Nov 14, 2011

DK CONRAD MURRAY: Daktari bingwa anayekabiliwa na kifungo kwa kumuua Michael Jackson bila kukusudia

Dk. Conrad Murray

LOS ANGELES
Marekani

WIKI hii, daktari binafsi wa aliyekuwa Mfalme wa Pop duniani, Michael Jakson, Dk. Conrad Murray, amekutwa na hatia ya kosa la mauaji bila kukusudia na mahakama moja mjini Los Angeles, Marekani, ambapo Baraza la wazee wa mahakama - wanaume saba na wanawake watano - walichukua siku mbili kujadili kesi na kufikia hukumu hiyo.

Michael Jackson alifariki Juni 25 mwaka 2009 kutokana na kuzidisha kipimo cha dawa ya usingizi. Na inasemwa kuwa Murray, 58, anaweza kukabiliwa na adhabu ya kwenda gerezani miaka minne na kupoteza leseni yake ya utabibu.

Wanasheria wa Dk. Murray walisema kuwa Michael Jackson alijidunga mwenyewe dawa hiyo wakati daktari wake akiwa nje ya chumba. Dk. Murray alipelekwa rumande baada ya kukutwa na hatia hadi wakati atakaposomewa adhabu yake, inayotarajiwa kutolewa Novemba 29.

Akielezea uamuzi wake, jaji alisema Dk. Murray kwa sasa ni mhalifu aliyekutwa na hatia na kwa kuwa anafahamiana na watu nje ya jimbo la California, inamaanisha hakuna uhakika kuwa daktari huyo ataweza kubakia bila kutoka katika jimbo hilo.

Dk. Murray alibaki kimya mahakamani hapo wakati hukumu ikisomwa. Baraza la wazee - lililoundwa na wazungu sita, Mmarekani mweusi mmoja na Wamarekani watano wenye asili ya Hispania - walijadili shauri hilo kuanzia Ijumaa hadi Jumatatu asubuhi.

Katika hoja za mwisho mahakamani siku ya Alhamisi, upande wa mashtaka ulisema Dk. Murray alisababisha kifo cha nyota huyo kutokana na uzembe, na hivyo kuwanyima watoto wa Jackson haki ya kuwa na baba.

Upande wa utetezi ulihoji kuwa Jackson alikuwa amejizoesha kutumia dawa, kitu ambacho kilisababisha kifo chake kutokana na kujipa kiwango kikubwa cha dawa huku daktari wake akiwa nje ya chumba katika jumba alilokuwa amekodi nyota huyo mjini Los Angeles.

Historia ya Murray

Dk. Conrad Murray ni daktari bingwa wa moyo (Cardiologist) na daktari binafsi. Alizaliwa Februari 19, 1953, katika eneo la St Andrews, Grenada. Alihamia Marekani mwaka 1980. Mwaka 1999, alianzisha kituo binafsi cha mazoezi. Michael Jackson alimwajiri kama daktari binafsi kwa ajili ya ziara ya tamasha lake mwaka 2009. Mwezi Juni 2009, Jackson alikufa kwa kuzidisha kiwango cha dawa. Dk Conrad ameshtakiwa kwa kuua bila kukusudia (manslaughter involuntary).

Maisha ya mwanzo na Mafunzo ya Utabibu

Daktari huyu ambaye amekumbana na utata wa kifo cha Mfalme wa Pop mnamo Juni 2009, hakutoka kwenye familia yenye fedha. Pamoja na mama yake Milta kutumia muda wake nchini Trinidad na Tobago akitafuta kazi nzuri yenye kulipa, Murray aliishi na bibi na babu yake wa upande wa mama, wakulima wa Kigrenada. Maisha ya familia yake iliyovunjika yalizungukwa na kukosekana kabisa kwa baba yake, Rawle Andrews, daktari wa eneo la Houston ambaye, hadi kifo chake mwaka 2001, alilenga kazi yake zaidi katika kutoa huduma ya matibabu kwa maskini. Conrad hakuwahi kukutana na baba yake hadi alipokuwa na miaka 25.

Alipofikisha miaka saba, Murray alihamishiwa nchini Trinidad na Tobago kuishi na mama yake, ambapo alipata uraia na kumaliza shule ya sekondari. Kama mama yake, Murray aliamua kufanya ili awe na maisha bora, alionesha kupendelea kufanya kazi kwa bidii katika umri mdogo. Baada ya shule ya sekondari alijitolea kufanya kazi kama mwalimu katika shule ya msingi Trinidad, uzoefu alioupata ulimfanya kufanya kazi kama karani wa forodha na bima ili kujilipia ada yamasomo yake ya elimu ya chuo. Katika umri wa miaka 19 alinunua nyumba yake ya kwanza, halafu baadaye akaiuza kwa faida ili pesa zimsaide katika masomo yake ya chuo kikuu nchini Marekani.

Mwaka 1980, miaka miwili baada ya kutembelea Houston kwa mara ya kwanza na kupata nafasi ya kujitambulisha mwenyewe kwa baba yake, Conrad akarudi Texas kujiandikisha katika Chuo Kikuu cha Texas Kusini, ambapo katika miaka mitatu tu alihitimu shahada ya sayansi ya tiba na baiolojia. Kuanzia hapo, alifuata nyayo za baba yake na kuhudhuria Chuo cha Tiba cha Mmarekani-Mweusi Meharry kilichopo Nashville, Tennessee.

Baada ya kufuzu Maharre, Murray alijiunga na mafunzo ya ziada katika Kliniki ya Mayo jimbo la Minnesota na kisha kukamilika makazi yake katika Chuo Kikuu cha Tiba cha Loma Linda Medical huko California. Kisha mafunzo mengine yalifuata; alisoma Cardiology (magonjwa ya moyo) katika Chuo Kikuu cha Arizona, na kurudi California, ambako hatimaye akafanya kazi kama mkurugenzi mwenza katika mpango wa kimataifa wa mafunzo ya magonjwa ya moyo katika Hospitali ya Kumbukumbu ya Sharp katika eneo la San Diego.
Kazi ya Tiba huko Las Vegas

Mwaka 1999, Dk Murray aliondoka California kwa mara ya pili na kuanza kivyake, akafungua kituo binafsi cha mazoezi katika eneo la Las Vegas. Akiiweka ofisi yake mashariki mwa mji, akifuata tena nyayo za baba yake – alikusudia si tu kutumikia utajiri wa mji, lakini mafanikio yake pia. Mwaka 2006, Murray alipanua wigo wake na kurudi katika mji ambapo baba yake alijitengenezea jina lake, akafungua Taasisi ya Moyo iliyoitwa ‘Acres Homes Heart and Vascular Institute’.
"Tumekuwa na bahati ya kuwa na Dk Murray na kliniki hiyo katika jamii hii," mgonjwa wa Houston, Ruby Mosley, aliliambia jalida moja. "Kuna wagonjwa wengi, wengi mno wanaomshukuru Mungu kwamba mtu huyu yupo hapa kwa ajili yao."

Wale ambao wamekuwa na mahusiano ya kifedha na daktari, hata hivyo, wanaweza kujisikia vinginevyo. Wasiolipa madeni, kesi za kisheria, na wenye madai ya kodi wamefuata maisha ya Dk Murray. Zaidi ya dola 400,000 katika hukumu ya mahakama peke yake zilitolewa dhidi ya kazi yake huko Las Vegas, na mwezi Desemba 2008 Murray, ambaye ana idadi isiyojulikana ya watoto, aliamriwa kutoa 3,700 kwa ajili ya malipo ya mtoto.

Kumtibu Mfalme wa Pop
Ukweli, ilikuwa ni hali ya madeni ya Dk Murray iliyoanzisha kufanya kazi na uhusiano wake Michael Jackson. Watu hawa wawili walikutana kwa mara ya kwanza mwaka 2006 wakati mwanamuziki huyo, alipozuru mara kwa mara Las Vegas, aliwasiliana na Dk Murray kuhusu kumtibu mmoja wa watoto wake kutokana na matatizo yasiyojulikana. Taarifa zinaonesha kwamba watu hao wawili wakawa marafiki na, Jackson alipoanza mipango ya ziara yake ya tamasha la 2009, alimuajiri Dk Murray kuwa daktari wake binafsi kwa mshahara wa dola 150,000 kwa mwezi.
Dhamira ya Jackson kumleta Murray, ingawa, yawezekana haikuhusiana na urafiki na zaidi ilihusiana na matatizo ya Jackson mwenyewe kuhusiana na tiba. Kufuatia kifo cha Jackson, polisi waligundua vyeti vya dawa zaidi ya 20 ndani ya nyumba yake ya kukodi ya Holmby Hills, ikiwa ni pamoja na methadone, fentanyl, percocet, dilaudid, na vicodin.

Pamoja na yote, Jackson aliathiriwa na tatizo la kukosa usingizi (Insomniac) na alisukumwa kutumia propofol na anesthetic, ili zimsaidie kupumzika. Pamoja na mchanganyiko wa dawa nyingine, Jackson alipenda kulala, mara nyingi alipendelea kuchanganya dawa na kuzifanya "maziwa" yake au "kinywaji cha kulalia." Lakini ilikuwa ni propofol aliyoonekana kuipenda hasa. Cherilyn Lee, muuguzi na mtaalam wa lishe aliyesajiliwa ambaye Jackson alimuajiri, aliiambia ABC News kwamba mwimbaji huyo alimwomba amnunulie dawa nyingi zaidi za kutumia. Muuguzi huyo alikataa.

Kifo cha Michael Jackson

Dk Murray, hata hivyo, alikuwa ni suala jingine. Wakati nyaraka za mahakama zilionesha hakuwahi kumnunulia dawa Jackson, katika kipindi cha wiki sita alizofanya kazi kwake, daktari huyo alimtundikia maji (intravenous drip) yenye mchanganyiko wa propofol - licha ya wasiwasi wake kwamba Jackson anaweza kuwa mwathirika wa dawa za kulevya.

Hiyo ilikuwa tarehe 25 Juni, 2009, wakati Jackson, akiwa amechoka na mazoezi ya muda mrefu katika Kituo cha Staples, Los Angeles, alikokwenda usiku wa manane, alirudi nyumbani na kujaribu kupata mapumziko. Alitumia njia iliyotumiwa mara kwa mara na Murray kwa mteja wake kumtundikia maji (IV) ili kuingiza propofol. Dk Murray pia alimpa Jackson lorazepam, dawa za kuondoa wasiwasi, na midazolam, dawa ya kulegeza misuli.

Kwa mujibu wa kumbukumbu, daktari alimwacha Jackson kwa dakika chache na kwenda bafuni. Aliporudi alimkuta Jackson akiwa na mapigo dhaifu ya moyo na alishindwa kupumua. Inasemekana, Murray mara moja alianza kutumia CPR kumfufua Jackson. Aidha, katika kile ambacho kimeongeza zaidi utata, Dk Murray pia aliongeza dawa nyingine ya kulevya, flumazenil, ili kujaribu kukabiliana na dawa ambazo tayari zilikuwa kwenye mzunguko wa damu katika mwili wa Michael Jackson. Baadhi ya wataalam wamesema kuwa matumizi ya dawa aliyoongeza Murray yanaweza kuwa ndiyo yaliyozidisha matatizo ya propofol mwilini.

Makala haya yameandaliwa na Bishop Hiluka kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya habari vya kimataifa.

No comments:

Post a Comment