Rais Mteule wa Niger, Mahamadou Issoufou
ALIYEKUWA Kiongozi wa Upinzani nchini Niger, Mahamadou Issoufou, ametangazwa na tume ya uchaguzi ya nchi hiyo kuwa mshindi wa urais katika uchaguzi wa marudio uliofanyika Jumamosi ya Machi 12, kwa kupata karibu asilimia 58 ya kura. Hii ilikuwa ni baada ya kuongoza katika duru ya kwanza ya uchaguzi uliofanyika mapema Januari.
Issoufou ambaye amewania nafasi hiyo kubwa ya kisiasa katika chaguzi mbili zilizopita na kushindwa na aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Mamadou Tandja, aliyeondolewa madarakani na jeshi la nchi hiyo mwaka mmoja uliopita.
Mgombea wa urais kupitia chama kilichokuwa kinatawala cha Tandja cha MNSD, Waziri wa zamani, Seini Oumarou, alipata asilimia 42 ya kura. Uchaguzi huo ulifanyika kwa nia ya kurudisha hali ya utawala wa kiraia katika nchi hiyo.
Mfano kwa Afrika
Jeshi la nchi hiyo, ambalo limeahidi kuachia ngazi ifikapo Aprili, lilisema kabla ya uchaguzi kwamba halikuwa likimuunga mkono mgombea yeyote. Tandja aliyekaa madarakani kwa miaka 10 kabla ya kuangushwa katika mapinduzi ya kijeshi ya Februari mwaka jana wakati akijaribu kuongeza muda wa kutawala hata baada ya ukomo wa muda wake kisheria kufika.
Rais huyo wa zamani kwa sasa yupo gerezani akikabiliwa na mashtaka ya rushwa. Jenerali Salou Djibo, ambaye aliongoza mapinduzi hayo ya kijeshi, alisema kuwa uchaguzi huo wa Jumamosi ulikuwa wa amani na mfano kwa nchi nyingine za Afrika.
Niger, taifa ambalo kwa kiasi kikubwa likiwa ni jangwa lipo Magharibi mwa Afrika, linahifadhi uranium na limevutia mabilioni ya dola katika uwekezaji. Hata hivyo, linabakia kuwa moja ya mataifa maskini zaidi duniani, na limeshuhudia idadi ya mapinduzi kadhaa tangu kupata uhuru wake kutoka Ufaransa mwaka 1960.
Kundi la Al-Qaeda limekuwa likilaumiwa kwa utekaji nyara na mauaji ya raia wa nchi za Magharibi katika ukanda huo miaka ya hivi karibuni.
Historia ya Mahamadou Issoufou
Mahamadou Issoufou amezaliwa mwaka 1952. Ni Rais wa Chama cha PNDS-Tarayya. Aliwahi kuwa Waziri Mkuu wa Niger kati ya 1993-1994 na Rais wa Bunge 1995-1996, na amekuwa akigombea katika kila uchaguzi wa rais tangu mwaka 1993.
Wakati wa Urais wa Mamadou Tandja (1999-2010), Issoufou alikuwa kiongozi mkuu wa upinzani.
Issoufou, kutoka kabila la Kihausa, alizaliwa katika mji wa Dandaji katika jimbo la Tahoua. Ni mhandisi kitaaluma, aliwahi kuwa Mkurugenzi wa Taifa wa Madini 1980-1985 kabla ya kuwa Katibu Mkuu wa Kampuni ya Madini ya Niger (SOMAIR).
Uchaguzi wa rais na kuteuliwa kuwa Waziri Mkuu 1993
Mwezi Februari mwaka 1993, uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi wa wabunge na rais ulifanyika nchini humo. Katika uchaguzi wa bunge, chama cha Issoufou, cha PNDS, kilishinda viti 13 katika Bunge la Taifa, na Issoufou mwenyewe alishinda ubunge kupitia chama hicho cha PNDS katika jimbo la Tahoua.
Pamoja na vyama vingine vya upinzani, PNDS kilijiunga katika umoja wa Alliance of the Force Change (AFC). Muungano huu ulifanikiwa kuwa na wabunge wengi wapya wa kuchaguliwa katika Bunge. Baadaye mwezi Februari 1993, Issoufou aligombea katika uchaguzi wa rais kupitia PNDS.
Alishindwa kwa kushika nafasi ya tatu, akiambulia asilimia 15.92 ya kura zote. Muungano (AFC) ukaamua kumuunga mkono aliyeshika nafasi ya pili, Mahamane Ousmane katika raundi ya pili ya uchaguzi, uliofanyika Machi 27. Ousmane alishinda uchaguzi, akimshinda Tandja Mamadou, mgombea wa MNSD, huku AFC ikiwa na idadi kubwa ya wabunge, Issoufou aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu tarehe 17 Aprili 1993.
Migogoro na kukamatwa 1994-1999
Tarehe 28 Septemba, 1994, Issoufou alijiuzulu katika kukabiliana na amri kutoka kwa Ousmane iliyotolewa wiki moja kabla kufuatia kudhoofisha mamlaka ya waziri mkuu, na PNDS kujiondoa kutoka muungano wa serikali. Hii ilisababisha umoja huo wa kitaifa kupoteza wabunge wake wengi, na ilisababisha kufanyika kwa uchaguzi mpya wa wabunge Januari 1995.
Issoufou na chama chake cha PNDS walitengeneza muungano na wapinzani wao wa zamani, MNSD, na katika uchaguzi wa Januari 1995, muungano huo ulishinda kwa idadi ndogo ya viti, Issoufou akachaguliwa kuwa Rais wa Bunge.
Hali hiyo mpya ilisababisha mgongano wa kisiasa, pamoja na mgogoro kati ya rais na serikali kuongezeka. Tarehe 26 Januari 1996, Issoufou aliiomba Mahakama Kuu kumuondoa Ousmane madarakani kwa madai ya kutokuwa na uwezo wa kuongoza. Siku iliyofuata, tarehe 27 Januari 1996, Ibrahim Bare Mainassara alichukua madaraka katika mapinduzi ya kijeshi. Issoufou, pamoja na Rais Ousmane na Waziri Mkuu Hama Amadou, walikamatwa na hatimaye kuwekwa kizuizini hadi Aprili. Waliweka kwenye televisheni na utawala wa kijeshi mwezi Februari kama sehemu ya kutoa maoni kuwa mapinduzi yalisababishwa na matatizo katika mfumo wa siasa na kuunga mkono mabadiliko katika mfumo.
Katika uchaguzi alishika nafasi ya nne baada ya kuambulia asilimia 7.60 ya kura. Huu ni uchaguzi wa rais wa ujanja ujanja uliofanyika tarehe 7-8 Julai 1996 uliompa Mainassara ushindi wa wazi. Pamoja na wagombea wengine watatu wa upinzani, Issoufou aliwekwa kizuizini siku ya pili ya upigaji kura na kushikiliwa kwa wiki mbili, baadaye, alikataa kukutana na Mainassara, na bila mafanikio rufani yake iligonga mwamba Mahakama Kuu akitaka uchaguzi ufutwe, na ndipo chama cha PNDS kikatoa wito wa maandamano.
Julai 26, alikamatwa tena na kuwekwa chini ya ulinzi, pamoja na kiongozi mwingine wa chama cha PNDS, Mohamed Bazoum. Wawili hao baadaye waliachiwa huru. Kufuatia maandamano ya kidemokrasia Januari 11 mwaka 1997, Issoufou, Ousmane na Tandja walikamatwa kwa pamoja na kushikiliwa mpaka Januari 23.
Kiongozi wa upinzani 1999 hadi 2011
Mainassara aliuawa katika mapinduzi mengine ya kijeshi mwezi Aprili mwaka 1999, na uchaguzi mpya ulifanyika mwishoni mwa mwaka huo. Katika raundi ya kwanza ya Uchaguzi wa rais uliofanyika Oktoba, Issoufou alikuwa wa pili, kwa kujipatia asilimia 22.79 ya kura.
Baadaye alishindwa na Tandja Mamadou katika raundi ya pili mwezi Novemba akiambulia asilimia 40.11 ya kura ikilinganishwa na asilimia 59.89 alizopata Tandja. Alikuwa kaingia katika raundi ya pili, baada ya kushindwa kufikisha kura za kutosha kwenye raundi ya kwanza akiungwa mkono na wagombea Hamid Algabid, Moumouni Adamou Djermakoye, na Ali Djibo, wakati Tandja akiungwa mkono na Ousmane.
Baada ya kutangazwa kwa matokeo yaliyoonesha ushindi wa Tandja, Issoufou alikubali matokeo na kumpongeza Tandja. Katika Uchaguzi wa Bunge wa Novemba 1999, Issoufou alichaguliwa tena kuwa mbunge wa PNDS kupitia jimbo la Tahoua.
Katika uchaguzi wa 2004, Issoufou alishindwa kwa kuambulia asilimia 34.47 ya kura na kumwacha Tandja akishinda kwa asilimia 65.53; Hata hivyo, matokeo hayo bado yalionekana ya kuvutia kwa Issoufou, kwa kuwa wagombea wengine walikuwa wamemuunga mkono Tandja katika raundi ya pili. Issoufou, aliyetangaza kupambana na rushwa katika kampeni yake, alimtuhumu Tandja kwa kutumia fedha za serikali kwa ajili ya kampeni, ikiwa ni pamoja na madai mengine ya kutokuwepo uwazi katika uchaguzi, na kusema kuwa uchaguzi huo haukuwa huru na wa wazi kama uchaguzi wa 1999.
Katika uchaguzi wa bunge mwezi Desemba 2004, Issoufou alichaguliwa kuwa Mbunge katika jimbo la Tahoua.
Mgogoro wa kisiasa 2009
Mwaka 2009, PNDS ilipinga kwa nguvu zote jitihada za Tandja kutaka kura ya maoni ya kuandikwa katiba mpya ambayo ingemfanya kugombea katika uchaguzi hata baada ya muda wa uongozi kuisha.
Katika mkutano wa kupinga uliofanyika jijini Niamey, tarehe 9 Mei 2009, Issoufou alimtuhumu Tandja kwa kutafuta “katiba mpya ya kumuwezesha kukaa madarakani milele” na uanzishwaji wa “Utawala wa kifalme na udikteta.” Kama kiongozi wa muungano wa upinzani wa Front for the Defence of Democracy (FDD), alitangaza kufanyika maandamano Juni 7, mwaka 2009 licha ya serikali kuyapiga marufuku.
Kama sehemu ya mgogoro wa kikatiba, Tandja alitangaza kushika mamlaka ya dharura tarehe 27 Juni. Issoufou alimtuhumu Tandja kufanya mapinduzi ya kijeshi, “kukiuka katiba na kupoteza maadili na uhalali wa kisiasa”, Issoufou alitoa wito kwa majeshi kupuuza maagizo yake na wito wa jumuiya ya kimataifa kuingilia kati. Issoufou aliwekwa kizuizini nyumbani kwake na jeshi la polisi tarehe 30 Juni.
Mgomo wa kitaifa uliitishwa na FDD na ulifanyika tarehe 1 Julai na kuonesha mafanikio fulani kwa msaada wa vyombo vya habari.
Kura ya maoni ilifanyika na kufanikiwa tarehe 4 Agosti 2009, licha ya hasira za upinzani na wito wa kususia. Akizungumza tarehe 8 Agosti, muda mfupi baada ya kutangazwa kwa matokeo ya kura hiyo ya maoni, Issoufou aliapa kwamba upinzani “utapinga na kupigana na mapinduzi yaliyotungwa na Rais Tandja kwa lengo la kuendelea kutawala kidikteta.
Tarehe 14 Septemba 2009, Issoufou alishtakiwa kwa matumizi mabaya ya fedha na kutolewa ndani kwa dhamana. Lakini yeye alisema alishtakiwa kwa sababu za kisiasa. Hatimaye aliondoka nchini humo. Tarehe 29 Oktoba 2009, vibali vya kimataifa kwa ajili ya kukamatwa kwa Issoufou na Hama Amadou vilitolewa na serikali ya Niger, na Issoufou akarudi Niamey kutoka Nigeria tarehe 30 Oktoba ili “kushirikiana na mahakama.”
Tandja aliondoshwa katika mapinduzi ya kijeshi Februari 2010 na serikali mpya ya mpito kufanya maandalizi kwa ajili ya uchaguzi wa mwaka 2011.
Makala haya yameandaliwa na Bishop J. Hiluka kwa msaada wa vyombo mbalimbali vya habari
No comments:
Post a Comment