Al-Saadi al-Gaddafi
NIAMEY
Niger
WAZIRI wa Masuala ya Haki wa Niger, Marou Amadou, amethibitisha kuwa Saadi Gaddafi aliyesemekana kuwemo katika msafara ulioelekea mji mkuu wa Niger, Niamey, kuwa yupo nchini humo. Lakini hadi sasa haijulikani Gaddafi mwenyewe yuko wapi.
Hadi sasa wapiganaji wanaokabiliana na vikosi vya Gaddafi sasa wanadhibiti maeneo mengi nchini Libya, ukiwemo mji mkuu Tripoli, na wamekuwa wakijaribu kuchukua udhibiti wa miji mingine, iliyo chini ya wanaomuunga mkono Gaddafi, ikiwemo miji ya Bani Walid na Sirte.
Jumapili ya wiki iliyopita vikosi vya waasi vilianza mashambulio katika mji wa Bani Walid, vikisaidiwa na mashambulio ya angani ya Nato. Maafisa wamesema vikosi vyao sasa viko karibu kufika katikati mwa mji wa Bani Walid.
Baadhi ya watu wa jamii ya Gaddafi wamekimbilia Algeria. Misafara kadhaa ya watu waliokuwa wakimuunga mkono Gaddafi imeonekana ikivuka mpaka wa Kusini mwa Libya na kuingia Niger hivi karibuni.
Msemaji wa serikali ya Niger na waziri wa masuala ya haki amesema kuwa Saadi Gaddafi alikuwa kwenye msafara huo na watu wengine wanane. Msemaji huyo anasema kuwa msafara huo ulikuwa njiani kuelekea Agadez Kaskazini mwa Niger na kwamba Saadi pamoja na alioandamana nao waliruhusiwa kuingia kwa kuzingatia misingi ya kibinaadamu.
Serikali ya Niger inautambua utawala wa Baraza la Kitaifa la Mpito la Libya, lakini ikasema bado hawajaamua kama watamruhusu Gaddafi kuingia nchini humo. Hata hivyo msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani amesema, serikali ya Niger imethibitisha kuwa itamweka mbaroni mtoto huyo wa Muammar Gaddafi, Saadi al Gaddafi.
Amesema ingawa Saadi hayupo kwenye orodha ya watu waliowekewa vizuizi vya azimio Na. 1970 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, lakini serikali ya Niger imeliarifu Baraza la Mpito la Taifa la Libya kuwa itashirikiana na baraza hilo katika kushughulikia suala la maofisa wa utawala wa Gaddafi wanaoingia nchini humo.
Waziri mkuu wa Niger aliwaambia waandishi wa habari kuwa, maofisa 32 wa utawala wa Muammar Gaddafi, akiwemo mtoto wake Saadi wamekwishaingia nchini Niger kwa nyakati tofauti kuanzia tarehe 2 mwezi huu.
Historia yake
Al-Saadi al-Gaddafi alizaliwa Mei 25, 1973, ni mtoto wa tatu wa Muammar al-Gaddafi. Saadi alikuwa mfanyabiashara wa Libya na mchezaji wa zamani wa mpira wa miguu. Pia alikuwa kamanda wa vikosi Maalum vya Libya na ameshiriki katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vya 2011 nchini Libya.
Taarifa ya Interpol (orange notice) imetolewa dhidi yake. Yeye ni sehemu ya baraza muhimu la baba yake. Mnamo 11 Septemba 2011, al-Saadi alikimbilia nchi hiyo jirani ya Niger, ambapo serikali imeamua kumpeleka kwenye mji mkuu wa Niamey na kumshikilia. Saadi amefunga ndoa na binti wa kamanda wa kijeshi wa Libya.
Saadi alicheza soka nchini Libya akiichezea timu ya Al Ahly ya Tripoli. Mnamo Juni 6, 2000, taarifa za BBC zilisema kwamba Saadi alikuwa na mkataba na mabingwa Maltese Birkirkara FC na alipaswa kuichezea timu hiyo katika Ligi ya Mabingwa. Lakini walishindwa kuafikiana.
Soka la Libya lilikuwa la upendeleo kwa Saadi. Moja ya sheria zilikataza kutangaza jina la mchezaji yeyote wa mpira wa miguu isipokuwa Saadi. Ni namba tu za wachezaji wengine zilizotangazwa badala ya majina yao. Waamuzi pia waliipendelea timu ya Saadi na vikosi vya usalama vilitumika kuzima maandamano yoyote dhidi ya timu hiyo.
Saadi aliingia mkataba na timu ya Perugia ya Italia inayoshiriki ligi kuu nchini humo (Serie A) mwaka 2003, ambapo aliichezea timu hiyo mechi moja tu kabla ya kushindwa kupima vipimo kwa ajili ya dawa za kulevya. Aliwahi kuwa kwenye bodi ya timu ya Juventus ya Italia, ambapo asilimia 7.5 ya hisa za timu inamilikiwa na muungano wa Libya, lakini aliamua kutojiunga tena na Perugia.
Pia alikuwa nahodha wa timu ya taifa ya kandanda ya Libya, nahodha wa klabu yake ya jijini Tripoli, na Rais wa Shirikisho la Soka la Libya.
Saadi alijiunga na timu iliyofuzu kucheza ligi ya mabingwa Ulaya mwaka 2005-06, Udinese Calcio, alicheza dakika kumi tu katika mechi ya mwisho wa msimu wa ligi dhidi ya Cagliari Calcio. Kisha alijiunga UC Sampdoria wakati wa msimu wa 2006-07, bila ya kucheza mechi hata moja.
Mwaka 2006, Saadi na Serikali ya Libya walizindua mradi wa kujenga mji eneo litakalokuwa na uhuru nusu mfano wa Hong Kong nchini Libya, likisambaa kilomita 40 kati ya mpaka wa Tripoli na Tunisia. Mji huo mpya ungejengwa kwa kutumia teknolojia ya hali ya juu, huku huduma za kibenki, vituo vya afya na elimu vikiwa havihitaji visa kuingia katika mji huo mpya.
Mji huo ungekuwa na uwanja wake wa ndege wa kimataifa na bandari kuu. Saadi aliahidi kuwepo uvumilivu wa kidini kwa wote; “masinagogi na makanisa” na hakutakuwa na ubaguzi katika mji huo mpya. Mji huo mpya ungekuwa na sheria za biashara za “Kimagharibi” alizodhani kuwa makampuni ya Ulaya na Marekani yangevutiwa kuwekeza biashara.
Saadi pia alichukua riba kubwa katika biashara nyingine nchini Libya ikiwemo kampuni ya Tamoil, ambayo ni kampuni ya kusafisha mafuta na masoko inayomilikiwa na serikali ya Libya. Saadi pia amewahi kuwa mdau na mkurugenzi mtendaji katika kampuni ya asili ya Los Angeles.
Mnamo Julai 2010, Saadi alitakiwa na mahakama ya Italia kuilipa Euro 392,000 hoteli ya kisasa yenye anasa nyingi ya Ligurian kama fidia ya kutolipa bili kwa kukodi mwezi mzima kabla ya muda mrefu aliokaa wakati wa majira ya joto ya 2007.
Vita vya wenyewe kwa wenyewe Libya
Mnamo 15 Machi, kulikuwa na taarifa ambazo hazikuthibitishwa kwamba rubani aliyejulikana kwa jina la Muhammad Mokhtar Osman, aliishambuliwa ngome ya Gaddafi ya Bab al-Azizia mjini Tripoli na kuharibu na pia kumjeruhi Saadi na ndugu yake, Khamis al-Gaddafi.
Akiongea na Shirika la Habari la Uingereza, BBC, askari wa Libya alidai kuwa Saadi mwenyewe aliamrisha kupigwa risasi kwa waandamanaji wasiokuwa na silaha katika mji wa Benghazi wakati alipotembelea kambi ya jeshi ya mji huo mwanzoni wa uasi. Saadi alithibitisha kuwepo katika kambi hiyo lakini alikanusha kutoa amri ya kuwashambulia waandamanaji.
Saadi alikuwa na nguvu kubwa katika mabadiliko ya majeshi ya serikali ya Libya na mbinu walizotumia. Badala ya kupambana na waasi kwa silaha nzito, mizinga na magari ya kivita - ambayo ingeweza kwa urahisi kujulikana na waasi na kisha kuharibiwa na ndege za kivita - vita dhidi ya waasi ilipiganwa katika vipande vidogovidogo, kwa haraka na uhodari.
Waasi hao walidai kumteka Saadi wakati wa vita ya Tripoli, mnamo 21 Agosti, lakini baadaye ikasemekana kuwa ulikuwa ni uongo.
Baada ya jumba la Saadi kutekwa na vikosi vya waasi wakati wa vita, ilitangazwa kupatikana DVD yenye picha za uchi za mashoga iliyoandikwa “Boyz Tracks” ikiwa miongoni mwa nyaraka katika ofisi ya jumba lake.
Agosti 24, Saadi aliwasiliana na CNN, na kusema kuwa alikuwa na mamlaka ya kujadili kwa niaba ya vikosi vya Gaddafi, na alitaka kujadili namna ya kusitisha mapigano na serikali ya Marekani na Nato. 31 Agosti, Saadi aliwasiliana na Al Arabiya, na kusema kwamba baba yake alikuwa tayari kujiuzulu, na kuomba mazungumzo na Baraza la Taifa la Mpito.
5 Septemba, alisema katika mahojiano na CNN kwamba hotuba ya jazba ya ndugu yake, Saif al-Islam, ilisababisha kuvunjika kwa mazungumzo kati ya vikosi vya Baraza la Taifa la Mpito na wafuasi wa Gaddafi katika eneo la Bani Walid, na alisema hajaonana na baba yake katika kipindi cha miezi miwili. Pia alidai kuwa msimamo wake ni kutoegemea upande wowote katika mgogoro na kutolewa kwa upatanisho.
11 Septemba, Saadi alikimbilia nchini Niger na aliruhusiwa kuingia kwa mujibu wa misingi ya kibinadamu. Kulingana na serikali ya Niger, wanapanga kumshikilia Saadi wakati wakifikiria nini cha kumfanya.
Makala hii imeandaliwa na Bishop J. Hiluka kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya habari vya kimataifa.
No comments:
Post a Comment