Feb 24, 2012

Ili kurudisha utamaduni wa kusoma vitabu, tuanzishe utaratibu wa kuwasomea watoto

Utamaduni wa kujisomea huanza tangu utotoni 
kama anavyoonekana mtoto Magdalena Hiluka


BISHOP HILUKA

Dar es Salaam

KUSOMA vitabu ni jambo zuri na muhimu sana katika maisha ya binadamu kwani mambo mengi muhimu katika dunia hii yapo katika maandishi, iwe kwenye vitabu au mitandao ya jamii, yakiwemo maneno ya Mungu kwa wale wenye imani za kiroho. Yote haya utayakuta katika maandishi, ndani ya vitabu. Kama huna utamaduni wa kujisomea vitabu au kuperuzi katika mitandao ya intaneti, basi usitegemee kupata habari nzuri, kuelimika zaidi na kujua mengi yanayotokea duniani.

Wiki chache zilizopita katika kuperuzi kwangu baadhi ya machapisho nikiwa na lengo la kujaribu kuongeza maarifa, nilikutana na makala moja kuhusu usomaji wa vitabu ambao Watanzania tumeuacha siku hizi, ingawa jambo hili limekuwa likiandikwa sana lakini nikiri tu kuwa makala hii ilinivutia sana, ndiyo maana leo nimeamua kuja na hoja hii.

Makala hii iliandikwa na mmoja wa waandishi wa vitabu wakongwe, Profesa Joseph Mbele, Mtanzania anayeishi Northfield, Minnesota, nchini Marekani. Profesa huyo aliandika akihimiza wazazi kupenda kuwasomea watoto wao vitabu ili kuwavutia kupenda kusoma, akifananisha na enzi zile za mababu na mabibi zetu, ambapo ilikuwa ni kawaida kwa wazee hao kukaa na watoto au wajukuu jioni na kuwasimulia hadithi.

Utamaduni huu ulikuwa ni sehemu ya maisha, na ingawa watoto walichukulia kama kitu cha kawaida lakini ilikuwa ni sehemu ya elimu waliyopewa hao watoto. Hapakuwa na shule tulizonazo leo, wala vitabu, lakini wazee walikuwa walimu bora, waliotumia mbinu mbalimbali, kama hizi hadithi, katika kuwaelimisha watoto.

Lakini siku hizi, japo tuna vitabu na shule karibu kila mtaa, lakini tunashindwa kutumia fursa ya kutumia vitabu kuendeleza elimu ya watoto! Sijui tatizo ni nini? 

Hivi tatizo ni nini hata pale tunapokosa uwezo wa kuwasimulia hadithi kwa mtindo wa mababu na mabibi zetu, tunayo fursa ya kuwasomea vitabu, lakini tunashindwa kuitumia na kujikuta tukiuendeleza ule msamiati ambao binafsi umekuwa ukiniudhi sana, wa “Watanzania hatuna utamaduni wa kusoma vitabu”.

Katika nchi za wenzetu, kama nchi aliyoitolea mfano Profesa Mbele ya Marekani, wamekuwa wanaendeleza utamaduni huu kwa kuwasomea watoto hadithi za vitabuni. Watoto wa Kimarekani wanategemea mzazi awasomee vitabu. Ni kawaida kwa mzazi kumsomea mtoto kitabu kabla hajalala.

Wamarekani wanajali sana utamaduni wa kusoma vitabu. Utawaona wazee, watu wazima, wake kwa waume, vijana, na watoto katika maduka ya vitabu. Utawaona wazazi wakiwa wanakuja na watoto wao. Utawasikia wakiongea na watoto kuhusu vitabu, wakiwasomea watoto vitabu, wakijibu maswali ya watoto, na kadhalika.

Hali hii ni tofauti sana na iliyopo hapa nchini mwetu Tanzania. Leo ni Ijumaa. Je, ni mzazi gani Mtanzania ambaye siku kama ya leo anaenda kwenye duka la vitabu? Ni mzazi gani ambaye anampeleka mtoto wake kwenye duka la vitabu?

ABD MANSOUR HADI: Kaimu Rais aliyekuwa mgombea pekee wa urais Yemen

Abd Rabbu Mansour Hadi

SANAA

Yemen



SIKU ya Jumanne wiki hii, raia wa Yemen waliamkia katika vituo vya kupigia kura kumchagua rais wao mpya baada ya nchi kukumbwa na ghasia kwa mwaka mzima. Kila mtu alikuwa anajua kuwa atakayeshinda ni makamu wa Rais wa nchi hiyo, Abd Rabbu Mansour Hadi.



Uchaguzi huo umefanyika baada ya mwaka mmoja wa ghasia na maandamano ya kupinga utawala wa Rais Ali Abdullah Saleh. Kabla ya uchaguzi huu kampeni zilikuwa zikiendelea kumuunga mkono makamu huyo wa rais, Abd Rabbu Mansour Hadi, ingawa ndiye aliyejitokeza na kuwa mgombea pekee asiye na mshindani.



Mshindi wa tuzo ya Nobel, raia wa Yemen, Bi Tawwakol Karman, aliwataka raia wote wa Yemen kujitokeza kumuunga mkono makamu huyo wa rais.



“Tunawaomba watu wote wa Yemeni wakiwemo vijana wajitokeze hii leo tarehe 21 Februari, sio kuunga mkono uchaguzi peke yake, bali kumuunga mkono Mansour Hadi kuwa Rais wa mpito katika kipindi hiki cha mpito,” alisema Bi Karman siku ya Jumanne wiki hii.



Huku Mshindi huyo wa Tuzo ya Nobel akimpigia debe Mansour Hadi kuwa rais, tayari imeripotiwa kuwa ghasia zimeanza upya nchini Yemen. Pia kumeripotiwa kuwepo kwa mfululizo wa milipuko na mashambulio katika vituo vya kupigia kura na sehemu nyingine.



Historia yake



Field Marshal Abd Rabbuh Mansur Al-Hadi alizaliwa mwaka 1945. Ni askari na mwanasiasa ambaye amekuwa Makamu wa Rais wa Yemen tangu tarehe 3 Oktoba 1994. Kati ya Juni 4  na Septemba 23, 2011 alikuwa akikaimu urais wa Yemen, wakati Ali Abdullah Saleh alipoondoka kwenda nchini Saudi Arabia kwa ajili ya matibabu, baada ya kujeruhiwa katika mashambulizi yaliyolenga ukumbi wa rais wakati wa maandamano ya kuipinga serikali ya  Yemeni mwaka 2011.



Ndipo, tarehe 23 Novemba, Abd Mansour al-Hadi akawa kaimu rais tena, baada ya Saleh kuachia madaraka "katika kile kinachosemwa ni kwa ajili ya kupata kinga dhidi ya mashtaka." Al-Hadi "anatarajiwa kuunda serikali ya umoja wa kitaifa na pia kutoa mwito wa kuitisha uchaguzi wa rais mapema ndani ya siku 90" wakati Saleh akiendelea kutumika kama rais kwa jina tu.



Maisha ya awali



Al-Hadi alizaliwa mwaka 1945 katika eneo la Abyan. Jina lake pia linaweza kuandikwa Abd Rabu Mansur Hadi, Abd Rabbah Mansour Hadi au Abdurabu Mansour Hadi, miongoni mwa vifupi vingine tofauti.



Alijiunga na Jeshi la Yemen Kusini mwaka 1970 na kuwa Meja Jenerali mwanzoni mwa mwaka 1990.



Kazi ya siasa



Alikuwa Makamu wa Rais wa Yemen baada ya Ali Salim al-Beidh kujiuzulu na kushindwa katika vita vya wenyewe kwa wenyewe. Al-Hadi aliteuliwa na Rais Ali Abdullah Saleh kama Makamu wa Rais tarehe 3 Oktoba 1994. Kabla ya uteuzi wake kama Makamu wa Rais, alikuwa Waziri wa Ulinzi.



Al- Hadi ndiye aliyejitokeza kuwa mgombea pekee katika uchaguzi wa rais uliofanyika siku ya Jumanne ya tarehe 21 Februari 2012. Ugombea wa Al-Hadi umeungwa mkono na chama tawala pamoja na bunge la upinzani. Ingawa kupiga kura kimsingi ni mfano wa demokrasia lakini ni sababu moja tu inayomfanya mgombea Al-Hadi ambaye tayari ni kaimu Rais kuungwa mkono, nayo ni nia ya kukamilisha uhamisho wa madaraka kutoka kwa Saleh kwenda kwa Al-Hadi.



Licha ya Al-Hadi kutumikia nafasi ya umakamu wa rais kwa kipindi kirefu cha miongo miwili, Hadi ni mtu ambaye raia wa Yemeni wanamfahamu kidogo mno. Kamanda wa zamani wa kijeshi kutoka Kusini, Al-Hadi, mwenye umri wa miaka 66, alikwama kwa Saleh wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Yemen kati ya Kaskazini na Kusini vya mwaka 1994. 



Katika miezi ya hivi karibuni, ikiambatana na kuanguka kwa Saleh, majukumu yanamwangukia yeye kusimamia mageuzi ya kikatiba, urekebishaji wa nchi hiyo na kusafisha njia kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa vyama vingi mwaka utakaofanyika mwaka 2014.



Hata hivyo, kwa sababu alijikuta akilazimika kufanya kazi kwa muda mrefu katika serikali ya Saleh, wengi bado wana shaka iwapo atakuwa na msimamo unaoweza kuleta mshikamano wa kisiasa na kuvunja ushawishi uliowekwa na bosi wake wa zamani. Mahudhurio ya chini ya watu siku ya Jumanne ni kama utabiri, inaweza kupunguza uhalali wake zaidi.



Vyanzo vya kidiplomasia vya Marekani viliyotolewa na WikiLeaks vimemuelezea Al-Hadi kama mzushi aliyepandikizwa, angalau ni mtu ambaye alikuwa akifurahia mshikamano mdogo miongoni mwa madalali wa madaraka nchini Yemeni.



"Bingwa anayedhaniwa wa mageuzi, msimamo wa Al-Hadi kama makamu wa rais kwa kiasi kikubwa ni sherehe na haiwezi kumfanya kuwa na ushawishi mkubwa kwa [serikali] watoa maamuzi," kulingana na taarifa za WikiLeaks za 2004.



"Pamoja na kutoka kanda ya kusini ya Abyan, Abd Mansour Al-Hadi aliongoza kampeni dhidi ya YSP (Yemeni social party), chama cha kijamaa cha Yemeni, na aliwahi kuwa waziri wa ulinzi wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.



"Kuteuliwa kwake katika serikali ya muungano mwaka 1994 kunachukuliwa kama malipo (hongo) kwa ajili ya huduma yake kwa eneo la kaskazini," kilisema chanzo cha WikiLeaks.



Chanzo hicho pia kilihusisha mkutano wake na balozi wa Marekani, Thomas Krajeski, ambapo Al-Hadi alimuambia mgeni wake huyo wa Marekani kwamba "Yemen itahitaji msaada wa Marekani katika kupunguza umaskini, kufanikisha mageuzi ya kiuchumi na kidemokrasia, na kuvutia uwekezaji wa kigeni".



Vyanzo vingine vya habari vya kimtandao vilihusisha uungaji wake mkono kwa uongozi wa Syria katika msuguano wake na Israeli, na tuhuma zake kwa Eritrea, ambapo Yemen ilipinga na kuzua mgogoro kuhusu visiwa vya Hanish katika Bahari ya Shamu mwaka 1995.



Eritrea, Al-Hadi aliisema kuwa, ilikuwa ni "thawra" (mapinduzi) zaidi kuliko kuwa "dawla" (nchi).  "Wao wanapambana na kila mmoja," alisema, kulingana na chanzo cha habari za kimtandao.



Makala haya yameandaliwa na Bishop Hiluka kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya habari vya kimataifa.

Feb 17, 2012

Serikali itamke wazi kuwa imeshindwa kudhibiti udanganyifu katika mtihani

Katibu Mtendaji wa NECTA, Dk. Joyce Ndalichako

BISHOP J. HILUKA
Dar es Salaam

HIVI karibuni Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta) limetangaza matokeo ya mtihani wa kumaliza sekondari mwaka jana 2011, ambao watahiniwa 3,303 wamebainika kuufanya kwa zaidi ya mara 10 ya mwaka juzi, hali inayotufanya tuamini kuwa udanganyifu huu umekuwa gonjwa lililokosa tiba kwa serikali yetu.

Katibu Mtendaji wa Necta, Dk. Joyce Ndalichako, alisema kuwa Baraza limefuta matokeo ya watahiniwa hao, ambao kati yao, 3,301 ni wa Mtihani wa Kidato cha Nne na wawili ni wa Maarifa (QT). kila mwaka msamiati huu wa udanganyifu umeendelea kutawala, si tu kwa matokeo ya kidato cha nne, bali hata darasa la saba au kidato cha sita. Hii inatufanya tuingiwe na wasiwasi kwa kuwa hawa waliohusika ndiyo watakaokuwa viongozi wa kesho, je, tutegemee nini kutoka kwa serikali watakayoiongoza?

Kila mwaka, nyakati kama hizi wakati matokeo ya mtihani kwa wanafunzi wanaomaliza elimu ya sekondari yanapotangazwa huambatana na baadhi ya wanafunzi kushangilia hali wengine wakibaki wameduwaa. Matokeo hayo huleta huzuni kwa walio wengi ambao hawakupata matokeo mazuri. Pia hili suala la baadhi yao au shule kadhaa kufutiwa matokeo kwa sababu za udanganyifu katika mtihani limekuwa ni sehemu ya matokeo hayo. Binafsi sishangai kila linaposikika.

Limekuwa la kawaida kwa kuwa matokeo haya hutumika kuwakejeli watoto wa mafukara na wazazi wao kwa kuwa wamewekwa kando na mfumo wa kijamii – kiuchumi unaowapendelea, kuwajenga na kuwaendeleza wachache huku ukiwapuuza, kuwachuja na kuwatupa walio wengi.

Mfumo wa kijamii – kiuchumi nchini umejengwa kitabaka, hautumiki kuleta usawa katika jamii bali unatumika kuzidisha tabaka kati ya matajiri na masikini. Enzi za Mwalimu Nyerere, matarajio na malengo ya mfumo wa elimu ilikuwa kwanza kupiga vita ujinga. Lengo lilikuwa kuhakikisha kila Mtanzania anajua kusoma na kuandika ili kuweza kujitegemea.

Huo ndio ulikuwa msingi ambao ulijengwa na Serikali ya Awamu ya Kwanza. Baada ya Mwalimu, awamu zilizofuata zilipaswa kuendeleza mambo muhimu yanayohitajika katika mfumo wa elimu bora. Hivi sasa tunajivuna kutimiza miaka 50 ya Uhuru, lakini bado hatujautazama upya mfumo wetu wa elimu unamsaidiaje Mtanzania wa karne hii ya sayansi na teknolojia, ikiwa ni pamoja na kutafuta tiba hii ya udanganyifu katika mitihani.

Hivi tunadhani tunajenga taifa la aina gani,
kama kila mwaka tutaendelea kushuhudia “maafa” haya ya udanganyifu kwa vijana ambao tunataraji siku moja watakuwa viongozi wa nchi hii? Hivi hata huu mfumo tulionao unamjengaje kijana wa Kitanzania kushindana na kijana wa Kikorea, Kihindi au Kimexico kama si kuhamasisha wizi wa mitihani?

Kwa mujibu wa Dk. Ndalichako, kama alivyonukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari kuhusu aina za udanganyifu, alisema kuwa ni pamoja na wanaokamatwa na wasimamizi ndani ya chumba cha mitihani wakiwa na ‘notes’, wanaofanyiwa mitihani na watu wengine, wanaosajiliwa kufanya mitihani kwa kutumia majina ya wengine wakati walishafanya mtihani na wanaokuwa na karatasi za majibu zenye miandiko tofauti au kuwa na miandiko tofauti katika karatasi ya somo moja.

Nyingine ni kubadilishana karatasi za maswali/vijitabu vya kujibia mtihani ili kuandikiana majibu, au kujadiliana ndani ya chumba cha mtihani, watahiniwa kukamatwa na booklet zaidi ya moja ambapo booklet moja hawakupewa na msimamizi na watahiniwa kubainika kuwa na kesi mbili tofauti; kama vile mfanano wa majibu, notes, kijitabu cha kujibia zaidi ya kimoja na kubadilishana karatasi za majibu au kijitabu cha kujibia mtihani.

Yote haya yanasababishwa na mfumo tulionao unaoangalia zaidi matokeo ya mtihani na si uelewa, huku tukitumia mfumo wa miaka saba ya elimu ya msingi, miaka mine ya sekondari na miwili ya sekondari ya juu kabla mwanafunzi hajakanyaga chuo chochote kupata mafunzo anayoweza kuyatumia.

Kwa maana hiyo, kijana anatumia miaka 13 akiwa hana ujuzi wowote! Je, katika miaka hii 13 anakuwa ameandaliwa kushindana na vijana wenziwe kutoka nchi nyingine kama hatafanikiwa kuingia chuo chochote?

Na huu mfumo wa mtoto kuanza elimu ya msingi akifundishwa masomo yote kwa Kiswahili isipokuwa somo la Kiingereza kwa miaka yote saba, kisha anapoanza sekondari masomo yote kufundishwa kwa Kiingereza isipokuwa somo la Kiswahili hatudhani kuwa ndiyo chanzo cha udanganyifu huu, kwa kuwa unayafanya masomo kuwa magumu zaidi na yasiyoeleweka kwa wanafunzi? Hatuoni kuwa mwanafunzi kujifunza mambo mageni kwa lugha ya kigeni ndiyo sababu ya wizi huu?

Mimi naamini kuwa mfumo huu unazalisha vijana wenye uwezo wa juu wa kukariri na si vijana wenye uwezo wa kufikiri na kuchambua mambo. Kama matarajio yetu ni kuhakikisha wanafunzi wanafaulu mitihani, basi tumepiga hatua kumi kurudi nyuma kwa kuwa kijana wa Kitanzania huandaliwa ili afanye mtihani, na hii ndiyo sababu ya udanganyfu tunaoulalamikia kila mwaka!

Tangu lini ubora wa elimu ukapimwa  kwa kushindanisha shule zipi zinatoa wanafunzi wengi wa daraja la kwanza, na si shule zipi zinatoa wanafunzi wenye uwezo wa juu wa kufikiri na kuchambua mambo?

Badala ya kuwapa watoto elimu ya kuwafanya wajitambue na kuendeleza vipawa vyao tunatumia muda mwingi kuwafanya wafaulu mitihani kitendo kinachohamasisha wizi wa mitihani. Mfumo wa kutathmini vipawa vya watoto kwa mitihani ya siku chache katika kipindi kirefu cha masomo hautufai na ndiyo sababu ya udanganyifu huu. Hivi hili serikali hailioni?

Nadhani sasa wakati umefika serikali iamue moja; kubadilisha mfumo wa elimu na kuwawajibishwa na kuwachukulia hatua kali wote waliohusika, au itangaze kuwa imeshindwa katika vita hii.

YUSUF RAZA GILANI: Apandishwa kizimbani kwa kukataa kuchunguza ufisadi wa mkuu wake

Yousaf Raza Gillani

Pakistan

MAHAKAMA kuu nchini Pakistan imetupilia mbali rufaa ya waziri mkuu wa nchi hiyo dhidi ya mashitaka yanayomkabili ya kudharau mahakama. Ina maana kuwa Yusuf Raza Gilani (pia huandikwa Yousaf Raza Gillani) atatakiwa kufika mbele ya mahakama kuu kusikiliza mashitaka dhidi yake ya kukataa kuchunguza tuhuma za ufisadi zinazomkabili rais wa nchi hiyo.

Waziri Mkuu hakuwa mahakamani siku kesi yake ilipotajwa, lakini wakili wake alisema Yusuf Raza Gilani hakudharau mahakama kwa kukataa kuchunguza madai ya ufisadi dhidi ya rais. Wakili huyo wa waziri mkuu, alisema Rais Asif Ali Zardari, akiwa mkuu wa nchi, sheria zinamlinda kutoshitakiwa.

Historia yake

Yusuf Raza Gilani (Mbunge) alizaliwa Juni 9, 1952, ni Waziri Mkuu wa 16 na wa sasa wa Pakistan, na makamu mwenyekiti wa chama cha kijamaa cha kidemokrasia, Pakistan Peoples Party (PPP). Gilani alipendekezwa kuhudumu katika ofisi ya ofisi ya waziri mkuu na kuwa waziri mkuu wakati chama chake kilipoanzisha serikali ya umoja na Pakistan Muslim League, Awami National Party, Assembly of Islamic Clergy na Muttahida Qaumi Movement (MQM), baada ya chama chake kupata ushindi mkubwa katika uchaguzi wa Bunge wa 2008. Ni waziri mkuu wa kwanza kutoka ukanda wa Wapakistanbi wanaozungumza lugha ya Saraiki, na pia waziri mkuu aliyehudumu kwa kipindi kirefu cha miezi 45 na kuongoza zaidi ya vikao 100 vya Bunge na baraza la mawaziri; mafanikio makubwa zaidi ya serikali ya kidemokrasia katika historia ya nchi hiyo.

Mafanikio yake ya kwanza yalikuwa kugombea ubunge 1988 na amekuwa mbunge mwandamizi wa jimbo la Multan-IV tangu mwaka 1988, akiongoza Wizara ya Utalii chini ya serikali ya waziri mkuu wa zamani, Benazir Bhutto. Baada ya chama chake kushinda katika uchaguzi wa bunge wa 1990, Gilani aliteuliwa na Benazir Bhutto kuwa Spika wa 15 wa Bunge, alihudumia hadi Februari 16, 1997. Februari 11, 2001, Gillani alifungwa na mahakama ya kijeshi akiweka chini ya Rais Pervez Musharraf, kwa shutuma na tuhuma za rushwa katika jela isiyofahamika sana ya Adiala, na alitolewa Oktoba 7, 2006.

Chama cha Gilani, PPP, kilipata ushindi mkubwa katika uchaguzi wa bunge wa mwaka 2008, na kwa ridhaa ya serikali ya mseto, Gilani aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu, akila kiapo kutoka kwa Rais Pervez Musharraf, tarehe 25 Machi, 2008. Katika kikao cha kwanza cha uzinduzi, Gilani alitangaza kuundwa kwa tume ya Ukweli na upatanisho, kupunguza bajeti na matumizi ya serikali, ujenzi wa ukanda ulioharibiwa kwa ukabila, elimu, ardhi, na mageuzi ya kilimo, ikifuatiwa na sera mpya ya nishati ya nyuklia. Mwaka 2009, Gilani aliwekwa katika nafasi ya 38 kama mtu mwenye mamlaka zaidi duniani na jarida la Forbes.

Asili yake

Gillani ni wa asili ya Iran na baba yake alikuwa mzao wa Syed Musa Pak, mtu wa imani ya kiroho ya Qadiri Sufism ambayo ilifuata asili yake kwa Abdul-Qadir Gilani wa Iran. Babu wa Yousaf Raza wa upande wa baba anatoka jimbo la Paktia, Afghanistan, lakini akaweka makazi nchini Iran baada ya kumuoa mwanamke wa Iran. Familia yake ilihamia Multan mwaka 1921 na baba yake Alamdar Hussain Gilani alikuwa kiongozi wa kisiasa wa Multan ambaye alitoa mchango mkubwa katika siasa za Pakistan. Hussain Gilani alikuwa mmoja wa watia saini wa Azimio la Pakistan mwaka 1940, na aliwahi kuongoza harakati za Pakistan. Mwaka 1953, Alamdar Hussain Gilani alikuwa waziri wa muda kwa Feroz Noon Khan, na pia alikuwa Waziri wa baraza la mawaziri baada ya Feroz Khan Noon kuteuliwa kuwa Waziri Mkuu mwaka 1958.

Elimu na familia

Gilani alizaliwa Juni 9, 1952 mjini Karachi, jimbo la Sindh, Magharibi mwa Pakistan. Muda mfupi tu, Gilani alihamia Multan, Jimbo la Punjab, alihudhuria mafunzo katika Chuo Kikuu cha Kikristo cha Forman. Alihudhuria katika Chuo cha Serikali na kupata shahada ya kwanza (BA) katika Uandishi wa Habari, na kufuatiwa na shahada ya uzamili (MA) katika Uandishi wa Habari wa Siasa kutoka Chuo Kikuu cha Punjab.

Gilani ameoa na ana watoto watano, wanne wa kiume, binti mmoja, na mmoja mjukuu. Mtoto wake mkubwa, Syed Abdul Qadir Makhdoom Gilani, alianzia kazi yake ya siasa Multan, na mwaka 2008, alimuoa mjukuu ya Pir Pagara Shah Mardan Shah II, kiongozi wa kisiasa na kidini wa Sindh mwenye ushawishi mkubwa. Watoto wake wengine watatu wa kiume, Ali Qasim Gilani, Ali Musa Gilani na Ali Haider Gilani walizaliwa mapacha watatu. Qasim Gilani kwa sasa anachukua shahada ya kwanza kutoka Chuo Kikuu cha Brunel London, ambapo Musa Gillani amemaliza shahada yake ya pili kutoka Chuo Kikuu Queen Mary cha London mwaka 2009.  Ali Haider Gilani anasoma katika Shule ya Uchumi ya Lahore, iliyopo Lahore.  Ali Musa Gilani baada ya kumaliza masomo yake kwa sasa anashiriki kikamilifu katika siasa. Jina la binti wa Yousaf Raza Gilani, ni Fiza Gillani.

Umma mtumishi

Kazi ya siasa ya Gilani ilikatishwa wakati wa sheria ya kijeshi wa Jenerali Zia-ul-Haq mwaka 1978, wa kwanza kujiunga na Kamati Kuu ya Pakistan Muslim League (PML), pamoja na Nawaz Sharif. Lakini hivi karibuni alijiondoa PLM, kutokana na tofauti za kisiasa.

Alichaguliwa kuwa Mbunge wa Bunge la Taifa (MNA) kwa mara ya kwanza akitokea Lodhran, kiti kinachoshikiliwa kwa sasa Saddique Baloch NA 154. Alikuwa pia mwanachama wa baraza la mawaziri katika serikali ya miaka mitatu ya Gilani akijiunga na Pakistan Peoples Party (PPP) mwaka 1988, kutokana na tofauti na Nawaz Sharif. Benazir Bhutto alichangia kwa kiasi kikubwa katika falsafa ya kisiasa ya Gilani na alikuwa waziri katika serikali ya Benazir Bhutto ya 1988-1990, alichaguliwa tena katika Bunge la Taifa kutoka kiti kingine NA 152, ambacho kwa sasa kinashikiliwa na Nawab liaqat ali, na alikuwa Waziri wa Utalii kutoka Machi 1989 hadi Januari 1990 na Waziri wa Nyumba na Ujenzi kuanzia Januari 1990 hadi Agosti 1990.  Baadaye, chini ya serikali nyingine ya Bhutto, akawa Spika wa Bunge mwezi Oktoba.

Kifungo

Yousaf Raza Gilani alikamatwa tarehe 11 Februari 2001, chini ya Ofisi ya Taifa ya Uwajibikaji (NAB), taasisi ya kupambana na rushwa, iliyoanzishwa na serikali ya kijeshi mwaka 1999, kwa madai kwamba alitumia vibaya mamlaka yake alipokuwa Spika wa wa Bunge. Hasa, alidaiwa kukodisha hadi watu 600 kutoka miongoni mwa wananchi wa jimbo lake na kuwaweka katika orodha ya mishahara ya serikali. NAB ilidai kuwa Gilani alisababisha hasara ya Rupia milioni 30 kila mwaka katika hazina ya taifa. Alikutwa na hatia na mahakama ya kupambana na rushwa iliyoundwa na Musharraf na alitumikia kifungo cha karibu miaka sita gerezani.

Jaribio la mauaji 2008

Gilani alikoswa kuuawa baada ya jaribio la mauaji lililofanywa tarehe 3 Septemba 2008, wakati mtu mwenye silaha asiyejulikana aliposhambulia gari lake lisilopenya risasi karibu na jiji la Rawalpindi, taarifa rasmi zimebainisha. Jaribio hilo lilitokea muda mfupi baada ya Gillani kurudi akitokea katika ziara ya kiofisi katika jiji la mashariki la Lahore. Msafara wake ulikuwa ukielekea Islamabad kutokea eneo la jeshi lenye ulinzi mkali la Rawalpindi. Msemaji wa Waziri Mkuu alisema Gilani na wafanyakazi wake hawakujeruhiwa.

Makala haya yameandaliwa na Bishop Hiluka kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya habari vya kimataifa.

Feb 15, 2012

Ubabe hausadii, njia sahihi itafutwe kutatua mgomo wa madaktari nchini

Wauguzi wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili wakitafakari wakati madaktari wakiwa bado kwenye mgomo

BISHOP HILUKA
Dar es Salaam

MIGOMO ya madaktari haikuanza leo, imeanza siku nyingi. Nakumbuka wakati wa Awamu ya Pili ya Rais Ali Hassan Mwinyi kulikuwa na mgomo mkubwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) na maeneo kadhaa uliosababisha madaktari kadhaa kufukuzwa kazi na baadaye kurudishwa tena kazini baada ya kukubaliana katika mambo fulani fulani. Mgomo uliibuka tena wakati wa Awamu ya Tatu ya Rais Benjamin William Mkapa, ambapo Waziri Mkuu wa wakati huo, Fredrick Sumaye alikwenda kuongea na madaktari na kuweka mambo sawa.

Mwaka 2006, miezi michache tu tangu serikali ya Awamu ya Nne kuingia madarakani, kulitokea tena mgomo katika hospitali hiyo hiyo ya Taifa ya Muhimbili (MNH), ambapo safari hii mgomo huu haukuungwa mkono kitaifa. Kwa kiasi kikubwa ulihusiana na ongezeko la posho na mishahara. Wakati huo serikali ndiyo kwanza ilikuwa imeingia madarakani miezi michache nyuma yake na baadhi ya wachambuzi walipinga hatua hiyo ya madaktari kwa kuwa waliamini haikuwa nafasi nzuri ya kudai ongezeko kubwa kabla serikali hiyo haijakaa chini kupitisha bajeti mpya.

Leo, miaka zaidi ya mitano baadaye inadhihirisha kuwa serikali imeshindwa kabisa au haitaki kushughulikia matatizo ya maslahi na mafao ya madaktari. Kwa nini? Binafsi sina jibu la haraka haraka. Naamini kuwa inaweza kufanya hivyo kama inaamua. Sasa tatizo ni nini? Hakuna tatizo ambalo linazungumzwa leo hii ambalo lilikuwa halijulikani miaka iliyopita.

Mgomo wa sasa hauwezi kwisha bila kumalizika. Hauwezi kumalizika kama ulivyolazimishwa ule wa mwaka 2006 ambapo serikali iliamua kuwatimua madaktari kwani tofauti na wa wakati ule huu wa sasa umeenea nchi nzima na tukio lolote la kutishia kuwafukuza madaktari (walioanzisha au walioshiriki) linaweza kuwafanya madaktari kuwa na msimamo mkali zaidi.

Ieleweke kuwa sishabikii mgomo wa madaktari kwani wanaoumia ni walalahoi, madaktari wanapoamua kugoma hasa kwa nchi nzima basi ni lazima taifa lishtuke. Tumefika mahali ambapo madaktari wa nchi nzima wanagoma! Hii inaashiria kuwa mambo yameshindikana kwa njia ya mazungumzo? Au watawala na wanasiasa wameshindwa kuweka uzito kwenye hoja za muda mrefu za madaktari hao?

Na sasa tumesikia hadi madaktari bingwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) nao wameamua kugoma! Madaktari bingwa wameungana na kamati ya madaktari inayosimamia mgomo na kuitaka Serikali kujibu hoja zilizowasilisha kwake haraka ili kumaliza tatizo hilo. Hii ni hatari kwa sisi wananchi wa kawaida, kama serikali na madaktari wataendelea kuvutana na serikali kuendelea kutumia ubabe na kushindwa kushughulikia tatizo hili la madaktari.

Na tangu haya yameanza kutokea hatujasikia kuna mtu kawajibika au kuwajibishwa kutokana na mgomo huu wa madaktari. Kwa nini? Ni kwa nini Serikali iliyokuwa ikilaumiwa kwa mgomo huu, kwa kuchelewesha posho za madaktari wanafunzi na kuwafanya wagome, ilipowalipa tu posho zao wakahamishwa kwa kile kinachoonekana ni kuwakomoa na kuwakomesha?

Ni dhahiri mgomo huu wa madaktari ulioanza kama cheche moja katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na kutokupewa uzito unaostahili na serikali, sasa umegharimu maisha ya wananchi walalahoi wengi na hata kuliingiza taifa katika hatua ngumu juu ya utoaji wa huduma za afya. Serikali ikubali kuwa imefanya makosa mengi kwenye sekta ya afya, wakati sasa umefika wa kupitia sera yake ili kuifanyia mabadiliko.

Mgomo huu pia umetikisa katika hospitali za mikoa ya Mwanza, Morogoro, Kilimanjaro, Tanga, Mbeya na Dodoma. Huduma za afya zimeathirika kwa kiasi kikubwa mno na kama mvutano huu wa serikali na madaktari utaendelea, hali itazidi kuwa mbaya. Nadhani suala la madaktari linahitaji hekima na busara zaidi kuliko nguvu na vitisho.

Naamini kuwa kama si serikali au tabia ya baadhi ya viongozi wake kupuuza malalamiko ya madaktari na kushindwa kuwa wepesi kutuliza jazba ya wataalam hawa wa afya mapema, imesababisha hali ya utoaji huduma za afya katika hospitali za umma kufikwa na hali hii ya mkanganyiko mkubwa.

Katika mapambano haya wanaoumia ni wananchi wa kawaida wanaotegemea huduma za afya katika hospitali hizi na wala si viongozi wa serikali wala madaktari, kwa hiyo ufumbuzi wa haraka wa mvutano huu unapaswa kutafutwa.

Mgomo huu umesababisha kwa zaidi ya wiki mbili huduma za kitabibu katika Hospitali ya Muhimbili, Taasisi ya Mifupa (MOI), Tasisi ya Saratani ya Ocean Road na hospitali za Temeke, Amana na Mwananyamala kuathirika sana.

Serikali badala ya kuendeleza ubabe ingechukulia mgomo huu wa madaktari kama changamoto, lazima uwe na matokeo ya kuboresha afya za wananchi, vinginevyo huko tunakoelekea ni kubaya sana.

Hivi sasa Bunge limeamua kuingilia kati mgomo huu wa madaktari kwa kuitaka Serikali kulitolea tamko tatizo hilo bungeni,na baadaye kuundwa timu ya wabunge kufuatilia suala hilo.

Mimi ninalipongeza Bunge kwa hatua hiyo, lakini nadhani, serikali na hususan Rais Jakaya Kikwete, kama mwajiri mkuu nchini alipaswa mapema kukutana na madaktari, kukaa nao meza moja, kuwasikiliza na kuwaeleza namna atakavyoshughulikia madai yao ama ni kwa nini yanashindikana. Kusema ukweli, hata kama watendaji wake wanashughulikia, lakini Rais Kikwete amechelewa sana kuingilia kati suala hili nyeti.

Madaktari pia wamekuwa wakilalamikia watendaji pale katika Wizara ya Afya kwa kutowajibika sawasawa na dharau. Mimi ninaamini kuna watu wa kuwajibika pale kufuatia kadhia hii. Kama machafuko katika Uwanja wa Mpira nchini Misri yaliyoua watu zaidi ya 70 yamesababisha Gavana wa Jimbo la Port Said, mkuu wa usalama nchini humo pamoja na Rais wa Shirikisho la soka la nchi hiyo kuwajibika kwa kujiuzulu, hapa mbona watu wanakufa lakini hakuna anayejizulu?
Naomba kuwasilisha.

BASHAR AL-ASSAD: Sasa akalia kuti kavu nchini Syria

Rais wa Syria, Bashar al-Assad

DAMASCUS

Syria



MUUNGANO wa nchi za Kiarabu unaendelea kutoa wito kwa Assad kukabidhi madaraka kwa naibu wake ambaye ataunda serikali ya muungano wa kitaifa na sasa unaungwa mkono na Marekani, Uingereza na Ufaransa. Lakini Moscow imesema kuwa mpango huo "hauna usawa" na "utatoa mwanya'' wa uingiliaji wa masuala ya ndani ya Syria.



Marekani imetoa wito kwa mataifa yote kutoa msimamo wao kuhusiana na kile ilichokitaja kuwa udhalimu serikali ya Syria. Imesema kuwa mataifa ya kirafiki yanayoitakia Syria utawala wa Kidemokrasia yanapaswa kuungana katika kumshutumu kiongozi wa taifa hilo Rais Assad. Waziri wa mashauri ya Kigeni wa Marekani, Hillary Clinton, alisema ni jambo la kusikitisha kuwa Urusi na China zilipiga kura za turufu kupinga azimio la kuikosoa Syria katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.



Alitoa wito kwa jamii ya kimataifa iunge mkono makundi ya upinzani nchini Syria. Ni wazi kwamba Marekani pamoja na wanadiplomasia wa mataifa mengine ya Magharibi wameghadhabishwa mno na hatua ya Urusi na China kupinga azimio la kuikosoa Syria.



Clinton alizungumza akiwa Bulgaria ambako amesema Marekani pamoja na mataifa mengine zitashinikiza Rais Assad aondoke madarakani. Alizungumzia kuhusu kuwekwa vikwazo zaidi pamoja na kuwataja watu ambao wanafadhili na kuipa silaha serikali ya Syria.



Mataifa ya magharibi yanajiandaa kupigia debe azimio kali kwenye mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusiana na mgogoro uliopo nchini Syria. Katibu mkuu wa muungano wa Mataifa ya Kiarabu Nabil al-Arabi anatarajiwa kutoa ombi kwa Baraza la Usalama kuunga mkono mpango mpya wa muungano huo unaotaka rais wa Syria Bashar al-Assad ajiuzulu.



Historia ya Assad



Bashar al-Assad alizaliwa Septemba 11, 1965, mbai na urais pia ni Katibu wa Mkoa wa Chama cha Ba'ath.  Baba yake Hafez al-Assad alitawala Syria kwa miaka 29 hadi kifo chake mwaka 2000. Al-Assad alichaguliwa mwaka 2000, na kuchaguliwa tena mwaka 2007, bila kupingwa.



Maisha ya awali



Bashar al-Assad alizaliwa katika Dameski, ni mtoto wa Aniseh (nee Makhluf) na Hafez al-Assad. Nyumba aliyokulia ilikuwa na vuguvugu la siasa chini ya kivuli cha baba yake, Hafez Assad, ambaye alichukua madaraka ya urais wa Syria katika Mapinduzi ya 1970. Tofauti na ndugu zake, Basil na Maher, dada zake Bushra, Bashar, alikuwa kimya na hakupenda siasa au kazi ya kijeshi.



Alipata elimu yake ya msingi na sekondari katika shule ya mchepuo wa Kiarabu-Kifaransa ya al-Hurriya, Damascus na alikuwa mwanafunzi mfano bora aliyefanya vizuri sana kimasomo. Mwaka 1982, alihitimu shule ya sekondari na kwenda kusomea tiba katika Chuo Kikuu cha Damascus. Mwaka 1988, Bashar Assad alihitimu masomo ya tiba na kufanya kazi kama daktari katika hospitali kubwa ya kijeshi, "Tishrin", nje kidogo ya Damascus.



Miaka minne baadaye, alikwenda Uingereza kuanza mafunzo ya Udaktari bingwa wa macho (Ophthalmology) katika Western Eye Hospital, sehemu ya makampuni ya mafunzo ya St Mary jijini London. Wakati huo Bashar hakuwa na matarajio ya kisiasa. Baba yake alimwandaa kaka wa Bashar, Basil al-Assad, kuwa rais wa baadaye. Hata hivyo, Bashar aliitwa mwaka 1994 kujiunga na jeshi, baada ya kifo cha Basil kisichotarajiwa katika ajali ya gari.



Kifo cha Basil



Muda mfupi baada ya kifo cha Basil, Hafez Assad alifanya uamuzi wa kumfanya Bashar kuwa mrithi wake mpya. Katika kipindi cha miaka sita na nusu iliyofuata, hadi kifo chake mwaka 2000, Hafez aliandaa utaratibu kwa ajili ya Bashar kuchukua madaraka. Maandalizi kwa ajili ya kipindi cha mpito yalifanywa katika ngazi tatu. Kwanza, alijengwa ndani ya jeshi na vyombo vya usalama. Pili, picha ya Bashar ilijengwa ili afahamike zaidi kwa umma. Na mwisho, Bashar alifanywa kuzoea taratibu za kuendesha nchi kabla.



Kupata sifa ya kijeshi, mwaka 1994 Bashar alijiunga katika chuo cha kijeshi cha Homs, Kaskazini mwa Dameski, na alipitia safu haraka hadi nafasi ya Kanali Januari 1999. Ili kuandaa msingi imara kwa Bashar katika jeshi, makamanda wakongwe walitakiwa kustaafu, na damu changa, maafisa vijana watiifu kwake walichukua nafasi zao. Sambamba na kazi yake ya kijeshi, Bashar alishiriki katika masuala ya umma. Alipewa mamlaka makubwa na akawa mshauri wa kisiasa kwa Rais Hafez al-Assad, mkuu wa ofisi ya kupokea malalamiko ya rufaa ya wananchi, na aliongoza kampeni dhidi ya rushwa. Kama mkuu wa kampeni dhidi ya rushwa, Bashar alipata uwezo wa kuondoa wapinzani wake wenye uwezekano wa kuwania urais.



Mwaka 1998, Bashar alichukua mamlaka ya faili la masuala ya Syria-Lebanon, ambalo lilikuwa linashikiliwa na aliyekuwa Makamu wa Rais, Abdul Khaddam tangu miaka ya 1970, mmoja wa viongozi wachache wa Sunni katika serikali ya Assad, ambaye hadi wakati huo alikuwa na uwezekano wa kuwa rais. Kwa kuchukua mamlaka ya masuala ya Syria nchini Lebanon, Bashar alikuwa na uwezo wa kushinikiza Khaddam akae kando na kusimika nguvu zake katika Lebanon.



Katika mwaka huo huo baada ya mashauriano madogo na wanasiasa wa Lebanon, Bashar alimweka Emile Lahoud, mshirika wake mwaminifu, kama Rais wa Lebanon na kumuweka kando Waziri Mkuu wa zamani wa Lebanon, Rafic Hariri, kwa kutolipa uzito jina lake katika nafasi ya waziri mkuu. Ili kudhoofisha zaidi mkakati wa zamani wa Syria nchini Lebanon, Bashar alimbadilisha balozi wa mrefu wa Syria nchini Lebanon, Ghazi Kanaan, na mshirika mwaminifu, Rustum Ghazali. Chini ya Bashar, rushwa ya Syria nchini Lebanon, ambayo tayari ilikuwa inakadiriwa kufikia dola bilioni 2.0 kwa mwaka katika miaka ya 1990, na kushindwa kudhibitiwa kulikosababisha kuanguka kwa benki ya Lebanon Al-Madina mwaka 2003.



Al-Madina ilitumiwa kuchukua fedha katika michezo ya kubahatisha (kamari) kinyume cha sheria ya mpango wa Umoja wa Mataifa wa mafuta-kwa-chakula nchini Iraq. Vyanzo vilisema kuwa kiasi kilichohamishwa kwa njia ya benki ya al-Madina ni zaidi ya dola 1 bilioni, na asilimia 25 kwenda kwa viongozi wa Syria na washirika wao wa Lebanon, miongoni mwa wapokeaji wa fedha hizi alikuwa ndugu wa Bashar Assad, Maher, mkwe wa Emile Lahoud, Elias Murr, na Ghazali.



Urais



Wakati Assad mkubwa alipokufa mwaka 2000, Bashar aliteuliwa kuwa kiongozi wa chama cha Ba'ath na Jeshi, na alichaguliwa kuwa rais bila kupingwa katika kile serikali ilichodai kuwa kuungwa mkono kwa wingi (asilimia 97.2 ya kura), baada ya Al Majlis Sha'ab (Bunge) kupunguza umri wa chini kwa mtu anayetaka kugombea kutoka 40 hadi 34 (umri Assad alipochaguliwa). Mei 27, 2007, Bashar alipitishwa tena kuwa rais kwa kipindi kingine cha miaka saba, pamoja na matokeo rasmi ya asilimia 97.6 ya kura katika kura ya maoni bila ya mgombea mwingine.



Katika sera yake ya ndani, amekuwa akikosolewa kwa kupuuza haki za binadamu, kushuka kwa uchumi, na rushwa. Katika sera zake za kigeni, Al-Assad ni mkosoaji mkubwa wa Marekani na Israeli. Chama cha Ba'ath kinabakia katika udhibiti wa bunge, na kikatiba ni "chama kinachoongoza" serikali.



Hadi anakuwa rais, Bashar al-Assad hakuwa akishiriki sana katika siasa; jukumu lake kwa umma lilikuwa ukuu wa Chama cha Kompyuta cha Syria, ambacho kilianzisha huduma ya Internet nchini Syria mwaka 2001. Al-Assad alithibitishwa kuwa rais kwa kura ya maoni bila kupingwa mwaka 2000.



Alitarajiwa kufuata njia huru zaidi kuliko baba yake. Katika mahojiano alisema kuwa aliona demokrasia nchini Syria kama 'chombo cha maisha bora' lakini baadaye alisema kuwa itachukua muda kwa demokrasia kukomaa na kwamba isiharakishwe.



Kisiasa na kiuchumi, maisha ya raia wa Syria yamebadilika kidogo tangu mwaka 2000. Mara baada ya kuchukua madaraka harakati za mageuzi zimefanywa kwa tahadhari katika Dameski, ambayo yalisababisha al-Assad kufunga gereza la Mezzeh na mamia ya wafungwa wa kisiasa kutolewa.



Makala haya yameandaliwa na Bishop Hiluka kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya habari vya kimataifa.