Mar 2, 2011

Joseph Kabila: Aonja machungu, nusura yamkute ya baba yake

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
Joseph Kabila

 Ramani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo

KINSHASA
Congo

WATU ambao bado hawajajulikana au ambao imeamuliwa wasitajwe majina yao, mapema wiki hii wameshambulia makazi ya Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Joseph Kabila, katika eneo la Gombe jijini Kinshasa, ambako katika eneo hilo kuna ofisi nyingi za balozi za nchi mbalimbali.

Tukio hilo limekuja katika mwaka ambao Rais Joseph Kabila anatarajiwa kumaliza muhula wake wa urais, na kutakuwa na uchaguzi mwingine hapo Novemba mwaka huu. Inasemekana walinzi wa makazi hayo walikuwa makini na kufanikiwa kuwaua washambuliaji 7 papo hapo na wengine kadhaa wamekamatwa.

Habari zimeendelea kusambaa kuwa kwa uchache, watu tisa wamekwishapoteza maisha katika tukio hilo la kushtukiza. Habari hizo zinadai kuwa watu waliokuwa wameshambulia makazi hayo ni makomandoo, na walikuwa na silaha kubwa za moto.


Inadaiwa wakati wa shambulizi hilo, Rais Kabila alikuwepo kwenye makazi yake, ingawa kuna taarifa nyingine zinazodai kuwa hakuwapo muda huo, ila alirejea baada ya kusikia kuna tukio katika makazi yake.

Mara baada ya milio ya risasi kusikika, watu waliokuwa karibu na makazi ya Rais Kabila walitawanyika. Wakati makala hii ilipokuwa ikiandaliwa, inasemekana barabara zote karibu na Makazi ya Kabila zilikuwa zimedhibitiwa kwa askari na vifaru vikiwa vimeziba njia zote za kuelekea makazi hayo ya Rais.


Tukio hili limekuja siku chache tu baada ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete kupitia nchi hiyo na kuwa na mazungumzo na Rais Joseph Kabila, jijini Kinshasa, kabla ya kurudi Tanzania. Rais Kikwete alisimama kwa muda mjini Kinshasa akitokea Abidjan, Ivory Coast na kufanya mazungumzo na Rais Kabila.

Harakati hizi za mapinduzi dhidi ya Kabila zimetokea kwa mara ya kwanza tangu alipokabidhiwa dhamana ya kuiongoza nchi hiyo ambayo ni ya tatu kwa ukubwa katika bara la Afrika mwaka 2001.

Ikumbukwe hata wakati wa uchaguzi mkuu uliomuweka madarakani mwaka 2006, kwenye duru ya kwanza ya upigaji kura ilishuhudia mapigano kati ya wafuasi wa Rais Kabila na aliyekuwa mpinzani wake mkubwa, Jean-Pierre Bemba, wakati matokeo yalipokuwa yanatangazwa.

Na katika duru ya pili ya upigaji kura, wafuasi wa Kabila na Bemba walikuwa wakisambaziana ujumbe mfupi wa simu za mkononi na barua pepe kila upande ukidai kuwa mgombea wao ameibuka na ushindi.

Hali hii ilimpelekea Mkuu wa Tume Huru ya Uchaguzi, Apollinaire Malumalu, kusema kuwa kuchapishwa kwa matokeo yasiyo rasmi kunaweza kusababisha ghasia. Malumalu alisema alisikitishwa na kutolewa kwa taarifa zisizo sahihi za matokeo ambazo zingeweza kuongeza hali ya wasiwasi.

Kwa mujibu mwanadiplomasia wa Magharibi aliyekaririwa na Shirika la Habari la Uingereza (Reuters), tume ya uchaguzi ilipewa shinikizo kutangaza sehemu ya matokeo ya awali kwa ajili ya kuondoa taarifa za uvumi. “Hii ni hatua nzuri,” alisema mwanadiplomasia huyo.

Matokeo ya awali yaliyotolewa yalithibitisha kuwa Kabila aliendelea kuwa mashuhuri katika maeneo ya Mashariki mwa nchi, ambako wapiga kura waliamini kuwa utawala wake umerejesha hali ya utulivu. Hata hivyo, Bemba, alipata kura nyingi kutoka upande wa Magharibi. Lakini mwisho wa yote, alikuwa ni Joseph Kabila aliyeibuka mshindi wa Urais wa nchi hiyo.

Historia yake

Joseph Kabila Kabange alizaliwa tarehe 4 Juni, 1971, katika mji mdogo wa wilaya ya Fizi mkoa wa Kivu Kusini katika Mashariki ya Kongo. Babake alikuwa mwanasiasa na kiongozi wa kikundi cha wanamgambo waasi waliopinga serikali ya Mobutu Sese Seko.

Joseph Kabila ni rais wa nne wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kondo (DRC). Inasemekana Joseph ni mtoto aliyeasiliwa (adopted) wa Laurent na Sifa Mahanya, hata hivyo kuna baadhi ya mashaka kama kuna usahihi wowote wa habari hizi.

Joseph Kabila aliingia madarakani baada ya kifo cha baba yake, Rais Laurent-Desire Kabila aliyeuawa kwa kupigwa risasi na wanajeshi tarehe 16 Januari, 2001. Ndipo wanasiasa wengine walipomteua mwana huyo wa Kabila kuwa rais baada ya baba yake.

Wengi, hasa wale walio katika utawanyiko wa Kongo, wanaamini kwamba Laurent-Desire Kabila hakuwa baba yake mzazi, lakini badala yake alikuwa baba yake wa kambo.

Wanasiasa wengi wa upinzani walitoa wito kufanyika kwa vipimo vya DNA ili kuthibitisha utambulisho wake kama ni mtoto halisi wa Laurent Kabila, lakini Kabila hakukubali kufanya hivyo.

Maisha na makuzi yake

Pamoja na familia ya baba yake, Joseph alihamia jijini Dare es Salaam, Tanzania. Alisoma shule ya msingi na ya sekondari katika miji ya Dar es Salaam na Mbeya. Inasemekana kuwa wakati ule alitumia jina la Hippolyte Kanambe Kazemberembe Kabange Mtwale kwa sababu za kiusalama.
 
Mwaka 1996 alijiunga na wanamgambo wa baba yake katika vita ya Kongo ya Mashariki. Baada ya ushindi wa wapinzani dhidi ya Mobutu, baba yake alikuwa Rais wa nchi na yeye alipelekwa masomoni kwenye chuo cha kijeshi huko China. Aliporudi alipewa cheo cha Jenerali jeshini na mwaka 2000 alipandishwa cheo kuwa Mkuu wa Majeshi nchini humo.
 
Tangu kuwa rais wa nchi mwaka 2001, Joseph Kabila alijitahidi sana kumaliza hali ya vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Kongo, akakubali kufika kwa walinzi wa amani wa Umoja wa Mataifa.

Desemba 2002 alikubali kuwepo kwa mapatano ya amani kati ya serikali yake na waasi yaliyokuwa msingi kwa ajili ya kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa na maandalizi ya uchaguzi wa mwaka 2006.

Katika uchaguzi wa kitaifa wa 30 Julai 2006 alipata kura nyingi kuwa rais lakini hakufikia nusu ya kura zote. Katika uchaguzi wa pili kati yake na Jean-Pierre Bemba, Kabila alishinda na kuthibitishwa kuwa Rais wa Kongo tarehe 17 Novemba, 2006. Hata hivyo, Joseph Kabila ameweka rekodi ya kuwa rais wa kwanza wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo aliyechaguliwa na wananchi wote katika uchaguzi huru.

Juni 2006 alimwoa Olive Lembe di Sita aliyekuwa mchumba wake wa miaka mingi na mama wa binti yake aliyezaliwa mwaka 2001.
Rais Kabila ni muumini wa madhehebu ya Kiprotestanti (Anglikana), na mkewe, Lembe di Sita ni muumini wa madhehebu ya Katoliki.

Makala hii imeandaliwa na Bishop J. Hiluka kwa msaada wa mashirika mbalimbali ya habari

No comments:

Post a Comment