Mtoto mwenye mtoto
BISHOP HILUKA
Dar es Salaam
KUNA siku chapisho moja la makala lilinivutia sana kuhusu vijana kujiingiza katika tabia za hatari. Makala ile ilieleza mambo yanayoweza kuwachelewesha au kuwakwaza vijana kutofikia malengo yao ya maisha kama : Dawa za kulevya, Ulevi, VVU/Ukimwi, Mimba kabla ya wakati n.k.
Katika makala hiyo, zilielezwa sababu zinazowafanya vijana (wasichana) kupata mimba kabla ya wakati, mwandishi alipendekeza namna ya kuwasaidia ili wasijikute katika mtego huu na pia waweze kufikia malengo yao katika maisha yao . Ingawa sababu hizi ziliwalenga wasichana moja kwa moja, hata hivyo, zinaweza kutumika kwa wavulana pia, kwa vile wavulana wanajiingiza katika mambo haya kirahisi kuliko wasichana.
Bibi Tricia M. Davis alifanya utafiti kati ya wasichana wapatao 500 wenye umri wa miaka chini ya 19, waliowahi kupata mimba zaidi ya mara moja. Katika utafiti wake ameeleza sababu saba zilizojitokeza na kuchangia katika hawa kupata mimba zaidi ya mara moja. Katika makala yake, “An Examination of Repeat Pregnancies Using Problem Behaviour Theory”, iliyochapishwa katika Jarida la Journal of Youth Studies (Vol. 5, no.3, 2002, pp.337-351), amefafanua kwa kina juu ya tatizo hili. Mimi nitajaribu kugusia tu kwa kadri ninavyoweza.
Imeelezwa kuwa sababu ya kwanza ni kutokuwa na malengo maalum katika maisha. Vijana wenye malengo endelevu katika maisha huwa wanachelewesha tendo la ndoa na hivyo kutopata mimba kabla ya wakati. Kijana anapokuwa amejiwekea malengo makubwa katika maisha yake, hakika atakuwa makini zaidi na daima atajiepusha na tabia zinazoweza kumfanya kutofikia malengo yake. Kwa mfano, ikiwa kijana fulani aliye katika kidato cha kwanza (Form I) na ana lengo la kuwa rubani wa ndege au kiongozi mashuhuri katika nchi au mtu yeyote maarufu, ni wazi atajishugulisha zaidi na mambo ya masomo.
Kutojithamini ambapo kijana kujiona hafai kwa chochote katika familia anamotoka au katika jamii ya watu inayomzunguka. Hisia hii inamfanya kujichukia na kupata msukumo wa kutaka kutafuta thamani ya nafsi yake kirahisi. Njia mojawapo ya kufanya hivi ni kujaribu mambo ya mapenzi. Kwa msichana wa hali hii ni rahisi kufikiri thamani yake inatokana na tendo hili la ngono kwani linaambatana na lugha nzuri wanazotumia wavulana na ahadi au zawadi anazoweza kupewa. Wasichana wanaotoka katika familia zisizo na upendo wa kweli kati ya wazazi ni rahisi kudanganyika na kutafuta thamani zao nje ya familia.
Kutowajibika humsababisha kijana kupata mimba kirahisi. Kutowajibika kuna maana ya mtu anavyoeleza matukio mbalimbali ya maisha yake na jinsi gani anavyojiepusha na tukio lile. Tabia hizi zaweza kuonekana hata katika mambo madogo madogo. Kwa mfano, kijana akidondosha kitu fulani na kusema, “Kitu hiki kimedondoka”, yeye anajaribu kutafsiri tukio lile kuwa hakuhusika nalo kabisa. Au mwingine anapovunja glasi na kusema, “Glasi imevunjika” anajaribu kutowajibika na tukio hilo . Sote tunatambua jinsi Adamu alivyotaka kujiepusha na kutokuwajibika kwa kosa alilofanya katika bustani ya Edeni. Mungu alipomuuliza, “Umefanya nini?” Adamu alimjibu Mungu, “Mwanamke uliyenipa ndiye alinidanganya nami nikala…” Adamu hakutaka kuwajibika na tendo lake. Hali kadhalika kijana mwenye mazoea ya kutowajibika katika mambo madogo madogo, ni rahisi kwake kujiingiza katika ngono na hatimaye kupata mimba bila kujali au kuwajibika. Wasichana wenye tabia ya kusema, “Shetani alinidanganya” au “Tulikuwa tunajaribu,” wanaonyesha dalili za kutowajibika na tendo walilofanya.
Ukosefu wa uchaji Mungu ambayo ni ile hali ya kijana kutojali mambo ya kiimani. Vijana wanaokuwa na hali hii ya kutojali mambo ya kidini na imani kwa ujumla wanajiweka katika mazingira rahisi zaidi ya kujiingiza katika tabia za hatari. Hii ni kwa sababu wanakuwa wamezamisha dhamiri zao zisiwasumbue wanapokuwa wamekosea. Kwa upande mwingine, vijana wanaojihusisha na vikundi mbalimbali vya kukuza imani, wanapata malezi mazuri juu ya dhamiri zao na hivyo hata kama wakikosa ni rahisi kwao kurudi katika msingi mzuri wa maadili.
Mazingira duni nyumbani pia huwafanya vijana kujiingiza katika tabia za hatari. Kama msichana anaishi na mzazi mmoja, kuna uwezekano wa binti kupata mimba mapema kutokana na kuathiriwa na mfano wa muundo wa familia anayoishi. Pia kwa wale wanaotoka katika familia ambazo mume na mke si waaminifu, kuna uwezekano mkubwa wa kijana kushawishika na kuanza mambo ya mapenzi mapema.
Mshinikizo wa rika unaweza kuwalazimisha vijana lakini si kwa sehemu kubwa! Vijana wanaweza kushawishika kufanya ngono au kujiingiza katika tabia za hatari kutokana na hadithi zinazosimuliwa na wenzao. Kila mmoja hujidai kuwa alijaribu mambo haya na kuelezea jinsi alivyojisikia. Hali hii inaweza kuchochea hamu ya kutaka kujaribu mambo ya hatari. Kama kijana tayari ana malengo na anajithamini si rahisi sana kupeperushwa na upepo huu wa masimulizi haya. Lakini kama kijana hana malengo maalum katika maisha na hajui thamani yake, basi ni wazi mshinikizo wa rika una nafasi kubwa ya kumpotosha.
Vijana wenye tabia ya kupenda kujaribu ili kujua ladha yake hata bila kujali madhara yake wanaweza kuingia katika mtego kirahisi. Kwa kufikiri kuwa wanaweza kujaribu tendo lolote la hatari mara moja tu na kuacha, kumbe kunaweza kuwa mtego wa kudumu.
No comments:
Post a Comment