Dar es Salaam
MWAKA huu 2011 nchi yetu itatimiza miaka 50 tangu ijipatie uhuru wake toka kwa wakoloni wa Kiingereza mwaka 1961, hii ni miaka mingi, na kama angekuwa ni binadamu basi huyu ni mtu mzima aliyepevuka na anayo mengi ya kujivunia kwani umri huu ni nusu karne.
Kama Taifa tuna kila sababu ya kujipongeza kufikia umri huu kama watu huru, tukiendelea kuvumiliana na kuwa wamoja, wenye kuelewana na wenye matarajio ya kuendelea kuwa wamoja kama taifa.
Nimevutwa kuandika makala hii baada ya kuguswa sana na hotuba ya Rais Jakaya Kikwete ya kuufunga mwaka 2010, pamoja na mambo mengine rais alizungumzia kufikia miaka 50 ya Uhuru wetu tukiwa na mambo mengi ya kujivunia katika nyanja mbalimbali yaliyofanywa: kama kudumisha uhuru na umoja wa nchi yetu. Hali yetu kisiasa, kiutamaduni, kiuchumi, kijamii, kiusalama na kimaendeleo...
Katika hotuba hiyo rais pia aligusia jambo ambalo kila Mtanzania alilisubiri kwa hamu kubwa: Katika Mpya. Rais alisema kuwa serikali imekusudia kuanzisha mchakato wa kuitazama upya Katiba ya nchi yetu kwa lengo la kuihuisha ili hatimaye kuwe na Katiba inayoendana na taifa lenye umri wa nusu karne.
Alisema kuwa ameamua kuunda Tume maalum ya Katiba, yaani Constitutional Review Commission. Tume itakayoongozwa na Mwanasheria aliyebobea, na itakuwa na wajumbe wanaowakilisha makundi mbalimbali katika jamii kutoka pande mbili za Muungano.
Katika hotuba hiyo, Rais Kikwete aliwataka Watanzania kutokuwa na jazba katika madai mbalimbali ya katiba na kuweka wazi kuwa Tume atakayounda haitabagua chama, rangi, dini na kwamba itaunganisha makundi yote ya jamii.
Lakini akatahadharisha kuwa pawepo kuvumiliana kwa hali ya juu pale watu wanapotofautiana mawazo. Pasiwepo kutukanana, kudharauliana, kushutumiana, kubezana, kuzomeana wala kushinikizana.
Binafsi nakubaliana kabisa na maneno ya rais; tusijadili katiba mpya kwa kufuata ushabiki, Watanzania tumekuwa ni watu wa kushabikia tu. Ukituita huku tunakuja ukitupeleka kule tunakwenda.
Kumekuwepo na wasiwasi miongoni mwa wanaharakati na wanasiasa hasa kutoka vyama vya ushindani kuwa kuundwa kwa tume kunaweza kusiwe na manufaa kwa kuwa tume hiyo itakuwa ikiwajibika kwa rais aliyeiteua na pengine kufuata matakwa yake.
Siku moja tu baada ya Rais Kikwete kutoa salamu za mwaka mpya ikiwemo ya kuonesha kukubaliana na kilio cha kuanza kwa mchakato wa Katiba mpya, watu mbalimbali wakiwemo wanaharakati, viongozi wa dini na wanasiasa wamekuwa na mitazamo tofauti.
Wengine wametahadharisha kuwa mjadala huu unaweza kutekwa nyara na serikali, na kusisitiza kuwa Katiba mpya haiwezi kamwe kupatikana kwa njia ya tume waliyoiita kuwa ni “Tume ya Kikwete ya kurekebisha Katiba” (Kikwete Constitutional Review Commission) wakiogopa kuwa inaweza kuchakachuliwa na CCM.
Wakitoa maoni yao baada ya hotuba ya Rais Kikwete, aliyoitoa usiku wa kuamkia mwaka mpya, baadhi ya viongozi wa siasa na dini, kwa nyakati tofauti walisema katiba ni mali ya Watanzania ambao wanahitaji kushiriki kwa kila hali kwa kuwa ndio wahusika wakuu.
waliomba kuwa Serikali na Vyama vya siasa wasiingize propaganda zao wakati wa mchakato wa kuandaa katiba moja.
Nakubaliana kabisa na kauli za viongozi wa dini kwani tunachotarajia kukifanya ni kitu muhimu mno kwa mustakabali wa nchi yetu. Pia nakubaliana na kauli ya rais kuwa nchi yetu imepiga hatua kiutamaduni, kiuchumi, kijamii, kiusalama na kimaendeleo... hatuwezi kusema kwamba miaka yote hii hakuna kilichofanyika, kwa maana ya kupiga hatua kutoka pale tulipokuwa mwaka 1961 hadi tulipo leo.
Lakini hata hivyo, umri wa miaka hamsini unapolinganishwa na mafanikio yaliyofikiwa, hasa tunapojilinganisha na mataifa mengine ambayo tulikuwa sawa mwaka 1961, najawa na hofu kwamba kazi iliyoko mbele yetu kama Taifa ni kubwa kuliko inavyoweza kuelezwa kwa maneno matupu ya kisiasa na ya kufurahishana.
Bado idadi kubwa ya Watanzania ni masikini wa kutupwa wanaoishi maisha ya chini ya dola moja ya Marekani kwa siku. Tumeendelea kuwa Taifa la wategemezi kwa wafadhili, hata pale rasilimali zetu zinapoturuhusu kujitegemea!
Sizioni tena juhudi za kujenga taifa la watu walio sawa bali kinachooneka sasa ni kuzidi kuibuka kwa matabaka ya wenye nacho wachache dhidi ya wengi hohehahe. Watanzania wanashindwa kufikia huduma muhimu za kijamii kama maji, afya, elimu na hata kushindwa kufikia fursa mbalimbali za kujiwezesha kiuchumi kwa sababu ya mifumo duni na dhaifu ya kuwawezesha, ikiegemea zaidi kwa wenye nguvu kiuchumi au mamlaka ya kiutawala.
Kwa maoni yangu, busara itumike wakati wa mchakato wa kujadili Katiba mpya, kwa vile Rais Kikwete na serikali yake wamekubali wazo la Katiba mpya, tuelekeze macho na masikio yetu yote sasa kwenye utaratibu wa kuipata hiyo katiba mpya na vitu gani tunavitaka kama hitimisho la mwafaka wetu kama taifa.
SOURCE: KULIKONI
No comments:
Post a Comment