Moses Wetangula
NAIROBI
Kenya
VITA kali kuhusu mgombea gani anayekubalika zaidi miongoni mwa jamii ya kabila la Luhya nchini Kenya kwa ajili ya kusimama kuwania nafasi ya urais nchini humo imezidi kupamba moto baada ya aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Moses Wetangula kusema kuwa na yeye anaingia kwenye kinyang'anyiro cha kuwania nafasi hiyo kubwa katika nchi.
Wetangula alianza pilikapilika hizo wakati akitafuta kuungwa mkono na jamii hiyo ya Waluhya katika kikao chake mjini Mombasa. Akiongea katika kikao cha kutaka kukiongoza chama cha Ford-Kenya, Wetangula alisema ameamua kuwania nafasi hiyo tangu jamii ilipofikiria kuwa anafaa kuwa makamu wa rais.
Mbio hizo za urais za Wetangula zinaongeza idadi ya vigogo wa Kenya ambao tayari wameonesha nia ama kutangaza rasmi kuwa watawania nafasi hiyo kubwa kabisa katika siasa za nchi hiyo. Kigogo mwingine aliyekwishatangaza nia ya kuutaka urais wa Kenya ni mwenyekiti wa chama cha Narc, Martha Wangari Karua.
Mbali na urais, Martha Karua pia alithibitisha kuwa atatetea nafasi yake ya ubunge kupitia Jimbo la Guchugu huku akiahidi kufanya kazi kwa ajili ya kuboresha afya na maisha ya Wakenya.
Hata hivyo, hisia za Wetangula zimekuja huku kukiwa na mgawanyiko wa maoni kuhusu nani anafaa kugombea urais wa Kenya mwaka 2012. Muungano wa kundi linalofahamika kama G7 limeshaweka msimamo kuwa litamuunga mkono Mbunge wa Saboti, Eugene Wamalwa.
Katika maombi yake kwa jamii ili imuunge mkono kwa ajili ya nafasi hiyo, Wetangula aliahidi kukifufua chama cha Ford-Kenya na kuelekeza lawama zake kwa mwenyekiti wa zamani wa chama hicho, Musikari Kombo kwa kukifanya chama hicho kuwa kama chumba cha mikutano (boardroom).
Wetangula walionesha haja ya jamii ya kuunganisha nguvu na kutangaza kuwa tayari amekitafutia chama cha Ford-Kenya ofisi zitakazokuwa makao makuu yake mjini Nairobi
"Mimi ni mgombea bora wa urais ambaye Kenya inapaswa kuwa naye, na ndiyo maana nimekuja kwenu kuomba ridhaa yenu ili kuijenga upya nchi hii," alisema.
Kwa kile kilichoonekana kama mashambulizi ya moja kwa moja kwa Wamalwa, Wetangula alisema kuwa mbunge huyo wa Saboti alikuwa anatumiwa na viongozi katika maeneo mengine kuwagawa watu wa jamii ya Waluhya, na hata kukigawa chama cha Ford-Kenya.
Akasema, "Mimi nina nguvu na uwezo wa kuongoza nchi na kuipeleka mbele, tunapaswa kutafuta namna ya kuungana na vyama vingine, ni bahati mbaya kwamba Waluhya hawana umoja hata wawapo bungeni."
Wetangula ni Mbunge wa Jimbo la Sirisia baada ya kuchaguliwa katika uchaguzi mkuu uliogubikwa na ghasia wa Desemba 2007.
Katika Baraza la Mawaziri lililoteuliwa na Rais Mwai Kibaki Januari 8, 2008, wakati nchi ikiwa imegubikwa na mgogoro ulioibuka baada ya matokeo ya uchaguzi wa rais, Wetangula aliteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje.
Historia yake
Moses Masika Wetangula amezaliwa tarehe 13 Septemba, 1956. Ni mwanasiasa wa Kenya na Mbunge anayewakilisha Jimbo la Sirisia. Amekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya tangu Januari 2008 hadi alipojiuzulu Oktoba, 27 mwaka jana.
Wetangula alisoma katika Shule ya Msingi ya Nalondo, halafu akaenda katika Shule ya Upili (Secondary) ya Teremi na baadaye Shule ya Friends, Kamusinga kabla ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Nairobi, ambapo alifuzu na kupata Shahada ya kwanza katika Sheria (LLB).
Aliteuliwa kuwa mbunge kwenye chama cha kisiasa cha Kanu kilichokuwa kikitawala wakati huo chini ya Daniel arap Moi baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 1992, na kuwatumikia Wakenya katika nafasi hiyo hadi mwaka 1997. Pia amewahi kushika vyeo vingine kadhaa vya umma kama hakimu na mwenyekiti wa Bodi ya Kurekebisha Umeme (Electricity Regulatory Board).
Wetangula pia alishiriki katika asasi kadhaa za kuleta fedha ili kuanzisha miradi ya kusaidia watu na amekuwa akitoa huduma za kisheria kwa wananchi mbalimbali. Anaaminika kwa kuhamasisha wanawake na vijana kuanzisha miradi kwa ajili ya kuzalisha na kujipatia kipato.
Wetangula alichaguliwa kuwa mbunge kwenye Bunge la Kenya katika uchaguzi mkuu wa rais na wabunge mwaka 2007. Baada ya uchaguzi ndipo rais Mwai Kibaki alipomteua Wetangula kuwa Waziri wa Mambo ya Nje mnamo tarehe 8 Januari 2008, wakati huohuo kukiwa na ghasia na mgogoro mkubwa kuhusiana na matokeo ya uchaguzi wa rais.
Mwezi wa Januari, baada ya nchi ya Uingereza kulalamika kuhusu uchaguzi wa rais, Wetangula alimwita na kumlalamikia Kamishna wa Uingereza, Adam Wood, na alisema kwamba "uchaguzi wetu hauhitaji muhuri wa mamlaka kutoka House of Commons".
Baada ya serikali ya mseto kukubaliwa kati ya Rais Mwai Kibaki na Waziri Mkuu Raila Odinga, kutokana na kile ambacho wote walidai kushinda katika uchaguzi wa rais, Wetangula bado aliendelea kushikiria cheo chake cha Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo katika Serikali ya Mseto, iliyotangazwa tarehe 13 Aprili, 2008.
Kashfa ubalozi Kenya jijini Tokyo
Moses Wetangula alijiuzulu nafasi yake ya Uwaziri tarehe 27 Oktoba, 2010 ili kutoa nafasi ya kufanywa uchunguzi kuhusiana na kashfa ya ununuzi wa jengo la ubalozi wa Kenya jijini Tokyo, Japan.
Mwingine aliyejiuzulu pamoja na Wetangula kufuatia kashfa hiyo alikuwa katibu wa Wizara hiyo ya Mambo ya Nje, Thuita Mwangi. Wote wawili walikuwa wanashutumiwa kwa kukiuka mapendekezo yaliyotolewa na wataalamu kuhusu gharama ya jengo hilo.
Kamati ya bunge kuhusu masuala ya nchi za nje na ulinzi, iliwasilisha taarifa bungeni ikipendekeza kuwa waziri Moses Wetangula na katibu huyo wajiuzulu, kufuatia sakata hilo linalokisiwa kuigharimu serikali ya Kenya dola za Marekani milioni 13.5. Pia kuliripotiwa kuwepo kashfa ya kupotea fedha katika ubalozi wa Kenya nchini Misri, Nigeria, Pakistan na Ubelgiji.
Kashfa hiyo iliibua mjadala mkali ndani ya Bunge la Kenya kuhusiana na ripoti hiyo. Japo aliamua kujiuzulu lakini Wetangula alikanusha tuhuma zote hizo. Tuhuma hizo za ufisadi ndizo zinazoonekana kuwa nzito kumgusa kiongozi mwandamizi mwenye dhamana kubwa katika serikali ya Kenya.
Kashfa hiyo iliibua mjadala mkali ndani ya Bunge la Kenya kuhusiana na ripoti hiyo. Japo aliamua kujiuzulu lakini Wetangula alikanusha tuhuma zote hizo. Tuhuma hizo za ufisadi ndizo zinazoonekana kuwa nzito kumgusa kiongozi mwandamizi mwenye dhamana kubwa katika serikali ya Kenya.
Makala haya yameandaliwa na Bishop J. Hiluka kwa msaada wa mashirika mbalimbali ya habari.
No comments:
Post a Comment