Feb 23, 2011

Kiongozi anapokiuka misingi ya haki za binadamu hukosa uhalali wa kuongoza

 Rais wa Libya, Kanali Muammar al-Gaddafi

 Waandamanaji wanaoupinga utawala wa Libya

BISHOP J. HILUKA
Dar es Salaam

JUZI Jumatano niliona taarifa kwenye televisheni iliyonishtua sana, kuwa kiongozi wa Libya, Kanali Muammar Gaddafi, licha ya kugoma kuondoka madarakani kutokana na kuwepo kwa maandamano makubwa ya kupinga serikali, aliliagiza jeshi lake kuwashughulikia wale wote wanaompinga na kutamka kuwa maadui wa Libya watauawa.

Katika hotuba yake kubwa tangu kuanza kwa vuguvugu, Gaddafi alisema dunia nzima inaitazama Libya na kuwa maandamano hayo yana “mhudumia shetani”. Aidha aliwaita waandamanaji kuwa ni mende au panya. Makundi ya haki za binaadamu yanasema zaidi ya watu 300 wameuawa tangu maandamano hayo yaanze.

Ghaddafi akizungumza kwa ghadhabu alisema ameleta heshima kwa Libya jambo ambalo hakuna anayeweza kubisha. Gaddafi amewasaidia sana wananchi wake katika mambo fulanifulani. Amefanikiwa sana kukuza uchumi wa Libya na kuwafanya waishi kama wapo peponi, lakini hiyo haimpi uhalali wa kukiuka misingi ya haki za binadamu na kutaka kutawala milele pamoja na kuanzisha utawala kama wa kisultani.

Kitendo cha kuamuru jeshi kuwashambulia kwa risasi za moto wananchi wanaoandamana kimeyafanya yale yote mazuri aliyoyafanya kufunikwa na mauaji yanayoendelea, hivyo kupoteza kabisa uhalali wa kuongoza.

Azimio la Umoja wa Mataifa kuhusu Haki msingi za Binadamu linatamka bayana na kusisitizia uhuru wa mawazo, hii ni dhamana ya kila Serikali kuhakikisha kwamba, watu wake wanatekelezewa uhuru huo, badala ya kuendekeza dhuluma, ubaguzi na mateso hata kama umesaidia kukua kwa uchumi wa nchi.

Kwa kweli kitendo alichokifanya Gaddafi kinaakisi hali halisi ya kisiasa katika bara la Afrika, karibu nchi zote (ikiwemo Tanzania) bado zina changamoto kubwa kama vile: kudumisha misingi ya haki na amani pamoja na kutetea zawadi ya maisha hasa ya wale ambao ni wanyonge zaidi ndani ya jamii.

Wakenya bado wanakumbuka kwa namna ya pekee, machafuko ya kisiasa yaliyojitokeza kunako mwaka 2007 mara baada ya uchaguzi mkuu. Si rahisi kufuta picha ya mateso na mahangaiko ya wananchi wa Kenya katika kipindi hiki, mateso ambayo hayakuwa na msingi wowote ule!

Uvunjwaji wa haki za binadamu ni tatizo kubwa barani Afrika. Sheria mbaya, mahakama zisizokuwa huru, na vyombo vya dola vinavyofanya kazi kwa kufuata matakwa binafsi ya viongozi wa serikali, badala ya katiba na sheria, vimesababisha haki za binadamu katika nchi zetu kuwa katika hali mbaya.

Jambo lingine ambalo ni kiashiria cha ukiukwaji wa misingi ya haki za binadamu barani Afrika (Tanzania ikiwemo) ni rushwa. Enzi za Awamu ya Kwanza, wakati wa Mwalimu Nyerere tulikuwa tukifundishwa kuwa rushwa ni adui wa haki, kwa kuwa inaua uchumi na kuwanyima wananchi haki ya maisha.

Lakini siku hizi rushwa imekuwa ni sehemu ya maisha yetu ya kila siku kiasi kwamba unaonekana mtu wa ajabu kama hupokei rushwa. Wapo watu waliomshangaa sana Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alipotangaza kuwa siku akichukua rushwa anaomba afe.

Siku hizi, hapa nchini hakuna huduma ya serikali isiyo na rushwa, kuanzia ngazi ya Serikali ya Mtaa hadi Serikali Kuu. Chanzo kikubwa cha rushwa ni ukiritimba wa madaraka, mishahara midogo ya watendaji Serikalini, maamuzi yasiyofuata taratibu zinazoeleweka na kulindana kwa kutowawajibisha wanaoshiriki vitendo vya rushwa.

Kimsingi shughuli zote za mwanadamu na mahusiano ya watu hapa duniani yalipaswa kuwa ni kwa ajili ya kuboresha hali yake kimwili, kiakili, kiroho na kuongeza ubora wa mahusiano yake na viumbe wengine. Hivyo, mchakato wa kila shughuli afanyayo ulipaswa kuwa katika namna ambayo haina dhuluma, uonevu, madhalilisho, taabu, ubaguzi, wala vikwazo kwa mwanadamu awaye yeyote na kwa kiumbe hai kingine chochote.

Kilele cha uwepo wa haki ni kuzalishwa na kutunzwa kwa furaha ya jamii na ya dola. Jamii kamwe haiwezi kuwa na furaha ya kweli kama haki haitawali na wala dola haliwezi kusimama imara pasipo kutunzwa kwa kiwango kikubwa haki ndani ya mipaka ya dola husika.

Jamii zote za wanadamu zina mfumo wa kimsingi wa kijamii, kiuchumi, na taasisi za kisiasa zilizo rasmi na zisizo rasmi. Ili kutambua kama mfumo fulani unaathiri mipangilio ya kijamii na una uhalali, mtu hana budi kutazama kukubalika kwa mfumo huo miongoni mwa watu wanaoongozwa na mfumo husika.

Uhuru wa kisiasa (mfano kuwepo kwa taasisi za demokrasia ya uwakilishi, uhuru wa kujieleza, wa vyombo vya habari na wa kukusanyika) uhuru wa kujumuika na kushirikiana na wanajamii uhuru wa mtu kwenda atakako na kuchagua kazi aitakayo bila kukinzana na misingi ya uadilifu, uhuru wa kupata haki binafsi zinazolindwa na utawala wa sheria.

Alamsiki

No comments:

Post a Comment