Aug 24, 2011

Kanali Gaddafi alishakosa uhalali wa kuongoza

Kanali Muammar Gaddafi

 Waasi wakikanyanga sanamu ya Gaddafi

BISHOP J. HILUKA
Dar es Salaam

WAKATI naandika makala hii (siku ya Jumatano), kulikuwepo taarifa za waasi kuyazingira na kuyadhibiti makazi ya kiongozi wa Libya, Kanali Muammar Gaddafi, mjini Tripoli, huku taarifa zingine zinasema kuwa kiongozi huyo ameapa kupigana na waasi hao hadi kifo au ushindi.

Televisheni inayomuunga mkono Kanali Gaddafi, al-Urubah, imesema kuwa kiongozi huyo ambaye bado hajulikani alipo, ametoa hotuba akisema kuwa kuondoka kutoka kwenye makazi yake kulikuwa ni “mpango”. Makazi hayo ndiyo yaliyokuwa maeneo ya mwisho chini ya udhibiti wa Kanali Gaddafi mjini Tripoli.

Waasi wamekuwa wakisheherekea mafanikio yao katika bustani ya Green Square, mjini Tripoli huku picha za televisheni zikiwaonesha wapiganaji hao wakiivunja sanamu ya kiongozi huyo na kuipiga mateke baada ya kuuteka Bab al-Aziziya siku ya Jumanne.

Akizungumza na redio moja mjini Tripoli, Kanali Gaddafi ameahidi “kifo au ushindi” katika mapigano dhidi ya majeshi ya NATO na waasi wa Libya, redio ya al-Urubah ilisema.

Siku za nyuma Kanali Gaddafi aliwahi kukaririwa kusema ameleta heshima kwa Libya, jambo ambalo siwezi kubisha kwani inaeleweka wazi kuwa Gaddafi amewasaidia sana wananchi wake katika mambo fulanifulani. Amefanikiwa sana kukuza uchumi wa Libya na kuwafanya waishi kama wapo peponi, lakini hiyo haikumpa uhalali wa kukiuka misingi ya haki za binadamu na kutaka kutawala milele pamoja na kuanzisha utawala kama wa kisultani.

Uhalali wa utawala wake uliisha pale alipoamuru jeshi kuwashambulia kwa risasi za moto wananchi waliokuwa wanaandamana na hivyo kupoteza kabisa uhalali wa kuongoza. Wengi waliokuwa wakimshangilia ilikuwa ni katika kujikomba tu, au walifanya hivyo kwa hofu ya kupoteza maisha yao.

Azimio la Umoja wa Mataifa kuhusu Haki msingi za Binadamu linatamka bayana na kusisitizia uhuru wa mawazo, hii ni dhamana ya kila Serikali kuhakikisha kwamba, watu wake wanatekelezewa uhuru huo, badala ya kuendekeza dhuluma, ubaguzi na mateso hata kama umesaidia kukua kwa uchumi wa nchi.

Kilichokuwa kinaendelea Libya kinaakisi hali halisi ya kisiasa katika bara la Afrika, nchi nyingi katika bara hili bado zina changamoto kubwa kama vile: kudumisha misingi ya haki na amani pamoja na kutetea zawadi ya maisha hasa ya wale ambao ni wanyonge zaidi ndani ya jamii.

Wakenya bado wanakumbuka kwa namna ya pekee, machafuko ya kisiasa yaliyojitokeza kunako mwaka 2007 mara baada ya uchaguzi mkuu. Si rahisi kufuta picha ya mateso na mahangaiko ya wananchi wa Kenya katika kipindi hiki, mateso ambayo hayakuwa na msingi wowote ule!

Uvunjwaji wa haki za binadamu ni tatizo kubwa barani Afrika. Sheria mbaya, mahakama zisizokuwa huru, na vyombo vya dola vinavyofanya kazi kwa kufuata matakwa binafsi ya viongozi wa serikali, badala ya katiba na sheria, vimesababisha haki za binadamu katika nchi zetu kuwa katika hali mbaya.

Kimsingi shughuli zote za mwanadamu na mahusiano ya watu hapa duniani yalipaswa kuwa ni kwa ajili ya kuboresha hali yake kimwili, kiakili, kiroho na kuongeza ubora wa mahusiano yake na viumbe wengine. Hivyo, mchakato wa kila shughuli afanyayo ulipaswa kuwa katika namna ambayo haina dhuluma, uonevu, madhalilisho, taabu, ubaguzi, wala vikwazo kwa mwanadamu awaye yeyote na kwa kiumbe hai kingine chochote.

Kilele cha uwepo wa haki ni kuzalishwa na kutunzwa kwa furaha ya jamii na ya dola. Jamii kamwe haiwezi kuwa na furaha ya kweli kama haki haitawali na wala dola haliwezi kusimama imara pasipo kutunzwa kwa kiwango kikubwa haki ndani ya mipaka ya dola husika.

Jamii zote za wanadamu zina mfumo wa kimsingi wa kijamii, kiuchumi, na taasisi za kisiasa zilizo rasmi na zisizo rasmi. Ili kutambua kama mfumo fulani unaathiri mipangilio ya kijamii na una uhalali, mtu hana budi kutazama kukubalika kwa mfumo huo miongoni mwa watu wanaoongozwa na mfumo husika.

Uhuru wa kisiasa (mfano kuwepo kwa taasisi za demokrasia ya uwakilishi, uhuru wa kujieleza, wa vyombo vya habari na wa kukusanyika) uhuru wa kujumuika na kushirikiana na wanajamii uhuru wa mtu kwenda atakako na kuchagua kazi aitakayo bila kukinzana na misingi ya uadilifu, uhuru wa kupata haki binafsi zinazolindwa na utawala wa sheria.

Alamsiki

JORGE CARLOS FONSECA: Mpinzani aliyeshinda urais wa Cape Verde

Jorge Carlos Fonseca

Cape Verde

JORGE Carlos Fonseca, mgombea wa upinzani ameshinda katika uchaguzi wa urais wa Cape Verde, dhidi ya Manuel Inocencio Sousa, kutoka chama tawala. Fonseca alipata takriban asilimia 55 ya kura zote katika duru ya pili ya uchaguzi siku ya Jumapili, ukilinganisha na Sousa aliyepata asilimia 45.

Fonseca kutoka chama cha upinzani cha Movement For Democracy (MFD), alishinda kwa zaidi ya asilimia 37 ya kura zilizopigwa katika duru la kwanza la uchaguzi, kabla ya uchaguzi wa marudio uliomwingiza madarakani.

Viongozi hao wawili wamewania nafasi hiyo baada ya Rais Pedro Pires kung'atuka kufuatia kumaliza vipindi vyake viwili.
Wachambuzi wanasema, Cape Verde ni moja ya nchi zenye demokrasia thabiti barani Afrika.

Fonseca, mwenye umri wa miaka 60, aliyekuwa waziri wa mambo ya nje alisema atalenga zaidi kuujenga uchumi wa Cape Verde. Amenukuliwa na shirika la habari la AFP akisema, "ushindi wangu ni wa kidemokrasia, kwa heshima ya watu wa Cape Verde walioamini mipango yangu."

Historia yake

Jorge Fonseca Carlos de Almeida amezaliwa 20 Oktoba 1950, ni mwanasiasa, mwanasheria na profesa wa chuo kikuu, ambaye kwa sasa ndiye mshindi wa urais wa Jamhuri ya Cape Verde, kutoka chama cha Movement for Democracy (MfD).

Jorge Fonseca alimaliza elimu yake ya msingi na ya sekondari kati ya Praia na Mindelo, na baadaye, elimu yake ya juu mjini Lisbon. Alihitimu shahada ya kwanza katika Sheria na shahada ya uzamili wa Sheria katika Kitivo cha Sayansi ya Sheria, Chuo Kikuu cha Lisbon.
Alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa uhamiaji wa Cape Verde kati ya 1975 na 1977, na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Cape Verde kati ya 1977 na 1979.

Alikuwa mkufunzi msaidizi wa Kitivo cha Sheria, Chuo Kikuu cha Lisbon kati ya 1982 na 1990, Profesa mwalikwa wa sheria ya jinai katika Taasisi ya Tiba kuchunguza mauaji ya Lisbon mwaka 1987 na mkurugenzi mkazi na profesa mwalikwa katika kozi ya Sheria na Utawala katika Chuo Kikuu cha Asia ya Mashariki, Macau mwaka 1989 na 1990. Pia alikuwa profesa msaidizi na mwenyekiti wa bodi ya Taasisi ya Sheria na Sayansi ya Jamii katika Cape Verde.

Kati ya 1991 na 1993 alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje katika serikali ya kwanza ya Jamhuri ya Pili, na mgombea wa Rais wa Jamhuri mwaka 2001, nafasi ambayo ameitumia tena katika uchaguzi wa Agosti 7, 2011, wakati huu kwa kutumia chama cha upinzani cha MfD, na kushinda katika raundi ya 1 (kwa asilimia 38 ya kura) na duru ya pili, na hivyo kuwa Rais wa nne katika historia ya uhuru wa Cape Verde.

Pia ni mwanzilishi na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa taasisi ya “Direito e Justica”, mwanzilishi na mkurugenzi wa gazeti la “Direito e Cidadania”, mshiriki wa gazeti la “Revista Portuguesa de Ciência Criminal”, na mwanachama wa bodi ya wahariri ya “Revista de Economia e Direito”.

Pia ni mwandishi wa vitabu kadhaa na makala zaidi ya hamsini za kisayansi na kiufundi katika uwanja wa sheria, na amechapisha vitabu viwili vya mashairi. Amepewa tuzo kadhaa na Serikali ya Cape Verde.

Makala hii imeandaliwa na Bishop Hiluka kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya habari vya kimataifa.

ANNA HAZARE: Mwanaharakati India anayeitoa jasho serikali kuhusu ufisadi

Anna Hazare

India

MWANAHARAKATI nguli nchini India, Anna Hazare, ameweka nadhiri ya kufanikisha mapinduzi nchini mwake wakati huu ambapo ameanza kutekeleza ahadi yake ya kufunga kula na kunywa kwa kipindi cha siku kumi na tano.

Mwanaharakati huyo anahurumiwa na wengi nchini India na tayari maandamano ya kumuunga mkono yanazidi kuvutia idadi kubwa ya watu kote nchini humo. Hazare anashinikiza kufanyika kwa mageuzi katika sheria za kupambana na rushwa na alikuwa amepanga kuanza kukesha bila chakula ili kushinikiza hilo lifanyike.

Watu wengi wanaomuunga mkono wamejitokeza na mabango huku wakikemea serikali wakitaka aachiwe huru. Raia hao wa India wanasema lazima serikali ichukue hatua za kukabili ufisadi uliokithiri nchini humo.

Uamuzi wa Mwanaharakati Hazare una lengo la kuishinikiza serikali nchini India kutunga sheria kali zaidi dhidi ya viongozi ambao wanajihusisha na vitendo vya ulaji rushwa vilivyotawala kwenye taifa hilo.

Hazare aliitaka serikali kushughulikia mapendekezo yake ya namna ya kushughulikia suala la rushwa siku moja baada ya kufanyika kwa sherehe za kumbukumbu ya uhuru wa nchi hiyo ambapo Waziri Mkuu, Manmohan Singh alitangaza mikakati ya kukabiliana na hali hiyo.

Hata hivyo, Singh, amemkosoa mwanaharakati huyo akisema, ingawa nia yake ni nzuri anatumia dhana potofu kulazimisha bunge lifuate matakwa yake. Mshirika wa karibu wa Hazare amesema kuwa sasa amekubali kuondoka jela baada ya polisi kuridhia kuwa anaweza kufanya mgomo huo wa kususia chakula kwa siku kumi na tano kwenye bustani moja mjini Delhi.

Hazare na wafuasi wake wapatao 1,200 walitiwa nguvuni na polisi wakiwa kwenye bustani ya JP Park saa chache kabla hawajaanza kususia chakula.

Mwezi April Hazare alivunja mgomo wake wa kususia chakula baada ya siku nne pale serikali ilipokubali kuwa anaweza kuhusika kuandaa muswada wa kupambana na ufisadi nchini humo ambapo kutakuwa ofisi maalum ya kuchunguza wanasiasa na watumishi wa serikali wanaoshukiwa kuhusika na ufisadi.

Serikali ya Waziri Mkuu Singh imekuwa ikikosolewa vikali kutokana na kushindwa kudhibiti vitendo vya ulaji rushwa ambavyo vimekuwa vikifanywa na baadhi ya mawaziri.

Historia yake

Kisan Baburao Hazare, maarufu kama ya Anna Hazare amezaliwa Juni 15, mwaka 1937 ingawa machapisho mengine yanaonesha kuwa alizaliwa Januari 15 mwaka 1940 katika eneo la Bhingar, Ahmednagar, wilaya ya Maharashtra.

Baba yake alikuwa mfanyakazi asiyekuwa na ujuzi wowote na alimiliki ekari 5 ya ardhi kwa ajili ya kilimo. Hali mbaya ya kilimo iliisukuma familia yao katika mtego wa umaskini na mwaka 1952, Hazare alihamia katika nyumba yake ya mababu huko Ralegan Siddhi. Alilelewa na mama mmoja asiye na mtoto aliyemlipia pesa kwa ajili ya elimu yake mjini Mumbai, lakini kukosekana kwa fedha kulimsukuma kuuza maua kwa ajili ya kuishi na aliacha masomo baada ya darasa la saba.

Mara baada ya kuajiriwa katika Jeshi la India na kupatiwa mafunzo ya udereva wa magari aliajiriwa mjini Punjab. Siku zake katika utumishi wa Jeshi alizitumika kusoma vitabu mbalimbali vya falsafa za wanafalsafa wakubwa kama Swami Vivekananda, Mahatma Gandhi na Acharya Vinoba Bhave. Mawazo yao ndiyo yaliyomuongoza kujitoa maisha yake kwa kazi ya jamii.

Makala hii imeandaliwa na Bishop Hiluka kwa msaada wa mashirika mbalimbali ya habari
 

Aug 17, 2011

Kukosekana kwa uzalendo halisi kunavyochangia matatizo Afrika

Rais Jakaya Kikwete

 Basil Mramba, aliyewahi kusema kuwa
bora Watanzania wale nyasi ili ndege 
ya rais inunuliwe kwa gharama yoyote

BISHOP J. HILUKA
Dar es Salaam

MAKALA zangu mbili zilizotangulia nilielezea kuhusu miaka 50 ya uhuru wetu na kugusia kwamba matatizo yetu yamesababishwa na kukosekana uzalendo, jambo ambalo limenifanya kuonekana mpinzani. Msomaji mmoja amehoji kama naelewa maana ya neno hilo, kwa kuwa nimeonekana kulitumia sana katika mambo ambayo yeye anadhani hayakupaswa.

Pia ameonesha wasiwasi wake kuwa makala zangu zilibeba ujumbe mmoja tu; kuikosoa Serikali ya Chama Cha Mapinduzi kwa mawazo ya kiupinzani. Japo hakunieleza waziwazi lakini alikusudia kuniambia kuwa mimi ni mpinzani wa serikali, kwa kupinga hata mazuri yaliyofanyika.

Ningependa kuweka wazi msimamo wangu kwake na kwa wengine kuwa mimi sina chama na wala sijawahi kuwa mwanachama wa chama chochote cha siasa katika maisha yangu. Kwa kifupi sitaki kuwa na chama, hivyo sifungwi na itikadi za chama chochote na siandiki kwa utashi wa chama au mtu mwingine, ndiyo maana nipo huru kutoa mawazo yangu.

Pia siipendi siasa kwa kuwa kwangu siasa ni “si hasa”, ila navutwa kuandika kuhusu siasa kwa kuwa napenda kutoa mchango wangu kuhusu mustakabali wa nchi yetu.

Nirudi kwenye mada husika - Uzalendo – nijuavyo neno hili maana yake ni mtu kuipenda nchi yake, uzalendo ni miongoni mwa tabia njema ambazo inatakiwa ziwe ni pambo la mtu. Tabia hii ina athari kubwa sana katika kuchochea maendeleo ya mtu binafsi na nchi yake kwa ujumla. Uzalendo humsukuma mtu kuithamini na kuionea fahari nchi yake, vitu ambavyo ni chachu na hamira ya maendeleo. Uzalendo humfanya mtu kuitakia mema nchi yake.

Kiongozi yeyote mzalendo husukumwa na mapenzi kwa nchi yake, hawezi kulazimisha kununua ndege ya rais ya mabilioni hata kama wananchi wake watakula nyasi. Kiongozi mzalendo hawezi kujilimbikizia mali haramu ambazo upatikanaji wake una utata. Je, viongozi matajiri wamefanya biashara gani madarakani hadi wakaupata utajiri walio nao kama si kukosa uzalendo kwa nchi yao? Hivi utajiri wa viongozi hawa umelipiwa kodi ya mapato? Ni kweli wana mapenzi ya dhati kwa Watanzania wenzao katika kuondokana na madhila ya umaskini yanayowasibu?

Kiongozi yeyote mzalendo hawezi kuchukua 'ten parcent' ili kupitisha mikataba ya kinyonyaji ambayo italeta maafa kwa wananchi na kumfaidisha mgeni ambaye akishapata akitakacho ataondoka zake. Leo hii pesa za kodi ya wananchi zinaishia kujenga mahekalu na kununua magari ya kifahari ya viongozi ili-hali wananchi wanaendelea kuwa masikini, wanaoishi chini ya mstari wa ufukara ambapo asilimia 80 yao wanaishi vijijini wakitegemea kilimo cha jembe la mkono.

Uzalendo ni kitu adimu sana katika serikali nyingi za Kiafrika japo watawala wawapo majukwaani huhubiri uzalendo utadhani ni nguo unayoweza kuinunua dukani au kwa machinga. Wanasahau kuwa uzalendo uko moyoni, uzalendo ni sumu ya unyonyaji, uzalendo ni sumu ya rushwa, uzalendo ni sumu ya ukandamizaji, uzalendo ni sumu ya uonevu, uzalendo ni dawa kwa wananchi.

Kukosekana kwa uzalendo huwafanya viongozi kujivua majukumu yao ya kuhakikisha wananchi wanapata fursa sawa katika kushiriki masuala ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Viongozi ambao hushirikiana na wafanyabiashara wasio waaminifu kufanya udanganyifu katika biashara kwa kuwauzia wananchi bidhaa zilizo chini ya kiwango cha ubora, kuwapunja katika mizani au kuwauzia kwa bei ya juu kupita kiasi.

Kiongozi au mwananchi mzalendo ni yule afikaye kazini mapema kwa muda utakiwao na kufanya kazi kikamilifu kwa mujibu wa taratibu za kazi, atokaye kazini kwenda nyumbani kwa muda uliopangwa. Ukosefu wa uzalendo ndiyo umefanya viwanda vingi kufa, mashirika ya umma yamekufa na kuongeza idadi ya wazururaji na wakaa vijiweni ambao walikuwa wameajiriwa kwenye mashirika hayo.

Ukosefu wa uzalendo unasababisha umasikini katika nchi nyingi za Kiafrika kuwa ni wa Kujitakia. Umasikini wa aina zote mbili: umasikini wa nchi na umasikini wa watu walio wengi katika ujumla wao. Yaani tunashindwa hata kujinasua kwenye hili moja la kuwa na umasikini wa watu tu huku nchi ikiondoka kwenye utegemezi wa wahisani, kama sasa ambapo bajeti yetu haikamiliki bila kutegemea wahisani.

Inapotokea serikali imekuwa masikini hadi kuendeshwa kwa misaada toka nje ya nchi huku ikiendeshwa na viongozi matajiri kuliko serikali yao, ndipo kunapokuwa na maswali, halafu mbaya zaidi na wananchi nao wakawa masikini hadi kufikia kiwango cha kushindwa kufanya lolote.

Umasikini umekuwa kikwazo dhidi ya demokrasia na kikwazo dhidi ya utawala bora kwa kuwa wezi wa mali za umma, walaji rushwa na mafisadi ndio wenye tabia za kuwanunua wapiga kura walalahoi kwa njaa na umasikini wa kupindukia.

Ni muhali bali uongo mweupe mtu kudai kuwa anaipenda nchi yake huku anawasahau wananchi wake ambao wamemfanya yeye awepo hapo alipo na kuneemesha kundi dogo la marafiki wake na familia yake. Kielelezo na nembo kuu ya kuonesha taswira ya uzalendo wake kwa nchi yake kiwe ni kuwahudumia wananchi wake; katika hali na mali.

Ni wajibu na jukumu la kila mmoja wetu kuipenda nchi yake. Mwanafunzi mwenye uzalendo na nchi yake ni yule anayesoma kwa hima juhudi na bidii huku akizingatia miiko na taratibu za elimu ambazo ni pamoja na kuwaheshimu walimu wake na kanuni zote za shule sambamba na kushirikiana na wenzake.

Naomba kuwasilisha...

JULIUS MALEMA: Kinda wa Afrika Kusini aliyezua utata masuala ya mashauri ya nchi za nje

Julius Malema

AFRIKA KUSINI

NI kama ilivyokuwa wakati viongozi wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) walipotoa tamko katika mkutano wa wajumbe wa Kamati ya Utekelezaji ya Baraza Kuu la Umoja huo na Jukwaa la Wahariri Tanzania, kwenye hoteli ya Peacock, mjini Dar es Salaam, kukemea bila woga, ndivyo ilivyotokea nchini Afrika Kusini kwa kiongozi mkakamavu wa tawi la vijana la chama tawala cha ANC, Julius Malema, ingawa ni kwa aina tofauti kidogo.

Julius Malema aliingilia kati masuala ya mashauri ya nchi za nje, alipotoa wito kuwa serikali ya nchi jirani ya Botswana, iliyochaguliwa kwa njia ya kidemokrasia inafaa kupinduliwa. Hata hivyo, tawi hilo la vijana la ANC, limeomba msamaha kwa chama.

Mapema mwezi huu, ANC ilililaumu vikali tawi lake la vijana, na kiongozi wake, Julius Malema, kwa matamshi hayo.

Historia yake

Julius Malema Sello amezaliwa 3 Machi 1981, katika eneo la Seshego, ni kijana mwanasiasa wa Afrika Kusini, na Rais wa Tawi la Vijana wa African National Congress (ANC). Malema yupo kwenye nafasi tata ya kisiasa nchini Afrika Kusini; akiibukia kwenye umaarufu kwa msaada wa rais wa ANC, na baadaye Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma.

Malema amekuwa akielezewa na wote, Zuma na Waziri Mkuu wa Limpopo kama "kiongozi wa baadaye" wa Afrika Kusini. Lakini pia amekuwa akitafsiriwa na wengine kama “maarufu asiyejali” mwenye uwezekano wa kuidhoofisha Afrika Kusini na cheche za ubaguzi wa rangi. Alipatikana na hatia ya kutumia lugha ya chuki mnamo Machi 2010.

Maisha ya awali na kazi

Malema alizaliwa katika eneo la Seshego, Mama yake alikuwa mfanyakazi wa ndani na mzazi pekee aliyemlea mwanaye. Alijiunga na Masupatsela ya ANC katika umri wa miaka tisa au kumi ambapo kazi yake kubwa ilikuwa ni kuyaondoa (kuyachana) mabango na matangazo yote ya chama cha National (mpinzani wa ANC) kinyume cha sheria.

Elimu

Ilimchukua Malema miaka minne kumaliza darasa la 8 na 9 la shule ya sekondari. Alimaliza darasa la 12 katika Shule ya Juu ya Mohlakaneng katika eneo la Seshego, Limpopo, akiwa na umri wa miaka 21, baada ya kuwa mtoro wa shule kwa muda wa miezi mitano katika mwaka huo. Matokeo yake ya mtihani wa darasa la 12 yaliyoonesha kupata alama mbaya yalichapishwa katika gazeti la taifa mnamao Oktoba 2008, yakionesha kumkejeli.

Kazi ya siasa

Malema alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa tawi la vijana la Seshego na mwenyekiti wa kikanda mwaka 1995. Mwaka 1997 akawa mwenyekiti wa Shirikisho la Wanafunzi wa Afrika Kusini (Cosas) wa jimbo la Limpopo, na alichaguliwa kuwa rais wa kitaifa wa shirikisho hilo mwaka 2001. Mwaka 2002, Malema aliongoza maandamano ya Cosas ya wanafunzi, katika mitaa ya Johannesburg yaliyofunikwa na matukio ya ghasia na uporaji.

Kiongozi wa Vijana wa ANC

Malema alichaguliwa kuwa rais waVijana wa ANC mwezi Aprili 2008. Uchaguzi - na mkutano – ulioelezewa na kile ambacho Malema mwenyewe alikisema baadaye kuwa "mwenendo wa yanayotokea". Uadilifu wa uchaguzi wake umekosolewa na kuhojiwa. Alichaguliwa tena bila ya kupingwa kwa awamu ya pili mnamo 17 juni 2011.

Ziara ya Zimbabwe, Aprili 2010
3 Aprili 2010, Malema alitembelea Zimbabwe, kwa kile kilichoelezwa kama ziara ya uzawa. Alitarajiwa kukutana na Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe. Alipotua Harare, Malema alisalimiwa na wafuasi wa Zanu-PF pamoja na Waziri wa Vijana na Uzawa wa Zimbabwe, Mwokozi Kasukuwere, na Mwenyekiti wa Vijana wa Zanu-PF, Absolom Sikhosana, pamoja na wafanyabiashara maarufu wa Zimbabwe.

Morgan Tsvangirai, Waziri Mkuu wa Zimbabwe, aliishutumu ziara ya Malema, baada ya Malema kukikosoa chama cha Tsvangirai, cha MDC. Wakati wa ziara hiyo, Malema alimuelezea Tsvangirai kama mshirika wa "mabeberu". Mashirikisho ya Vijana wa Zimbabwe yaliikosoa ziara ya Malema, yakitoa maelezo yake ya ubaguzi wa rangi na madai ya rushwa. Wakati wa ziara yake kulizua hofu kwamba Afrika Kusini itafuata mageuzi ya ardhi kama ya Zimbabwe. Malema pia aliilaumu MDC kwa kuanzisha ghasia za kisiasa nchini Zimbabwe, na kutetea rekodi ya kisiasa na haki za kibinadamu ya Robert Mugabe.
Baada ya Malema kurudi kutoka Zimbabwe, Vijana wa ANC walitoa taarifa kumsifu Mugabe na sera zake za kutaifisha ardhi Zimbabwe. Pia walitoa wito kwa vijana wa Afrika Kusini wa kufuata mfano wa vijana wa Zimbabwe, na kushiriki katika kilimo ili kupunguza utegemezi wao juu ya wakulima wa kizungu. Msaada wa Malema ndani ya Vijana wa ANC bado ni imara.

Kushiriki katika mikataba ya nchi

Taarifa juu ya kuhusika kwa Malema katika zabuni za nchi (mikataba) ilianza kuonekana Novemba 2009. Maswali kuhusu maisha yake binafsi yalitolewa na vyombo vya habari Afrika Kusini. Machi 2010, alijibu madai hayo katika mkutano uliofanyika kampasi ya chuo kikuu, Malema, aliimba wimbo wa mapambano "piga risasi Makaburu", na aliwakemea wanasiasa wa upinzani. Pia alimshambulia Katibu Mkuu wa COSATU, Zwelinzima Vavi.

Agosti 2010, ilitolewa ripoti iliyomsafisha Malema kushiriki kwake katika zabuni za nchini katika mkoa wa Limpopo. Hii ilipokelewa kwa wasiwasi na baadhi ya watu.

Vitisho kwa waandishi wa habari
Wiki chache baada ya utata wa zabuni kuibuka kwa mara ya kwanza, Vijana wa ANC walitoa maelezo binafsi ya Mhariri wa Uchunguzi wa City Press, Dumisane Lubisi, mke wake na watoto wake, ikiwa ni pamoja na namba zao za vitambulisho, maelezo ya benki, anuani ya makazi na maelezo ya gari zao. Lubisi alikuwa ametoa taarifa kuhusu kiwango duni cha ujenzi wa miradi katika Limpopo uliofanywa na makampuni ya Malema.

Vijana wa ANC walitoa madai kuwa walikuwa na ushahidi kuwa waandishi walikuwa wanapokea rushwa katika mambo kadhaa. Katika majibu, kundi kubwa la waandishi wa habari wa kisiasa walilalamika kwa mamlaka mbalimbali ndani ya ANC na Jukwaa la Wahariri la Afrika Kusini (SANEF) wakisema kwamba taarifa hiyo ilikuwa kama jaribio la kuwatisha wasichapishe habari zaidi, na kama tishio kwa uhuru wa vyombo vya habari.

Ufafanuzi wa vyombo vikubwa vya habari

Malema anajulikana kwa taarifa zake tata na mara kwa mara amekuwa akishutumiwa. Awali, wachora katuni, Zapiro na Jeremy Nell mara nyingi walimchora akiwa amevaa nepi. Hivi karibuni, wasifu wa Malema kwa umma umeongezeka, amekuwa akielezwa na wakosoaji katika vyombo vya habari kama "kiongozi wa kisiasa anayeshawishi watu kwa kutumia hisia badala ya fikra zao". Pia alitajwa katika orodha ya watu wasio na ushawishi ya gazeti la Time kwa mwaka 2010.

Kupatwa hatia kwa kauli za chuki

Machi 15, 2010 Malema alipatikana na hatia ya kutumia lugha ya chuki katika Mahakama ya Usawa, akatozwa faini ya R50 000 na kuamriwa kuomba msamaha, kufuatia tukio la 2009 alipowaambia kundi la wanafunzi wa Cape Town, katika Mkutano wa Wanafunzi wa Afrika Kusini (SASCO) kwamba mwanamke aliyemshitaki Rais wa ANC, Jacob Zuma kwa ubakaji alipata “wakati mzuri” kwa sababu baada ya kuamka asubuhi alipata “kifungua kinywa na fedha za teksi”. Kufuatia hukumu hiyo SASCO walionesha "furaha", na kumshambulia Malema kwa “matumizi mabaya” ya jukwaa ambalo SASCO walimpa.

Malema alitoa taarifa mbalimbali kuhusu Wachina nchini Afrika Kusini katika chakula cha jioni cha Umoja wa Wanafunzi wa Afrika Kusini na Wayahudi Aprili 2011. Aliwakebehi wawekezaji wa China ambao "hawakuleta chochote nchini" na kukosoa Uwekezaji wa China nchini Afrika Kusini, kuhoji Afrika Kusini kujihusisha na biashara ya Brazil, Russia India na China.

Makala haya yameandaliwa na Bishop J. Hiluka kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya habari vya kimataifa.

Aug 10, 2011

Miaka 50 ya uhuru uchumi unakua, huku umasikini ukizidi kuongezeka!

Baba wa Taifa, mwalimu Julius Nyerere

Abeid Aman Karume, Rais wa Kwanza wa Zanzibar

BISHOP J. HILUKA
Dar es Salaam

WIKI iliyopita niliandika makala yenye kichwa cha habari “Miaka 50 ya uhuru, kiwango cha elimu mmh”, iliyoibua hisia tofauti kwa wasomaji, baadhi wakikubaliana nami na wengine wakionesha kunishangaa eti kwa kutoyaona mazuri ya nchi hii.

Walionishangaa walinilaumu kwa kuandika mambo ambayo kwa mtazamo wao ni ya kupotosha huku wakiniuliza endapo ningechaguliwa kuwa rais au waziri ningefanya nini? Msomaji mmoja alinipigia simu kuonesha jinsi alivyokerwa na jinsi nilivyowasilisha suala la kukosekana kwa uzalendo kwa viongozi wetu.

Naomba niweke bayana kwamba kila mtu ana mitazamo yake katika mambo mbalimbali, nilichoandika ulikuwa mtazamo wangu binafsi na wala sitaandika anavyofikiri mwingine au kwa utashi wa mtu mwingine. Lakini nitazidi kusisitiza kuwa hapa tulipofika ni kwa sababu ya kukosekana uzalendo.

Nchi hii imeingiwa na ugonjwa mbaya sana wa mmong'onyoko wa misingi ya utawala bora, umoja na mshikamano wa kitaifa; maadili na utu wema, jambo linalowatumbukiza walio wengi katika umaskini.

Huko nyuma tulizoea kuambiwa kuwa ‘cheo ni dhamana’ na kwamba ‘uongozi ni utumishi’, lakini siku hizi kupata cheo ni kuula! Neno 'kuula' limeanza kama lugha ya mtaani ambayo ina tafsiri pana kidogo. Moja ya tafsiri ni 'mambo kuwa mazuri (kunyooka)'.

Bahati mbaya tumefika mahala tumejisahau kabisa, wala hatukumbuki tena kwamba cheo ni dhamana. Kwa miaka ya hivi karibuni wazo la cheo ni dhamana limepotelea mbali na kusahauliwa kama lilivyosahauliwa Azimio la Arusha. Tunawezaje kupata viongozi wazuri kama kila mmoja anafikiri nafasi aliyonayo ni haki yake, ni mali yake, na ni stahili yake?

Zama hizi mtu anaruhusiwa kuwa na kampuni na akajipa tenda ya kutoa huduma ofisini kwake, anaruhusiwa kutembea dunia nzima kwenye makongamano na warsha kwa kutumia hela za wananchi, ukiwa na cheo kikubwa utawapa ajira watoto na dugu zako wote ofisi waipendayo.

Zama hizi mtumishi wa umma anajengewa nyumba ya kuishi ya thamani ya mabilioni ya shilingi na akikaribia kustaafu anakopeshwa kwa vimilioni vichache, pia ni zama ambazo kufikishwa mahakamani kwa ubadhirifu inategemea umekwapua kiasi gani, kama ni kikubwa, dola yenyewe inatamka kuwa hukamatiki!

Ni zama ambazo ukiwa mtumishi wa umma mwenye cheo kikubwa unaweza kusomesha mwanao nchi yoyote uitakayo bila mawazo ya karo, si hivyo tu kutibiwa nje si kwa magonjwa ya moyo tu bali hata mafua, muhimu cheo kizuri cha kuhudumia umma.

Wakati tukijiandaa kwa maadhimisho ya miaka hamsini tangu kupata uhuru wa kisiasa, inasikitisha kuona kwamba, sehemu kubwa ya utajiri na rasilimali ya Tanzania iliyopaswa kuwa ni kwa ajili ya mafao ya wengi, inaendelea kuwanufaisha watu wachache ndani ya jamii, kinyume kabisa na mipango na mikakati iliyowekwa na waasisi wa Taifa hili, wakati wa kupigania uhuru; misingi ya uadilifu, uzalendo na umoja wa kitaifa inazidi kumong'onyoka siku hadi siku, hali ambayo inasababisha kustawi kwa ubinafsi, ufisadi na kinzani za kijamii.

Kumong'onyoka kwa misingi ya utawala bora; umoja na mshikamano wa kitaifa, maadili na utu wema; uzalendo, utu na heshima ya kila Mtanzania na wala si mali anayomiliki, kumesababisha Watanzania wachache kuendelea kufaidika na rasilimali ya nchi, wakati kundi kubwa la watu likiendelea kuogelea katika dimbwi la umaskini, ujinga na maradhi.

Yote haya yamesababishwa na kukosekana kwa uzalendo, jambo linalofanya kundi dogo la watu kufaidi utajiri wa rasilimali na madini wa nchi hii, wakati kuna mamilioni ya watu wanakufa kwa njaa, magonjwa na umaskini katika nchi yenye utajiri wa maliasili na madini ambazo, kimsingi zinapaswa kuwa ni kwa ajili ya mafao ya wengi.

Tanzania kadiri ya vigezo vya Mashirika ya Fedha ya Kimataifa ni kati ya nchi masikini zaidi duniani, lakini imekuwa na mvuto mkubwa kwa wawekezaji kutoka sehemu mbalimbali za dunia, wanaokimbilia nchini kutafuta madini.

Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Tanzania imefanikiwa kuuza dhahabu yenye thamani ya zaidi ya dola bilioni mbili nukta tano, lakini, cha kushangaza imeambulia dola millioni mbili nukta saba, hali inayoonesha kimsingi, ukosefu wa haki na usawa katika soko la kimataifa. Matajiri wanaendelea kufaidika na mikataba ya madini, wakati kuna mamillioni ya watu wanaokufa kwa baa la njaa, umaskini na magonjwa, katika maeneo haya yenye rasilimali na utajiri mkubwa kiasi hiki.

Kukosekana kwa uzalendo kumesababisha hata ndani ya nyumba za ibada; kwa maana ya Makanisa na Misikiti, harufu ya ufisadi inasikika hali ambayo inadunisha mchakato mzima wa kutafuta haki na usawa katika soko la kimataifa, kwa ajili ya mafao ya wengi.

Baadhi ya watu wanaendekeza rushwa na ufisadi; maadui wakuu wa haki na usawa kama alivyobainisha Mwalimu Nyerere wakati fulani. Masuala haya yameleta mpasuko wa kijamii ambao kwa sasa ni hatari kubwa kwa ustawi na maendeleo ya Watanzania.

Mikataba ya madini, imeendelea kuwanufaisha wawekezaji kutoka nje ya nchi na wananchi wa Tanzania kuendelea kuogelea katika umasikini wa kipato, licha ya kuzungukwa na utajiri wa rasilimali. Uchumi wa Tanzania utaendelea kudidimia, ikiwa kama hatutarudisha uzalendo wa kuipenda nchi yetu.

Rushwa na ufisadi vinaendelea kuota mizizi katika mioyo ya watu, jambo ambalo itakuwa vigumu kulifuta kwa kipindi kifupi, kama ilivyo dhana ya udini, iliyoibuliwa na baadhi ya wanasiasa kwa mafao yao binafsi.


MANUEL PINTO DA COSTA: Arudi madarakani baada ya kutawala miaka ya 70 kwa ‘mkono wa chuma’

Manuel Pinto da Costa

SAO TOME

MWISHONI mwa wiki iliyopita imeshuhudia wapiga kura nchini Sao Tome na Principe wakimchagua kiongozi wa wakati wa uhuru wa Taifa hilo dogo la Afrika Magharibi kuwa Rais wao.

Manuel Pinto da Costa, mchumi wa ‘Ki-Marxist’ mwenye umri wa miaka 75, ambaye alitawala visiwa hivyo kwa 'mkono wa chuma' kwa miaka 15 baada ya uhuru kutoka kwa utawala wa mkoloni wa Kireno mwaka 1975.

Ulikuwa ni uchaguzi wa amani siku ya Jumapili iliyopita katika visiwa vya Sao Tome na Principe wakati wa duru ya pili ya uchaguzi wa rais uliomuingiza madarakani kiongozi huyo wa zamani wa wakati wa uhuru wa taifa hilo dogo lililopo Afrika Magharibi.

Tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1991, Rais amegawana madaraka na Waziri Mkuu.

Pinto da Costa, mwenye umri wa miaka 75, amepata ushindi mwembamba dhidi ya mgombea kutoka chama cha Waziri wake mkuu katika duru ya pili ya uchaguzi siku ya Jumapili iliyopita. Mgombea aliyeshindwa, Evaristo Carvalho, ambaye ni Spika wa Bunge la nchi hiyo alipata asilimia 47 ya kura.

Hakuna tukio baya lililoripotiwa wakati vituo vya kupigia kura vya taifa hilo la visiwa vidogo kufungwa ilipotimu saa 12:00 jioni kwa saa za huko. "Mchakato wa kupiga kura upo kila mahali, katika Sao Tome na nje ya nchi. Kazi ya kuhesabu kura imeanza," alisema msemaji wa tume ya uchaguzi, Joao Ramos alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari.
Watu karibu watu 92,000 walipiga kura, kutoka kwenye idadi ya watu wa nchi hiyo ambayo ni 200,000. Baadhi ya watu 30,000 walijitoa katika raundi ya kwanza mnamo Julai 17 na vijiji vitano vilianzisha mgomo wa kupiga kura katika maandamano kupinga hali duni ya maisha katika visiwa.

Hata hivyo, Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) kupitia kipindi chake cha Network Africa limeelezwa kuwa wakazi wengi wa visiwa hivyo wapatao 165,000 ni vijana na hawana kumbukumbu za enzi za utawala wa chama kimoja wa da Costa.

Lakini wanatarajia Rais Mteule kuweka shinikizo kadhaa kwa serikali inayoongozwa na Waziri Mkuu Patrice Trovoada – kutatua baadhi ya matatizo ya nchi. Kampeni za Pinto da Costa zililenga katika utengamano wa kisiasa na aliahidi kupambana na ufisadi uliosambaa.

Visiwa vya Sao Tome na Principe, vilivyokuwa mwanzoni wazalishaji wa kwanza kwa kakao vina utajiri wa mafuta na uzalishaji wa kibiashara utaanza miaka michache ijayo.

Hata hivyo umezuka mjadala juu ya namna gani matumizi yake yatafanyika na kusababisha hali tete ya kisiasa.

Historia ya da Costa:
Manuel Pinto da Costa amezaliwa mnamo 5 Agosti 1937, ni mchumi na mwanasiasa ambaye aliwahi kuwa Rais wa kwanza wa nchi hiyo baada ya uhuru. Amechaguliwa tena katika uchaguzi wa Agosti 2011 kutumikia muhula wa pili. Anatarajiwa kuanza rasmi madaraka hayo mnamo 3 Septemba 2011.

Akiwa mkuu wa nchi hiyo baada ya uhuru mwaka 1975 hadi 1991, aliongoza kwa kusimika mfumo wa ujamaa wa chama kimoja cha siasa cha Movement for Liberation of Sao Tome and Principe (Kireno: Movimento de Libertação de São Tomé e Príncipe, MLSTP). Pia aliwahi kuwa waziri mkuu mara mbili, mara ya kwanza chini ya rais wa kwanza wa kidemokrasia wa nchi, Miguel Trovoada.

Alipata elimu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Ujerumani (Ujerumani Mashariki), na anaongea kwa ufasaha lugha za Kireno na Kijerumani.

Hadi miaka ya mwanzo ya 1990, chama chake (MLSTP) kiliimarisha mahusiano ya kina na Angola na chama tawala cha MPLA, kwa Pinto da Costa mwenyewe alifurahia zaidi uhusiano wa kirafiki kati yake na Jose Eduardo dos Santos, Rais wa Angola, wakipanua zaidi urafiki wao wa wakati wao walipokuwa vijana.

Mwaka 1991, ulipohalalishwa mfumo wa vyama vingi na kufuatiwa na uchaguzi wa kwanza chini ya mfumo wa kidemokrasia, Pinto da Costa hakugombea uchaguzi na badala yake alitangaza kustaafu siasa.

Chama chake cha MLSTP hakikuwa na mgombea mbadala wa Pinto da Costa na kumfanya Travoada Miguel achaguliwe kuwa rais bila kupingwa. Pamoja na kauli yake ya awali ya kustaafu siasa, Pinto da Costa alirejea kugombea katika uchaguzi wa 1996, lakini alishindwa kwa ushindi mwembamba na Trovoada kwa kupata asilimia 47.26 ya kura zote. Mwaka 2001, aligombea tena dhidi ya Rais anayemaliza muda wake, Fradique de Menezes, ambaye alishinda kwa wingi wa kura katika raundi ya kwanza.

Pinto da Costa alichaguliwa kuwa kiongozi wa chama cha MLSTP mnamo Mei 1998. Alijiuzulu katika chama mnamo Februari 2005 na Guilherme Posser da Costa alichaguliwa kushika nafasi yake.

Katika uchaguzi wa mwezi Julai 2011, Pinto da Costa aliingia kwenye kinyang'anyiro kama mgombea binafsi. Alishinda uchaguzi katika duru ya kwanza lakini akishindwa kupata asilimia zinazotosha kuchukua madaraka.

Katika duru hiyo alipata asilimia 35.58 ya kura baada ya kampeni zake za uchaguzi kulenga kuwepo haja ya utulivu katika taifa ambayo alidai kuwa limeshuhudia mawaziri wakuu 18 wakiwa madarakani katika miaka 21 tu baada ya nchi kuingia katika mfumo wa vyama vingi mwaka 1990. Pia aliahidi kupambana na ufisadi mkubwa ambao umedumaza maendeleo ya kiuchumi ya Sao Tome.

Mpinzani wake, Carvalho, mwenye umri wa miaka 70, alipata asilimia 21.74 ya kura katika duru ya kwanza ya uchaguzi, ni mwanachama wa chama cha Independent Democratic Action (Kireno: Acção Democratica Independente, ADI). Pia aliahidi kupambana na rushwa kama ahadi ya ilani yake muhimu.

Chini ya sheria ya Sao Tome, rais anayemaliza muda wake, Fradique de Menezes, ambaye alichaguliwa kwa mara ya kwanza mwaka 2001 na kuchaguliwa tena mwaka 2006, hawezi kugombea kwa mara ya tatu.

Katika tukio linalosemekana kutohusiana na siku ya kupiga kura ya Jumapili, mtu mmoja mwenye umri wa miaka 37 alipigwa risasi na kuumizwa katika mguu na walinzi wa Waziri wa Vijana na Michezo wa Sao Tome, Abnildo d'Olivera.

Katika raundi ya pili ya marudio ya uchaguzi mnamo tarehe 7 Agosti, da Costa alimshinda mpinzani wake, Evaristo Carvalho kutoka chama tawala cha Independent Democratic Action, kwa kupata asilimia 58 ya kura.

Wakati wa kampeni zake zilizolenga haja ya siasa za utulivu na ahadi za kukabiliana na ufisadi mkubwa. Jitihada zake zilipata sapoti kubwa kutoka kwa wagombea wengine wakubwa, akiwemo Waziri Mkuu wa zamani, Maria das Neves, ambaye alidai kuwa "mpango wa Pinto da Costa utaleta matumaini zaidi kwa nchi yetu".

Baadhi ya wachambuzi wa mambo, hata hivyo, walionesha wasiwasi wao kwamba ushindi wa rais huyo wa zamani unaweza kurejesha enzi za utawala wa kimabavu ulioonekana katika kipindi chake cha zamani cha madaraka.

Makala haya yameandaliwa na Bishop J. Hiluka kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya habari vya kimataifa.

Aug 3, 2011

Miaka 50 ya uhuru wetu, kiwango cha elimu mmh!

 Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, 
Dk. Shukuru Kawambwa

 Minara pacha ya Benki Kuu (BOT)

Ndege ya Rais aina ya Gulfstream 550

BISHOP J. HILUKA
Dar es Salaam

KUMBE wewe ndiyo Bishop? Ninasoma sana makala zako... una upeo mkubwa mwanangu, siyo huyu rafiki yako hana akili! Kakosa hata nafasi ya ualimu?” ananiambia mama Beka, mkazi wa Kinondoni, mara baada ya kutambulishwa kwake na mwanaye ambaye ni rafiki yangu.

Kauli yake imenifanya kuandika makala nyingine kuhusu elimu. Nimewahi kuandika makala kadhaa kuhusu mfumo wetu wa elimu na sikuwa na sababu ya kuendelea kuandika kuhusu elimu. Ikizingatiwa kuwa hivi karibuni ilitolewa ripoti ya utafiti kuhusu elimu na Shirika la Utafiti la Uwezo, ambapo Tanzania tunazidiwa na jirani zetu, Kenya na Uganda.

Naamini wengi wameisoma ripoti hiyo, binafsi sikupata nafasi ya kuisoma na sielewi wametoa sababu zipi za kudorora elimu yetu, lakini kwa kauli kama ya mama Beka, naamini sababu zipo wazi kabisa.

Kwanza nakubaliana na wanaosema kuna tofauti kubwa sana ya wasomi wa sasa na wa zamani, hasa waliosoma enzi za utawala wa kikoloni na miaka michache baada ya uhuru. Katika kipindi hicho, japo elimu ilikuwa bidhaa adimu kwa wananchi wazawa, waliobahatika kusoma walisomesheka na kuwa watu muhimu sio tu katika ulingo wa ajira lakini hata katika jamii zao.

Kwa kweli huwezi kumlinganisha mhitimu wa darasa la saba wa leo na yule wa wakati huo kwa kuwa mfumo wa elimu uliopo sasa umechakachuliwa sana. Tumefika mahala mtu aliyekosa kuchaguliwa kwenye chaguzi zingine ndio anayejiunga na ualimu! Ndio maana hata mama Beka anamshangaa mwanaye kukosa hata nafasi ya ualimu?

Imesemwa kuwa athari ya mwalimu aliyefeli inajidhihirisha hata kwa wale anaowafundisha, kwa kuwa hawatokuwa na upeo mkubwa, matarajio yao yatakuwa madogo, na nchi itazidi kuwa masikini kwani itakuwa na idadi kubwa ya watu wasiojiweza na wenye uwezo mdogo wa kujikwamua kimaisha. Mwalimu aliyefeli hawezi kujiamini anapofundisha na aghlabu hawezi kukidhi mahitaji ya wanafunzi hasa wale wenye uwezo mkubwa wa kuhoji mambo ambao mara nyingi huitwa wasumbufu na walimu wasiojimudu.

Kwa muda mrefu, vyuo vya ualimu nchini vimekuwa vikidahili wanafunzi wenye alama za chini kusomea ualimu ikiwa ni mojawapo ya mikakati ya serikali kukabiliana na uhaba wa walimu shuleni. Na hivi karibuni Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, alikiri bungeni kuwa ili kupunguza tatizo la uhaba wa walimu, vyuo hivyo vimekuwa vikiwapokea hata wanafunzi waliopata daraja la nne!

Mi' nadhani, utaratibu wa kudahili wanafunzi wasio na sifa stahiki kwa kisingizio cha kukabiliana na uhaba wa walimu shuleni una athari zaidi kuliko manufaa. Kwanini taaluma ya ualimu iendelee kuwa kapu la kuwapokea watu wasio na uwezo? Walimu wa aina hii tunaowaamini kufundisha wanetu, ni kweli wanawajengea ufahamu wanafunzi kuhusu rasilimali zao?

Takwimu zilizomo katika kitabu cha Takwimu za Msingi za Elimu Tanzania (BEST) kilichotolewa mwaka 2007 zinaonesha kuwa hadi mwaka huo, Tanzania ilikuwa na walimu 2663 tu waliothibitishwa kati ya walimu 18,463 waliokuwa wakifundisha!

Hivi kweli wanafunzi wanaohitimu katika ngazi mbalimbali za elimu wanafahamu kuwa wamekwenda shule ili wazifahamu rasilimali zao na matumizi yake? Mi' nadhani tatizo liko kwa viongozi wa sasa kukosa uzalendo na kupenda kujilimbikizia mali! Kwani hadi miaka ya tisini kiwango cha elimu kilikuwa bora japo nafasi zilikuwa chache!

Viongozi wabinafsi hushindwa hata kupanga vipaumbele kwa maslahi ya taifa. Sidhani kama ununuzi wa ndege ya rais na rada lilikuwa jambo muhimu zaidi kuliko kujenga vituo vya afya, madarasa ya kutosha, maabara na kadhalika. Siamini kama ujenzi na baadaye ukarabati wa ukumbi mpya wa Bunge ulikuwa muhimu kuliko kuweka madawati kwenye shule zote za msingi nchi nzima! Au ujenzi wa minara pacha ya BOT ulikuwa muhimu kuliko kuboresha mazingira ya kazi kwa walimu na askari wanaoishi kwenye nyumba ambazo hazijakarabatiwa tangu alipoziacha mkoloni!

Kufifia kwa utaifa, uzalendo na uwajibikaji ndiyo chanzo kikuu cha mambo kwenda ovyoovyo katika nchi hii japo tunajisifu kufikia miaka hamsini ya uhuru huku tukiwa tumefanikiwa kuanzisha sekondari katika kila kata, shule ambazo hazina walimu wala maabara na hakuna kiongozi yeyote ambaye anasomesha watoto wake huko!

Enzi zile tulikuwa tunasoma na watoto wa viongozi wa juu serikalini, wakiwemo watoto wa marais! Siku hizi hakuna kitu kama hicho! Viongozi wote wanasomesha watoto wao katika shule bora za binafsi, zenye walimu wazuri. Unategema kutakuwa na walimu bora kwenye shule za walalahoi?

Sawa tumefanikiwa kuongeza shule za sekondari zinazoingiza wanafunzi wengi kidato cha kwanza, lakini vipi kuhusu ubora wa elimu? Mi' nadhani kujisifu kwa kujenga sekondari nyingi zinazopokea wanafunzi wengi bila kujali ubora wa elimu wanayoipata ni kufilisika kimawazo.

Kama ulikuwa na wanafunzi 10 wakashinda 2, hapa hakuna sifa ya ubora. Na mwaka unaofuatia ukawa na wanafuzi 30 wakashinda 5 bado hakuna Ubora. Wanaohesabu ushindi wa watoto toka wawili kwenda watano kuwa ni ongezeko basi tumefilisika kwa sababu kuna watoto ishirini na tano wameshindwa kwenda mbele!

Unapokuwa 'bachela' utapika chakula kwa kiwango cha kukutosha wewe na upimaji wa shibe lazima uwe kwa mtu mmoja, lakini huwezi kuhesabu mafanikio kwa kupika chakula kingi wakati hali halisi inasema umepika chakula hicho kwa sababu ya ongezeko la wageni. Jambo la msingi ni kupima malengo ya ongezeko lenyewe kama watu wote wamekula na kushiba.

0755 666964
bjhiluka@yahoo.com

ISAIAS AFEWERKI: Serikali yake yajiunga tena Igad ili kuepuka kutengwa kimataifa

Isaias Afewerki

ASMARA
Eritrea

ERITREA ni nchi ya Afrika Kaskazini-Mashariki. Upande wa Magharibi imepakana na Sudan, upande wa Kusini imepakana na Ethiopia, na Kusini-Mashariki kuna nchi ya Djibout. Mashariki na Kusini-Mashariki Eritrea ina pwani ndefu ya Bahari ya Shamu. Eneo hili hujulikana pia kama Pembe ya Afrika. Nchi hii inaongozwa na Isaias Afewerki tangu ilipojikomboa kutoka Ethiopia mwaka 1991.

Jina la nchi hii lilitungwa mnamo mwaka 1890 na wakoloni wa Italia kutokana na neno la Kigiriki "erythraia" linalomaanisha “bahari nyekundu”. Hii ni kwa sababu Bahari ya Shamu iliitwa "Sinus Erythraeus" na mabaharia Wagiriki au “Mare Erythraeum” kwa Kilatini na Waroma wa kale – maana yake ni "bahari nyekundu" – tazama Kiingereza “Red Sea”.

Eritrea imeruhusiwa kujiunga tena na shirika la maendeleo la Afrika Mashariki, Igad, baada ya kujitoa kama mwanachama mwaka 2006.

Katibu mtendaji wa Igad, Mahboub Maalim, ameiandikia serikali ya Eritrea kuiarifu kuwa ombi lake la kutaka kujiunga tena limekubalika na watapokewa na wanachama kwa moyo mkunjufu.

Utawala wa mjini Asmara uliamua kufuta uanachama wake wa Igad baada ya mahasimu wao Ethiopia kutuma majeshi yake nchini Somalia kupambana na vikosi vya umoja wa mahakama ya Kiislamu waliokuwa wanatawala sehemu kubwa ya Kusini mwa nchi hiyo.

Mwezi uliopita Igad ilipendekeza kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liiwekee vikwazo serikali ya Eritrea kufuatia vitendo vyake vya kushirikiana na kundi la wapiganaji wa Al Shabaab wanaoipinga serikali ya mpito ya Somalia.

Wadadisi wanasema huenda utawala mjini Asmara umeamua kujiunga tena na Igad ili kuepuka mikakati ya jumuiya ya kimtaifa kuitenga au kuiwekea vikwazo.

Wiki iliopita tume maalum inayochunguza utekelezaji wa vikwazo vya kuingiza silaha nchini Somalia, ilidai kwenye ripoti yake kuwa Eritrea ilihusika na mpango wa kushambulia mkutano wa viongozi wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika uliofanyika mwezi Januari mwaka huu.

Ingawa mpango huo ulitibuliwa na vyombo vya usalama nchini Ethiopia, tume hiyo ilisema harakati za Eritrea za kuhujumu usalama katika eneo la Afrika Mashariki ikishirikiana na wanachama wa Al Shabaab zipo wazi.

Hata hivyo serikali ya Eritrea imekanusha madai hayo na badala yake kunyooshea mahasimu wao Ethiopia ambao wanasema ndio chanzo cha uvumi huo.

Uhusiano kati ya Eritrea na Ethiopia upo katika hali mbaya kufuatia mzozo wao kuhusu umiliki wa mji wa Badme ulioko kwenye mpaka wa nchi hizo mbili. Licha ya mahakama ya kimataifa kuamua kuwa mji huo upo nchini Eritrea, utawala wa Addis Ababa umekataa kutii amri ya mahakama hiyo.

Historia ya Afewerki

Isaias Afewerki amezaliwa mjini Asmara, tarehe 2 Februari 1946. Ni Rais wa kwanza na wa sasa wa Eritrea, aliyeongoza kundi la Eritrean People's Liberation Front hadi kupata ushindi kwa watu wa Eritrea katika kujikomboa mnamo Mei mwaka 1991, hivyo kumaliza miaka 30 ya mapambano ya ukombozi wa silaha waliyoyaita kwa jina la "Gedli".

Maisha ya awali na kuingia madarakani

Afewerki alijiunga na Eritrean Liberation Front (ELF) mwaka 1966, na mwaka uliofuata alipelekwa China kupata mafunzo zaidi ya juu ya kijeshi. Miaka minne baadaye aliteuliwa kuwa kamanda wa jeshi la ELF. Hata hivyo, akitoa sababu ya tofauti ya kiitikadi, yeye na kikundi kidogo cha wapiganaji walijitenga na ELF na kuanzia kikundi kingine cha Eritrean People's Liberation Front (EPLF).

Ilipoonekana wazi kuwa EPL ilielekea kusambaratika, EPLF kiliungana na makundi mengine mawili ambayo yalikuwa yamejitenga kutoka ELF kabla: kundi la PLF1, lililoongwa na Osman Saleh Sabbe, na kundi lingine lililojulikana kama OBEL.

Mwaka 1976, EPLF ilijimega kutoka kundi la Sabbe baada ya kutia saini makubaliano ya umoja na ELF (Mkataba wa Khartoum). Isaias Afewerki ndiye aliyekuwa kiongozi wa EPLF wakati wa harakati za muda mrefu kwa ajili ya uhuru wa Eritrea ambao hatimaye ulipatikana baada ya miaka 30 ya mapambano ya silaha.

Mwezi Aprili 1993, Umoja wa Mataifa ulisimamia kura ya maoni kuhusu uhuru, na mwezi uliofuata Eritrea ilitangazwa huru. EPLF ilijibadili jina na kuwa People's Front for Democracy and Justice (PFDJ) mnamo Februari 1994 kama sehemu ya maandalizi yake ya kujikaribisha yenyewe kuwa chama cha siasa katika Eritrea ya kidemokrasia.

Hata hivyo, kutokana na ukweli kwamba Eritrea ilijikuta kwenye vita kutokana na mgogoro wa mpaka na Ethiopia tangu mwaka 1998, wakaandaa Katiba ya Eritrea na utekelezaji wake umewekewa muda usiojulikana. Lakini bado PFDJ inatawala Eritrea.

Mwaka 2001, kundi lililoundwa na maafisa 15 wa juu wa serikali, lililojulikana kama G-15, lilitoa barua ya wazi kuikosoa serikali ya Isaias Afewerki kuwa ipo "kinyume cha sheria na katiba" na kutoa wito kwa ajili ya utekelezaji wa katiba iliyotayarishwa. Hata hivyo, maombi yao hayakufaulu na wawanachama wa kundi la G-15, kumi na mmoja kati yao wakawekwa kizuizini nchini Eritrea na bado hawajashtakiwa.

Baada ya Uhuru

Baada ya uhuru wa Eritrea mwaka 1991 na mwaka 1993 baada ya kura ya maoni, Afewerki akawa mkuu wa nchi wa kwanza. Katika miaka ya kwanza ya utawala wake katika serikali hii mpya, taasisi ya utawala iliwekwa katika muundo. Hii ni pamoja na marekebisho ya miundo ya utawala kutoka juu hadi chini na mfumo wa mahakama ya muda iliyochaguliwa kupanua mfumo wa elimu katika mikoa mingi iwezekanavyo.

Mnamo Novemba 1993, Rais aliamuru kufungwa kwa askari wastaafu waliopigana vita vya ukombozi kwa kuandamana kuhusu hali ya maisha magumu katika kambi ya kijeshi. Shirika huru pekee la haki za binadamu lilifungwa. Mwaka 1997, Rais aliamuru kufungwa kwa mashirika yote ya maendeleo ya kimataifa kufanya kazi katika nchi hiyo.

Uchaguzi wa rais, ulipangwa kuwa mwaka 1997, lakini haikutokea na Eritrea bado ni ya chama kimoja, ikitawaliwa na People's Front for Democracy and Justice (PFDJ), chama pekee kilichoruhusiwa kufanya kazi. Mwezi Mei 2008, Afewerki alitangaza kuwa uchaguzi utaahirishwa kwa “miongo mitatu au minne” au zaidi.

Pia mwaka 1998 mgogoro wa mpaka na nchi jirani ya Ethiopia ulioashiria barugumu la vita kamili. Mnamo Septemba 2001, Afwerki alitoa amri ya kukamatwa kwa wanachama kumi na mmoja wa ngazi za juu zaidi katika utawala wake, wengi wao wakiwa ni rafiki zake wa karibu na wenzake aliopigana nao pamoja bega kwa bega vita vya ukombozi kwa karibu miongo minne. Walikamatwa kwa 'kutuhumiwa uhaini', wakapewa adhabu ya kifo kwa kutoa wito wa mageuzi ya kidemokrasia.

Aina zote za vyombo vya habari mpaka sasa vinadhibitiwa na serikali. Eritrea ni nchi pekee ya Afrika kutokuwa na vyombo vya habari vya binafsi. Mwaka 2009, Waandishi Wasiokuwa na Mipaka waliiweka Eritrea katika nafasi ya chini kabisa katika orodha ya nchi katika Ripoti ya Uhuru wa Habari, nyuma ya Korea Kaskazini.

Makala haya yameandaliwa na Bishop J. Hiluka kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya habari vya kimataifa.