Feb 17, 2011

Mjadala wa Katiba unapogeuzwa ushabiki wa Simba na Yanga!

Richard Tambwe Hiza

BISHOP J. HILUKA
Dar es Salaam

IJUMAA ya tarehe 21 Januari, kuanzia saa tatu usiku nilikuwa nimejipumzisha nyumbani nikifuatilia kipindi cha Kipima Joto kinachorushwa na televisheni ya ITV, niliguswa sana na mjadala huo hasa mada ya Katiba iliyokuwa ikiongelewa siku hiyo ingawa nilihisi kuwa kulikuwa na kila dalili nisingepata kile nilichokihitaji.

Mjadala huo uliongozwa na Reinfred Masako na ulihudhuriwa na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Propaganda wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Richard Tambwe Hiza, Dk. Sengondo Mvungi (NCCR-Mageuzi), John Mnyika (Chadema), Lucas Limbu (CUF) na Mama Ussu Malya (TGNP).

Katika washiriki wote ni Tambwe Hiza aliyenivutia kiasi cha kuamua kuandika makala hii. Nimemfahamu Tambwe kwa muda mrefu ambaye alivuma zaidi alipokuwa NCCR-Mageuzi, umaarufu wake ulipanda kiasi cha kuteuliwa kugombea ubunge mwaka 1995.

Mimi si mkereketwa wala mwanaharakati wa kudai Katiba mpya ingawa naamini kuwa ipo haja ya kuiangalia upya hii tuliyonayo ili kurekebisha mambo yaliyopitwa na wakati, lakini naamini kabisa kuwa Tambwe anajua kwa kiasi fulani umuhimu wa Katiba ya nchi na mahitaji ya wananchi kuhusu Katiba. Ile hoja ya kwamba wananchi hawaijui Katiba iliyopo haimaanishi kuwa hawahitaji Katiba nzuri itakayowahakikishia kupata haki zao za msingi ikiwemo maisha bora waliyoahidiwa na Rais Kikwete.

Wananchi wanaponung'unikia vitendo vya matumizi ya nguvu vinavyofanywa na polisi, rushwa, ukosefu wa miundo ya usawa ndani ya jamii, ubadhirifu wa mali ya umma pamoja na kukosekana maadili mema yanayozingatia tunu za msingi za maisha ya kifamilia, inaonesha dhahiri kuwa wanaijua vizuri Katiba kwa kutaja mambo yanayohitaji kurekebishwa kwenye Katiba ili kuwapa maisha bora.

Kuwa na watunga sera, wachumi na viongozi wa serikali wasiotoa kipaumbele kwa fursa za kazi na uzalishaji na kusukumwa na uchu wa kupata faida kubwa, kulitumbukiza Taifa katika hali mbaya ya uchumi na kumong'onyoka kwa maadili katika nyanja mbalimbali za maisha ni mambo yanayoigusa Katiba yetu moja kwa moja hata kama wananchi hawavijui vifungu vinavyotakiwa kurekebishwa.

Hata pale wananchi wanapolalamika kukosa viongozi wanyenyekevu, waadilifu, wakweli, wasiopenda makuu na wenye kuelewa maana ya Uongozi na umuhimu wa kuhamasisha na kutetea haki za jamii zao na si kujifikiria wao kwanza ni kuielewa Katiba vizuri sana kuliko hata wale walioiona Katiba, kuisoma na kukariri vifungu.

Wakati huu ambapo tunaisubiri Tume itakayoteuliwa na Rais Kikwete kuhusu Katiba mpya (ingawa sijamsikia Rais akisema Katiba mpya) tunapaswa kuachana na malumbano yenye ushabiki wa kisiasa na kuangalia mahitaji halisi ya jamii yetu kwani wananchi wanaendelea kudidimia katika lindi la umaskini, ukosefu wa fursa za ajira pamoja na mfumuko wa bidhaa na huduma. Pia idadi kubwa ya watoto wanashindwa kuendelea na masomo kutokana na hali ngumu ya maisha pamoja na kupanda kwa gharama za maisha, kiasi cha kuwafanya wananchi kukata tamaa.

Katika kipindi hiki nadhani wanasiasa, wanaharakati na viongozi wa dini wanapaswa kuzidisha mshikamano utakaochangia upatikanaji wa fursa za ajira, mapambano dhidi ya baa la njaa, ujinga na umaskini, kulinda na kudumisha utu na heshima ya kila mwanadamu na hasa walalahoi ambao wanajikuta utu na heshima yao haithaminiwi tena kutokana na hali ngumu ya kiuchumi.

Wasomi na watunga sera wanapaswa kutafuta mbinu zitakazoweza kujenga mfumo mpya wa uchumi nchini, utakaotoa kipaumbele kwa binadamu na mahitaji yake ya msingi badala ya kutawaliwa na uchu wa mali, heshima na madaraka.

Kwa nini nilihisi mjadala usingenipa kile nilichokihitaji? Nimekuwa na wasiwasi mkubwa sana na uelewa wa Tambwe Hiza. Kwa kweli kwa wale waliopata fursa ya kumsikiliza kwenye mjadala huo na hata mijadala mingine mbalimbali watakubaliana nami kwamba huyu mtu anakosa uelewa na badala yake hutanguliza mbele ushabiki.

Naamini CCM ina watu wengi makini sana na wenye uelewa mkubwa katika masuala ya Katiba ambao wangeweza kuwakilisha, lakini inashangaza kuona CCM kila mara ikiwakilishwa na Tambwe katika mijadala mizito ingawa ameonekana kuwa na uelewa mdogo katika kupambanua na kuchambua mambo.

Sina shaka wananchi wa Jimbo la Temeke waliliona hili siku nyingi na kumnyima fursa ya kuwaongoza. Tambwe amewahi kugombea ubunge katika jimbo la Temeke mara sita na kubwagwa.

Kwa mara ya kwanza aligombea kupitia NCCR-Mageuzi mwaka 1995 na kubwagwa na Ramadhan Ali Kihiyo wa CCM. Mwaka 1996 aligombea tena kupitia Chama cha Wananchi (CUF) katika uchaguzi mdogo, kufuatia kujiuzulu kwa Kihiyo kwa matatizo ya afya, lakini alibwagwa na Augustine Mrema (NCCR-Mageuzi).

Tambwe aligombea tena kupitia CUF baada ya Augustine Mrema kutangaza kujiengua kutoka NCCR-Mageuzi na kujiunga na Tanzania Labour ambapo kisheria alikuwa amepoteza wadhifa wake wa ubunge, hata hivyo Tambwe alishindwa na John Kibaso wa CCM.

Mwaka 2000 aligombea tena kupitia CUF akabwagwa na Hadija Kusaga wa CCM na alijaribu tena mwaka 2005 kupitia CUF lakini akabwagwa na Abbas Mtemvu (CCM), na mwaka jana 2010 alijaribu kugombea kupitia CCM lakini akabwagwa katika kura za maoni na Mbunge wa sasa, Abbas Mtemvu.

SOURCE: KULIKONI

No comments:

Post a Comment