Mitambo ya Dowans
Rostam Aziz
BISHOP J. HILUKA
Dar es Salaam
NAKUMBUKA enzi zile tukiwa bado wadogo kabla ya kuenea hizi televisheni zilizozagaa kila mahali tulipenda sana kwenda kuangalia sinema za Kihindi kwenye majumba ya sinema kwa sababu zilikuwa ni ndefu tofauti na sinema zingine, yaani unaangalia na unapata uhondo mwingi: vionjo vingi, unaburudika zaidi na unaona thamani ya pesa uliyotoa ikilingana na kiburudisho unachopata.
Bado nazikumbuka enzi hizo za kina Amitabh Bachchan, Rishi Kapoor, Vinod Khanna, Danny Denzongpa, Mithun Chakraboti, Govinda, Sunjey Dati, Rajesh Khanna, Ramesh Deo, Sumitra na wengine wengi. Sinema zilizotamba enzi hizo ni kama Namak Halal, Disco Dancer, Andhaa Kanoon, Sholay, Kasam Paida Karne Wale Ki, Nastik na nyinginezo. Kwa kweli kipindi hicho ilikuwa unaangalia sinema mpaka unachoka lakini haiishi hamu.
Uhondo ule wa sinema za Kihindi sasa hivi umehamia kwenye tamthilia zilizojizolea umaarufu mkubwa za 'Prison Break', 'Twenty Four Hours' na 'The Unit' ambazo zimeonekana kutishia uhondo wa picha ndefu za Kihindi.
Hapa Tanzania wasanii mbalimbali wamejitokeza kutengeneza sinema nyingi na kuzilazimisha ziwe ndefu mfano wa zile za Kihindi kwa mfumo wa 'Part 1 na 2', na kuishia kutuondolea uhondo tuliokuwa tukiupata kwenye sinema za Kihindi ambao nikiri kuwa haukuwa na mfano wake. Hizi za kwetu za part 1 na 2 zimeshindwa kabisa kukidhi matarajio ya watazamaji kwa kuwa hadithi na visa vinaboa kabla hata sinema haijafika nusu.
Lakini kuna kundi fulani limeamua kuja na sinema kabambe ambayo ilianzia kwenye igizo dogo lenye maudhui ya vita dhidi ya rushwa na ufisadi la Richmond, igizo linaloonesha jinsi watawala walivyo tayari kuumiza wananchi wao ili kutibu majeraha yao wenyewe au rafiki zao. Muendelezo ya igizo hili hatimaye ulizaa filamu ndefu, lakini tamu.
Sinema hii ndefu ilianza kama mzaha vile: wahusika wakuu wakiwa ni wale wanaojua kufisadi Taifa hili. Jinsi sinema ilivyoanza wengi tulidhani itaishia sehemu moja tu ya Richmond, kumbe jamaa ni wajanja sana kwani walipoona kuwa Watanzania tumepiga kelele nyingi kuhusu Richmond, wakatubadilishia 'Angle' na kutuwekea sehemu ya pili ya filamu; Dowans. Na hapo ndipo picha lilipoanza kunoga zaidi.
Naomba nikiri kuwa mwandishi wa kisa hiki cha kusisimua cha Richmond/Dowans ni mwandishi mahiri sana mwenye kuijua vyema kazi yake. Hubadilisha kisa (plot) cha sinema kila anapoona ipo haja ya kufanya hivyo bila kuharibu maudhui yake, mwanzoni tulipohoji tuliambiwa kuwa mmiliki wa Dowans hajulikani! Wakati huohuo Waziri wa Nishati na Madini akikomalia kuilipa Dowans!
Upepo ulipobadilika ghafla baada ya kelele nyingi zilizopigwa na wananchi, mmiliki wa Dowans akajitokeza na kukataa kupigwa Picha. Ila alitaja kuwa alitoa mamlaka kwa Mbunge wetu (ingawa Mbunge huyo aliwahi kuikana) kuisimamia Kampuni ya Dowans hapa Tanzania!
Watazamaji wa sinema hii walitaka kuamini lakini wakaishtukia sehemu hii, mwandishi akaona tena tunaipigia sana kelele Dowans kuwa inaibia Watanzania kwa kutaka ilipwe tozo kufuatia hukumu ya ICC. Akajaribu tena kubadilisha 'angle' na kutangaza kuwa serikali ikinunua mitambo ya Dowans watafuta kesi. Watanzania wakagoma tena safari hii kwa kelele kubwa sana. Sasa ameleta kitu kipya zaidi kinachoitwa Symbion Power!
Hapa ndipo sinema hii inaponoga zaidi, kwani alichokifanya mwandishi wa kisa hiki ni kuuhadaa umma wa Watanzania na mgawo wa umeme ili tuingie mkenge wa nguvu, na tuikukubali Symbion Power ambayo ni Mrithi wa Dowans.
Hii yote ni kuwafanya Watanzania majuha wasiojua kitu au kusoma alama za nyakati. Mimi binafsi hainiingii akilini kuwa Symbion Power na watuhumiwa wa Richmond/Dowans ni vitu viwili tofauti, nahisi kuwa ni walewale ila wamebuni mkakati huu wa kuibua kampuni hii ili kufuta madoa ya Richmond/Dowans usoni kwao. Na tusije kushangaa kuona Tanesco inaingia mkataba na kampuni hiyo ili ituuzie umeme.
'Angle' ya mwandishi katika kisa hiki imebadilika sana baada ya kuona kwamba jina la Dowans halitakiwi kabisa na Watanzania ametuletea jina jipya, na kama tuliukataa umeme wa Dowans basi tutasahau itakapoanza Symbion Power. Na wote tutapongeza maana tutaiona kama mkombozi kwa kuwa tayari tumeghiribiwa kwanza kwa kuletewa mgawo wa umeme mkali ili ionekane kuna shida.
Kampuni ya Symbion Power ni ya Kimarekani yenye makao yake makuu Washington DC, ambayo imethibitisha kwamba imekwishaweka sahihi mkataba wa ununuzi wa mitambo hiyo iliyopo Ubungo Dar es Salaam. Kuthibitishwa huko kulisemwa na Meneja Mtendaji wa Symbion, Paul Hinks, kwa wanahabari katika hoteli ya Kilimanjaro Kempinsky.
Hata hivyo kuna taarifa kuwa mwandishi wa habari, Timoth Kahoho amewasilisha ombi chini ya hati ya dharura kuomba Wakurugenzi wa Kampuni za kufua umeme za Dowans Holdings SA na Dowans Tanzania Limited, wakamatwe kwa kudharau amri ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, baada ya kuchapishwa kwa habari kuwa mitambo ya Dowans imeuzwa kwa Kampuni ya Symbion Power ya Marekani kwa thamani ya Dola za Marekani milioni 120.
Kwangu mimi sinema hii ndefu ya Richmond/Dowans ina mafundisho mazuri sana kwa jamii; mojawapo ni kuwa nchi yetu haipaswi kabisa kuwa na umeme ulio imara kwa kuwa watu watakosa ulaji. Mgawo wa umeme ni lazima uwepo hata kama tulikwishaambiwa kuwa utabaki kuwa historia.
Bila mgawo wa umeme zile kampuni zao za kuuza majenereta zitakufa. Hivyo kwao mgao wa umeme ni dili zuri, zuri mno. Dili litakalowahakikishia ulaji milele na kuendelea kujenga heshima ya kuwa na vitambi vya kuvimbiwa ufisadi.
Wasiwasi wangu tu ni kuhusu mwisho wa sinema hii ndefu isiyochosha, kwani watawala wakizidisha ulafi, wa kunywa mchuzi wote, wananchi wanaweza kuingilia kati na kuamua kumwaga ugali, kama watawala wakimwaga mboga. Yatakayotokea baada ya hapo ni dhambi kuyaeleza.
Naomba tusifikie huko.