Pedro Rodriguez Pires
PRAIA
Cape Verde
KAMATI ya taasisi ya Mo Ibrahim mjini London imemtangaza aliyekuwa rais wa Cape Verde, Pedro Rodriguez Pires, kuwa mshindi wa tuzo ya utawala bora, kutokana na mafanikio yake katika kuleta demokrasia, uimara na neema katika visiwa hivyo.
Kamati hiyo imesema katika tangazo lake mwanzoni mwa wiki hii mjini London kwamba, katika uongozi wa Pedro Pires wa miaka 10 katika visiwa vya Cape Verde (Rasi ya Verde), kwenye pwani ya Magharibi mwa Afrika, Pedro Verona Pires, aliweka msingi wa kuwaondoa wananchi wake 200,000 kutoka kwenye umasikini.
Kutokana na utawala wake bora, Pires alitambulika duniani kwa sera zake za kutekeleza haki za binadamu. Kamati hiyo ya Mo Ibrahim inayoshughulikia zawadi hiyo ilisema kuwa Pires, aliyeachia madaraka mwezi Agosti, amesaidia sana kuifanya nchi hiyo kuwa "yenye demokrasia, utulivu na kustawi zaidi".
Tuzo hiyo inatakaiwa kutolewa kila mwaka kwa kiongozi anayechaguliwa kidemokrasia na kuondoka madarakani kwa hiari. Lakini hapajakuwa na mshindi kwa miaka miwili iliyopita, na kamati hiyo ilisema kuwa hakukuwa na mgombea aliyestahili kupokea tuzo hiyo katika kipindi hicho.
Tuzo hiyo ya dola za Marekani milioni tano, inayotolewa kwa zaidi ya miaka 10, ni zawadi yenye thamani kubwa duniani inayotolewa kwa mtu binafsi. Washindi wa awali wa tuzo hiyo ni aliyekuwa rais wa Botswana, Festus Mogae na wa Msumbiji, Joaquim Chissano.
Kabla ya kumpa tuzo hiyo wanakamati wa Mo Ibrahim wametilia maanani kwamba Rais huyo mstaafu, Pedro Rodriguez Pires, alilikataa wazo la kuibadilisha katiba ili kumwezesha kugombea urais tena. Mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 77 ameutumia muda wa miaka 50 wa maisha yake katika shughuli za kisiasa.
Rais huyo mstaafu aliuweka msingi uliokigeuza kisiwa chake cha Cape Verde kuwa na mfano wa demokrasia, uimara wa kisiasa na neema. Katika maelezo yaliyotolewa mjini London na Kamati ya Mo Ibrahim wanakamati wametilia maanani kwamba kisiwa cha Rasi ya Verde ni mfano wa mafanikio ya kiuchumi, kijamii na kisiasa barani Afrika.
Pedro aliyatetea maadili ya ubinadamu kama alivyosema baada ya kutangazwa mshindi wa Tuzo ya Mo Ibrahim, katika harakati zake za kisiasa alikuwa na kaulimbiu ya maneno matatu - Kazi, Ukweli na Utiifu".
Historia ya Pires
Pedro Pires Verona Rodrigues alizaliwa Aprili 29, 1934, katika kisiwa cha Cape Verde na alisoma kwenye shule ya msingi na ya sekondari katika kisiwa hicho kabla ya kwenda kwenye Chuo Kikuu cha Lisbon nchini Ureno mnamo mwaka 1956. Lakini kabla ya kuhitimu shahada yake, aliitwa ili kulitumikia jeshi la Ureno kama afisa wa kikosi cha anga.
Lakini mnamo mwaka 1961 pamoja na vijana wengine wa Kiafrika aliondoka Ureno kimya kimya, na kujiunga na chama cha ukombozi wa Guinea na Cape Verde, PAIGC kilichokuwa kinaongozwa na Amilcar Cabral mpigania uhuru jarabati.
Alifanya bidii ya kuwahamasisha vijana wa nchi yake kwa ajili ya harakati za ukombozi. Mnamo mwaka 1974 Pires aliuongoza ujumbe wa chama chake cha PAIGC kwenye mazungumzo na serikali ya Ureno juu ya kuleta uhuru wa Cape Verde. Na tarehe 5 ya mwezi wa Julai mwaka 1975 Cape Verde alitangaza uhuru wake.
Hata hivyo Pires amekuwa Rais wa Cape Verde kuanzia Machi 2001 hadi Septemba 2011. Kabla ya kuwa Rais, alikuwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo kuanzia 1975 na aliutumikia wadhifa huo kwa muda wa miaka 16 hadi 1991, kabla ya kuwa Rais mwaka 2001.
Baadaye mwaka huohuo wa 1991 aliamua kugombea katika uchaguzi uliofanyika kwa mara ya kwanza katika kisiwa chake cha Cape Verde kwa njia za kidemokrasia, baada ya chama tawala cha African Party for the Independence of Cape Verde (PAICV) kuamua kuruhusu demokrasia ya vyama vingi mnamo Februari 1990, lakini alishindwa.
Mwaka mmoja kabla mnamo 1990, Pires alikuwa amechukua nafasi ya Rais Aristides Pereira kama Katibu Mkuu wa PAICV mwezi Agosti 1990. Hata hivyo, katika wakati huu chama chake cha PAICV kilipoteza nafasi katika uchaguzi wa vyama vingi wa rais na wabunge uliofanyika mapema mwaka 1991 na Pedro akabaki kuwa mpinzani.
Katika mkutano wa chama mnamo Agosti 1993, nafasi ya Katibu Mkuu iliyokuwa ikishikiliwa na Pires ilichukuliwa na Aristides Lima, baada ya yeye kuchaguliwa kuwa Rais wa chama. Kama mgombea aliyepitishwa na chama kwa nafasi ya urais mnamo Septemba 1997, kwenye mkutano wa chama, alikabiliwa na José Maria Neves na kumshinda kwa asilimia 68 ya kura. Aliamua kujiuzulu nafasi ya urais wa PAICV mwaka 2000 katika maandalizi yake kwa ajili ya uchaguzi wa urais katika mwaka uliokuwa ukifuata na alikuwa akikabiliwa na Neves. Alitangaza rasmi nia yake ya kugombea urais wa Cape Verde tarehe 5 Septemba, 2000.
Pires alikuwa mgombea kupitia PAICV katika uchaguzi wa rais wa Februari 2001, akimshinda Waziri Mkuu wa zamani, Carlos Veiga, wa Movement for Democracy (MpD) katika raundi ya pili kwa kura 17 tu. Pires alichukua madaraka mnamo Machi 22; chama cha MpD kiligomea uzinduzi wake, kikisema kuwa uchaguzi ulikuwa umefunikwa na "mchakato usiokuwa wa uwazi".
Baada ya kuwa Rais, Pires alimteua Neves kuwa Waziri Mkuu. Aligombea tena katika awamu ya pili katika uchaguzi wa rais uliofanyika tarehe 12 Februari 2006 na kumshinda tena Veiga, safari hii alishinda katika raundi ya kwanza tu kwa kiwango cha asilimia 51 kwa asilimia 49 alizopata mpinzani wake.
Mwezi Mei mwaka 2008, alitoa tahadhari kuwa kulikuwa na safari ndefu katika kuundwa kwa Umoja wa Mataifa ya Afrika, yeye akipendekeza kwamba ushirikiano wa kikanda utangulizwe kabla ya muungano wa bara nzima. Alihudhuria Mkutano wa Kimataifa wa Tokyo wa Maendeleo ya Afrika (TICAD-IV) kwa wakati huu.
Nchi ya Cape Verde
Cape Verde ni nchi ya visiwa katika Bahari ya Atlantiki mbele ya pwani ya Afrika ya Magharibi. Umbali wake na Senegal ni kilomita 460. Eneo la visiwa vyake 15 (funguvisiwa) lina ukubwa wa kilomita za mraba 4,033.
Mji mkuu wa nchi hiyo ni Praia uliopo katika kisiwa cha Santiago. Visiwa vyake vinavyounda nchi ya Cape Verde vipo jumla ya visiwa 15 ambavyo vipo katika vikundi viwili:
- Visiwa "juu ya upepo" (Barlavento): Santo Antao, Sao Vicente, Sao Nicolau, Sal, Boa Vista na visiwa visivyokaliwa na watu vya Santa Luzia, Branco na Razo.
- Visiwa "chini ya upepo" (Sotavento) ni pamoja na Maio, Santiago, Fogo, Brava na visiwa visivyo na watu vya Ilheus Secos ou do Rombo.
Miji mikubwa zaidi ni (sensa ya mwaka 2005): Praia (wakazi 113,364), Mindelo (wakazi 70,611), Santa Maria (wakazi 17,231), Pedra Badejo (wakazi 9,488) na Sao Filipe (wakazi 8,189).
Hadi kufika kwa Wareno funguvisiwa vya Cape Verde havikuwa na watu. Wareno walianzisha mashamba ya miwa na kuleta watumwa kutoka bara la Afrika. Cape Verde ilikuwa pia kituo muhimu cha biashara ya watumwa kati ya Afrika na Amerika. Wahamiaji kutoka Ulaya walikuwa pamoja na Wayahudi Wareno waliokataliwa kukaa kwao Ureno. Idadi kubwa ya wakazi wa visiwa hivi ni chotara kati ya Waafrika na Wareno.
Makala haya yameandaliwa na Bishop Hiluka kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya habari vya kimataifa.
No comments:
Post a Comment