Feb 17, 2011

TEODORO OBIANG: mungu-mtu wa Guinea ya Ikweta aliyekabidhiwa dhamana kuiongoza Afrika

 Teodoro Obiang Nguema Mbasogo

Addis Ababa
ETHIOPIA

KAMA itaanzishwa tuzo ya bara ambalo marais wake wameshika madaraka kwa muda mrefu kuliko mabara mengine duniani, nadhani bara la Afrika litaweka rekodi ambayo haiwezi kuvunjwa na bara lingine lolote.

Katika Afrika, viongozi wengi wamekuwa na tabia ya kuingia madarakani kwa kuchaguliwa katika uchaguzi wa kidemokrasia kwa mujibu wa katiba, lakini muda wao wa uongozi unapomalizika wanakuwa vinara wa kubadilisha katiba ili waendelee kutawala.

Na kama itatokea kuwa hawakuchanguliwa kwa kura za wananchi katika uchaguzi mkuu, basi watatumia kila aina ya hila, ujeuri na madaraka waliyonayo kulazimisha ushindi kimabavu.

Hayo yametokea katika nchi nyingi za bara hili, mfano mdogo tu ni nchi za Kenya, Uganda na Zimbabwe. Hata yanayotokea katika nchi za Afrika ya Kaskazini; Tunisia, Algeria na Misri ni mfano hai.

Nchi ndogo iliyopo Magharibi ya Afrika ya Kati, Jamhuri ya Guinea ya Ikweta imemtoa kiongozi wa Umoja wa Afrika kutokana na kikao cha viongozi wakuu wa nchi za Afrika kumchagua rais wa nchi hiyo ndogo kuwa mwenyekiti mpya wa Umoja wa Afrika (AU).

Rais Teodoro Obiang Nguema Mbasogo ndiye rais wa Jamhuri ya Guinea ya Ikweta, na Mwenyekiti mpya wa Umoja wa Afrika, huku suala la Ivory Coast likiwa linatazamiwa kupewa kipaumbele cha kwanza na viongozi wa Umoja wa Afrika (AU) waliokuwa wakikutana mwishoni mwa wiki iliyopita na mwanzoni wiki hii mjini Addis Ababa, Ethiopia.

Nchi hii imepakana na Cameroon kwa upande wa Kaskazini, Gabon kwa upande wa Kusini na Mashariki, na Ghuba ya Guinea kwa upande wa Magharibi, ambapo kisiwa cha Sao Tome na Principe vipo Kusini-Magharibi mwa Jamhuri ya Guinea ya Ikweta.

Nchi hii ilikuwa koloni la Hispania ambapo iliitwa Guinea ya Uhispania, na maeneo yake ambayo yanajulikana (kwa bara kama Rio Muni), na pia kisiwa cha Bioko ambapo mji mkuu umo na Malabo (ambayo iliitwa, Santa Isabela).

Jina la nchi hii linatokana na kuwa nchi hii ipo karibu na Ikweta na pia ipo karibu na Guba la Guinea.

Ni nchi pekee katika bara la Afrika ambayo inatumia lugha ya Kispaniola kama lugha rasmi ya Taifa, hasa ukiacha maeneo ya Hispania iliozungukwa na bara, Ceuta na Melilla na nchi-Isiyotambuliwa-kimataifa ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kiarabu ya Sahara.

Rais Teodoro Obiang, alianza harakati za kuingia madarakani katika Jamhuri ya Guinea ya Ikweta mwaka 1979 na kufanikiwa. Baada ya katiba kufanyiwa marekebisho mapya aliendelea kuitawala nchi hiyo hadi Desemba 2002, alipochaguliwa tena kuendelea na wadhifa wake kwa kipindi kingine cha miaka saba kwa mujibu wa katiba ya taifa hilo.

Katika uchaguzi wa mwaka 2002, Teodoro Obiang alipata ushindi wa asilimia 97.1 ya kura zote zilizopigwa. Lakini matokeo hayo yalizua machafuko makubwa yakipingwa kuwa hayakuwa halali na mpinzani wake mkubwa, Simon Mann.

Uchaguzi mwingine wa urais katika Guinea ya Ikweta ulifanyika Novemba 29, 2009 ambapo wagombea watano wa urais akiwemo Teodoro Obiang Nguema ambaye pia ni mwenyekiti wa chama tawala cha Demokrasia cha nchi hiyo waligombea nafasi ya urais kwenye uchaguzi huo.

Kwenye kampeni za uchaguzi wa rais zilizoanza tarehe 5 mwezi huo, Rais Nguema alijigamba kuwa angeungwa mkono na idadi kubwa ya watu kuliko ile ya kwenye uchaguzi wa mwaka 2002 ambao alipata asilimia 97.1 ya kura.

Teodoro Obiang ni nani hasa?
Teodoro Obiang Nguema Mbasogo amezaliwa Juni 5, 1942, ndiye rais wa Jamhuri ya Guinea ya Ikweta, ambaye ameshika wadhifa huo tangu mwaka 1979 na sasa amekuwa Mwenyekiti mpya wa Umoja wa Afrika (AU).

Maisha ya awali
Obiang alizaliwa katika ukoo wa Esangui eneo la Ocoacan, alijiunga na jeshi wakati wa kipindi cha ukoloni, na kuhudhuria Mafunzo ya Jeshi Zaragoza, Hispania.

Alipanda hadi kufikia nafasi ya Luteni wakati wa uchaguzi wa Francisco Nguema Macias. Katika kipindi cha Macías, Obiang alishika nafasi mbalimbali za kiuongozi, ikiwa ni pamoja na kuwa mkuu wa mkoa wa Bioko, mkuu wa Gereza la Black Beach, na kiongozi wa Ulinzi wa Taifa.

Urais
Aliingia madarakani baada ya kumpindua Francisco Macias tarehe 3 Agosti 1979 kufuatia mapinduzi ya umwagaji damu. Macías alifunguliwa kesi kuhusiana na harakati zake katika uongozi wake uliopita na kuhukumiwa adhabu ya kifo.

Harakati hizo zilikuwa ni pamoja na mauaji ya kimbari ya Bubi. Aliuawa tarehe 29 Septemba 1979 kwa kupigwa risasi.

Obiang alitangaza kuwa serikali yake mpya itaanza kufanya kazi mpya ya kuijenga nchi kutoka kwa serikali ya kikatili na ya kikandamizaji ya Macias. Obiang alirithi nchi hiyo ikiwa haina hazina na yenye idadi ya watu iliyoshuka hadi kufikia theruthi ya mwaka 1968, na asilimia 50 ya idadi ya wananchi wake wa zamani wapatao milioni 1.2 waliohamishwa kupelekwa aidha Hispania, au nchi jirani ya nchi za Afrika, au kuuawa wakati wa utawala wa kidikteta wa rais aliyemtangulia.

Obiang alishika rasmi madaraka ya urais mwezi Oktoba, 1979.
Katiba mpya ya nchi hiyo ilipitishwa mwaka 1982, wakati huohuo, Obiang akichaguliwa kwa kipindi cha miaka saba ya urais. Alichaguliwa tena kuwa rais mwaka 1989 akiwa mgombea pekee katika nafasi hiyo.

Baada ya vyama vingine vya siasa kuruhusiwa, alichaguliwa tena kuiongoza Jamhuri ya Guinea ya Ikweta mwaka 1996 na 2002 kwa asilimia 98 ya kura katika chaguzi zilizolalamikiwa kukumbumbwa na ulaghai na waangalizi wa kimataifa. Mwaka 2009, alichaguliwa tena kwa asilimia 97 ya kura huku kukiwa na madai ya kuwepo udanganyifu na vitisho.

Serikali ya Obiang ilibaki na sifa ya wazi ya kimabavu hata baada ya vyama vingine vya siasa kuruhusiwa rasmi mwaka 1991. Ingawa utawala wake ulionekana kuzingatia utu kuliko ule wa mjomba wake, lakini wengi wanadhani umekuwa wa kikatili zaidi kadiri miaka inavyozidi.

Waangalizi wengi ndani na nje ya nchi hiyo wanaona kuwa serikali yake ni moja kati ya serikali zinazoongoza kwa rushwa, ukandamizaji na zisizokuwa za kidemokrasia katika dunia ya leo.

Jamhuri ya Guinea ya Ikweta kwa sasa haina tofauti na serikali ya chama kimoja, kinachoongozwa na chama cha Obiang cha Democratic Party of Equatorial Guinea (PDGE).

Mwaka 2008, mwandishi wa habari wa Kimarekani, Peter Maass alimwita Obiang kuwa mtawala dikteta mbaya zaidi, mbaya zaidi kuliko Robert Mugabe wa Zimbwabwe. Katiba ya nchi hiyo inampa madaraka makubwa Obiang, ikiwa ni pamoja na nguvu ya kutawala kwa amri.

Wabunge wote wa bunge la taifa kasoro mmoja tu katika bunge lenye wabunge mia moja ni wa chama cha PDGE cha Obiang au ni wale wanaoambatana nacho. Upinzani umeathiriwa sana na ukosefu wa vyombo huru vya habari kama njia muhimu kwa ajili ya kutoa maoni yao. Vyombo vyote vya habari ama vinamilikiwa na serikali au kudhibitiwa na washirika wa Obiang (Kituo kimoja cha redio binafsi, kwa mfano, kinamilikiwa na mtoto wa Obiang).

Ukiukwaji chini ya utawala wa Obiang ni pamoja na “mauaji haramu yanayofanywa na vikosi vya usalama, utekaji nyara uliosababishwa na serikali, askari wa usalama kuwatesa wafungwa na mahabusu, hali inayohatarisha maisha katika magereza na vizuizini, kutokujali, ukamataji holela, na kuweka watu kizuizini.”

Julai 2003, redio inayoendeshwa na serikali ilimtangaza Obiang kuwa mungu ambaye “ana mawasiliano ya kudumu na Muumba” na “ana uamuzi wa kuua bila mtu yeyote kumzuia na bila kwenda kuzimu.” Yeye binafsi aliwahi kutoa ufafanuzi unaolingana na huo mwaka 1993.

Pamoja na yote hayo, bado anadai kuwa yeye ni mcha Mungu na Mkatoliki aliyewahi kualikwa Vatican na Papa Yohane Paulo II na baadaye tena na Papa Benedict XVI. Mtangulizi wake, Macias pia aliwahi kujitangaza kuwa mungu.

Kama alivyokuwa mtangulizi wake na madikteta wengine wa Afrika kama vile Idi Amin na Mobutu Sese Seko, Obiang amejipa mwenyewe vyeo kadhaa. Pia anajichukulia kama El Jefe (Bwana Mkubwa).

Jarida la Fobes linaloandika habari za matajiri wa dunia hii linadai kuwa Obiang ni mmoja wa Marais tajiri sana, akiwa na mali zenye thamani ya zaidi ya dola milioni 600 za Kimarekani.

Makala hii imeandaliwa na Bishop J. Hiluka kutokana na vyanzo mbalimbali vya habari.

SOURCE: KULIKONI

No comments:

Post a Comment