Wauguzi wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili wakitafakari wakati madaktari wakiwa bado kwenye mgomo
BISHOP HILUKA
MIGOMO ya madaktari haikuanza leo, imeanza siku nyingi. Nakumbuka wakati wa Awamu ya Pili ya Rais Ali Hassan Mwinyi kulikuwa na mgomo mkubwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) na maeneo kadhaa uliosababisha madaktari kadhaa kufukuzwa kazi na baadaye kurudishwa tena kazini baada ya kukubaliana katika mambo fulani fulani. Mgomo uliibuka tena wakati wa Awamu ya Tatu ya Rais Benjamin William Mkapa, ambapo Waziri Mkuu wa wakati huo, Fredrick Sumaye alikwenda kuongea na madaktari na kuweka mambo sawa.
Mwaka 2006, miezi michache tu tangu serikali ya Awamu ya Nne kuingia madarakani, kulitokea tena mgomo katika hospitali hiyo hiyo ya Taifa ya Muhimbili (MNH), ambapo safari hii mgomo huu haukuungwa mkono kitaifa. Kwa kiasi kikubwa ulihusiana na ongezeko la posho na mishahara. Wakati huo serikali ndiyo kwanza ilikuwa imeingia madarakani miezi michache nyuma yake na baadhi ya wachambuzi walipinga hatua hiyo ya madaktari kwa kuwa waliamini haikuwa nafasi nzuri ya kudai ongezeko kubwa kabla serikali hiyo haijakaa chini kupitisha bajeti mpya.
Leo, miaka zaidi ya mitano baadaye inadhihirisha kuwa serikali imeshindwa kabisa au haitaki kushughulikia matatizo ya maslahi na mafao ya madaktari. Kwa nini? Binafsi sina jibu la haraka haraka. Naamini kuwa inaweza kufanya hivyo kama inaamua. Sasa tatizo ni nini? Hakuna tatizo ambalo linazungumzwa leo hii ambalo lilikuwa halijulikani miaka iliyopita.
Mgomo wa sasa hauwezi kwisha bila kumalizika. Hauwezi kumalizika kama ulivyolazimishwa ule wa mwaka 2006 ambapo serikali iliamua kuwatimua madaktari kwani tofauti na wa wakati ule huu wa sasa umeenea nchi nzima na tukio lolote la kutishia kuwafukuza madaktari (walioanzisha au walioshiriki) linaweza kuwafanya madaktari kuwa na msimamo mkali zaidi.
Ieleweke kuwa sishabikii mgomo wa madaktari kwani wanaoumia ni walalahoi, madaktari wanapoamua kugoma hasa kwa nchi nzima basi ni lazima taifa lishtuke. Tumefika mahali ambapo madaktari wa nchi nzima wanagoma! Hii inaashiria kuwa mambo yameshindikana kwa njia ya mazungumzo? Au watawala na wanasiasa wameshindwa kuweka uzito kwenye hoja za muda mrefu za madaktari hao?
Na sasa tumesikia hadi madaktari bingwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) nao wameamua kugoma! Madaktari bingwa wameungana na kamati ya madaktari inayosimamia mgomo na kuitaka Serikali kujibu hoja zilizowasilisha kwake haraka ili kumaliza tatizo hilo . Hii ni hatari kwa sisi wananchi wa kawaida, kama serikali na madaktari wataendelea kuvutana na serikali kuendelea kutumia ubabe na kushindwa kushughulikia tatizo hili la madaktari.
Na tangu haya yameanza kutokea hatujasikia kuna mtu kawajibika au kuwajibishwa kutokana na mgomo huu wa madaktari. Kwa nini? Ni kwa nini Serikali iliyokuwa ikilaumiwa kwa mgomo huu, kwa kuchelewesha posho za madaktari wanafunzi na kuwafanya wagome, ilipowalipa tu posho zao wakahamishwa kwa kile kinachoonekana ni kuwakomoa na kuwakomesha?
Ni dhahiri mgomo huu wa madaktari ulioanza kama cheche moja katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na kutokupewa uzito unaostahili na serikali, sasa umegharimu maisha ya wananchi walalahoi wengi na hata kuliingiza taifa katika hatua ngumu juu ya utoaji wa huduma za afya. Serikali ikubali kuwa imefanya makosa mengi kwenye sekta ya afya, wakati sasa umefika wa kupitia sera yake ili kuifanyia mabadiliko.
Mgomo huu pia umetikisa katika hospitali za mikoa ya Mwanza, Morogoro, Kilimanjaro, Tanga, Mbeya na Dodoma . Huduma za afya zimeathirika kwa kiasi kikubwa mno na kama mvutano huu wa serikali na madaktari utaendelea, hali itazidi kuwa mbaya. Nadhani suala la madaktari linahitaji hekima na busara zaidi kuliko nguvu na vitisho.
Naamini kuwa kama si serikali au tabia ya baadhi ya viongozi wake kupuuza malalamiko ya madaktari na kushindwa kuwa wepesi kutuliza jazba ya wataalam hawa wa afya mapema, imesababisha hali ya utoaji huduma za afya katika hospitali za umma kufikwa na hali hii ya mkanganyiko mkubwa.
Katika mapambano haya wanaoumia ni wananchi wa kawaida wanaotegemea huduma za afya katika hospitali hizi na wala si viongozi wa serikali wala madaktari, kwa hiyo ufumbuzi wa haraka wa mvutano huu unapaswa kutafutwa.
Mgomo huu umesababisha kwa zaidi ya wiki mbili huduma za kitabibu katika Hospitali ya Muhimbili, Taasisi ya Mifupa (MOI), Tasisi ya Saratani ya Ocean Road na hospitali za Temeke, Amana na Mwananyamala kuathirika sana .
Serikali badala ya kuendeleza ubabe ingechukulia mgomo huu wa madaktari kama changamoto, lazima uwe na matokeo ya kuboresha afya za wananchi, vinginevyo huko tunakoelekea ni kubaya sana .
Hivi sasa Bunge limeamua kuingilia kati mgomo huu wa madaktari kwa kuitaka Serikali kulitolea tamko tatizo hilo bungeni,na baadaye kuundwa timu ya wabunge kufuatilia suala hilo .
Mimi ninalipongeza Bunge kwa hatua hiyo, lakini nadhani, serikali na hususan Rais Jakaya Kikwete, kama mwajiri mkuu nchini alipaswa mapema kukutana na madaktari, kukaa nao meza moja, kuwasikiliza na kuwaeleza namna atakavyoshughulikia madai yao ama ni kwa nini yanashindikana. Kusema ukweli, hata kama watendaji wake wanashughulikia, lakini Rais Kikwete amechelewa sana kuingilia kati suala hili nyeti.
Naomba kuwasilisha.
No comments:
Post a Comment