Mflame Mswati III
SWAZILAND
KIONGOZI mwandamizi wa Kianglikana wa Swaziland, Askofu Meshack Mabuza, ametoa wito kwa mfalme Mswati III kuachia madaraka ya kisiasa ili kuipa nafasi serikali ya kidemokrasia.
Askofu Mabuza aliliambia shirika la habari la Uingereza, BBC kwamba mfumo wa serikali wa "mambo ya kale" umeiingiza nchi katika mgogoro mzito wa fedha na uchumi. Mfalme Mswati, mwenye wake 13, ni kiongozi pekee mwenye kushikilia mamlaka yote ya nchi Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Anashutumiwa kwa kiasi kikubwa kuhusishwa na ufisadi, lakini akaahirisha sherehe zake za kufikisha miaka 25 madarakani mwaka huu kutokana na msukosuko wa fedha nchini humo.
Mpaka sasa Swaziland imekataa kupokea mkopo wa dola za Marekani milioni 355 kutoka Afrika Kusini kuisaidia kulipa gharama mbalimbali, baada ya Pretoria kuitaka nchi hiyo kufanya mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi.
Askofu Mabuza, askofu wa Kianglikana wa Swaziland, aliiambia BBC kuwa matatizo ya Swaziland hayatokwisha iwapo uongozi huyo utaendelea kuwepo madarakani.
Alisema, "Jawabu kwa hakika litatokana na mabadiliko ya uongozi wa serikali ya kiutamaduni, kikabaila, na mambo ya kale."
"Lazima ibadilishwe na uongozi wa kidemokrasia wa vyama vingi."
Taarifa ya serikali iliyoonekana kabla ya kutolewa rasmi - iliyotiwa saini na mhasibu anayekaimu, AF Mabila - ilisema malipo ya mishahara ya wafanyakazi wa serikali ya Novemba yamesogezwa hadi Desemba.
Msemaji wa serikali, Percy Simelane, aliiambia BBC kuwa Baraza la Mawaziri limekuwa likijadili suala hilo tangu Jumamosi, lakini mpaka sasa hamna muafaka wowote uliofikiwa.
Serikali imesema mgogoro wake wa fedha umesababishwa na msukosuko wa uchumi duniani na kuporomoka kwa mapato ya uongozi huo kutoka umoja wa ushuru wa forodha wa Kusini mwa Afrika (Sacu), kufuatia makubaliano mapya ya ushuru wa forodha mwingi.
Lakini askofu Mabuza, anayetarajiwa kuachia madaraka mwezi ujao, alisema hivyo ni "visababu".
Alisema, "Matatizo ya kiuchumi yalikuwepo hata kabla ya kuporomoka kwa uchumi wa dunia kwa sababu imekuwa kama hakuna ukuaji wa kiuchumi."
"Nchi hii imefika hatua ya kuporomoka kabisa."
Kumekuwa pia na wasiwasi kuwa hospitali za taifa zinaweza kuishiwa na dawa za kufubaza ukimwi ARVs kutokana na upungufu wa fedha. Swaziland, yenye jumla ya watu milioni 1.2, ni miongoni mwa nchi zenye idadi kubwa ya walioathirika na ukimwi duniani.
Takriban watu 230,000 wanaishi na virusi vya ukimwi, ambapo 65,000 wanategemea hospitali za taifa kuwapa dawa hizo za ARV.
Vyama vya kisiasa vinazuiwa Swaziland, ambapo Mfalme Mswati amekuwa madarakani tangu mwaka 1986.
Wakosoaji wanaishutumu familia hiyo ya kifalme kwa kuwa na matumizi makubwa kupita kiasi, licha ya idadi kubwa ya watu wake kuishi maisha ya kimaskini.
Msukosuko wa kiuchumi umechochea maandamano dhidi ya uongozi wa mfalme Mswati, lakini wachambuzi wamesema ufalme huo bado unapewa heshima kubwa na Waswaziland wengi wanaothamini mila na desturi zao.
Historia ya Mswati III
Mswati III amezaliwa Makhosetive Dlamini mnamo Aprili 19, 1968. Mwaka 1986, alimrithi baba yake, Sobhuza II, kama mkuu wa ufalme huo wa Kusini mwa Afrika. Anachukuliwa kuwa mfalme mmoja wa wafalme wa mwisho kabisa duniani, kuwa na mamlaka ya kuteua Waziri Mkuu wa nchi, baraza la mawaziri, na mahakama. Hata hivyo, ana wajibu wa kiwango fulani kwa mila za Swaziland na hana mamlaka ya kuchagua mrithi wake.
Mswati III anajulikana kwa tabia yake ya anasa na ndoa ya mitala, na amekuwa akikosolewa nje ya nchi kwa kutafuta maslahi yake binafsi kwa gharama ya nchi yake, moja ya mataifa maskini zaidi dunia. Mwaka 2001 alijaribu kukabiliana na janga la UKIMWI kwa kutaja usafi wa ibada, 'umchwasho', unaopiga marufuku wanawake chini ya umri wa miaka 18 kufanya ngono. Ndani ya Swaziland, Mswati anaheshimiwa kama mtu maarufu. Hata hivyo, sera zake na aina ya maisha yalisababisha maandamano ya ndani na kukosolewa kimataifa.
Yeye ni mmoja wa watoto wengi wa mfalme Sobhuza II (aliyekuwa na wake 70, watoto 210 na wakati wa kifo chake aliacha wajukuu 1000). Alizaliwa katika Hospitali ya Kumbukumbu ya Raleigh Fitkin, miezi minne kabla Swaziland haijapata uhuru kutoka Uingereza. Waliporuhusiwa kutoka hospitali na mama yake, wakaenda kuishi katika moja ya makazi ya mfalme Sobhuza Etjeni karibu na Masundwini Palace. Jina lake la kuzaliwa lilikuwa Makhosetive (Mfalme wa Mataifa).
Akiwa vijana, alihudhuria Shule ya Msingi ya Masundwini na Shule ya Lozitha. Alifanya mtihani wa kumaliza elimu ya Msingi mnamo Desemba 1982 na kupata daraja la kwanza na kupata tuzo katika masomo ya Hisabati na Kiingereza. Alijihusisha zaidi katika ulinzi wa kifalme, na kuwa kijana wa kwanza kujiunga na Jeshi la Umbutfo la Swaziland (USDF).
Mfalme Sobhuza II alipofariki mwaka 1982, Halmashauri Kuu ya Taifa (Liqoqo) ilimchaguwa kijana mwenye umri wa miaka 14, Makhosetive (Mswati III), kuwa mfalme ajaye. Kwa miaka minne iliyofuata wake wawili wa marehemu mfalme Sobhuza II, Malkia Dzeliwe Shongwe (1982-1983) na Malkia Ntombi Tfwala (1983-1986), walitumikia wakati mfalme mtarajiwa akiendelea na elimu yake nchini Uingereza, shule ya Sherborne, kabla ya kuitwa nyumbani kuchukua madaraka.
Alitambulishwa kama Crown Prince mwezi Septemba 1983 na alitawazwa ufalme Aprili 25, 1986, akiwa na umri wa miaka 18 na siku 6, na hivyo kumfanya kuwa mfalme mwenye umri mdogo kutawala hadi kuibuka kwa Mfalme Jigme Khesar Namgyel Wangchuck wa Bhutan mnamo Desemba 14, 2006; pia alikuwa kiongozi mdogo wa nchi hadi alipoibuka Joseph Kabila kuchukua madaraka mnamo Januari 26, 2001, nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Mfalme na mama yake, aliyepachikwa jina la Indlovukazi (Tembo Mkuu wa Kike), kutawala kwa pamoja.
Mwaka 2004, Mswati alianzisha katiba mpya ambayo inaruhusu uhuru wa kusema na mkutano kwa vyombo vya habari na umma, lakini wakibakia katika mfumo wa jadi 'Tinkhundla'. Ingawa Amnesty International waliikosoa katiba mpya kuwa duni katika mambo fulani, waandishi wa habari wa Swaziland waliuambia mikutano wa vyombo vya habari vya Kanda (MISA), kwamba wao wako huru kuripoti kama watakavyo.
Katika jitihada za kukabiliana na VVU na UKIMWI mwaka 2001, mfalme alitumia mamlaka yake ya jadi kuomba muda wa kuheshimu usafi wa ibada (umcwasho), ambao huwatia moyo mabinti wote wa Swaziland kujiepusha na mahusiano ya kimapenzi kwa miaka mitano. Ibada hii inapiga marufuku mahusiano ya kimapenzi kwa Waswazi chini ya miaka 18 kuanzia Septemba 9, 2001 na 19 Agosti 2005, lakini miezi miwili tu baada ya kupiga marufuku, yeye mwenyewe alivunja amri hii kwa kuoa msichana wa miaka 17, aliyekuja kuwa mke wake 13. Kama desturi, alitozwa faini ya ng'ombe, ambayo aliipa.
Mswati amekuwa akikosolewa kwa maisha yake, hasa na vyombo vya habari. Kufuatia upinzani wa ununuzi wake wa magari ya kifahari, ikiwa ni pamoja na gari la anasa la dola 500,000, alipiga marufuku kupigwa picha magari yake. Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa zamani wa Ofisi ya mfalme, manunuzi yalikuwa binafsi na mfalme wa Swaziland anapata mshahara mkubwa kama Mkuu wa Nchi, ana uwekezaji ndani na nje ya nchi na anamiliki kiasi kisichojulikana cha hisa katika makampuni mbalimbali ndani ya Swaziland.
Kwa mujibu wa jarida la Forbes la 2009, orodha ya wafalme matajiri duniani, mfalme Mswati ana mali yenye thamani ya dola za Marekani Million 200. Hii haijumuishi jumla ya dola 10 bilioni ambazo baba yake mfalme Sobhuza II, aliziweka kwenye mfuko kwa ajili ya taifa la Swaziland wakati wa utawala wake, ambapo Mswati III ni mdhamini.
Makala haya yameandalia na Bishop Hiluka kwa msaada wa vyombo mbalimbali vya habari vya kimataifa.
No comments:
Post a Comment