Aung San Suu Kyi
KIONGOZI anayetetea sera za
kidemokrasia nchini Myanmar (zamani ilijulikana kama Burma ), Aung San Suu Kyi, amekubali kuapishwa pamoja na
wabunge wa chama chake na hivyo kumaliza mzozo wa kisiasa uliokuwepo. Suu Kyi
amesema uamuzi wake umetokana na matakwa ya raia ambao wanamtaka kuingia
bungeni.
Chama chake cha NLD
kilisusia kuapishwa kutokana na maandishi kwenye kiapo hicho. Kiapo kilichozua
utata kinawataka wabunge kuapa kulinda katiba ambayo iliandikwa chini ya
utawala wa kijeshi. Wabunge wapya wanatarajiwa kuanza vikao vyao wiki hii.
Hali hiyo imemfanya Katibu
Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon kuyataka mataifa ya Magharibi kulegeza
zaidi vikwazo vyao dhidi ya Myanmar ikiwa njia bora ya kuunga mkono mabadiliko ya
kidemokrasia katika taifa hilo
la kusini mwa Asia .
Katibu Mkuu huyo
amezungumza hayo alipolihutubia bunge la nchi hiyo wiki hii, sehemu ya ziara
yake ya siku tatu nchini Myanmar . Hotuba hiyo aliitoa baada ya mazungumzo yake na
Rais Thein Sein.
Pamoja na Umoja wa Mataifa
kufanikiwa kutuma ujumbe wake wa usaidizi katika eneo hilo hivi karibuni lakini bado watu wengi wameendelea
kuishi katika mkwamo mkubwa huku hali hiyo ikitabiriwa huenda ikawa mbaya zaidi.
Sambamba na yanayotokea
sasa Mwanadiplomasia wa ngazi ya juu kabisa katika Umoja wa Ulaya Catherine
Ashton nae yupo Myanmar kwa ajili ya mazungumzo na rais wa taifa hilo baada ya
umoja huo kusimamisha vikwazo vyake dhidi ya taifa hilo .
Historia yake
Aung San Suu Kyi alizaliwa
Juni 19, 1945, ni mwanasiasa, kiongozi wa upinzani na Katibu Mkuu wa National
League for Democracy (NLD) nchini Myanmar . Katika uchaguzi mkuu wa 1990, NLD kilishinda kwa
asilimia 59 ya kura za kitaifa na asilimia 81 (392 kati ya 485) za viti katika
Bunge. Hata hivyo, tayari alikuwa kawekwa kizuizini nyumbani kabla ya
uchaguzi. Alibaki kizuizini nchini Myanmar kwa karibu miaka 15 kati ya 21 kuanzia 20 Julai
1989 hadi kutolewa kwake miaka ya karibuni mnamo Novemba 13, 2010, na kuwa
mmoja wa wafungwa wa kisiasa maarufu zaidi.
Suu Kyi alipokea Tuzo ya Rafto
na Tuzo ya Sakharov mwaka 1990 na Tuzo ya Amani ya Nobel mwaka 1991. Mwaka 1992
alituzwa Tuzo ya Jawaharlal Nehru na serikali ya India na Tuzo ya Kimataifa ya Simón Bolívar kutoka
serikali ya Venezuela . Mwaka 2007, Serikali ya Canada ilimfanya kuwa raia wa heshima wa nchi hiyo, kwa wakati
huo, alikuwa mmoja wa watu wanne tu waliopokea heshima hiyo. Mwaka 2011, alitunukiwa
tuzo ya medali ya Wallenberg.
Aprili 1, 2012, chame chake
cha upinzani, NLD, kilitangaza kuwa alichaguliwa kwenye Pyithu Hluttaw, bunge
la Myanmar, kuwakilisha jimbo la Kawhmu; chama chake pia kilishinda viti 43 kati
ya 45 katika bunge hilo. Matokeo ya uchaguzi yalithibitishwa na tume rasmi ya
uchaguzi siku iliyofuata.
Suu Kyi ni mtoto wa tatu na
wa kike pekee wa Aung San, anayeonekana kuwa baba wa kisasa wa Myanmar .
Aung San Suu Kyi alipata
jina lake kutoka kwa ndugu watatu: "Aung San" kutoka kwa baba yake, "Suu"
kutoka kwa bibi yake upande wa baba na "Kyi" kutoka kwa mama yake,
Khin Kyi. Mara nyingi huitwa Daw Aung San Suu Kyi. Daw si sehemu ya jina lake,
lakini ni jina la kiheshima, sawa na madame, kwa ajili ya wanawake watu wazima,
wanaoheshimiwa, maana halisi ya "shangazi."
Suu Kyi alizaliwa eneo la Rangoon (sasa linaitwa Yangon ). Baba yake, Aung San, alianzisha jeshi la kisasa la Myanmar na aliongoza mazungumzo ya uhuru wa Burma (sasa Myanmar ) kutoka milki ya Uingereza mwaka 1947; aliuawa na
wapinzani wake mwaka huo. Suu Kyi alikulia kwa mama yake, Khin Kyi, akiwa na
kaka zake wawili, Aung San Lin na Aung San Oo, eneo la Rangoon. Aung San Lin
alikufa akiwa na umri wa miaka nane, alipozama ziwani. Kaka yake mkubwa alihamia
San Diego , California , na kuwa raia wa Marekani. Baada ya kifo cha Aung
San Lin, familia ilihamia nyumba ya Ziwa Inya ambapo Suu Kyi alikutana na watu
wa asili tofauti sana , wenye maoni ya kisiasa na dini. Alipata elimu
katika Shule ya Kiingereza ya Methodist kwa muda mwingi wa utoto wake nchini Burma , ambako alibainisha kuwa na kipaji cha kujifunza
lugha. Ni Mbuddha. .
Mama yake, Khin Kyi,
alipata umaarufu kama mtu muhimu wa kisiasa katika serikali mpya ya Burma . Aliteuliwa kuwa balozi wa Burma nchini India na Nepal mwaka 1960, na Suu Kyi alimfuata huko, alisoma
katika Shule ya Convent ya Yesu na Maria, New Delhi na kuhitimu shahada ya siasa katika Chuo cha Lady
Shri Ram mjini New
Delhi mwaka
1964. Suu Kyi aliendelea na elimu yake katika Chuo cha St Hugh, Oxford , na kupata shahada katika Falsafa, Siasa na Uchumi
mwaka 1969. Baada ya kufuzu, aliishi mjini New York kwenye familia rafiki na kufanya kazi katika Umoja
wa Mataifa kwa miaka mitatu, hasa juu ya masuala ya bajeti. Mwaka wa 1972, Aung
San Suu Kyi alifunga ndoa na Dr Michael Aris, msomi wa utamaduni wa Tibet , aliyeishi nje ya nchi huko Bhutan . Mwaka uliofuata alijifungua mtoto wao wa kwanza,
Alexander Aris, jijini London ;
mtoto wao wa pili, Kim, alizaliwa mwaka 1977. Baadaye Suu Kyi alipata shahada
ya uzamivu (PhD) katika Shule ya Oriental and African Studies, Chuo Kikuu cha London mwaka 1985.
Mwaka 1988 Suu Kyi alirudi Burma , kwa mara ya kwanza na kwa mama yake aliyekuwa mgonjwa
lakini baadaye akaongoza harakati za demokrasia. Ziara ya Aris kwenye Krismasi
1995 iligeuka kuwa mara ya mwisho kwake na Suu Kyi kuonana, Suu Kyi alibakia Burma na uongozi wa kidikteta wa Burma ulikataa kumpa Aris hati ya kuingia tena nchini
humo. Aris aligundulika kuwa na saratani ya kibofu mwaka 1997 iliyoonekana
baadaye kuwa mwisho. Licha ya kuomba msaada kutoka watu maarufu na mashirika,
ikiwa ni pamoja na Marekani, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan na
Papa Yohane Paulo II, serikali ya Burma haikumpatia Aris hati ya kuingia nchini humo, ikisema
kuwa hawakuwa na vifaa vya kumhudumia, na badala yake ilimtaka Aung San Suu Kyi
kuondoka nchini akamtembelee. Kwa wakati huo alikuwa huru kwa muda kutoka
kizuizi cha nyumbani lakini alishindwa kuondoka kwa kuogopa angeweza kukataliwa
kurudi akiondoka, hakuwa na imani na serikali hiyo ya kijeshi.
Aris alifariki siku yake ya
kuzaliwa tarehe 27 Machi 1999, akiwa na miaka 53. Tangu mwaka 1989, mke wake alipowekwa
kizuizini nyumbani kwake, alikuwa ameona mara tano tu, ya mwisho ikiwa ni siku
ya Krismasi mwaka 1995. Suu Kyi pia alitenganishwa na watoto wake, ambao
wanaishi nchini Uingereza, lakini kuanzia mwaka 2011, wamekuwa wakimtembelea nchini
Burma .
Akipata msukumo kutoka kwa falsafa
ya Mahatma Gandhi ya siasa zisizo za vurugu na hasa dhana ya Kibuddha, Aung San
Suu Kyi aliingia kwenye siasa kusaka demokrasia, alisaidia kupatikana kwa chama
cha NLD Septemba 27, 1988, lakini aliwekwa kizuizi cha nyumbani tarehe 20 Julai
1989. alipewa sharti la kuachiwa uhuru kama ataondoka nchini humo, lakini alikataa.
Makala haya yameandaliwa na Bishop Hiluka kwa msaada
wa vyanzo mbalimbali vya habari vya kimataifa.
No comments:
Post a Comment