Jun 3, 2011

UNYWAJI MAZIWA: Tunakatishwa tamaa na wachakachuaji

 Bidhaa za Kiwanda cha Tanga Fresh katika maonyesho hayo

 Baadhi ya wanafunzi wa shule mbalimbali za msingi za Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam wakiandamana kwenye barabara ya Kawawa kuadhimisha kilele cha wiki ya uhamasishaji unywaji wa maziwa

BISHOP J. HILUKA
Dar es Salaam

WIKI hii ilikuwa ni ya maadhimisho ya wiki ya unywaji maziwa ambapo Bodi ya Maziwa Tanzania kwa kushirikiana na Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi iliandaa maadhimisho ya Wiki ya Uhamasishaji wa Unywaji wa Maziwa Kitaifa yaliyofanyika mkoani Dar es Salaam kuanzia tarehe 28 Mei mpaka 31 Mei, 2011.

Maadhimisho hayo ya kitaifa yalihusisha uhamasishaji wa unywaji maziwa yaliyoambatana na maonesho ya bidhaa zitokanazo na maziwa yanayozalishwa Tanzania, pamoja na Mkutano wa mwaka wa Baraza la Wadau wa maziwa

Kaulimbiu ya Wiki ya Uhamasishaji wa Unywaji wa Maziwa mwaka 2011 ilikuwa ni Kunywa maziwa kwa afya yako; Jenga uchumi wa nchi yako’.

Madhumuni ya Wiki ya Uhamasishaji wa Unywaji wa Maziwa yalikuwa na lengo kuu la kuhamasisha unywaji wa maziwa kwa afya ya binadamu kwa kuwa maziwa ni chakula bora kwa watu wa rika zote na kutoa taarifa kuhusu changamoto na fursa za sekta ya maziwa katika kuondoa umasikini kwa Watanzania.

Pamoja na hayo Wiki ya Uhamasishaji wa Unywaji wa Maziwa inachangia katika kuboresha soko la maziwa na bidhaa zake na pia kutoa fursa kwa wadau kukutana na kubadilishana uzoefu katika kuendeleza sekta ya maziwa.

Imekuwa ikisemwa kuwa pamoja na kuwa Tanzania ni nchi ya tatu kwa wingi wa mifugo katika Bara la Afrika, lakini Watanzania wengi hawana kabisa utamaduni wa kunywa maziwa, kula mayai na nyama kama wenzao wa Uganda na Kenya!

Kwa maana hiyo, kwa kuwa hatuna utamaduni wa kunywa maziwa, wananchi wa Kenya ndio wanaoongoza kwa kunywa maziwa wakifuatiwa na Uganda na Rwanda ingawaje sisi tumejaaliwa kuwa na mifugo wengi ambao wangetosheleza mahitaji yetu ya vyakula hivyo.

Kwa mujibu wa tafiti mbalimbali zilizofanywa, unywaji wa maziwa nchini uko chini sana na inasemwa kwamba mtu mmoja anakunywa lita 40 tu za maziwa kwa mwaka, tofauti na viwango vilivyowekwa na Shirika la Chakula Duniani (FAO), ambapo viwango vya FAO vinataka kila mtu anywe maziwa lita 200 kwa mwaka.

Napenda niseme wazi kama mwananchi na Mtanzania kuwa mimi ni mmoja wa watu wanaopenda sana wanywe maziwa, nikiwa nayahitaji maziwa kwa sababu kuu mbili: kwanza nayahitaji maziwa kwa ajili ya afya yangu, hasa ikizingatiwa kuwa nina vidonda vya tumbo na maziwa hunipa ahueni kubwa, na sababu ya pili ambayo ni ya kiafya vilevile kutokana na kutumia muda mwingi kwenye kompyuta, ambapo kuna madhara ya mionzi tunashauriwa kunywa maziwa kila mara ili kuepuka madhara hayo ya mionzi.

Si kwambwa hatupendi kunywa maziwa bali kuna mambo kadhaa kama nitakavyoyaeleza baadaye; moja ya matatizo makubwa yanayotukatisha tamaa ni kwamba maziwa mengi yanayouzwa maeneo ya mijini hususan Dar es Salaam si maziwa halisi kama wafanyabiashara wa maziwa wanavyotaka tuamini, kwa kuwa wafugaji tayari huwa wamekwishayachakachua kwa kuongeza maji ili yawe mengi.

Na haiishii hapo tu kwani yakishafika kwa wafanyabiashara nao hupenda kuchukua maziwa hayo kiasi kidogo na kuchanganya na maziwa ya unga au wakati mwingine hata unga wa ngano, kisha wanatia mafuta kidogo ili kupata utando wa mafuta juu yake.

Maziwa ya moto yanayouzwa kwenye vibanda vingi jijini Dar es Salaam, pindi ukiyatia mdomoni huwezi kuisikia ile radha ya maziwa, na pia huwa yana utando wa mafuta ambao si wa kawaida hasa kwa mtu anayeyafahamu vizuri maziwa halisi.

Lengo la wafanyabiashara kuamua kuchakachua maziwa ni ili wapate faida kubwa bila kujua kwamba wanajiharibia soko na wakati huohuo kuhatarisha afya za watumiaji kwani hata hayo maji wanayotumia kuchakachua sidhani kama ni maji salama.
Sababu nyingine inayosababisha Watanzania kuonekana kuwa hawapendi kunywa maziwa ni kutokana na kuendelea kwa umasikini na hali ngumu ya kiuchumi katika ngazi za kifamilia na kitaifa, hali hii imefanya afya za wananchi ziendelee kuwa hatarini kutokana na ugumu wa maisha na hivyo kufanya hata baadhi ya vyakula muhimu ikiwemo maziwa kuwa anasa kwa Mtanzania wa kawaida.

Kauli mbalimbali zinazotolewa na baadhi ya viongozi na watafiti kwamba eti Watanzania wafundishwe (waelimishwe) kuhusu umuhimu wa kula nyama, mayai na kunywa maziwa, kwangu mimi nahisi kama hiki ni kichekesho cha mwaka! Ni kichekesho kwa kuwa sidhani kama kuna Mtanzania asiyejua umuhimu wa vyakula hivyo kwa mwili wa binadamu!

Wanapodai kuwa tuelimishwe, wanatuelimisha katika lipi wakati tuna kliniki zimejaa nchini takriban kila kijiji, ni nani ambaye hajawahi kufundishwa au ambaye mama yake hajafundishwa umuhimu wa vyakula hivyo? Inaposemwa kuwa Watanzania hawanywi maziwa, hawali nyama na mayai sio kwa sababu hawana elimu ya umuhimu wa lishe hiyo bali hawana imani na maziwa yanayouzwa na wafanyabiashara wetu na pia hali ya kiuchumi haiwaruhusu kufanya hivyo!

Maziwa pekee yanayoonekana kuaminika miongoni mwa jamii zetu au kuwa halisi ni yale yanayosindikwa viwandani ambayo hata hivyo kwa hali halisi ya kiuchumi ya Watanzania wengi ni sawa na anasa kuyanunua.

Naomba, maadhimisho haya ya wiki ya kunywa maziwa, wahusika pia wangetumia fursa hiyo kunyoosheana kidole kwa kujiharibia soko kwa kuchakachua maziwa. Lakini pia ni jukumu la Serikali kuchukua hatua na kuangalia jinsi ya kudhibiti uchakachuaji huu ili kulinda afya za Watanzania na kwa kufanya hivyo, biashara hiyo itakuwa kubwa na hata Serikali itapata mapato kupitia kodi.

No comments:

Post a Comment