Mar 9, 2011

Blaise Compaore: Mpatanishi maalum wa taasisi ya kieneo ya ECOWAS

 Rais wa Burkina Faso, Blaise Compaore

Ouagadougou
BURKINA FASO

HALI tete ya usalama katika mji wa Abidjan ambapo vifaru na askari wa Umoja wa Mataifa (UN) wa kulinda amani vinaonekana vikishika doria katika viunga vya mji huo inaashiria kazi ngumu ya kumshawishi rais anayeng'ang'ania madaraka, Laurent Gbagbo hata baada ya kuonekana ameshindwa katika uchaguzi.

Kumekuwepo taarifa za mapigano, mauaji na kufungwa barabara kadhaa kutokana na wafuasi wa viongozi hao kuchoma moto matairi barabarani na kuweka vizuizi katika viunga vya jiji la Abidjan.

Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, Alassane Ouattara alitangazwa na Tume ya Uchaguzi kumshinda mpinzani wake, Laurent Gbagbo, matokeo ambayo hata hivyo, yalipinduliwa na Mahakama ya Katiba ambayo ilisema Gbagbo ndiye mshindi hivyo kusababisha nchi hiyo kuwa na marais wawili, kila mmoja akiongoza kipande chake cha nchi, Gbagbo akiongoza Kusini na Ouattara akiongoza sehemu ya Kaskazini.

Jopo la usuluhishi wa mgogoro wa Ivory Coast lililoteuliwa na wakuu wa AU ni Rais wa Mauritania, Mohamed Ould Abdel Aziz, kama mwenyekiti, Jacob Zuma wa Afrika Kusini, Idriss Deby wa Chad, Jakaya Kikwete wa Tanzania na Rais wa Burkina Faso, Blaise Compaore ambaye ni mpatanishi maalum wa taasisi ya kieneo wa Jumuiya ya Uchumi ya Afrika Magharibi (Ecowas).

Blaise Compaore ni nani hasa?

 Kapteni Compaore

Blaise Compaore amezaliwa tarehe 3 Februari, 1951, na amekuwa Rais wa Burkina Faso tangu mwaka 1987.

Rais Compaore mwenye umri wa miaka 60, aliyekuwa kapteni wa jeshi la nchi hiyo, ni mwanzilishi wa chama tawala cha siasa nchini humo, cha Congress for Democracy and Progress. Alichukua madaraka katika mapinduzi ya 1987 kupitia mapinduzi ya kijeshi ya umwagaji damu ambapo mtangulizi wake Thomas Sankara aliuawa.

Alichaguliwa kuwa Rais mwaka 1991, katika uchaguzi uliogomewa na upande wa upinzani, na ameendelea kuchaguliwa tena na tena kuiongoza nchi hiyo mwaka 1998, 2005 na mwaka jana 2010, japo kumekuwa na upinzani uliojitokeza hasa wakati wa kampeni za uchaguzi kwa lengo la kumwondoa madarakani.

Wapinzani wa Compaore wanasema kuwa ameshindwa kumaliza tatizo la umasikini katika nchi hiyo. Burkina Faso ni moja kati ya nchi masikini sana ulimwenguni. Nchi hiyo isiyo na bandari imekumbwa na mapinduzi ya kijeshi mara tano tangu ilipopata uhuru mwaka 1960.

Compaore amejipatia umaarufu kwa kuituliza nchi hiyo tangu alipoingia madarakani kwa mapinduzi hayo ya kijeshi. Akiwa kiongozi anayetuhumiwa kusaidia makundi ya waasi wanaozusha migogoro katika ukanda wa Afrika Magharibi, Compaore sasa amejijengea jina la upatanishi akisuluhisha migogoro ya nchi za Togo, Ivory Coast na Guinea.

Mwanasheria na mchambuzi wa siasa nchini humo, Halidou Ouedraogo, aliyesaidia sana kufanya mabadiliko ya msingi katika siasa za nchi hiyo mwaka 2002, aliwahi kukaririwa kuwa tatizo la vyama vya upinzani nchini humo ni kugawanyika hadi kufikia vyama 150. Alisema vyama hivyo licha ya kugawanyika vina mtazamo mmoja lakini vimeshindwa kuungana na kuwa chama kimoja.

Burkina Faso iko karibu na mwisho wa vipimo vya Umoja wa Mataifa vya maendeleo vinavyopima hali ya maisha ya watu kwa ujumla, ikishikilia nafasi ya 161 kati ya nchi 169. Ina kiwango kikubwa cha ukosefu wa ajira na elimu duni. Wananchi wengi hutegemea kilimo cha kujikimu huku nchi hiyo ikitegemea zao la pamba kwa biashara.

Licha ya umasikini huo, Burkina Faso huzalisha madini ya dhahabu kwa wingi yanayohuisha uchumi wa nchi hiyo kwa kiasi kikubwa. Wimbi la mfumo wa vyama vingi lilipoingia Afrika mwanzoni mwa miaka ya 1990, Burkina Faso ilifanya uchaguzi na Compaore alishinda vipindi viwili vya miaka saba kati ya mwaka 1991 na 1998.

Compaore alipanda ngazi ya kijeshi na mtangulizi wake, Thomas Sankara wakiwa washiriki wa siri ya “maofisa wakomunisti” waliolenga kupambana na ufisadi nchini humo.

Sankara aliyekuwa Rais wa tano wa Burkina Faso baada ya kufanyika kwa mapinduzi ya kijeshi, ndiye aliyebadilisha jina la nchi hiyo kutoka Upper Volter na kuwa Burkina Faso.

Mapinduzi yaliyomuweka Thomas Sankara madarakani yaliandaliwa na Blaise Compaore, yakiungwa mkono na serikali ya Libya ambayo, kwa wakati huo, ilikuwa kwenye mzozo wa vita na Ufaransa wakati wa uvamizi wa Chad. Washiriki wengine muhimu katika mapinduzi hayo walikuwa Kapteni Henri Zongo, Meja Jean-Baptiste Boukary Lingani na Kapteni Thomas Sankara aliyeteuliwa kuwa Rais.

Mapinduzi ya mwaka 1987

Mwaka 1987, Sankara alipinduliwa na wanajeshi wenzake na nafasi yake ikashikiliwa na Blaise Compaore.

Compaore alichukua madaraka tarehe 15 Oktoba, 1987 katika mapinduzi yaliyopelekea kuuawa Rais Thomas Sankara, mtangulizi wake. Compaore aliyaelezea mauaji ya Sankara kama “ajali”, lakini hali hiyo haijawahi kuchunguzwa.

Baada ya kuchukua madaraka ya urais, aliimarisha sera nyingi zilizoanzishwa na Sankara, akidai kwamba sera zake zilikuwa “zinasahihisha” mapinduzi ya Burkina Faso.

Awali Compaore alitawala kwa ushirika wa pamoja na Henri Zongo na Jean-Baptiste Boukary Lingani, mwezi Septemba 1989, Zongo na Boukary walikamatwa, wakashtakiwa kwa madai ya kuwa na mipango ya kuipindua serikali, wakanyongwa.

Uchaguzi wa 1991 na 1998

Compaore alichaguliwa kuwa Rais mwaka 1991 katika uchaguzi uliogomewa na vyama vikuu vya upinzani wakigoma kwa maandamano wakihoji maana ya Compaoré kuchukua madaraka ya kwanza kwa asilimia 25 tu ya wapiga kura. Mwaka 1998 alichaguliwa tena.

Uchaguzi wa 2005

Agosti 2005, alitangaza nia yake ya kugombea uchaguzi wa rais. Wanasiasa wa upinzani waliona hili kama kuvunja katiba kutokana na marekebisho ya katiba ya mwaka 2000 yaliyoweka ukomo wa rais wa awamu mbili, na kupunguza muda mrefu wa miaka saba hadi miaka mitano.

Wafuasi wa Compaore walilipinga hili, wakisema kuwa marekebisho hayawezi kutumika haraka hivyo, na Oktoba 2005, Baraza la kikatiba lilitoa maamuzi kwamba kwa sababu Compaoré alikuwa bado yupo madarakani mwaka 2000, marekebisho hayo yasingeweza kutumika mpaka mwisho wa muhula wake wa pili, na hivyo kumruhusu kugombea kwenye uchaguzi wa 2005.

Novemba 13, 2005, Compaoré alichaguliwa tena kuwa Rais, akiwashinda wapinzani 12 kwa kupata asilimia 80.35 ya kura. Ingawa vyama 16 vya upinzani vilitangaza kuungana dhidi ya Compaoré katika mbio za urais, hata hivyo hakuna aliyetaka kuachia nafasi kwa kiongozi mwingine katika umoja huo, na mkataba wao ukashindwa.

Kufuatia ushindi huo Compaoré aliapishwa kwa kipindi kingine mwezi Disemba 20, 2005.

Uchaguzi wa 2010

Chama tawala kilisisitiza kubadilisha Katiba ya nchi ili aendelee kugombea mara nyingi atakavyo, jambo lililopingwa na vyama vya upinzani na Kanisa Katoliki.

Zaidi ya watu milioni tatu kati ya 16 milioni wa nchi hiyo walijiandikisha kupiga kura na walipiga kura katika vituo 12,600 vilivyoenea nchi nzima. Kwa idadi hiyo, nusu ya wakazi wa nchi hiyo wako chini ya umri wa miaka 14. Idadi hiyo ilishusha hadhi ya uchaguzi huo kuwa huru na wa haki.

Katika uchaguzi wa 2010, Compaore alikuwa akipambana na vyama sita vya upinzani, japo mmoja alikuwa mgombea binafsi. Kati yao alikuwepo mwanasheria, Stanislas Benewinde Sankara, aliyepata asilimia tano ya kura mwaka 2005 ukilinganisha na Compaore aliyepata asilimia 80.

Siku ya kupiga kura, wananchi walijipanga kwenye mistari tangu saa 12 asubuhi. Hakukuwa na matatizo makubwa yaliyoripotiwa hadi mwisho wa mchakato wa kura. Hata hivyo, kulikuwa na baadhi ya wapiga kura katika Mji Mkuu wa Ouagadougou waliokuwa na vyeti vyao vya kuzaliwa walioshindwa kupiga kura kwa kukosa sifa za kupiga kura.

Majukumu ya Kimataifa na Kikanda

Mwaka 1993, Rais Compaoré aliongoza ujumbe wa Burkina Faso ambao walishiriki katika Mkutano wa Tokyo wa Kimataifa wa Maendeleo ya Afrika uliokuwa wa kwanza.

Compaoré amekuwa akifanya kazi kama mpatanishi katika masuala ya kikanda.

Makala hii imeandaliwa na Bishop J. Hiluka kwa msaada wa mashirika mbalimbali ya kimataifa

No comments:

Post a Comment