Mar 23, 2011

Bila kudhibiti Kifua Kikuu, Tz bila Ukimwi haiwezekani

 Nembo inayoonesha kuwa Kifua Kikuu na Ukimwi ni magonjwa pacha

 Muuguzi akitoa huduma kwa Mgonjwa mwenye VVU pamoja na TB

BISHOP J. HILUKA
Dar es Salaam


Alhamisi ya 24 Machi 2011, wiki hii ni maadhimisho ya siku ya Kifua Kikuu Duniani, kwa hapa Tanzania maadhimisho ya siku hii yanafanyika mjini Musoma mkoani Mara yakiwa na kaulimbiu ya “Shiriki kikamilifu katika kupambana na Kifua Kikuu”. Kitaifa, takwimu zinaonesha kuwa mkoa wa Mbeya ndiyo unaoongoza kwa kuwa na wagonjwa wengi wa Kifua Kikuu (TB) nchini.

Maadhimisho haya huwa yana lengo la kuamsha ari ya wadau mbalimbali duniani wakiwamo wagonjwa, watafiti, wataalam wa afya, viongozi wa serikali, wanasiasa na jamii kwa ujumla kutumia mbinu mpya katika udhibiti wake. Baadhi ya mbinu zinazotumiwa ni pamoja na kuongeza jitihada za utafiti wa kugundua tiba mpya, kuwasaidia wagonjwa kupata tiba sahihi na kuhamasisha jamii kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya Kifua Kikuu (TB).

Takwimu zilizopo, Mkoa wa Mbeya ndiyo unaoongoza kwa kuwa na wagonjwa wengi wa TB huku maambukizi yakiwa yamefikia kiwango cha asilimia 8, Iringa ni asilimia 7, Dar es Salaam asilimia 6, Kigoma ndio yenye maambukizi kidogo ya asilimia 3.

Taarifa za kitaalam zinasema kuwa siku hizi kumekuwa na ugonjwa wa kifua kikuu sugu, unaojulikana kama
Multi Drug Resistance Tuberculosis (MDR-TB), unaosababishwa na dawa kushindwa kufanya kazi vizuri au mgonjwa kutotumia dawa kwa mpangilio maalum na kufuata ushauri uliotolewa na wataalam wa matibabu.

Shida kama hii hutokea ikiwa mgonjwa ametumia dawa kwa njia isiyotakikana au alianza matibabu akakosa kumalizia ile miezi sita inayohitajika. Kawaida, inachukua miezi sita au zaidi kutibu kabisa ugonjwa wa Kifua Kikuu. Hata hivyo, mgonjwa akianza matibabu, baada ya muda kidogo hujihisi yuko sawa. Kama atakatiza matibabu, kuna hatari kwamba vimelea vilivyo mwilini mwake hujiunda upya na kujiongezea nguvu kiasi kwamba dawa aliyokuwa akiitumia haiwezi kumtibu tena.

Kifua Kikuu sugu wakati mwingi hakitibiki na mtu anayeugua aina hii ya Kifua Kikuu anaweza kuusambaza ugonjwa huu vilevile kama TB ya kawaida. Matibabu ya mgonjwa wa Kifua Kikuu sugu (MDR-TB) yanagharimu mara ishirini zaidi ya yule aliye na TB ya kawaida. Matibabu ya mgonjwa wa Kifua Kikuu sugu yanaweza kuchukua muda wa miezi kumi na nane.

Nchini Tanzania takwimu zinaonesha kuwepo wastani wa watu 63,000 wanaougua Kifua Kikuu kila mwaka, ambao ni sawa na wagonjwa 173 kila siku.

Kifua Kikuu ni ugonjwa wa kuambukiza ambao husababishwa na vimelea vidogo vidogo aina ya bakteria visivyoonekana kwa macho bali kwa kutumia darubini viitwavyo ‘tubercle bacilli’.

Wengi wetu tuna vimelea vya TB mapafuni mwetu lakini hii haimaanishi kwamba tunaugua ugonjwa huu. TB huwashambulia hasa wale wenye ukosefu wa kinga mwilini unaosababishwa na kutokula chakula kizuri, matumizi ya dawa za kulevya au wanaougua magonjwa mengine.

TB ya mapafu ndio imeenea zaidi. Hata hivyo, vimelea vya TB vinaweza kusafirishwa kutoka mapafuni kupitia damu hadi sehemu nyingine za mwili na kusababisha viungo viathiriwe na TB.

Njia kuu ya maambukizi ya Kifua Kikuu huambukizwa kwa njia ya hewa ambayo ina vimelea vya ugonjwa huo. Kifua Kikuu kinaambukizwa kwa njia ya hewa kutoka kwa mgonjwa mwenye Kifua Kikuu kwenda kwa watu wengine. Hali hii hutokea hasa katika sehemu zenye msongamano wa watu au nyumba ambazo hazipitishi hewa na mwanga wa kutosha.

Vimelea vya TB pia hupatikana kwenye mate ya mgonjwa. Wakati mgonjwa anakohoa, kupiga chafya au kutema mate kiholela, vimelea vya TB husambazwa kwa njia ya hewa.

Ingawa imekuwa ikisemwa kuwa Kifua Kikuu ni ugonjwa wa tatu baada ya Malaria na Ukimwi ambao unasumbua na kupoteza maisha ya Watanzania, lakini ugonjwa huu unapaswa kutiliwa mkazo zaidi kwani utafiti unaonesha kuwa asilimia 30 ya vifo vya watu walioathirika kwa Ukimwi vinatokana na Kifua Kikuu, hivyo ile kampeni ya Rais Kikwete ya 'Tanzania bila Ukimwi inawezekana' haiwezi kufanikiwa kama hatutakuwa makini na ugonjwa huu.

Inakadiriwa kuwa asilimia 10 ya waathirika wa Ukimwi wana maambukizo ya Kifua Kikuu na asilimia 50 ya wagonjwa wa Kifua Kikuu wana maambukizo ya Virusi vinavyoambukiza Ukimwi (VVU). Hali hii inafanya Kifua Kikuu kuwa miongoni mwa changamoto kubwa katika mapambano dhidi ya Ukimwi hapa nchini.

Takriban watu zaidi ya milioni mbili hufariki kwa ugonjwa wa Kifua Kikuu kila mwaka duniani, na asilimia kubwa ya vifo hivyo vinatokea barani Afrika, hususan Kusini mwa Jangwa la Sahara. Tanzania ni nchi ya 14 kati ya nchi 22 zenye idadi kubwa ya wagonjwa wa kifua kikuu duniani.

Wengi wa wagonjwa hawa wako katika umri wa miaka 15 na 45 ambao ndiyo umri wa wazalishaji mali na ustawi wa taifa kwa ujumla. Licha ya kupoteza maisha ya wananchi wengi, athari nyingine za kuendelea kuwepo kwa magonjwa haya hapa nchini ni kudumaza uchumi wa nchi, hali ambayo inafanya jamii ya Watanzania kuendelea kuwa katika lindi la umaskini.

Shirika la Afya Duniani, WHO mwaka jana 2010, lilizindua mpango wa kupambana na ugonjwa wa Kifua Kikuu katika kipindi cha miaka mitano ili kuokoa maisha ya wagonjwa milioni mbili wanaofariki dunia kila mwaka kutokana na ugonjwa huo. Mkakati huo unapania kuboresha majaribio, uchunguzi na tiba kwa ugonjwa wa Kifua Kikuu na mpango mzima unatarajiwa kugharimu kiasi cha Dola za Kimarekani bilioni 47.

Watalaam wa ugonjwa wa Kifua Kikuu wanasema kwamba, kama hakuna hatua madhubuti dhidi ya ugonjwa wa Kifua Kikuu, kiasi cha watu milioni kumi, watakuwa wamepoteza maisha ifikapo mwaka 2015, kutokana na magonjwa yanayoweza kutibika. Shirika la Afya Duniani limesema kwamba, Kifua Kikuu ni kati ya magonjwa ya kale, lakini, ukigundulika mapema, ukapata tiba muafaka ni ugonjwa unaotibika kabisa. Afrika na India ni kati ya sehemu zilizoathirika zaidi na ugonjwa wa Kifua Kikuu.

Shirika la Afya Duniani linapania kuboresha huduma ya tiba kwa wagonjwa wa Kifua Kikuu kwa asilimia tisini, ifikapo mwaka 2015 sanjari na kuhakikisha kwamba, wagonjwa wote wa Ukimwi wanapimwa pia ugonjwa wa Kifua kikuu. Takwimu zinabainisha kwamba, wagonjwa wengi wa Ukimwi wanaosumbuliwa pia na Kifua Kikuu, hufariki zaidi kwa ugonjwa huu.

Dalili za ugonjwa wa Kifua Kikuu:
-Kukohoa mfululizo kwa muda wa wiki mbili au zaidi
-Kutoa makohozi mazito/ yaliyochanganyika na damu au mate yaliyo na damu
-Uchovu na kuishiwa nguvu mwilini
-Kukonda au kupoteza uzito wa mwili
-Kupoteza hamu ya kula
-Kutokwa na jasho jingi usiku wakati mtu amelala hata wakati wa baridi
-Maumivu ndani ya kifua
-Kuishiwa na pumzi au kupumua kwa shida
-Homa za wakati wa jioni

Aina za Kifua Kikuu:
Kuna aina mbili za Kifua kikuu (TB); Kifua Kikuu cha mapafu (Pulmonary Tuberculosis) na Kifua Kikuu cha nje ya mapafu (Extrapulmonary Tuberculosis).
TB ya mapafu nayo imegawanyika sehemu mbili:
-TB inayoambukiza ambayo vimelea vinagunduliwa katika makohozi, ambao ndiyo ugonjwa hatari zaidi unaochukua asilimia 90 ya aina zote za ugonjwa wa Kifua Kikuu.
-TB isiyoambukizwa na vimelea katika makohozi.

Kifua Kikuu kinatibika na kupona kabisa kwa kupata dawa zinazopatikana katika hospitali, hivyo kwa yeyote anayeugua ugonjwa huu anatakiwa kuzingatia tiba kama atakavyoelekezwa na daktari, na wengine tunatakiwa tujenge mazoea ya kupima afya zetu kabla ugonjwa huu haujamaliza nguvu kazi ya taifa letu.

0755 666964
bjhiluka@yahoo.com

No comments:

Post a Comment