Feb 17, 2011

SALVA KIIR MAYARDIT: Atakuwa rais wa kwanza wa nchi mpya ndani ya Afrika mwaka 2011?

 Salva Kiir Mayardit

Juba
SUDAN

KURA ya maoni nchini Sudan ambapo wapigaji kura wataamua iwapo Sudan Kusini ijitenge na Sudan Kaskazini na kujitawala kama taifa huru au la imepangwa kufanyika Januari 9 mwakani huku ikikumbwa na hofu ya kutokea mvutano mkubwa.

Salva Kiir Mayardit ndiye kiongozi wa harakati hizi za kutaka kujitenga Sudan Kusini. Mwanasiasa huyu alitambua kuwa alikuwa na nafasi finyu ya kuchaguliwa kuwa rais wa taifa la Sudan kutokana na siasa za nchi hiyo katika uchaguzi wa Aprili 2010. Hivyo akaamua kusaka mamlaka ya kidemokrasia ya kuiongoza Sudan Kusini – nafasi anayoishikilia tangu kifo cha ghafla ya mtangulizi wake, John Garang, mwaka 2005.

Baada ya kucheleweshwa kwa muda, hatimaye wapiga kura kutoka Sudan Kusini wamejiandikisha kushiriki kura ya maoni hapo mwakani. Taarifa za BBC zilizotolewa Novemba 15 mwaka huu zilisema kuwa shughuli nzima ya kujiandikisha ilitarajiwa kuchukua siku 17, kabla ya kuanza rasmi kwa kampeni za kura ya maoni.

Kura hiyo ni mojawapo ya maafikiano ya mpango wa amani wa mwaka 2005 uliomaliza vita vya wenyewe kwa wenye vya zaidi ya miongo miwili. Kumekuwa na hali ya wasiwasi nchini Sudan baada ya kuzuka tofauti kati ya Sudan Kusini na Sudan Kaskazini juu ya utaratibu wa kufanyika kura hii lakini makundi hayo yanaarifiwa kufikia mwafaka wa kutatua tofauti zao.

Chini ya mwafaka huu suala la jimbo linalozozaniwa la Abyei litatatuliwa na Rais wa Sudan na mwenzake wa Sudan Kusini. Hata hivyo vyombo vya habari vimeendelea kuripoti kuwa kura ya maoni iko shakani kutokana na kutoafikiwa kwa muafaka wa jimbo hilo la Abyei lenye utajiri wa mafuta.

Lakini imeafikiwa kwamba iwapo Sudan Kusini itaamua kujitawala kama taifa huru mipaka kati ya nchi hizo mbili isifungwe na masuala ya uraia yakubaliwe kati ya mataifa hayo mawili. Tangazo hili huenda likasaidia sana kupunguza uhasama kati ya pande hizo mbili ambao umedhihirika kabla ya kura hiyo kufanyika Januari mwakani.

Sudan Kusini inakisiwa kuwa na wapiga kura milioni tano na ni dhahiri kwamba raia hao watapiga kura ya uhuru wa taifa lao kujitenga. Watu wa eneo la Kusini wengi wao ni Wakristo na watu wa imani za kijadi na wakazi wa eneo la Kaskazini wengi wao ni Waislamu na Waarabu.

Umoja wa Mataifa unazingatia kuongeza vikosi vya kulinda amani katika mpaka wa Sudan Kaskazini na Kusini, wakati nchi hiyo ikijiandaa kupiga kura ya maoni kwa ajili ya kujitenga kwa eneo la Kusini.

Akizungumza katika baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Alain LeRoy alisema kuwa wanapanga kuhamisha vikosi kutoka maeneo mengine ya Sudan na kuvipeleka katika eneo hilo la mpaka, huku akitoa wito pia wa jeshi hilo kuongezewa nguvu kimataifa.

Imefahamishwa kuwa Umoja wa Mataifa unalenga kuisaidia Sudan kutayarisha na kutoa ulinzi kwa ajili ya kura hiyo juu ya kugawanywa kwa Sudan na kuwa mataifa mawili ya Sudan Kusini na Sudan Kaskazini.

Kura ya maoni nchini Sudan Kusini na katika jimbo la Abyei ni sehemu ya makubaliano ya amani yaliyofikiwa mwaka 2005 kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu nchini humo, takriban miongo miwili na kusababisha vifo vya watu zaidi ya milioni mbili.

Kwa upande wake, Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Suzan Rice amesema kuna uwezekano kwa muda kuongeza wanajeshi 10,000. Hatua ambayo mkuu wa Operesheni za kulinda amani za Umoja wa Mataifa ameona kwamba haitasaidia.

Alain LeRoy alisema hata kama jeshi hilo la Umoja wa Mataifa nchini Sudan litaongezewa nguvu hakutaweza kuzuia uhasama kati ya Kaskazini na Kusini, iwapo hali ya wasiwasi juu ya kura ya maoni ikiwa bado ipo.
Aliwaambia wajumbe kutoka mataifa 15 wanachama katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba njia nzuri iliyopo kuweza kuzuia kurudia tena kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo ni kujidhatiti ili kufikia makubaliano ya kisiasa katika kutekeleza masuala muhimu yaliyobakia.

Kwa upande wake, Balozi wa Sudan katika Umoja wa Mataifa Daffa-Alla Elhag Ali Osman ameonya kwamba hatua hiyo ya kukiimarisha kikosi hicho cha UNMIS inaweza kuwa ushauri mbaya. Aliwaambia waandishi wa habari ni muhimu kwanza kufikia makubaliano juu ya masuala ya kisiasa ambayo bado hayajapatiwa ufumbuzi, kama vile suala la mpaka.

Hali ya wasiwasi imeongezeka katika kipindi hiki, kwa pande zote mbili za Kusini na Kaskazini kulaumiana, huku kila upande ukiimarisha majeshi yake katika mpaka wa Kaskazini na Kusini.

Katika hatua nyingine Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki moon ameelezea wasiwasi wake na hali ilivyo katika jimbo lenye utajiri wa mafuta la Abyei. Hakuna tume yoyote inayoshughulikia kura ya maoni iliyotumwa na viongozi katika eneo hilo bado hawajafikia makubaliano na serikali ya Khartoum juu ya nani anafaa kupiga kura au mipaka yake.

Habazi zinabainisha kwamba, Jumuiya ya kimataifa bado ina wasiwasi na matokeo ya kura ya maoni itakayopigwa, kutokana na wasiwasi kwamba, inaweza kuzua vita vingine kama matokeo yatakuwa kinyume na matazamio ya wengi.

Lakini ili amani ya kweli iwepo njia pekee ni kutenganisha tamaduni hizi mbili, ambazo daima zimekuwa zikipingana kwa kipindi kirefu na kusababisha maafa makubwa kwa jamii ya Wasudan hasa watu wa eneo la Kusini.

SALVA KIIR NI NANI HASA?
Salva Kiir Mayardit amezaliwa mwaka 1951. Alichukua nafasi ya kiongozi wa Kusini na naibu kiongozi wa taifa baada ya kifo cha John Garang aliyekufa katika ajali ya helikopta Agosti 2005 - wiki tatu tu baada ya kuapishwa kuwa Makamu wa Rais. Kiir anapenda kuvaa kofia ya cowboy ambayo imekuwa ndiyo nembo yake maalum.

Ingawa Kiir amekuwa makamu wa rais wa Sudan kwa miaka mitano, lakini ametumia zaidi muda wake akiwa Kusini - hali inayoonesha dalili zote kuwa lengo lake siku zote lilikuwa kuipatia uhuru Sudan Kusini.

Mwaka 2009, alielezea hisia zake waziwazi, akisema: “Kura ya maoni ijayo ni uchaguzi kati ya kuwa raia wa daraja la pili katika nchi yako mwenyewe, au kuwa mtu huru katika hali yako ya kujitegemea”.

Kama ilivyo kwa wananchi wengi wa Kusini, Kiir alipiga kura kwa mara ya kwanza mwaka 2010. Kiir kwa kawaida huwa si msemaji sana mbele ya umma na amekuwa akiongoza kupitia kivuli cha Garang. Lakini alikuwa mtu muhimu kwa watu wake na alikuwa kiongozi wa kijeshi wa kundi la waasi wa kusini, Sudan People's Liberation Movement (SPLM).

Alihusika katika hatua za mwanzo za mazungumzo ya mpango wa amani mwaka 2005 - yaliyomaliza miaka 21 ya vita vya wenyewe kwa wenyewe - na alikuwa anajulikana kwa serikali ya Khartoum kabla ya kuwa makamu wa rais kama sehemu ya mpango huo.

Kiir alijiunga na harakati za waasi kusini mwa Sudan mwishoni mwa 1960. Wakati Rais Jaafar Numeiri akifanya mazungumzo ya amani na waasi mwaka 1972, Kiir aliibuka na kuwa afisa wa cheo cha chini.

Mwaka 1983 uasi Kusini uliibuka upya na Garang alitumwa kukomesha uasi huo - lakini badala ya kukomesha, alijiunga nao. Kiir alikuwa, pamoja na Garang, mmoja wa waanzilishi wa SPLM, na kuibuka kuwa kiongozi wa tawi la kijeshi.

Tofauti na mtangulizi wake, Kiir hajaenda shule na inasemwa kuwa hotuba zake za muda mrefu huwa zinachosha. Kiir pia anatoka katika jamii ya Dinka kama ilivyokuwa kwa Garang, ingawa wawili hao wanatoka koo tofauti.

Kutokana na kwamba kabila la Dinka ni kubwa Kusini mwa Sudan, Kiir anatarajia kupata sapoti kubwa katika eneo la Kusini. Jaribio la kutaka kumuondoa Kiir kwenye nafasi yake ya mkuu wa jeshi karibu zisababishe mgawanyiko mkubwa ndani ya SPLM mwaka 2004. Tatizo liliisha pale tu Garang alipobatilisha wazo hilo.

Kama mwanaharakati wa zamani wa waasi, SPLM ya Kiir bado inapaswa kuonesha kwamba iko tayari kukubali upinzani. Uchaguzi Kusini mwa Sudan uligubikwa na madai ya vitisho dhidi ya wale walioonekana kuwapinga wagombea wa SPLM. Hii ilizua hofu kwamba “Sudan Mpya”, kama inavyoitwa wakati mwingine, inaweza isiwe nchi ya kidemokrasia.

Taarifa za mwezi Januari 2010 kwamba Kiir hatagombea uchaguzi wa Aprili wa rais wa Sudan, lakini atazingatia zaidi uchaguzi wa rais wa Sudan Kusini ilitafsiriwa kwa maana ya kwamba kipaumbele cha SPLM ni uhuru wa Sudan Kusini.

Kiir alichaguliwa kwa asilimia 93 ya kura katika uchaguzi wa 2010. Ingawa chaguzi zote katika ngazi ya kitaifa na kanda zilikosolewa mno na wanaharakati wa kidemokrasia na waangalizi wa kimataifa, kuchaguliwa tena kwa Kiir ilibainishwa na baadhi ya vyombo vya habari kuwa “Hatua Moja” muhimu katika mchakato.

Kufuatia kuchaguliwa tena, Omar al-Bashir alimteua tena Kiir kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Sudan kwa mujibu wa katiba ya mpito. Katika hotuba yake aliyoitoa mjini Juba, Kiir aliahidi demokrasia, usawa na haki kwa watu wote wa Kusini mwa Sudan. Mashoga, hata hivyo, hawatakubalika katika nchi hiyo mpya, alisema. “Hii si katika tabia zetu [...] haipo na kama mtu yeyote anataka kuiingiza Sudan [...] itapingwa na kila mtu,” aliiambia Radio Netherlands Worldwide.

Makala hii imeandaliwa na BISHOP J. HILUKA kwa msaada wa vyombo mbalimbali vya kimataifa.

SOURCE: KULIKONI

No comments:

Post a Comment