Oct 7, 2011

HERMAN KOJO: Mjasiriamali wa Ghana anayefananishwa na Bill Gates

 Herman Kojo Chinery-Hesse

ACCRA
Ghana

MFANYABIASHARA wa Ghana, Herman Kojo Chinery-Hesse, hujulikana kama Bill Gates wa Ghana, na amekuwa wa kwanza kutajwa katika mfululizo maalum wa vipindi vya shirika la utangazaji la Uingereza la BBC kama ndoto ya Afrika inayoangaza kati ya wajasiriamali wa bara hilo.
Kampuni ambayo Chinery-Hesse aliibuni kwa ushirika miongo miwili iliyopita, SOFTtribe Limited, huenda ikawa haijajitanua duniani kama ile kampuni ya Microsoft lakini imeimarika na kuwa mojawapo wa mashirika makubwa ya programu za kompyuta katika Afrika ya Magharibi.

Chinery-Hesse alisamehe fursa ya kujiendeleza kimaisha nchini Marekani alikosoma au Uingereza ambako aliwahi kufanya kazi kwa miaka michache, na badala yake kuamua kuanzisha biashara nchini Ghana.

Alianza kuandika programu za kompyuta chumbani alikolala katika nyumba ya wazazi wake katika wakati ambapo sio watu wengi walitambua umuhimu wa mapinduzi ya kompyuta barani Afrika.

Kampuni yake hatimaye ikaanza kuunda programu za kompyuta za uongozi wa biashara na sasa ina zaidi ya wateja 250, yakiwemo mashirika kadhaa ya kimataifa kama vile Ford Foundation, Nestle, na Unilever. SOFTtribe Limited pia ni mshirika wa maendeleo wa kampuni ya Microsoft katika kanda.

"Imekuwa kama burudani. Si rahisi kusema haiwezekani. Sidhani kuwa mimi ni mtu mwenye kipaji. Nadhani mtu yeyote anaweza kufanya hayo awe makini na awe tayari kusubiri miaka. Mbinu niliyotumia ni kwamba nilijihusisha katika biashara nikiwa sitarajii kuwa tajiri katika kipindi cha miaka 2," Chinery-Hesse aliliambia shirika la BBC.

"Wakati fulani kwa kipindi cha miezi sita kampuni yetu haikupokea hundi zozote na ilitulazimu kugawana kiasi kidogo cha pesa tulizokuwa nazo. Kulikuwa na nyakati ambapo hatukuwa na fedha zozote kulipa mishahara wakati tulipokuwa na madeni."

Kwa maoni yake miongoni mwa vitu viwili muhimu katika biashara ni ustahamilivu na uaminifu.
"Katika biashara yoyote; lazima uamini kwamba inanufaisha kote kote. Mtu anayenunua lazima anufaike na wewe pia lazima unufaike, la sivyo haitaendelea."

Hapana shaka mojawapo ya sababu za kufanikiwa kampuni yake ni kwamba kuanzia mapema sana aliamua kubuni programu ya kompyuta ambayo imetengenezwa mahsusi kwa mazingira ya bara la Afrika.
"Nadhani kuna fursa kubwa sana barani Afrika, hali ya umasikini mkubwa, kuna mengi ambayo hayakufanywa; lakini hii si sayansi ngumu, ukiwa na nidhamu usiogope kujitosa," Chinery-Hesse anawaambia wengine wanaozingatia kuwa wajasiriamali.

"Inawezekana, na nadhani ingewapasa watu wengine kufanya hivyo, na kama hatutajichukulia hatua, basi wageni watakuja Afrika kama tunavyoona na watafanya wakitakacho."

Makala hii imeandaliwa na Bishop Hiluka kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya habari

No comments:

Post a Comment