Feb 17, 2011

Filamu ya Dowans, nani muongozaji nani staring?

 Waziri Mkuu, Mizengo K. Pinda

Mwanasheria Mkuu, Jaji Frederick Werema

 Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja

BISHOP J. HILUKA

JUMANNE wiki hii nilipigiwa simu na msomaji mmoja wa makala zangu wa muda mrefu aliyetaka kujua maoni yangu kuhusu tamko la serikali kupitia Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja wa kukubali kirahisi kuilipa kampuni feki ya Dowans mabilion ya fedha za wananchi kwa kisingizo cha kuharakisha malipo ya dola za Marekani 65, 812, 630.00 ili deni hilo lisizae riba kubwa.

Msomaji huyo pia alitaka afahamishwe kuhusu uhalali wa kisheria wa miliki ya Dowans kwa mali za Richmond na kwa nini Serikali haikutaifisha mali za Richmond? 
 
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema, na Waziri Ngeleja, kwa nyakati tofauti wamepata kunukuliwa wakisema taifa halina njia ya kukwepa faini hiyo.

Kwa kweli sikumbuki nilimjibu nini msomaji huyo, lakini siku iliyofuata, yaani Jumatano nilipata taarifa za tamko la Wanaharakati wa Haki za Binadamu na Mitandao ya Kijinsia nchini kupanga kuzuia malipo hayo Mahakama Kuu. Ndipo nilipojikuta nikiyakumbuka maswali niliyoulizwa na msomaji wangu, na nilipokuwa nikiyatafakari kwa kina niligundua kuwa sakata hili halina tofauti na maigizo ya filamu tulizozoea kuziangalia.

Kwa nini nalifananisha sakata hili na filamu? Kitu cha kushangaza ni kwa nini serikali inang'ang'ania kuilipa haraka Kampuni ya Dowans wakati bado kuna utata na kulikuwa na nafasi ya kuendelea na shauri hilo? 
 
Pia kwa nini serikali inataka kulipa haraka kabla ya kikao cha Baraza la Mawaziri, ambacho kingeweza kujadili kwa kina hasa kutokana na utata wake kuliko kufanya maamuzi ya haraka. Hapa lazima kuna jambo.

Nadhani kila mmoja anazifahamu filamu na pengine ameshaangalia filamu kadhaa ambazo kwa kawaida huwa na mhusika mkuu (staring) ambaye huwa hafi japo cha moto hukiona. Staring katika filamu wakati fulani hulemewa na kuzidiwa lakini mwisho wa yote hushinda. Filamu huambatana na kuigiza mambo kwa kuyakuza (danganya toto) ambayo hulenga zaidi kwenye kuburudisha.

Suala la Dowans ni filamu (ingawa kwa maudhui tofauti) kwa sababu mambo yanayoendelea ndani ya sakata hili ni ya ajabu sana. 
 
Filamu hii inaanzia ambapo serikali inang'ang'ana kuilipa Kampuni iliyosemwa kuwa imeingia mkataba wa kitapeli na yenye watu wasiojulikana walioliibia taifa kwa kiwango cha kutisha, mkataba ulioingiwa na viongozi wa taifa hili ambao wanajulikana lakini hawajafikishwa mahakamani hadi sasa.

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kwa kushirikiana na wanaharakati wa haki za kijinsia nchini wamewasilisha pingamizi Mahakama Kuu kupinga Serikali isiilipe kampuni ya Dowans Sh 97 bilioni zilizotokana na hukumu ya Mahakama ya Usuluhishi ya Biashara ya Kimataifa (ICC).

Mahakama hiyo ilikuwa imesikiliza malalamiko ya Dowans dhidi ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na kuamua iilipe fidia hiyo baada ya kubaini kuwa ilivunja mkataba kinyume cha taratibu.

Kwa kawaida kabla ya malipo hayo kufanyika, hukumu hiyo ya ICC inapaswa kusajiliwa na Mahakama Kuu ya Tanzania, lakini wanaharakati hao wamekusudia kuweka pingamizi kuzuia mchakato huo usifanyike hivyo Dowans isilipwe.

Hapa natoa angalizo tu: isije ikawa ni mchezo tu unachezwa, kama ilivyokuwa wakati wa sakata la Tanzania iliponunua rada ya kijeshi kutoka Uingereza kwa paundi milioni 28 ambazo ni sawa na sh bilioni 70, mwaka 2002. Wabunge walipaza sauti zao kuwa rada hiyo isinunuliwe, wanaharakati nao walipaza sauti zao kukataa ununuzi huo lakini wakati wakikataa ununuzi huo hawakuwa na taarifa kuwa tayari rada ilikuwa imeshatua nchini na imefungwa.

Pia kwenye suala la malipo kwa Dowans isije ikawa wanaharakati wanakwenda mahakamani wakati tayari Dowans wameshachukua chao! Hii ni filamu ya aina yake ambayo japo tunaishabikia lakini itatumaliza kabisa na kutuacha watupu tukiwaacha mafisadi kuchukua kila kitu na kupelekea kifo chetu na cha vizazi vijavyo.

Ni kama alivyosema Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta kuwa Dowans wanacheza mchezo katika makaratasi ili wajipatie mabilioni ya shilingi za Watanzania na kwamba kitendo cha kuwailipa itakuwa ni matumizi mabaya ya fedha za walipa kodi.

Kwa kweli kwa hili imani ya wananchi kwa serikali imepungua, serikali inapaswa iachane kabisa na usiri kwenye suala hili la malipo kwa Kampuni ya Dowans na kuweka bayana mazingira yaliyopelekea Tanzania kushindwa katika shauri hilo ambayo yanatutatanisha.

Maelezo ya Ngeleja kwenye taarifa yake kuhusiana na tozo/uamuzi wa mahakama ya kimataifa ya usuluhisho, yamezidi kuongeza utatanishi unaowafanya wananchi wazidi kupunguza imani yao kwa serikali.

Hivi uhalali wa kampuni za Richmond, Dowans ya Costa Rica na Dowans (T) Limited ya Tanzania ni upi hadi serikali itake kulipa haraka kiasi hicho?
Sijui filamu hii itaishaje, yetu macho.

SOURCE: KULIKONI 

No comments:

Post a Comment