Nov 16, 2011

Tutatatua migogoro yetu kwa mitutu ya bunduki hadi lini?

 Askari wa kutuliza ghasia wakiwa tayari kuwakabili 
wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam

 Picha hii inaonesha matokeo ya vurugu jijini Mbeya

BISHOP HILUKA
Dar es Salaam

IMEKUWA ni kawaida kuona ama kusikia polisi wakiwashambulia kwa risasi za moto na mabomu wananchi waliogoma, wanaoandamana, wanafunzi wa vyuo vikuu waliogoma, wafanyabiashara ndogondogo wasioridhishwa na taratibu za watawala, wananchi wanaoishi maeneo ya migodi wanaodai haki zao huku wakiwa hawaridhishwi na ‘uporaji’ wa urithi wao huo, na migogoro mingine mingi katika sehemu tofauti za nchi.

Matukio ya aina hii katika nchi hii yamekuwa ni ya kawaida na hayajaanza leo, yamekuwa yakitokea mara kwa mara katika sehemu kadhaa nchini, hasa katika miji mikubwa. Na mara zote kumekuwepo taarifa za watu ama kujeruhiwa au taarifa za mauaji ya watu kadhaa.

Matukio haya yametamalaki kila pembe ya nchi yetu, kuanzia kwenye maeneo ya migodi, vyuo vikuu, hadi kwenye maeneo ya wafanyabiashara ndogondogo maarufu kwa jina la machinga.

Kwa hali inavyoonekana, Serikali haioni tena umuhimu wala haja ya kutafuta suluhu kwa kufanya mazungumzo na makundi mbalimbali ya kiraia na kijamii inapotokea pande hizo mbili zinapotofautiana, na imeamua kutumia njia inayodhani inafaa 'ya mitutu ya bunduki na mabomu' kwa kutumia vikosi vyake vya ulinzi kama njia muafaka ya utatuzi wa migogoro inayojitokeza!

Kibaya zaidi ni kwamba, mauaji haya yanazidi kujitokeza katika Serikali ambayo imejivika joho la utawala bora na kudai kuwa imebobea na kuitekeleza dhana ya utawala bora kwa vitendo.

Wakati huko nyuma ingeliwezekana watu kujiuzulu kwa mauaji na manyanyaso kwa wananchi kama ilivyotokea kwa Ali Hassan Mwinyi akiwa waziri, siku hizi hata polisi wanapodhihirika kutumia nguvu kubwa ambayo haikuhitajika katika kuua wananchi hakuna hatua wanazochukuliwa.

Nakubaliana kabisa na kauli ya Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Yuda Thadeus Ruwa-Inchi, wa Kanisa Katoliki, pale alipowataka viongozi wa serikali kutambua kuwa amani na usalama haviwezi kulindwa wala kudumishwa kwa kutumia nguvu kubwa za jeshi na matumizi ya silaha kali, bali ni kwa kila kiongozi kuwatendea haki watu wake.

Mfano hivi karibuni, katika kipindi cha siku saba tu kumekuwepo matukio yaliyowahusisha polisi na wananchi ambapo polisi walitumia risasi za moto na mabomu hata pale ambapo hakukuwa na haja ya kufanya hivyo.

Hapa jijini Dar es Salaam, polisi waliwatia nguvuni wanafunzi 46 wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa kuandamana kuishinikiza Serikali kuwapa wenzao 1,000 mikopo ya elimu ya juu. Kabla ya kuwakamata, polisi walitumia mabomu na kutoa vipigo kwa wanafunzi hao waliokuwa wanaelekea sehemu za Ubungo kupeleka ujumbe huo kwa wananchi.

Eneo hilo la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam liligeuka uwanja wa mapambano baina ya jeshi la polisi na wanafunzi wa chuo hicho walioandamana kushinikiza kupatiwa mikopo ya elimu. Hata hivyo, vurugu hizo zilisababisha shughuli zote za chuo hicho kusimama kwa saa kadhaa.

Kuna picha fulani niliiona ambayo kwa kweli haikunipendeza kabisa, ambapo askari wawili wa kiume walionekana kumdhalilisha mwanafunzi wa kike, huku wenzao saba wakiwa wameelekeza mitutu ya bunduki kwa mwanafunzi huyo!

Jijini Arusha polisi walikuwa katika mapambano makali na viongozi na wafuasi wa Chadema waliowatia mbaroni na kuwafungulia mashtaka kwa tuhuma za kufanya mkusanyiko kinyume cha sheria na kukataa kutii amri halali ya polisi.

Na huko Mbeya, risasi na mabomu vilitawala sehemu kubwa ya jiji hilo na kusababisha kifo cha mtu mmoja na kujeruhi watu kadhaa. Vurugu hizo zilitokana na operesheni iliyofanywa na askari wa Jiji la Mbeya iliyokuwa na lengo la kuwaondoa wafanyabiashara wadogo (Wamachinga) katika mitaa ya jiji hilo. Katika vurugu hizo, watu 235 walikamatwa na polisi.

Mapambano hayo yaliyoanza majira ya saa 2.30 asubuhi katika maeneo ya Mwanjelwa na kusambaa kwa kasi katika mitaa mingi ya jiji hilo, yalisababisha kufungwa kwa barabara zote na hakukuwa na gari linaloingia ama kutoka katikati ya jiji.

Polisi zaidi wakiwa na silaha waliwasili na kuanza kuwashambulia wananchi kwa risasi bila kujali kama ni mfanyabiashara ama watembea kwa miguu. Katika mapambano hayo, mtu mmoja Abel Mwalukali, alipigwa risasi katika mkono wake wa kulia uliovunjika vibaya, na kukimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mbeya kwa matibabu. Pia kuna taarifa ya watu wengine kupigwa risasi za moto na kujeruhiwa.

Lakini pamoja na mapambano hayo, vurugu hizo zilizoendelea bila kukoma na jeshi la polisi kwa kushirikiana na JKT kambi ya Itete hawakufanikiwa kutuliza ghasia hizo. Pongezi za pekee ni kwa Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi, maarufu kama Sugu kwa kuacha kikao cha Bunge mjini Dodoma na kwenda mjini Mbeya ambako alifanikiwa kuzima vurugu hizo kwa njia ya kidiplomasia.

Kwa kweli Sugu ametoa somo kubwa sana kwa viongozi wa Serikali na vyombo vyake vya ulinzi na usalama kuwa, wananchi wanahitaji kiongozi anayewasikiliza na kutafuta suluhisho la matatizo yao, na kamwe migogoro haiwezi kuzimwa kwa mitutu ya bunduki.

Alamsiki.

No comments:

Post a Comment