VITAL Kamerhe, mwenye umri wa miaka 52, aliwahi kuwa mshirika wa rais wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Joseph Kabila, lakini sasa yuko upande wa upinzani. Akiwa mmoja wa waasisi wa chama cha PPRD cha Kabila, Kamerhe aliongoza kampeni za urais mwaka 2006 za Kabila.
Baadaye Kamerhe alikuwa spika wa bunge, hadi alipozozana na rais Kabila kuhusiana na makubaliano ya siri na rais ya kuruhusu Rwanda kupeleka wanajeshi wake Mashariki mwa nchi kuwasaka waasi mapema mwaka 2009.
Kamerhe ni mzaliwa wa upande wa Mashariki katika mkoa wa Kivu, na alijitoa serikalini na kuanzisha chama chake cha UNC. Vital Kamerhe ni mwanasiasa na msomi anayezungumza vyema Kifaransa na Kiingereza, pamoja na lugha rasmi nne za Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.
Amekuwa akijiuza kwa wapiga kura wake - kama mfano - kwa kujifananisha na rais wa zamani wa Brazil, Ignacio Lula da Silva.
"Nina uhakika kuwa eneo letu kijiografia na rasilimali, DRC kwa sasa ni kama tembo aliyelala, na ataamka kama Brazil," alisema.
Wakati wa kampeni za uchaguzi wa rais wa mwaka huu mtindo wake wa kufanya kampeni ulikuwa ni wa kiubunifu, alifanya mikutano katika maeneo wanayoishi watu maskini na kufanya mihadhara ya majadiliano ambapo watu walikuwa huru kumuuliza maswali moja kwa moja.
Lakini wafuasi wengi wa upinzani bado wanamuona kama mtu aliye karibu sana na Rais Kabila, ingawa alikuwa mmoja wa wagombea waliokuwa wakichuana na rais Kabila.
Historia yake
Vital Kamerhe Lwa Kanyiginyi Nkingi amezaliwa 1959, ni mwanasiasa wa Kongo. Spika wa zamani wa Bunge la Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo na Waziri wa Habari, kwa sasa bado ni rais wa heshima wa Bunge la Taifa, mwanzilishi na kiongozi wa chama cha UNC (Union pour la Nation Congolaise) na alikuwa mgombea katika uchaguzi wa urais mwaka huu katika DRC.
Maisha ya awali na elimu
Alizaliwa katika eneo la Bukavu, Sud-Kivu, mnamo Machi 4, 1959, Vital Kamerhe ni mtoto wa Constantine Kamerhe Kanyginyi na Alphonsine Mwa Nkingi. Asili yake ni kutoka jamii ya Shi ya utawala wa Walungu, ameoa na ni baba wa watoto 9.
Alianza elimu yake katika shule ya msingi katika eneo la Bukavu na kisha katika eneo la Goma. Kisha akaendelea na elimu yake huko Kasai, katika Gandajika, ambako alimaliza shule ya msingi. Miaka ya shule 1975 hadi 1976 na 1976 hadi 1977, alihudhuria katika Chuo cha Sadisana (zamani kikijulikana kama Chuo cha St Francois-Xavier) katika eneo la Kikwit Sacré-Coeur, mkoa wa Bandundu. Baadaye alihamia Kananga (Mkoa wa Kasai) na hatimaye, baada ya mwaka mmoja, alihamia Mbuji-Mayi ambako alipata shahada yake mwaka 1980 (Institut Mulemba). Uzoefu huu ulimuongoza kujifunza lugha zote nne ya taifa la Kongo yaani Kikongo, Lingala, Kiswahili na Tshiluba. Vilevile anazungumza kwa ufasaha Kifaransa.
Kutoka hapo yalimalizia masomo yake katika Chuo Kikuu cha Kinshasa, ambapo alipata shahada yake katika Uchumi mwaka 1987. Aliamua kukaa hapo kama mkufunzi msaidizi.
Kazi ya siasa
Wakati wa utawala wa Mobutu:
Kamerhe ilianza kazi yake ya kisiasa mwaka 1984 akiwa na chama cha UDPS (Union pour la Démocratie et le Progrès Social). Katika kipindi cha mpito cha kidemokrasia wakati wa utawala wa Mobutu, alikuwa mwanachama wa RSF (Rassemblement des forces Sociales et Federalistes) cha Vincent de Paul Lunda Bululu na pia alikuwa rais wa Jeunesse de l'Union Sacrée de l'opposition Radicale et Alliés (JUSORAL), jumuia ya vijana ya chama cha upinzani. Kati ya 1993 na 1995 alifanya kazi kadhaa za umma:
1993: Mkurugenzi wa Baraza la Mawaziri wa Wizara ya Mazingira, Utalii
1994: Mratibu wa Baraza la Mawaziri la Waziri Mkuu
1994-1995: Mkurugenzi wa Baraza la Mawaziri kwa Waziri wa Elimu ya Juu na Chuo Kikuu, Mushobekwa Kalimba wa Katana, mwanachama wa RSF ya Lunda Bululu.
Kuna baadhi ya utata juu yake kama aliwahi kuwa mwanachama wa jumuia ya vijana wa Mobutu (Frojemo), iliyoongozwa na Jenerali Etienne Nzimbi Ngbale Kongo wa Basa, ukweli ambao mpinzani wake mara nyingi huutumia kumdhoofisha.
Wakati wa utawala wa Kabila:
Wakati wa utawala wa Laurent Kabila, Kamerhe alikuwa naibu mkuu wa wafanyakazi wa Etienne-Richard Mbaya, waziri wa ujenzi, kisha:
Kuanzia 1997 hadi 1998: Mkurugenzi wa Jeshi la Kujenga Taifa (huduma ya nusu-kijeshi zilizoanzishwa na Laurent Kabila)
Mwaka 1998: Kansela wa Fedha katika Wizara ya Ulinzi wa Taifa, akiwa na Jenerali Denis Kalume, na hatimaye kuwa naibu kamishina mkuu wa mambo ya MONUC.
Nafasi katika mchakato wa amani ya kanda ya Maziwa Makuu
Ni mwanachama mwanzilishi wa chama cha PPRD mwaka 2002, Vital Kamerhe alikuwa mmoja wa viongozi walioongoza katika mchakato wa amani katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, hata akapachikwa jina la utani “le Pacificateur”, yaani “mpatanishi”. Akiwa Kamishna Mkuu wa Serikali mwenye dhamana ya kufuatilia mchakato wa amani katika kanda ya Maziwa Makuu, alikuwa ni mmoja wa wazungumzaji wakuu wa mpango wa amani 2002. Mwaka 2003, aliteuliwa kuwa Waziri wa Habari na Maelezo katika serikali ya mpito.
Nafasi katika Kampeni ya Uchaguzi Mkuu wa 2006
Mwezi Julai 2004, alichukua uongozi wa PPRD na kuandaa kampeni za uchaguzi za Joseph Kabila, ambapo alipata sifa kubwa mno. Alichaguliwa kuwa mbunge wa Bukavu na kupata alama ya juu nchini humo na mnamo Desemba 29, 2006 alichaguliwa kuwa rais wa Bunge.
Maendeleo ya hivi karibuni
Mwaka 2009, akiwa rais wa Bunge alimhoji rais Joseph Kabila na chama chake mwenyewe kuhusu shughuli za ‘Umoja Wetu’ ambazo zimesababisha askari elfu kadhaa wa Rwanda kupelekwa ndani ya Kongo bila kulitaarifu bunge. Januari 21, 2009, alitoa taarifa kwenye Radio Okapi akieleza masikitiko yake kuhusu shughuli ya pamoja ya kijeshi kati ya jeshi la Kongo na Rwanda katika eneo la Kivu, iliyofanywa bila kulitaarifu Bunge na Seneti na hivyo kukiuka kifungu cha 213 cha katiba.
Tarehe 25 Machi, 2009, alitangaza kujiuzulu nafasi ya Rais wa Bunge. Mnamo Desemba 14, 2010, Kamerhe alijiuzulu rasmi uanachama wa PPRD na kutangaza kugombea katika uchaguzi wa rais wa 2011 na kuunda chama chake kipya, UNC, ambacho kilizinduliwa rasmi mnamo Februari 2011.
Makala haya yameandaliwa na Bishop Hiluka kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya habari vya kimataifa
No comments:
Post a Comment