wa Tuareg, Tandja alitangaza kuwa “watu wanadai nibaki.” Kisha msemaji wake akaainisha mpango wa jinsi kura ya maoni inavyoweza kufanyika katikati ya 2009, na kuifanyia kazi Katiba ya Sita ya Jamhuri ya Niger, ambayo haitakuwa na ukomo wa muda kwa Rais.

Mapinduzi ya 2010:
18 Februari 2010, wakati wa mkutano wa serikali katika ikulu ya rais, askari waasi walishambulia na kumpindua Tandja katika mapinduzi ya kijeshi, na kuanzisha Serikali ya Baraza la Kijeshi linaloitwa Baraza Kuu kwa ajili ya Matengenezo ya Demokrasia (CSRD). Tandja akakamatwa na kushikiliwa katika kambi ya kijeshi nje ya jiji la Niamey.

Makala haya yameandaliwa na Bishop J. Hiluka kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya habari.

No comments:

Post a Comment