May 25, 2011

SAMUEL WANJIRU: Nyota ya riadha Afrika Mashariki iliyozimika ghafla

 Samuel Wanjiru

NAIROBI
Kenya

ILIKUWA alfajiri ya kuamkia Jumapili, Mei 15, 2011 ambapo Taifa la Kenya na Afrika Mashariki kwa ujumla, hasa wapenzi wa mchezo wa riadha, walipopata pigo kubwa baada ya kumpoteza mwanariadha mahiri aliyekuwa mshindi wa mashindano ya mbio ndefu za Olimpiki ya mwaka 2008 yaliyofanyika nchini China, Samuel Wanjiru “Sammy”.

Kifo cha kijana huyo kimeacha pigo kubwa katika medani ya michezo, kutokana na Wanjiru kufariki dunia akiwa na umri mdogo, ambao bado alikuwa anategemewa kwa maendeleo na ustawi wa taifa lake. Wanjiru amefariki akiwa na umri wa miaka 24, ambapo kifo chake hadi sasa duru za kipolisi nchini Kenya zipo katika uchunguzi wa kina.

Mashabiki wa riadha duniani kote wanaendelea kutuma salamu za rambirambi kwa familia ya mwanariadha huyo. Wanjiru amewahi kuweka rekodi ya dunia katika mbio ndefu (Marathon) kule nchini China katika mashindano ya mwaka 2008, amefariki dunia baada ya kuanguka kutoka katika ghorofa ya kwanza ya nyumba yake iliyoko katika mji wa Nyahururu.

Polisi katika eneo hilo wamesema kuwa kifo cha mwanariadha huyo kimetokea baada ya kuanguka kutoka ghorofa ya kwanza ya nyumba yake na bado uchunguzi unaendelea kubaini Tukio hilo ni la kukusudia ama ajali.

Samuel wakati wa uhai wake alijikuta matatani mara kwa mara baada ya kutiwa nguvuni na polisi kwa tuhuma za kutishia kumuua mke wake, Triza Njeri, baada ya kutokea mtafaruku baina yao, lakini pia alipatikana na makosa ya kumiliki silaha kinyume cha sheria.

Waziri mkuu wa Kenya, Raila Odinga amezunguzia kifo cha mwanariadha huyo kuwa ni pigo kubwa kwa matazamio ya Kenya ya kushinda medali ya dhahabu kwenye michezo ya Olimpiki ya mwaka ujao mjini London, pia sio tu kimeacha pengo kwa familia na marafiki zake bali pia kwa taifa na wapenda michezo duniani kote.

Wanariadha mashuhuri duniani pamoja na wapenzi wa riadha wamekuwa wakielezea masikitiko yao kufuatia kifo hicho cha ghafla cha bingwa wa Olimpiki wa mbio za Marathon.

Habari zaidi za siku ya tukio zilibainisha kuwa mwanariadha huyo alirudi nyumbani usiku akiandamana na mwanamke mwingine, na baadaye mke wake, Triza Njeri alikuja akawakuta chumbani, na kwa hasira akafunga mlango wa chumba hicho huku akimwambia mumewe anakwenda kuwaarifu polisi.

Haijabainika ikiwa Wanjiru aliruka nje kujiua, au kumfuata mkewe, au kwenda kufungua mlango wa chumbani. Polisi waliwahoji wanawake hao wawili kubaini kilichotokea.

Mwezi Desemba Wanjiru alishtakiwa kwa kutishia kumuua mkewe, kumiliki bunduki kinyume cha sheria na pia kumjeruhi mlinzi wa nyumbani. Baada ya mkewe kutupilia mbali kesi inayomhusu walirudiana, na Wanjiru alitazamiwa kufika mahakamani kuhusiana na shitaka la kumiliki silaha kinyume cha sheria.

Ilitazamiwa na wengi kwamba mwanariadha huyo angeweza kuvunja rekodi ya dunia ya mbio za Marathon ambayo kwa sasa inashikiliwa na Haile Gebreselassie wa Ethiopia. Haile ameelezea masikitiko yake kufuatia kifo hicho.
Najiuliza ikiwa sisi kama jamii ya wanariadha tungeweza kusaidia kuepusha tukio hilo,” alisema Haile kwenye mtandao wa Twitter.

Katibu mkuu wa chama cha riadha nchini Kenya, David Okeyo, amesema kifo cha Wanjiru ni pigo kubwa kwa Kenya.
Alikuwa mwenye furaha na tulitazamia angevunja rekodi ya dunia ya mbio za marathon hivi karibuni,” alisema Okeyo.

Bingwa wa zamani wa dunia, Paul Tergat pia kutoka Kenya amesema nchi hiyo imepoteza mwanariadha chipukizi mwenye kipaji.
Ni habari za kusikitisha sana, na ni pigo. Alikuwa mwenye umri mdogo na alikuwa na nafasi ya kukimbia kwa miaka mingi,” alisema Tergat.

Pia kuna habari kuwa Mahakama nchini Kenya imezuia mazishi ya mwanariadha huyo ili kupisha uchunguzi wa kina wa kujua sababu ya kifo chake, huku kamera za CCTV zikishindwa kutoa ushahidi wa moja kwa moja.

Hakimu Anyara Emukule alikubali kutoa siku 14 za uchunguzi, baada ya mama mzazi wa Sammy, Hanna Wanjiru kuiomba mahakama hiyo kumzuia mkwe wake, Teresia Njeri, asiendelee na mazishi ya mumewe. Mama Hanna Wanjiru amekuwa akisisitiza kuwa mwanawe aliuawa na kudai kuwa kulikuwa na damu kwenye chumba alichokuwa anakaa.

Mwili wa marehemu huyo utaendelea kubaki kwenye nyumba ya Lee ya kuifadhia maiti hadi hapo mahakama ya Nakuru itakaposikiliza ushahidi wa pande zote mbili. Mama huyo amemshutumu mkwewe Njeri kwa kuandaa shughuli za mazishi bila kumshirikisha. Pia, hataki kumtambua Njeri kama mke wa mwanae, japokuwa watu wote pamoja na polisi wanamtambua mke huyo.

Historia yake
Samuel Kamau Wanjiru alizaliwa Novemba 10, 1986 katika mji wa Nyahururu. Alikuwa mwanariadha wa Kenya ambaye mbio zake maalum ni mbio za masafa marefu. Amekuwa mwanariadha maarufu katika umri mdogo na kuvunja rekodi ya dunia ya nusu marathon alipokuwa na umri wa miaka 18. Mwaka 2007, alivunja rekodi ya kukimbia ya kilomita 20 na kuboresha rekodi ya nusu marathon kwa zaidi ya sekunde ishirini.

Alihamia hadi marathon kamili na alishinda katika Michezo ya Olimpiki ya Beijing ya mwaka 2008 kwa muda ambao ulikuwa ni rekodi ya Olimpiki wa saa 2:06:32 na kuwa Mkenya wa kwanza kushinda medali ya dhahabu ya Olimpiki katika marathon. Mwaka uliofuata, alishinda marathon zote mbili za London Marathon na Chicago Marathon, kwa kukimbia marathon ya kasi zaidi milele kurekodiwa katika nchi za Uingereza na Marekani.

Wanjiru alianza mbio akiwa na umri wa miaka 15. Mwaka wa 2002, alihamia Japan na akajiunga na shule ya sekondari ya Sendai Ikuei Gakuen katika sehemu ya Sendai, ambapo alihitimu mwaka 2005. Kisha alijiunga na timu ya raidha ya Toyota Kyushu iliyokuwa inafunzwa na mshindi wa medali ya fedha katika mbio za marathon katika Olimpiki ya mwaka 1992, Koichi Morishita.

Muda bora wa Wanjiru katika mbio za mita 5,000 ni dakika 13:12.40, muda aliyouweka akiwa na umri wa miaka 17 mnamo Aprili 2004 mjini Hiroshima, Japan. Akiwa na umri wa miaka 18 tu, Wanjiru alivunja rekodi ya dunia ya nusu marathon, hii ikiwa Septemba 11, 2005 katika Nusu marathon ya Rotterdam kwa muda wa dakika 59:16 na akaivunja rasmi rekodi ya Paul Tergat nusu-marathon ya dakika 59:17.

Hii ilitangulia mapema wiki mbili kwa kuboresha rekodi ya vijana ya dunia ya mita 10,000 kwa karibu sekunde 23 katika michezo ya IAAF Golden League Van Damme Memorial Race mnamo Agosti 26. Rekodi yake ya dunia ya vijana ya dakika 26:41.75 ilikuwa nzuri sana kumpa nafasi ya tatu katika mbio hizo nyuma ya rekodi ya dunia ya Kenenisa Bekele ya dakika 26:17.53 na ya Boniface Kiprop ya dakika 26:39.77.

Ilikuwa ni Kiprop ambaye alikuwa anashikilia rekodi ya dunia ya vijana (dakika 27:04.00) ambayo iliwekwa katika michuano hiyo mwaka uliokuwa umepita kabla yake.

2007-2008
Kwa mara nyingine Wanjiru alichukua tena rekodi ya dunia ya nusu marathon, ambayo Haile Gebreselassie alikuwa amevunja mapema mwaka 2006, kwa dakika 58:53 mnamo 9 Februari 2007 katika nusu marathon ya Ras Al Khaimah na kuiboresha kwa muda wa dakika 58:33 mnamo 17 Machi, 2007 katika City-Pier-City Loop katika mji mkuu wa Hague nchini Uholanzi.

Huku akiiboresha rekodi yake binafsi pia alivunja rekodi ya dunia ya Haile Gebrselassie katika mbio za kilomita 20 kwa muda wa dakika 55:31, uboresho wa sekunde 17.

Wanjiru alikimbia marathon yake kamili ya kwanza katika marathon ya Fukuoka mnamo Desemba 2, 2007 na kuishinda mbio hiyo kwa njia ya kusisimua kwa rekodi ya kozi ya saa 2:06:39. Katika marathon ya London ya mwaka 2008, alimaliza katika nafasi ya pili na kuivunja 2:06 kwa mara ya kwanza. Katika Olimpiki ya mwaka 2008, Wanjiru alishinda medali ya dhahabu katika marathon katika muda wa rekodi ya Olimpiki ya saa 2:06:32 na kuvunja rekodi ya awali ya saa 2:09:2 iliyowekwa na Carlos Lopes wa Ureno katika Olimpiki mwaka 1984.

2009
Wanjiru alikuliwa akisema, “katika muda wa miaka mitano inayokuja najihisi nina uwezo wa kukimbia mbio za marathon kwa muda chini ya saa 2”. Aprili 2009, Wanjiru alishinda marathon ya London kwa muda wa saa 2:05:10.

Alifurahishwa sana na fanikio lake na kusema kuwa alitumai kuvunja rekodi ya dunia ya Haile Gebrselassie baadaye. Katika Nusu Marathon ya Rotterdam, Wanjiru alikimbia kwa muda wa saa 1:01:08 mnamo 13 Septemba, mbio ambayo ilishawahi kushindwa na Sammy Kitwara kwa muda wa dakika 58:58.

Oktoba 2009, Wanjiru alishinda Marathon ya Chicago kwa muda wa saa 2:05:41 na kuweka rekodi mpya ya kozi katika mji huo mkuu na muda wa kasi zaidi katika marathon kukimbiwa nchini Marekani. Ushindi wake katika miji mikuu ya London na Chicago ulimsaidia kufikia nafasi ya juu ya orodha kuu ya dunia katika Marathon mwaka 2009 na kumtuza jackpot ya dola 500,000 za Marekani.

Mdogo wake Wanjiru, Simoni Njoroge ni mkimbiaji wa masafa marefu, na binamu wake, Joseph Riri ni mwanariadha wa daraja ya dunia katika mbio za marathon.

Makala haya yameandaliwa na Bishop J. Hiluka kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya habari


No comments:

Post a Comment