Feb 17, 2011

Elimu ya Uraia kwanza

 Kijana akisoma katiba ya Tanzania
 
BISHOP J. HILUKA
Dar es Salaam

HAKI na wajibu wa kiraia ni mambo ambayo yamefafanuliwa kwa undani katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.

Kwa mujibu wa Katiba, serikali ina wajibu wa kulinda na kuwahakikishia raia wake usalama wao na mali zao, kuwajengea raia mazingira mazuri ya kisiasa, kiuchumi, kijamii na kiutamaduni, pia kuhakikisha kuwa wananchi wanaishi maisha bora kwa kuwapatia huduma za msingi kama vile maji, elimu, afya na huduma zingine muhimu.

Baada ya hotuba ya rais ya kuuaga mwaka 2010 na kuzungumzia haja ya kuipitia katiba iliyopo ili kuihuisha, kumezuka mjadala uliowagawa Watanzania katika makundi mawili; moja likitaka mabadiliko haya yafanyike sasa na jingine likihofia kwa kuwa hiyo katiba iliyopo inayolalamikiwa bado hawaijui hivyo wanadhani kuwa wataburuzwa kwenye mchakato huu kwa maslahi ya wachache.

Pia kumejitokeza baadhi ya viongozi wastaafu waliotaka Watanzania wapatiwe elimu ya angalau ya mwaka mmoja juu ya Katiba, kabla ya kuanza kukusanya maoni yao.

Viongozi hao ni Mbunge mstaafu wa Kwela, Dk. Chrisant Mzindakaya ambaye pia alimpongeza Rais Jakaya Kikwete kwa kusoma ‘alama za nyakati’ kuhusu Katiba mpya, na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, aliyempongeza Rais Kikwete kwa kukubali mabadiliko ya Katiba na kutoa mwito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kutoa maoni yao wakati ukifika.

Tunapozungumzia juu ya elimu ya uraia, nini maana na Umuhimu wa Elimu ya Uraia?

Kutokana na machapisho mbalimbali niliyoyasoma inasemwa kuwa Elimu ya Uraia ni mafunzo yanayotolewa kwa wananchi ili kuwapa stadi na ufahamu, maadili, maarifa na mwelekeo unaowawezesha kushiriki kikamilifu katika masuala ya umma na kuwatayarisha kwa majukumu ya kijamii.

Vilevile, Elimu ya Uraia inawapa wapiga kura maarifa na ufahamu kuhusu masuala ya demokrasia, utawala bora na mchakato wa uchaguzi hasa katika demokrasia ya vyama vingi ambapo kunakuwa na ushindani mkubwa wa kisiasa.

Elimu ya uraia huwapa wananchi stadi na kuwahamasisha kushiriki kikamilifu katika uchaguzi na kuhakiki rasilimali za umma.

Hapa utagundua kuwa elimu ya uraia inapaswa itolewe nchini na imshirikishe kila mwananchi wa nchi hii bila ya kuwepo kwa ubaguzi wa aina yoyote.

Katika tafiti mbalimbali zilizowahi kufanywa na asasi mbalimbali ikiwemo Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa-UNDP, zimebainisha kuwa bado Watanzania walio wengi hawashirikishwi kwa ukamilifu kwenye masuala ya elimu: makundi yaliyobainika kutoshirikishwa kwa ukamilifu ni pamoja na vijana, wanawake, watu wenye elimu duni na walemavu.

Vyombo vya habari pamoja na kujaribu kuihabarisha na kuielimisha jamii kuhusu yanayoendelea nchini, pia vinapaswa kuwa mstari wa mbele hivi sasa tunapoelekea kwenye mchakato wa katiba mpya kutoa elimu ya uaria ili kuleta msukumo, mwelekeo na changamoto ambayo itawawezesha wananchi kuzijua haki zao hata pale mjadala wa katiba mpya utakapowafikia na kuufanya kuwa wa mafanikio makubwa.

Kukosekana kwa elimu ya uraia kwa wananchi hapa Tanzania ni moja ya mambo ambayo yamekuwa yakichangia kwa kiasi kikubwa kudumaa kwa demokrasia nchini.

Elimu ya uraia sio muhimu kwa Tanzania tu bali kwa nchi yoyote ile, kwani inalenga katika kumfanya mwananchi wa nchi husika kutambua haki yake ya msingi na hivyo kumfanya awe na maamuzi sahihi hasa kinapokuja kipindi cha uchaguzi au katika masuala muhimu ya kitaifa kama hili la sasa ambapo wananchi watapaswa kujiunga katika mjadala wa katiba mpya na mambo mengine muhimu kwa mustakabali wa nchi yetu.

Elimu ya Uraia inapaswa kutolewa muda wote na haipaswi kusubiri wakati wa uchaguzi tu ili kuwafanya wananchi wajitambue na kuelewa haki na wajibu wao katika taifa.

Kumekuwepo na imani kwa wengi kuwa elimu ya uraia ina maana ya elimu kwa wapiga kura, na hivyo kusababisha makundi mbalimbali ya kutoa elimu ya uraia nchini Tanzania kujitokeza kwa wingi kutoa elimu hiyo wakati wa kuelekea kwenye uchaguzi mkuu.

Hata baadhi ya asasi na vyombo vya habari vimeingia kwenye mkumbo huo kwa kusisitiza utoaji wa elimu hiyo wananchi wakati wa kuelekea uchaguzi mkuu tu, baada ya hapo elimu haitolewi.

Kwa mtazamo huo ndiyo maana kuna msomaji mmoja alinipigia simu kuniuliza kuwa baada ya uchaguzi kuna umuhimu gani wa wananchi kupata elimu ya uraia, aliniuliza hivyo baada ya kusikia taarifa za viongozi wastaafu kutaka iwepo elimu kabla ya mchakato wa katiba mpya.

Kwa vyovyote vile, Watanzania wanahitaji elimu ya uraia ili waweze kufanya maamuzi sahihi sio kwenye masuala ya uchaguzi au wakati wa mchakato wa katiba mpya tu, bali kwenye mambo mbalimbali ya msingi na yenye maslahi ya taifa hili.

Elimu ya uraia pia inapaswa kuachana na mwelekeo wa sasa ambapo wananchi hufundishwa tu haki zao, na kusahau kuwafundisha juu ya wajibu wao. Pia elimu hiyo izingatie masuala ambayo yatamfanya mtu kuendesha maisha yake ya kila siku: uchumi, jinsi ya kujitegemea, stadi za maisha na mambo mengine kama hayo.

Hivyo taasisi mbalimbali zilizo mstari wa mbele katika kutoa elimu ya uraia zinapaswa kutambua umuhimu wa elimu hii kwa Watanzania wakati wote.

Elimu ya uraia ni suala ambalo limekuwa likizungumzwa kwa muda mrefu na baadhi ya nchi jirani za Kenya, Msumbiji na Uganda ambazo tayari zina mikakati ya taifa ya elimu ya uraia. Vipi kuhusu sisi Tanzania?

Sina taarifa kamili kama serikali yetu ina mkakati wa taifa kuhusu elimu ya uraia, ikiwa ni pamoja na kuratibu na kuweka vigezo vya ubora.

Kama hakuna basi inapaswa ianze sasa kuratibu na kutoa elimu ya uraia kwa makundi mbalimbali. Elimu ambayo imekuwa ikitolewa hapa nchini na vikundi vingi imekuwa haitolewi kwa utaratibu na wala hakuna vigezo vya ubora, hivyo hufanya kukosekana tathmini ya kujua kama wanaotoa elimu hiyo wana sifa zinazohitajika au hawana.

SOURCE: KULIKONI 

No comments:

Post a Comment