Mar 9, 2011

Dhana ya mwanamke kuwezeshwa iangaliwe upya

 Kinamama wakiandamana kuadhimisha siku ya Wanawake Duniani

 Spika wa Bunge wa kwanza mwanamke Tanzania, 
Anne Makinda


BISHOP J. HILUKA
Dar es Salaam

JUMANNE ya tarehe 8 Machi wiki hii ilikuwa ni siku ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ikiwa na kaulimbiu ya “fursa sawa za elimu, mafunzo, sayansi na teknolojia: Njia sahihi ya wanawake kupata ajira bora.”

Serikali ya Tanzania ni moja ya serikali ambazo zimekuwa mstari wa mbele kusisitiza umuhimu wa kumwezesha mwanamke kwa usemi kuwa “mwanamke akiwezeshwa anaweza”. Ninajaribu kutofautiana na usemi huu kwa kiasi kikubwa kwa kuwa unachangia kumdumaza mwanamke badala ya kumsaidia.

Neno kuwezeshwa lililotafsiriwa kutoka neno la Kiingereza;
Empower, ambalo kwa tafsiri iliyotolewa inakusudia kumhurumia mwanamke apate anachostahili, yaani ategemee huruma ya mwanaume katika mambo yake, ingawa tafsiri sahihi ilipaswa isiwe kumuwezesha bali kumpa idhini na mamlaka kama neno lenyewe lilivyo; “empower”.

Tunapaswa kubadilika na kuacha mambo ya kudai kuwa mwanamke hawezi bila kuwezeshwa kwa kuwa ndiyo yanayosababisha ajione duni zaidi. Nasema hivyo, kwa kuwa neno “akiwezeshwa” limepelekea wanawake wengi kushindwa kufanya mambo makubwa ya kuleta mabadiliko katika jamii kwa sababu wanangojea kuwezeshwa (huruma) jambo ambalo ni baya kwa maendeleo ya mtu yeyote.

Kama kweli serikali inataka kufanikisha hili kwa dhati haina budi kusimama kidete kupinga dhuluma na manyanyaso dhidi ya wanawake, kwa kuweka sera nzuri za kiuchumi na kijamii kwa ajili ya maendeleo ya wanawake. Vyombo vya upashanaji habari havina budi kulinda na kuheshimu utu wa mwanamke na kamwe asigeuzwe kuwa kivutio cha matangazo ya biashara. Sheria ziwe wazi kwamba, manyanyaso ya kijinsia kwa wanawake na wasichana ni kosa la jinai na wahusika wawajibishwe.

Mashirika ya Dunia yamefafanua usawa wa kijinsia ikihusiana na haki za binadamu, hasa haki za wanawake na maendeleo ya kiuchumi. Unicef inafafanua usawa wa kijinsia kama "kusawazisha uwanja wa kucheza kwa wasichana na wanawake kwa kuhakikisha kwamba watoto wote wana fursa sawa ya kuendeleza vipaji vyao.

Dhana ya kusubiri kuwezeshwa imekuwa inawafanya kinamama washindwe kusimama kwa miguu yao, na hata wenye uwezo nao wanataka kubebwa hivyo wananyimwa sifa ya kusema wamefaulu.

Ukweli ni kwamba mwanamke ana uwezo mkubwa wa kufanya mambo makubwa kuliko mwanamume, kwa mfano ukiangalia kwa upande wa wanafunzi shuleni, si jambo la kushangaza kumkuta mwanafunzi wa kike akiongoza kitaaluma na kuwashinda wanafunzi wa kiume kwa umbali mkubwa.

Ipo mifano ya baadhi ya wanawake ambao wamefanikiwa baada ya kujiona wanaweza na kuamua kujikita katika shughuli za kibiashara na kuacha utegemezi.

Licha ya mabadiliko yanayoendelea kufanywa na serikali yetu, lakini bado mfumo dume umeendelea kutawala. Serikali inapaswa iunde sera na sheria zitazowawezesha wanawake kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa jamii, kwa kutambua mchango wa wanawake ndani ya jamii zao.

Pamoja na kuwepo sheria za kumlinda mwanamke na hata kuundwa vyombo mbalimbali vya kumuwezesha mwanamke, bado kuna tatizo la utendaji mdogo wa vyombo hivyo kwa kuwa jamii bado haijaelimika kuhusu haki za mwanamke.

Hata mwanamke mwenyewe ambaye ndiye mlengwa bado hajajikubali kuwa ni kiumbe kinachopaswa kujiamini, kwa sababu mpaka sasa baadhi ya wanawake hawajiamini kama wanaweza kufanikiwa bila ya kuwa na mwanamume.

Imefikia wakati sasa mwanamke anapaswa ajitambue na kujikubali kama kiumbe kinachoweza kuibua chachu ya mabadiliko na maendeleo katika jamii. Mwanamke ajitume ili jamii imkubali na kumpa nafasi ya kuchangia katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo.

Mwanamke anapaswa aijue thamani yake mwenyewe, na mahusiano kati yake na mwenzi wake yaliyo sawa. Katika uhusiano wowote, huwepo hali ya kutoa-na-kupokea, hivyo anapaswa kuelewa, kwa ujumla, thamani yake katika ushirika ni sawa na ile ya mwenzi wake. Mwanamke anapaswa kujifunza jinsi ya kumiliki sauti yake na kudai maoni yake. Awe makini na jinsi wanawake wanavyochukuliwa kijamii na wanaume katika mazungumzo.

Atambue maneno na lugha inayoleta upendeleo wa mawasiliano ya kijinsia. Afanye jitihada za makusudi kubadili lugha ambayo huashiria kwa maeneo kadhaa kutumika kama ni upendeleo fulani. Maeneo mawili ya kuangaliwa yanayotumika kama upendeleo wa kijinsia ni pamoja na nafasi ya maamuzi ili kukidhi idadi ya wanawake serikalini na sera zinazoamua jinsia katika shule/uajiri.

Ile dhana ya kumchukulia mwanamke kama kiumbe dhaifu, asiye na sauti ya kuchangia masuala mbalimbali ya familia na badala yake hupewa jukumu la kukaa nyumbani kupika, kutafuta maji na mengineyo inapaswa iondolewe.

Mwaka 1975 Umoja wa Mataifa uliutangaza kuwa ni mwaka wa wanawake duniani. Kwa mara ya kwanza, siku ya wanawake kimataifa ikaadhimishwa tarehe 8 March, 1977, kwa kukazia haki za wanawake na changamoto ya kudumisha haki na amani. Tangu wakati huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wakati wa maadhimisho ya wanawake duniani huwa anatoa ujumbe na changamoto zinazoikabili Jumuiya ya Kimataifa kuhusu masuala ya wanawake.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, wakati wa ziara yake Barani Afrika ameshuhudia manyanyaso na dhuluma wanazofanyiwa wanawake na wakati wote wa ziara yake, amelizungumza tatizo hilo na viongozi mbalimbali wa Afrika. Amekemea vitendo vinavyodhalilisha utu na heshima ya wanawake.

No comments:

Post a Comment