Anwar Ibrahim
KUALA LUMPAR
KIONGOZI wa upinzani nchini Malaysia , Anwar Ibrahim ameondolewa makosa ya ulawiti katika kesi iliyochukua karibu miaka miwili. Mwanasiasa huyo alituhumiwa kufanya ngono na aliyekuwa msaidizi wake wa kiume. Hata hivyo jaji wa mahakama hiyo alisema uchunguzi wa DNA haukutoa ushahidi wowote.
Punde baada ya mahakama kutangaza uamuzi huo, jamaa wa Anwar walionekana kububujikwa na machozi ya furaha huku wafuasi wake wakishangilia uwamuzi huo. Wafuasi wa mwanasiasa huyo waliokusanyika nje ya mahakama mjini Kuala Lumpar wamekuwa wakisisitiza kwamba kesi hiyo haikufaa kufunguliwa tangu kuwasilishwa kwa tuhuma za ulawiti.
Hii ni mara ya pili Anwar ameshtakiwa kwa kufanya ulawiti. Kesi dhidi yake zimesababisha kuwepo na msisimko mkubwa wa kisiasa nchini Malaysia kwa zaidi ya muongo mmoja. Anwar Ibrahim ametaja kesi hiyo kama iliyochochewa kisiasa japo serikali imekanusha kuhusika kwa vyovyote.
Huku uchaguzi mkuu ukitarajiwa karibuni, chama tawala ambacho kimekuwa madarakani kwa zaidi ya nusu karne kinakabiliwa na upinzani mkali kutoka mrengo wa upinzani unaoongozwa na Anwar.
Historia yake
Anwar Ibrahim amezaliwa 10 Agosti 1947 ni mwanasiasa wa Malaysia ambaye aliwahi kuwa Naibu Waziri Mkuu wa Malaysia 1993 hadi1998. Mapema katika kazi yake, Anwar alikuwa mshirika wa karibu wa Waziri Mkuu, Mahathir Mohamad, lakini baadaye alijitokeza kama mkosoaji maarufu wa serikali ya Mahathir.
Mwaka 1999, alihukumiwa kifungo cha miaka sita jela kwa rushwa, na mwaka 2000, miaka mingine tisa kwa kulawiti. Mwaka 2004, Mahakama Kuu iliipindua hukumu yake ya pili na kumuachia. Julai 2008, alikamatwa kwa madai ya kumlawiti mmoja wa wasaidizi wake wa kiume, lakini aliachiwa huru mwaka 2012.
Tarehe 26 Agosti 2008, Anwar alishinda tena uchaguzi wa Pauh Permatang na kurejea Bungeni kama kiongozi wa upinzani wa Malaysia . Amesema ipo haja ya kuwepo uhuru, ikiwa ni pamoja na mahakama huru na vyombo vya habari huru, ili kupambana na rushwa iliyotapakaa ambayo anaona inaisukuma Malaysia kwenye umasikini.
Kuanzia 1968 hadi 1971, akiwa mwanafunzi, Anwar alikuwa rais wa chama cha wanafunzi wa Kiislamu. Alikuwa pia mmoja wa waasisi wa kamati ya Vuguvugu la Vijana wa Kiislamu wa Malaysia , ambayo ilianzishwa mwaka 1971. Pia alichaguliwa kuwa Rais wa Baraza la Vijana wa Malaysia . Mwaka 1974, Anwar alikamatwa wakati wa maandamano ya wanafunzi dhidi ya umaskini na njaa vijijini. Hii ilitokana na tetesi kuwa familia ilikufa kutokana na njaa katika kijiji cha Baling, katika jimbo la Kedah, pamoja na ukweli kwamba haikuwahi kutokea. Alifungwa jela chini ya Sheria ya Usalama wa Ndani, inayoruhusu kuwekwa kizuizini bila kufunguliwa mashitaka, na alikaa kizuizini kwa miezi 20 katika Kituo cha Kamunting.
Mwaka 1968-1971, alilelewa katika Umoja wa Kitaifa wa Wanafunzi wa Kiislamu wa Malaysia akiwa rais wa Muungano. Mwaka 1982, Anwar, aliyekuwa kiongozi mwanzilishi na rais wa pili wa chama cha vijana wa Kiislamu, aliwashangaza wafuasi wake kwa kujiunga na United Malays National Organisation (UMNO), iliyoongozwa na Mahathir Mohamad, aliyekuwa waziri mkuu mwaka 1981. Alipanda safu ya kisiasa haraka: kazi yake ya kwanza ilikuwa ni Waziri wa Vijana, Utamaduni na Michezo mwaka 1983, baadaye, aliongoza wizara ya kilimo mwaka 1984 kabla ya kuwa Waziri wa Elimu mwaka 1986. Kwa wakati huo, uvumi ulienea kuwa Anwar kupanda hadi nafasi ya Naibu Waziri Mkuu kitu kilichokuwa jambo la kawaida nchini Malaysia kwa Waziri wa Elimu kushika nafasi ya Naibu Waziri Mkuu.
Kipindi cha uongozi wake kama Waziri wa Elimu, Anwar alianzisha sera mbalimbali katika mitaala ya shule kitaifa. Moja ya mabadiliko makubwa aliyofanya ni kuipa jina jipya lugha ya taifa kutoka Bahasa Malaysia na kuwa Bahasa Melayu, moja ya makabila nchini Malaysia kitendo kilichokosolewa na wasio wa kabila hilo .
Mwaka 1991 aliteuliwa kuwa Waziri wa Fedha. Mwaka 1993, akawa Naibu Waziri Mkuu wa Mahathir baada ya kushinda Unaibu Rais wa UMNO dhidi Ghafar Baba. Kuna taarifa Anwar alitumia fedha nyingi ili kuungwa mkono. Ilidaiwa pia alitumia fedha za siasa ili kupata nafasi yake kama makamu wa rais wa UMNO.
Mwishoni mwa miaka ya 1990, hata hivyo, uhusiano wake na Mahathir ulianza kuzorota, ulisababishwa na kutofautiana juu ya utawala. Wakati Mahathir hayupo, Anwar alijichukulia hatua kali za kuboresha mifumo ya uongozi wa nchi hiyo ambayo ilikuwa tofauti na sera za Mahathir za kibepari.
Matarajio ya Kisiasa
Novemba 2006, Anwar alitangaza mpango wa kugombea ubunge mwaka 2008. Anwar amekuwa mkosoaji wa sera za serikali tangu kuachiliwa kwake kutoka gerezani, hasa utata wa Sera Mpya ya Uchumi, ambayo inatoa usawa wa kijinsia kwa Bumiputras. Sera zinazoweka idadi maalum ambayo lazima ifikiwe. Pia ni Mshauri wa Parti Keadilan Rakyat, chama ambacho mke wake, Dk Wan Azizah ni rais.
Tarehe ya uchaguzi wa 2008, hata hivyo, ilipangwa kuwa Machi 8, 2008, na kuzua mzozo ambapo chama cha Barisan Nasional kilitoa wito wa kufanyika uchaguzi huo mapema kwa nia ya kuzima mipango ya Anwar kutaka kurudi Bungeni. Mke wa Anwar, Wan Azizah Wan Ismail, alitangaza kuwa angejiuzulu ili kurejesha kiti chake cha ubunge wa Permatang Pauh ili kulazimisha uchaguzi ambao Anwar atagombea. Alipoulizwa kuhusu uwezekano wa Anwar kuwa Waziri Mkuu ajaye, kiongozi wa zamani, Tun Dr Mahathir, alijibu kwa vijembe, "Labda awe Waziri Mkuu wa Israel ".
Madai ya ngono
Katika Baraza Kuu la UMNO, kitabu, "Sababu 50 Kwanini Anwar Hawezi Kuwa Waziri Mkuu" kilisambazwa chenye picha pamoja na shutuma za rushwa dhidi ya Anwar. Kitabu kimeandikwa na Khalid Jafri, mhariri wa zamani wa gazeti la serikali, ‘Utusan Malaysia ’ na aliyekuwa mhariri mkuu wa gazeti wa jarida lililoshindwa la Harian National. Anwar aliomba amri ya mahakama kuzuia usambazaji zaidi ya kitabu na kufungua kesi dhidi ya mwandishi kwa kashfa. Polisi walimshtakiwa mwandishi wa kitabu kwa kuchapisha habari za uongo. Miongoni mwa madai katika kitabu ni kwamba Anwar ni shoga. Polisi waliamuriwa kuchunguza ukweli wa madai hayo. Katika kile gazeti la Sydney Morning Herald liliita "ukweli wa kisiasa uliopangwa", Anwar alishtakiwa kwa kulawiti, alikutwa na hatia na kuhukumiwa miaka 15 jela.
Mwaka 1999, Anwar alifungua kesi dhidi ya Waziri Mkuu Mahathir ya kashfa, kwa madai ya kutamka shutuma za vitendo kinyume na maadili na kumwita Anwar shoga katika mkutano wa waandishi habari nchini Malaysia . Hukumu hii iligeuzwa mwaka 2004, na Anwar akatoka gerezani. Mwandishi wa kitabu alikufa mwaka 2005 kwa ugonjwa wa kisukari, lakini si kabla ya Mahakama Kuu kumkuta na hatia ya kashfa na kutakiwa kulipa fidia ya mamilioni. Mahakama Kuu, Machi 8, 2010 ilitoa uamuzi kuwa kutimuliwa kwa Anwar mwaka 1998 kutoka Baraza la Mawaziri kulikofanywa na Mahathir kulikuwa halali kikatiba.
Tarehe 29 Juni 2008, iliripotiwa kuwa msaidizi wa Anwar Ibrahim alitoa ripoti polisi ya madai kuwa alilawitiwa na Anwar. Anwar alisema kuwa uwezekano wa hukumu ya kifungo jela kutokana na madai inaweza kuwa jaribio la kumuondoa kwenye nafasi ya kiongozi wa upinzani kufuatia kuongezeka kwa wafuasi wake na ushindi katika uchaguzi. Pia alisaini kuwa hana hatia na alitoa ushahidi katika mfumo wa taarifa za matibabu.
Kesi hii imefutwa tarehe 9 Januari 2012, karibu miaka miwili baada ya kesi kuanza, baada ya Jaji Mohamad Zabidin Mohd Diah, kumuona Anwar hana hatia ya kulawiti. Jaji aligundua kuwa ushahidi wa DNA uliowasilishwa na upande wa mashtaka haukuwa sahihi, na kumwachia huru Anwar.
Madai ya mkanda wa ngono uliofichwa
Machi 21, 2011 video ya ngono ilionekana ambayo ilidaiwa kumshirikisha Anwar Ibrahim. Siku moja baadaye, Anwar Ibrahim alifungua malalamiko polisi. Polisi kwa sasa wanafanya uchunguzi dhidi ya watu watatu ambao waliionesha video hiyo. Watu hao ni waziri kiongozi wa zamani wa Malacca, Tan Sri Abdul Rahim Thamby Chik, mfanyabiashara Datuk Shazryl Eskay Abdullah na mweka hazina wa zamani wa Perkasa, Datuk Shuaib Lazim.
No comments:
Post a Comment